UCHAMBUZI

Tatizo si Upemba, ni uelewa

Hii ni makala niliyoiandika wiki iliyopita kujibu makala ya mwandishi Abdul-Ghaffar Idrissa katika gazeti la Nipe Habari la tarehe 20 Novemba 2009 kwa jina la “Je, tatizo ni huu Upemba wetu?”

Itakuwa kosa la kimantiki ikiwa makala ya Abdul-Ghaffar Idrissa ‘Je, tatizo ni huu ‘Upemba’ wetu?’ iliyochapishwa na gazeti hili wiki iliyopita, haikuchangiwa. Na, kwa hakika, si kuchangiwa kwa sababu ya ushindani, bali kwa lengo la kuweka rekodi sawa ili wafuatizi wetu waone pande zote mbili za shilingi.

Nitajitahidi, kadiri niwezevyo, kuongelea kilichozungumzwa na sio kumuongelea mwandishi wa makala hiyo. Hata hivyo, kwa kuwa ninachangia kitu ambacho mimi mwenyewe ninahusiana nacho, ni vyema nikatangaza kabisa maslahi yangu kwacho.

Kwanza, mimi ni Mzanzibari mwenye asili ya Pemba ambaye ninakiamini Chama cha Wananchi (CUF) si kwa sababu ya Upemba wangu (maana wako Wapemba ambao si CUF, kwa mfano, kama unavyoweza kumsoma Abdul-Ghaffar katikati ya mistari yake), bali kwa kuwa nakubaliana na kile kinachosimamiwa na CUF, yaani mabadiliko ya kweli katika nchi yangu ya Zanzibar na Jamhuri nzima ya Muungano.

Pili, na muhimu zaidi, makala hii inakuja katika wakati ambao Wazanzibari wanaongea wakiwa wamekaa juu ya daraja linalowakutanisha na sio tena kupitia nyuma ya kuta zinazowatenganisha. Kwa hivyo, huu ni muda ambao tunatakiwa, kwa maslahi ya nchi yetu tukufu, kuangalia wapi tunakutana na sio wapi tunatengana.

Hata hivyo, kwa maslahi hayo hayo ya umoja wa nchi yetu, lazima tuukane uongo wote unaosemwa dhidi ya nchi hii na watu wake (au kundi fulani la watu hao) kusudi tukubaliane kuwa tunakotokea kulikuwa siko na, hivyo, kwa pamoja tuione hoja na haja ya kwenda palipo ndipo.

Ni hili tu ndilo linalonipa uthubutu wa kuichangia makala husika, nikiamini kwamba si watu wa kundi la kina Abdul-Ghaffar wala wa kundi langu, ambao tumefaidika na hali ilivyokuwa, bali sote tutafaidika ikiwa tutakubali mabadiliko katika nchi yetu tunayoiamini na kuipenda. Baada ya dibaji hiyo, ufuatao ndio mchango wangu.

Kwanza, kusema kwamba serikali za Chama cha Mapinduzi (CCM) ziliruhusu mfumo wa vyama vingi kwa lengo la kufungua milango ya demokrasia nchini, ni kuwa mdhahania zaidi kuliko kuwa mhalisia. Ni rahisi zaidi kutoa mifano hai ya kuthibitisha kuwa serikali hizo hazikuruhusu mfumo wa vyama vingi kwa dhamira njema, bali tu kwa kuelemewa na kuzidiwa na shinikizo la ndani na nje. Kwa hakika hasa, kama nilivyowahi kuandika miaka nane iliyopita kwenye gazeti la Rai, ”Uvyama Vingi wa Tanzania ni Uchama Kimoja Uliohalalishwa”, nikimaanisha kuwa mfumo wetu wa vyama vingi umewekwa tu kuhalalisha chama kimoja kushikilia na kuendelea kubakia madarakani, na si vyenginevyo.

