Mungu nakushitakia, mja wako madhulumu
Sina pa kuelekea, ila kwako ya karimu
Nguvu zishaniishia, taabani mahmumu
Yarabi nisaidia, londoke hili dhalimu
Yarabi nisaidia, londoke hili dhalimu
Lipotee baidia, linisahau dawamu
Likitaka nirudia, ulipofuwe uyunu
Likome kunidamia, na kunyonya yangu damu
Likome kunidamia, na kunyonya yangu damu
Mjao nateketea, kwa dude hili dhalimu
Hadhi yangu ‘shapotea, siyo tena ya kadimu
Rabi lipoteze njia, lileweshe kwa naumu
Rabi lipoteze njia, ulilevye kwa naumu
Macho siweze fumbua, lishindwe kunihujumu
Nipate jitutumua, kujenga yangu kaumu
Na mbele kuendelea, bila ya lolo dhalimu
Hamad Hamad
25 Aprili 2011
Copenhagen
Sikia wangu Hamadi, Yasini ni dawa kweli
Ila ubio uzidi, ndo iwe makubuli
Itoe hiyo baridi, umshindilie mbali
Vinginevyo ‘takuzidi, adui dhalimu hili
Talishinda talishinda, ya abu ahmadi
Lishanza avya midenda, nilionavyo limaji
Lashindwa tu kusarenda, lijifanyavyo kaidi
Langu kukaza ubinda, na kuongeza sipidi.