Si wa hili u wa lipi, uso tambua utuo
Wajitambulisha vipi, kuilinda heshimayo
Moyo wangu haunipi, kuvaa si yangu nguo
Huu ndio uswahili, kwawo najifakharisha
Najifakharisha kwayo, fakhari ya Uswahili
Tatanga kila kituo, hapa ndipo manzili
Na mwisho wa zangu mbio, ‘tanikuta Zanzibari
Huu ndio uswahili, kwawo najifakharisha
Naona fakhari sana, kula kwa mkono wangu
Si kwa vijiko na nyuma, nikajifanya mzungu
Maamkizi ya heshima, nawapa wakubwa wangu
Huu ndio uswahili, kwawo najifakharisha
Lugha ni kubwa bahati, Mola aliyotupayo
Siwezi kuisaliti, haipenda nyingineyo
Yanibeba kitikiti, naipigia chapuo
Huu ndio uswahili, kwawo najifakharisha
Na mswahili ni yupi, kama si wa Zanzibari
Kwengine ni kapikapi, hapa ‘sa ndio asili
Sikusudii dhihaki, nachonga watu ukali
Huu ndio uswahili, kwawo najifakharisha
Sikusudii dhihaki, nachonga watu ukali
Nawataka washiriki, kwa hili kulijadili
Wanambe kwengine kupi, kwa uswahili asili
Huu ndio uswahili, kwawo najifakharisha.
Hamad Hamad
Aprili 26, 2011
Copenhagen