UCHAMBUZI

Kikwete na Mapinduzi yake, Wazanzibari na ‘mchezo’ wao

Rais Jakaya Kikwete alikuja mjini Zanzibar tarehe 25 Januari 2009 na akanukuliwa akiapa kwamba hatamvumilia yeyote anayeyachezea Mapinduzi. Kwa hakika hakikuwa kiapo tu, bali pia kilikuwa ni kitisho: “Kama mtu hajipendi, achezee Mapinduzi aone.” Ilikuwa kauli nzito, lakini si ngeni kutoka kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), hasa wanaotokea Tanganyika, na hilo ndilo shughuliko kuu la makala hii. Ninahoji kwa nini viongozi wa Tanganyika wawe wakali ‘kuyalinda’ Mapinduzi ya Zanzibar!

Mimi ni kijana wa Kizanzibari na Mapinduzi yanayoapiwa kulindwa hapa ni yale ya tarehe 12 Januari 1964 ambayo yaliiondosha madarakani serikali ya mseto wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP). Zaidi ya asilimia 60 ya sisi Wazanzibari wa leo hatukuyaona Mapinduzi hayo. Sasa ninajiuliza, ikiwa Mapinduzi yenyewe ni hayo, kwa nini yamfanye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ale kiapo hicho cha ‘kuyalinda’ dhidi ya ‘atakayeyachezea’? Au kuna Mapinduzi mengine? Au kuna maana zaidi ya Mapinduzi ambayo haijasemwa hapa?

Ninapotafuta majibu ya masuali kama hayo, ndipo ninapojikuta kulazimika kuziangalia nadharia zilizopo kuhusu Mapinduzi yenyewe. Nagundua kuwa kuna haja ya kwanza kujibu suali: Nini hasa kilitokezea tarehe 11 Januari 1964?

Nadharia zipo tatu: mbili zimezoeleka, moja ngeni. Ya kwanza inasema kuwa siku hiyo kundi la vijana wa tabaka la chini lilipandwa na hasira kutokana na kuendelea kwa hali ngumu ya maisha, huku wakiwa hawaoni dalili yoyote ya mabadiliko yoyote ya kiuchumi na kisiasa yanayoweza kuwanufaisha. Wakaamua kuelekeza hasira zao kwa tabaka la juu na tabaka la kati, waliyoamini kuwa yanafaidi uchumi wa Zanzibar peke yao. Na kwa kuwa Mji Mkongwe ulikuwa kitovu cha matabaka hayo, vijana wa tabaka la chini wakaamua kuuteketeza kwa moto.

Kwa bahati kundi jengine la vijana wa chama cha Umma, kilichokuwa kikiongozwa na Abdirahman Babu, likaingilia kati mpango huo na ‘kuupa sura ya kimapinduzi’ badala ya uasi tu wa kijamii. Matokeo yake ndiyo kupinduliwa kwa serikali ya ZNP/ZPPP na kuingia madarakani kwa serikali ya Afro Shirazi Party/Umma Party (ASP/UP).

Kwa hivyo, Mapinduzi lilikuwa tukio la kushtukizia tu, ambalo lilikuwa halikupangwa kitaalamu na ambalo, kama si uingiliaji kati wa vijana hao wa Umma, ambao wengi wao walikuwa ni wa tabaka la kati wakiwa na elimu nzuri na mafunzo ya kijeshi kutoka nchi za iliyokuwa Kambi ya Mashariki, basi pengine ungelikuwa uasi mdogo ambao ungelidhibitiwa na askari wachache wa serikali.

Hii ndiyo nadharia inayozungumzwa sana na kundi la wachambuzi wa Ki-marx na Ki-Lenin ambao kwao wao mabadiliko yoyote katika jamii ni matokeo ya msuguano wa kitabaka (class struggle). Hapana shaka, Babu na wafuasi wake (kwa sababu zao wenyewe) waliipigia sana chapuo nadharia hii hata imekuwa ni sehemu ya kumbukumbu za kimaandishi (literature) zilizopo kuhusu tukio hilo lililobadilisha mstatili wa mambo Zanzibar.

