UCHAMBUZI

Mzee Nabwa, tunaendelea kukukumbuka

Siku kama ya leo, miaka minne iliyopita, mtu ninayemchukulia kama ‘baba’ yangu, linapokuja suala la uandishi wa habari, Ali Mohammed Nabwa, alihitajiwa na Mola wake, akiwa kalazwa kwenye hospitali ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam. Ilikuwa siku ngumu sana kwangu, na kwa wenzangu ambao tulimchukulia yeye kama shujaa wa tasnia ya habari Zanzibar. Mzee Nabwa alituchukua na kutulea kupitia gazeti lake la Dira Zanzibar, si mimi tu, bali waandishi wengi chipukizi katika mwanzoni mwa muongo uliopita.

Sikuwa nikijuilikana sana kabla ya mwaka 2002 nilipojiunga na Dira, ingawa baadhi ya makala zangu zilishawahi kutokeza katika gazeti la Rai linalochapishwa Dar es Salaam mwaka mzima nyuma.

Ni jukwaa la Dira Zanzibar, ndilo lilinipa wasaa na wasta wa kuandika mawazo yangu, yakasomwa, yakafahamika, na kwayo nikajuilikana kile ninachokisimamia. Dira halikuwa gazeti tu, ndivyo ambavyo kila siku Mzee Nabwa alitwambia. Ilikuwa taasisi. Na kama zilivyo taasisi zote makini, basi Dira nayo ilikuwa na misheni na visheni yake. Katikati yake palikuwa pamesimama Uzanzibari, Wazanzibari na Zanzibar.

Marehemu Ali Nabwa
Marehemu Ali Nabwa

Hiyo ndiyo Dira ambayo Mzee Nabwa, kwa kushirikiana na wenzake, akina Ismail Jussa, Salim Bimani, Salim Said Salim na Ally Saleh, waliijenga, na kutualika sisi wanagenzi katika fani ya habari kusaidia kuweka fito. Na jengo likasimama imara kwelikweli.

Ndani ya miezi sita tu ya kuanzishwa kwake, tayari lilishakuwa gazeti linalotegemewa, kwa upande mmoja, na kuogopewa kwa upande mwengine, lakini kwa pande zote likawa linaheshimiwa. Walilipenda na kulitegemea ambao walikuwa wakikubaliana na mtazamo na msimamo wake, walilichukia na kuliogopa waliokuwa hawakubaliani nalo. Lakini hata hao waliolichukia na kuliogopa, waliliheshimu sana.

Leo ni mwaka wa tisa tangu gazeti hili lipigwe marufuku na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini nasikitika kusema kuwa si sisi tuliokuwemo kwenye uendeshaji wake, wala wale waliokuwa nje yake, ambao wameweza kuanzisha tena gazeti kama lile. Hapana, nakusudia taasisi kama ile. Majaribio kadhaa yamefanyika hapa katikati, lakini ni bahati mbaya kwamba, labda kwa kukosekana mtu mwenye ujasiri, ueledi na kujitolea kwa Nabwa, hakuna jaribio lililowezekana.

Sisi wengine wakati serikali inaifunga Dira, tuliiambia kwamba ilikuwa inafunga mlango mmoja tu, mengine kumi ilishakuwa wazi na kamwe haitafungika tena. Mwenyewe, Mzee Nabwa, akaiambia kuwa inafunga banda, ilhali farasi alishatoka. Sote tukaapa kwamba, hata kama Dira imefungwa, ule udira wake hautakufa.

Wakati tumeshindwa kulifufua Dira kama gazeti, naamini kabisa kwamba tumefanikiwa kuendeleza misheni na visheni ya Dira, iliyoasisiwa na kulelewa na Marehemu Mzee wetu, Ali Mohammed Nabwa.

Ndio maana, nikiwa huku mbali niliko leo hii, nageuka nyuma na kutazama ngazi nilizokwea hata kufika hapa, njia niliyopita hata nikajikuta nilipo. Sioni chengine zaidi ya Nabwa na Dira.

Shaaban Robert anasema katika kitabu chake cha wasifu wa muimbaji maarufu wa Zanzibar,  Siti bint Saad, kwamba mwimbaji huyo aliwahi kutukanwa na wapinzani wake kwa kauli hii:

“Siti bint Saadi umekuwa mtu lini?
Kama si sauti, ungekula nini?”

Mimi leo hata nikitukanwa kwamba:

“Mohammed Ghassany waringa kwa lipi?
Kama si Nabwa na Dira, ungekuwa wapi?”

Basi naapa kwa Mola Aapiwaye, kwamba wala sitaliona hilo ni tusi. Bali kwangu itakuwa ni fakhari kunasibishwa na mtu na taasisi ambayo niliiamini na naendelea kuiamini hadi leo, maana nyuma yake kulikuwa kuna misheni na visheni ya maisha na uhai wangu: Uzanzibari!

Bila ya shaka, sote ni wa Mungu na sote kwake tunarejea. Mzee Nabwa amerejea kwa Muumba wake miaka minne iliyopita, lakini husemwa kwamba, kuishi katika nafsi za uliowawacha nyuma, hakuitwi kwamba ni kufa.

Nabwa anaishi ndani ya nafsi yangu, kama anavyoishi pia katika nafsi za Salma Said, Ismail Jussa, Salim Bimani, Jabir Idrissa, Salim Said, Ally Saleh, Muzdalifat, Zubeida na bila ya shaka kwenye nafsi za Wazanzibari wote, waliosoma na kuathiriwa na maandishi yake. Kwamba yake hayakuwa maandishi tu, ilikuwa harakati!

Allah amghufirie madhambi yake na aufanye mwema ujira wake. Ndoto yake kwangu naiona ikichukua sura ya kutimia. Nami naahidi itazidi kutimia kwa mapenzi ya Mungu na radhi za mzee wangu huyu.

3 thoughts on “Mzee Nabwa, tunaendelea kukukumbuka”

  1. Ewe mola Msamehe makosa yake na Pepo iwe wakazi yake Aamin. Ni ukweli mtupu ulio uongea huyu mzee sikuwa nikimjua kabla ya gazeti la Dira, gazeti la dira limenifungua macho, nasema kunifungua macho kwani baada ya kuanza kulisoma gazeti hilo nilianza kuwa na mtazamo tofauti na wamwanzo kuhusu siasa na historia ya zanzibar, nilikuwa nimiögoni mwa wale waliobebeshwa historia chafu ya dhiki na dhulma.

  2. Ibn Hamdun aliwahi kusema ” Nikifa msijemkangalia wapi nilipozikwa angalieni yale niliyoyacha kwenu” Naam alhabib mimi ni katika wale nilifunza na Mzee Nabwa kupitia dira mpaka leo humkumbuka mzee wet huyu kwa kuzipitia tena na tena nakala zote za dira kwani nilizinunua kutoka tolea namba 1 mpaka lile la mwisho. hadi leo ukizisoma makala zilizomo katika dira bado unahisi ndio kwanza zimeandikwa leo hii. Mungu amsamehe madhambi yake na ajaalie kabri lake kuwa ni sehemu ya bustani za peponi na sio shimo miongoni mwa mashimo ya motoni. Aamin

  3. Sisi tulikupenda lakini mola alikupenda zaidi, alitoa changamoto kubwa kwa wazanzibari na bado wazalendo wenye roho kamayaho wana iendeleza.
    Mungu akupe malazi mema peponi amin

Leave a Reply to hamza Cancel reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.