Upweke waadhabisha, pekeyo unapokuwa
Maisha huwa yachosha, la raha karaha lawa
‘Kiona watu wacheka, utasema wazomewa
Upweke nao maradhi
Upweke watunyofowa, ndani kwa ndani watula
Wakondefu tushakuwa, kukosa zetu aila
Tuyafanyayo hayawa, twadhalilika madhila
Upweke nao ni nduli
Upweke wasononesha, myoyoni joto watia
Furaha waiondosha, arijojo ‘kapotea
Hata kijilazimisha, ‘taishia kupumbaa
Upweke si jambo zuri
Upweke ‘kikufumbata, maisha ‘tayachukiya
Sononeko sononeka, nani atakusikia?
Utatamani kucheka, ukose la kuchekea
Upweke ni pigo baya
Upweke ‘kikugubika, saa huwa zasimama
Dakika zikazunguka, zikenda kinyuma nyuma
Utachoka hangaika, usiweze tenda jema
Upweke nao watisha
Upweke sifaye chafu, wapiga nyoyo na macho
Utawa na kila kitu, usione kifaacho
Kuruba na wako watu, ndicho peke utakacho
Upweke haushindika
Nsikize nyimbo ipi, ya kunitoa upweke?
Ntende matendo yapi, upweke unikopoke?
Dawa ya upweke ipi, nibwie na nijipake?
Upweke gonjwa thakili
© Hamad Hamad
March 12, 2011
Copenhagen
SWADAKTA BA HAMAD
Ba Hamadi wanikuna, maneno uyanenayo
Unavyovipanga vina, waugusa wangu moyo
Upweke hauna mana, ukizowea wenzio
Upweke ni ukatili
Hata uwe na dinari, mafedha na mayakuti
Au uwe jemedari, upigiwae saluti
Upweke una hatari, utapata kibuhuti
Upweke ! nh!