Nadharia ya pili inasema kwamba, kilichotokezea siku hiyo kilikuwa ni matokeo ya maandalizi ya ASP ya muda mrefu. Waafrika wenye uchungu na waliovunjwa moyo na matokeo ya kura katika chaguzi zote – kuanzia ule wa 1961 hadi wa 1963 – sasa waliamua kujitolea muhanga, wakasuka mipango ikasukika, na siku hiyo wakachukua mapanga na mashoka na kuivamia serikali kibaraka iliyokuwa chini ya usultani wa Kiarabu wa Jamshid bin Abdullah Busaidy na kuipindua.

Kwa mtazamo huu, yale yalikuwa Mapinduzi yaliyofanywa na Waafrika walio wengi dhidi ya utawala wa Waarabu wachache. Kiongozi wa Mapinduzi hayo alikuwa ni Abeid Amani Karume na kikundi cha watu 14 (Committee of Fourteen) ndicho kilichokuwa dhamana wa tukio zima.

Nadharia hii inayaangalia Mapinduzi kama tukio la kikabila na kama matokeo ya kawaida pale wachache wanapowatawala wengi bila ya ridhaa yao. Waafrika wengi dhidi ya Waarabu wachache. Muasisi wa nadharia hii, kwa hakika hasa, ni Julius Nyerere na propaganda yake ilienezwa vyema kupitia Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) kwa kushirikiana vyema na aliyekuwa mkoloni, Dola ya Uingereza. Hii ndiyo nadharia inayotumiwa na wachambuzi wengi wa Tanganyika hadi leo.

Nadharia ya tatu, na ambayo inaweza kuwa ngeni, inasema kwamba kilichotokezea siku hiyo ni majeshi ya dola ya kigeni, na hapa inakusudiwa Tanganyika, kuivamia nchi ya Zanzibar, kuiangusha serikali katika usiku wa tarehe 11 Januari, na kisha majeshi hayo yakarudi Tanganyika alfajiri yakiwacha nyuma waasi waliokuwa wametayarishwa kitambo kuendelea na mauaji na kukamilisha zoezi la kuunda serikali nyingine.

Nadharia hii inayaangalia Mapinduzi yale kama mavamizi ya dola moja dhidi ya nyengine katika mifano inayofanana na kile Indonesia ilichokifanya wakati Ureno alipoondoka Timori ya Mashariki na au Morocco ilichokifanya baada ya Hispania kuondoka Sahara. Nadharia hii inakwenda mbele kusema kwamba ni baada ya kujaribu Zanzibar na kufanikiwa, ndipo Nyerere ‘akatamukiwa’ na akawa anapeleka majeshi yake katika nchi nyengine za jirani kusaidia kile kilichoitwa wakati huo “Mstari wa Mbele Katika Ukombozi wa Afrika.”

Kuna simulizi zinazosema kuwa wakati Mfalme Jamshid alipowasili Portsmouth, Uingereza, kwa hifadhi ya kisiasa, alisema kwamba yeye hakupinduliwa na Wazanzibari, bali majeshi ya kigeni (Tanganyika) ndiyo yaliyoivamia nchi yake (Zanzibar). Inasemekana Nyerere na Baraza la Mapinduzi waliipata kauli hiyo na iliwatetemesha, kwani ilikuwa ikijenga hoja katika sheria za kimataifa dhidi ya ‘utakatifu’ wa Nyerere na Mapinduzi ‘yake.’ Hima ukapitishwa mkakati wa ‘kuisahaulisha’ kabisa kauli hii; na kama ni kweli, basi mkakati huo ulifanikiwa maana hadi unasoma makala hii huenda ikawa ni mara yako ya mwanzo kusoma au kusikia haya.

Baada ya kuziangalia nadharia hizi tatu, sasa nikaona kuwa ni rahisi kujibu maswali ambayo nimeyauliza hapo juu. Kwa mfano, unapoipiganisha nadharia ya tatu kwa ya pili chini ya kivuli cha kauli kama hizi za akina Kikwete (za kulinda Mapinduzi dhidi ya anayeyachezea), unapata mwangaza wa jawabu nyengine nyingi hata kwa maswali ambayo hukuwahi kujiuliza mwanzoni. Nitafafanua.

