Sitazikusanya sifa, mabindoni haziweka
Hangoja siku ukifa, ndipo haja zitamka
Sifa hazitena sifa, msifiwa ‘kisha uka
‘Takusifu tangu leo, upate kujitambua
Wengi huwa wasifiwa, mauti kisha wakuta
Ukaona wapambiwa, sifa ziso mlahaka
“Marehemu alikuwa, mtu asokasoreka”
‘Tasaidiani sifa, kwa asiye zisikia?
Kama ni miko kusifu, mtu asijapo kufa
Mie ntaikashifu, miko ntaikiuka
‘Tamsifiani mfu, sifa zisizomfika?
‘Takusifu tangu leo, sharafuyo uijue
Wino upi utoshao, sifazo kuandikiza
Wapi ‘taweka kituo, kusema ‘shazimaliza
Nipewe chaki na mbao, sizisozi ‘tazisaza
‘Takusifu tangu leo, singoji haja chelewa
Nakusifu tangu leo, u’hai ukejiweza
Siku uto’jifiyayo, sisemi taja nyamaza
‘Tatizama wasifuo, na kina wakijiliza
‘Takusifu tangu leo, ujue ‘shakusifia
Kuna kufa mie kwanza, sifa ‘ta’ ‘shaziandika
Ajizi seifanyiza, sifazo hazilimbika
Nekusifu nekiweza, na mwenyeo ‘kaitika
Sifazo zesheheneza, idadi hazetajika
© Hamad Hamad
February 21, 2011
Copenhagen