Si Serikali ya Muungano (SMT) wala ya Zanzibar (SMZ), zote zikiwa chini ya CCM, ambazo zimewahi kuwa tayari kwa ajili ya mfumo huu. Hilo limethibitishwa mara kadhaa kwa kauli na vitendo vya wenye mamlaka kwenye serikali hizo. Wacha nidondoe mifano michache kuthibitisha hoja yangu: Mfano mmoja ni wa kuuawa kwa mtu wa mwanzo kabisa kule Shumba Mjini, wilaya ya Micheweni, Pemba, wakati akipachika bendera ya CUF mwaka 1992, na kosa kubwa likiwa ni hilo la kupachika bendera halali katika tawi halali la chama halali cha siasa.

Mfano mwengine ni kauli ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa SMT baina ya 1990 hadi 2005, Fredrick Sumaye, ambaye akiwa Arusha aliwaambia wazi wafanyabiashara kwamba anayetaka mambo yake yamnyookee na asipate matatizo kwenye biashara, basi aiunge mkono CCM. Maana yake ni kuwa mfanyabiashara asiyeiunga mkono CCM ataharibikiwa. Na huo ndio ukweli!

Mfano wa tatu ni kauli za wawakilishi wawili wa CCM kwenye Baraza la Wawakilishi la Zanzibar katika kipindi cha 1995 – 2000, Hafidh Ali Tahir na Asha Bakari Mtama, ambao kwa nyakati tafauti wakiwa ndani ya chombo hicho walisema kwamba Serikali ya Zanzibar ilipatikana kwa Mapinduzi, hivyo haitochukuliwa kwa vikaratasi, wakimaanisha kuwa kura za wananchi katika chaguzi haziwezi kuiondoa CCM madarakani. Na huo ndio umekuwa ukweli tangu 1995, 2000 hadi 2005 ambapo si kura za wananchi zilizoamua nani ashikilie na nani asikamate madaraka ya nchi!

Mfano mwengine ni kauli ya aliyekuwa mwenyekiti wa CCM na Rais wa SMT baina ya 1995 hadi 2005, Benjamin Mkapa, ambaye alisema kwamba angelitumia nguvu zake binafsi na za dola kuhakikisha kuwa CCM inaendelea kubakia madarakani. Na hivyo ndivyo alivyofanya mwaka 2000 na akarudia mwaka 2005 kwa kumwaga vikosi vya majeshi na silaha nzito nzito kwenye visiwa vya Zanzibar kama kwamba nchi iko kwenye vita.

Matokeo ya kauli zote hizo yalionekana katika vitendo vilivyofanywa na vyombo vya dola, vikosi vya SMZ na makundi ya vijana tunaowatambua hapa Zanzibar kama Janjaweed, ambapo kwa pamoja wameua, wamenajisi, wameharibu na kuiba mali na pia kupiga na kutesa wananchi wasio na hatia ndani ya Unguja na Pemba, baina ya mwaka 1992 hadi 2005. Lengo ni kulinda Mapinduzi!

Nihitimishe nukta hii ya kwanza kwa kusema kwamba, serikali ambayo imeleta mfumo wa vyama vingi kwa minajili ya kuwapa watu fursa ya kuchagua wanaowataka kuwaongoza, kamwe isingekuwa ya mbele kuwafanyia watu hao vitimbi vya kuwazuia kuitumia haki hiyo.

Pili, kusema kwamba watu wa kisiwa cha Pemba waliupokea mfumo wa vyama vingi kiupotofu ni zaidi ya kuwadharau. Kwa hakika, kilichotokea hasa ni kuwa watu walipelekewa mfumo wa vyama vingi uliopotoshwa kama inavyoonesha mifano ya hapo juu, na hata hivyo wakajitahidi kuishi nao kama ulivyo. Kwamba Wapemba waliamua kuishi na mfumo huu kwa kuikataa CCM kiujumlajumla, huko hakumaanishi hata kidogo kwamba walipotoshwa na kuzungwa na mmoja wa kiongozi wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kama inavyoelekea kuwa hoja ya Abdul-Ghaffar!