Nadharia ya tatu inasema hivi: tarehe 11 Januari 1964, Amiri Jeshi Mkuu wa Tanganyika anaamuru kikosi maalum cha jeshi lake kwenda Zanzibar usiku na kuipindua serikali changa ya mwezi mmoja. Baada ya wiki moja, nadharia ya pili inasema, Amiri Jeshi huyu ambaye pia ndiye Rais wa Tanganyika, anazungumza na maafisa wa kibalozi na baadhi ya waandishi na kuyaelezea Mapinduzi ya Zanzibar kama tukio lililokuwa la lazima kuwapa nguvu Waafrika waliokuwa wengi dhidi ya utawala wa Waarabu wachache. Kwa nini Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanganyika anakuja na tafsiri hii? Anahusika?

Ndiyo, anahusika. Mimi nakubaliana na nadharia ya tatu, yaani kilichofanyika tarehe 11 Januari 1964, ulikuwa ni uvamizi wa dola moja dhidi ya nyengine, kwa maana ya kwamba serikali ya Tanganyika ilituma majeshi yake kuivamia Zanzibar na kuiondosha serikali madarakani, kwa mfano ule ule iliokuja kuufanya miaka kumi baadaye kwa kutuma majeshi yake kwenda kumuondoa rais wa Uganda, japo kwa sababu na malengo tafauti.

Kwa hivyo, leo hii unapomsikia kiongozi wa Muungano (ambaye kwa bahati ndiye pia kiongozi mkuu wa Tanganyika na Amiri Jeshi Mkuu) anaapa kuyalinda Mapinduzi, ana sababu za kufanya hivyo. Anayalinda kwa kuwa Mapinduzi haya ni yake katika kiwango na namna ile ile yalivyokuwa pale mwaka 1964. Yalifanywa na nchi yake dhidi ya nchi nyengine na ana kila wajibu wa kuhakikisha kuwa yanadumu.

Lakini kufika hapa nikajiuliza, hivi kwa nini Tanganyika iliipindua Zanzibar? Nikapata nadharia nyengine tatu. Moja ni woga wa Tanganyika kwamba, kuwa na jirani ambaye alikuwa anapiga hatua za kimaendeleo kwa kasi (kwa kiwango cha wakati ule) kungelikuwa na athari mbaya za kisiasa kwake, kwani wananchi wa Tanganyika wangekuja kuinuka na kudai maendeleo kama waliyokuwa wanayapata Wazanzibari kutoka kwa serikali yao. Hapa inakumbushwa kwamba hadi yanafanyika Mapinduzi, Zanzibar ilikuwa inajitegemea kiuchumi na inatoa misaada kwa nchi nyengine, ina wataalamu wa kutosha wa kizalendo na ina akiba ya kutosha kwa uwekezaji wa ndani katika hazina yake.

Nadharia ya pili ni kwamba, Zanzibar ilikuwa dhaifu kijeshi na kiulinzi na, kwa hivyo, ingeliweza kirahisi kutumiliwa na maadui wa Tanganyika kuishambulia hasa katika msuguano wa Vita Baridi. Inakumbushwa hapa kuwa Uingereza, pamoja na kuwa ilikuwa imekubali kutoa ulinzi kwa nchi nyengine za Afrika Mashariki zilizokuwa makoloni yake (Tanganyika, Uganda, Kenya na Yemen), ilikuwa imekataa kufanya hivyo kwa Zanzibar, na hivyo kwa makusudi kabisa kuiwachia iwe rahisi kuvamiwa, kushambuliwa na kudhuriwa.

Na nadharia ya tatu, ambayo ndiyo ninayokubaliana nayo, ni kuwa Nyerere alikuwa na ndoto za kujenga himaya kubwa ya utawala. Kwa hakika, hata jina la Tanzania, ambalo ulikuja kupewa mchanganyiko wa nchi hizi mbili (Tanganyika na Zanzibar), halikuwa limetokana na Tanganyika na Zanzibar kama inavyosemwa na baadhi ya watu. Jina hili linatokana na Tanganyika na Azania, na Azania ni upwa wote wa Afrika Mashariki, vikiwemo visiwa vya Komoro, Ushelisheli na Bukini.

