Udugu tulionao, si wa damu si nasabu
Si wa ndewe si sikio, si jamaa si karabu
Udugu masingizio, kuzidiana hesabu
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda
Mwananyika eniona, ‘mekaa nimetulia
Bukheri mwana mwanana, usoni naendelea
Akajifanya yu mwema, “ati” anisaidia
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda
Si kwamba neukubali, udugu na Mwananyika
Nejua he’mtu bali, ulikuwa ni mzuka
Wetumwa ni majangili, kuja nitia wahaka
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda
Udugu udugu gani, yeye pima miye nyanda?
Udugu uso mizani, yuanenepa nakonda
Nikikwama mijibani, yeye mbele yuasonga
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda
Udugu udugu gani, udugu wa kunyonyana
Mwananyika maluuni, nachuma yuakusanya
Sina kitu mfukoni, kwake i tele hazina
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda
Udugu udugu upi, bila ya misingi yake
Haki yangu siipati, changu chake chake chake
‘mefika sasa wakati, kila mmoja kivyake
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda
Nshachoka nshachoka, zigo hili mabegani
Udugu nawe hakika, ushafika ukingoni
Katangetange na nyika, zinga wapya wahisani
Udugu na Mwananyika, siwezi ushanishinda
Siutaki ukhiwani, usiokuwa na kheri
Nauvua kwa Yasini, Jowsheni na Ha’badiri
Saba w’arbaini, sinina ‘shastahmili
Udugu nawe hakika, siuwezi unishinda!
© Hamad Hamad
April 19, 2011
Copenhagen
kake udugu unao vya kuupangusa huna
udugu usio kwao wala usio na shina
kake utakufa nao hata kama ukikana
hata kama ukikana udugu umwo mwilini
kunaugauza jina silo lile la zamani
kunaupa hadhi bwana! ukubanduke kwa nini?
ukubanduke kwa nini udugu uloulea?
kheri wewe wende chini wowo upate elea
hata ningekuwa mimi kamwe nisingekwatia
singekwatia muhudi haadhirika njiani
ngekugida gidigidi hasasambua vya ndani
wataka nyuma nirudi nichekwe ni hata nyani!?
hilo katu Abadan!!!