Katika Jamhuri hii ya Muungano wa Tanzania, si Pemba pekee ambako watu wameutumia mfumo huu dhidi ya chama tawala. CCM imewahi kukataliwa kijumlajumla kwenye maeneo ya Uchaggani mwaka 1995. Wachagga hawa, kama ilivyokuwa kwa Wapemba, hawakuwa wameemewa wala kughumiwa. Walikuwa wanaamini kwamba miaka 30 ya kutawaliwa na CCM ilishatosha. Sasa walitaka mabadiliko na kura zao, waliamini, zingeweza kuleta mabadiliko hayo.

Hata hivyo, hakuna siku imewahi kuandikwa kwamba Wachagga walikuwa wamezugwa na Augustine Mrema kama vile inavyoandikwa dhihi ya Wapemba wamezugwa na Maalim Seif. Kwa nini? Ni kwa kuwa Mrema ni Mchagga na Maalim Seif ni Mpemba? Tatizo, kwa hivyo, si Upemba wa Wapemba, bali ni mawazo mgando yasiyoona mbali ya wachambuzi wa mambo wasiojuwa mambo.

Niliwahi kuandika kwenye gazeti la Dira Zanzibar mwaka 2003, kwamba kuwajua Wapemba na wanachokiamini kuna ulazima wa kuvivaa viatu walivyovivaa wao na kujuwa wapi na wapi vinabana. Si suala tu la kuwa na kutokuwa Mpemba, bali ni suala la kuwa tayari kuisafisha akili kusudi iweze kuupokea uhalisia. Nihitimishe nukta hii ya pili kwa kusema kwamba, Wapemba ni walimu na sio wapotofu wa siasa.

Tatu, kusema kwamba mfumo wa vyama vingi umewafanya Wapemba waache shughuli za kujiletea maendeleo kama vile kilimo, kwa kujiona wana jukumu la pekee la kukiingiza chama chao cha CUF madarakani ili kiwabadilishie hali, ni zaidi ya kuwasemea uongo. Labda tushuke chini moja kwa moja kuuangalia uhalisia hata kwa mifano mepesi na rahisi.

Mimi, kwa mfano, kwa sasa si mkaazi wa Pemba, lakini nimekuwa nikitembelea nyumbani mara kwa mara. Ninachokishuhudia huko ni kuwa, hata mama yangu mwenye zaidi ya miaka 60 hivi sasa, bado anashinda shamba kwenye mpunga, muhogo na migomba yake. Na nikiondoka lazima anifungie shehena ya kuchukua. Ninapopanda meli kurudi hapa Unguja ninapoishi, meli huwa zimesheheni kila aina ya mazao ya chakula yanayolimwa Pemba, ambayo ama huwa ni zawadi kama ninayopewa mimi na mama yangu au ni biashara inayokwenda sokoni Mwanakwerekwe.

Kwenye karafuu nako, licha ya SMZ kuendeleza ukiritimba wake wa kuwa mnunuzi pekee wa zao hilo, hivi ninavyoandika makala hii vijana wa Kipemba wamefunga makambi katika milima ya Mkoani, Mtambwe na Pandani wakichuma karafuu. Kwengineko kote katika Jamhuri hii ya Muungano, tunawaona vijana hao hao wa Kipemba kwenye pirika zote za maisha. Abdul-Ghaffar akiwa mmoja wao, utawakuta wamejaa Kariakoo (Dar es Salaam), Darajani (Unguja), Namanga, Tunduma, Arusha, bali hata Ulaya, Marekani na Arabuni. Wako kwenye kazi za kujiajiri, kuajiriwa na wengine wamewaajiri wenzao. Wako kwenye kazi vyuoni wanasoma na wanasomesha, wako viwandani wanaunda na kuzalisha. Wamo mashambani wanalima na kuvuna. Hivi Wapemba wawe wachapakazi vipi tena ili mwandishi aridhike kwamba jamaa zake hawakukaa kuisubiri CUF tu iingie madarakani ili iwajazie mapesa mifukoni mwao?

Nimalizie nukta hii ya tatu kwa kusema kwamba kuwa kwao CUF hakujawahi kuwafanya Wapemba kulegea au kulemaa wakisubiri wajazwe mapesa mifukoni mwao na Maalim Seif. Hali ya maisha ya Pemba ni ngumu, lakini wenyewe wamekuwa wakifanya kila mbinu kujinasua nayo. Ni kweli wana matarajio sana na CUF, kama walivyo Watanzania wengine pia, lakini matarajio hayo ni kupata serikali ambayo inajenga mazingira bora ya wananchi kujiletea maendeleo bila vikwazo vilivyopo sasa.

