Wao…
Msimu wao ni leo, wao wao kupendana
Kuvaa nyekundu nguo, na maua kupeana
Iishapo leo yao, mapenzi hayapo tena
‘Kangoja mwaka ujao, wakaja pendana tena
Wewe…
Nimekupenda zamani, bila mwenyewe kujua
Hakuweka qalbini, ja yungi ukatuliya
Ikapita mitihani, ya penzi kutahiniwa
Yote tukaibaini, na shahada tukapewa
Sisi…
Mapenzi yetu matamu, tamu ya kuendelea
Sio kitu cha msimu, kitu cha kukingojea
Yapo daima dawamu, milele ‘taendelea
Yamo yandani ya damu, milini yatutembea
Mimi…
Ningekuwa na ujuzi, wa mvua kuitengeza
‘ngetengeza ya mapenzi, mwilini hakuroweza
Na moyoni ‘ngebarizi, rovyi rovyi hakurovya
Hilo ‘ngefanya daima, si jambo la leo moja
Dua…
Ingekuwa twaraduzwa, siku yetu kujifia
‘ngetaka niwe wa kwanza, peponi kutangulia
Henda hapatengeneza, pahali petu kukaa
Yote nikisha maliza, ukaja hakupokea
Ombi…
Kwa Mungu wangu muumba, ombi nampelekea
Jambo moja kumuomba, inshaallah ‘takabalia
Penzi letu kulilinda, milele lije bakia
Na siku yetu ya kwenda, peponi twende ishia.
© Hamad Hamad
February 14, 2011
Copenhagen