Nne, si kweli kwamba wabunge – wawe wa chama tawala au wa upinzani – wana jukumu na au uwezo la kuleta maendeleo katika maeneo wanayotokea. Kwa kumnukuu Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho Bungeni, ”wabunge hawawezi kutoa breakfast, dinner na lunch kwa wapiga kura wao. Wanachoweza kufanya ni kuchochea tu huduma za maendeleo zielekezwe kwenye majimbo yao.”

Labda mwandishi akipata fursa atueleze kile ambacho kimeweza kufanywa na wabunge wa Upinzani katika maeneo ambayo Upinzani unaongoza upande wa pili wa Muungano, kama vile Karatu na Kigoma Kaskazini. Atusaidie pia namna SMT inavyowachukulia wapinzani akilingalisha na SMZ. Mwisho atubainishie yapi yaliyofanywa na wabunge wa CCM hapa Unguja. Hapo tutaweza kuona namna ambavyo wabunge wa Upinzani kutoka Pemba walivyoshindwa kabisa kuisaidia Pemba kimaendeleo. Katika taaluma yetu ya habari huwa tunasema kwamba ”asiyetafiti hana haki ya kuandika”. Kwa hili, nadhani mwandishi amekiuka mipaka yake.

Nimalizie nukta hii ya nne kwa kusema kwamba, ikiwa Pemba imeshindwa kupata maendeleo yoyote yale kwa miaka yote hii 17 ya vyama vingi, si kwa kuwa Wapemba wamewapeleka Bungeni wapinzani, bali ni kwa kuwa sera za maendeleo zinazosimamiwa na serikali za CCM hazijaipa kipaumbele Pemba.

Kwa hakika, kuna mifano kadhaa ambapo wabunge kutoka Pemba wamejitutumua kuikaba SMT ipeleke maendeleo Pemba, lakini tukubaliane kwamba kuna mambo mawili yanayotanza hapa: Kwanza, muundo wetu wa Muungano unayaweka mambo ya ndani ya Zanzibar kama elimu, afya, barabara, maji na umeme kuwa yasimamiwe na SMZ, na hivyo mbunge si eneo lake. Pili, kuna makosa makubwa ya kisiasa ambayo Wazanzibari tuliyafanya. Upande mmoja SMZ ilijisahau kwamba ni serikali ya wote. Ikajikita makusudi kwenye misingi ya kibaguzi dhidi ya wananchi wake. Upande mwengine wapinzani hawakutaka kuipa SMZ heshima yake ya kuwa serikali. Wakajizoesha kuishi bila ya kuutambua wala kuuhisi uwepo wa serikali.

Lakini nimalizie kama nilivyoanza kwa kusema kwamba, huu ni wakati ambao Wazanzibari tumeamua kuzika tafauti zetu. Tumeamua kubadilika na kuibadilisha nchi yetu. Tumeamua kusema basi tena kwa yale yote ambayo huko nyuma yalituumiza na kuumiza mustakabali wa nchi hii na vizazi vyetu.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, ameamua kunyoosha mkono wa maridhiano na utangamano wa kitaifa kwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Amani Karume. Maalim Seif hakusukumwa na chochote chengine isipokuwa kwa maslahi ya Zanzibar. Dkt. Karume naye ameupokea mkono huo. Imani yetu ni kwamba, naye Rais Karume ameongozwa na maslahi ya Zanzibar pia. Kwa hivyo, tupeane nafasi ya kuthibitisha mapenzi yetu kwa Zanzibar. Na kwa hilo, hatuna la kupoteza hata moja, isipokuwa tuna mengi ya kupata ndani ya Zanzibar Mpya! And Yes, We Can!

2 thoughts on “Tatizo si Upemba, ni uelewa”

  1. I’ve been instructed that the porch will no extended host meals vans and are planning a a lot more company eatery upon the premises. Incorporates everybody read this

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.