Kwa lugha nyepesi ni kwamba Tanganyika iliivamia Zanzibar na kuikalia na msamiati wa tendo hilo ukaitwa ‘Mapinduzi.’ Sasa kuchezea Mapinduzi, kwa hivyo, ni kuchezea azma, dhamira na mbinu za Tanganyika dhidi ya Zanzibar. Vivyo, kulinda Mapinduzi ni kudumisha azma, dhamira na kuendeleza mbinu za Tanganyika dhidi ya Zanzibar.

Kadiri nilivyokuwa ninapata majibu ya maswali yangu ya mwanzoni, ndivyo nilivyopata hamu ya kujiuliza maswali mengine ya ziada. Kwa mfano, baada ya kauli ya Kikwete na kwa kuhusisha na kauli kama hiyo ya mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, pale mwaka 2005 kule Micheweni aliposema kwamba ameapa kuyalinda Mapinduzi, na matendo yake ya kumwaga vikosi vya kivita kwenye uchaguzi wa 2000, mauaji ya Januari 2001, na luteka la kijeshi la 2005 nchini Zanzibar, ni nani ‘mchezeaji wa Mapinduzi’ hapa Zanzibar leo hii? Nirudi kwenye mgogoro wa kisiasa wa 1995, 2000 na 2005? Hapana, huko ni mbali sana.

Afanaalek! Si kuanzia katikati ya mwaka jana, Wazanzibari wamekuwa wakijikusanya pamoja kutetea mamlaka zaidi kwa nchi yao ndani ya Muungano? Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), pamoja na udhaifu mwingi ilionao, kwa mfano, ilimwambia Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba Zanzibar ni nchi, yeye aliposema si nchi. Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna alifikia umbali wa kujitolea muhanga kwa lolote litakalokuwa, lakini alinde dhamira ya Zanzibar kuwa nchi. Waziri mwengine, Hamza Juma, amefikia umbali wa kusema kuwa Zanzibar itajiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam (OIC) kivyake ikiwa Serikali ya Muungano inakokota mguu. Waziri anayehusika na nishati, Mansoor Yussuf Himidi, ameshasema si mara moja wala mbili kuwa mafuta ni mali ya Wazanzibari na hilo ni vyema likaeleweka na kuheshimika hivyo tu.

Huo ni upande mmoja: wa CCM Zanzibar na SMZ tu. Kuna upande wa pili ambao ndio hasa injini ya kusimamia hadhi na heshima ya Zanzibar kisiasa – Chama cha Wananchi (CUF). Si Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, amezifufua na kuzipa mwelekeo mpya jitihada za Wazanzibari kuitetea heshima yao ndani ya Muungano? Si viongozi wengine, kama Juma Duni, wameutangazia ulimwengu mzima kuwa Zanzibar haijawa huru chini ya himaya ya Tanganyika? Si Ismail Jussa amefikia umbali wa kuwaahidi viongozi wa SMZ uungwaji mkono wa asilimia mia moja katika kuitetea nchi yao, hata ikibidi kuwapa ngome ya binaadamu (human shield) kama wataletewa vifaru na mizinga vya Serikali ya Muungano? Si Soud Yussuf Mgeni ametamka wazi kwamba sasa kugawiwa kwa misingi ya vyama kumefikia mwisho? Kwamba Zanzibar kwanza, u-CCM na u-CUF baadaye?

Ikiwa hivi ndivyo, basi Wazanzibari hawa ndio wanaoyachezea ‘Mapinduzingwa Matukufu.’ Na hawa – wawe CCM wawe CUF – ndio Amiri Jeshi Mkuu aliowalilia kiapo, maana wanachofanya ni kupingana na azma, dhamira na mkakati wa Tanganyika kwa Zanzibar.

Huo ndio ukweli wenyewe na khabari ndiyo hiyo. Ni bahati mbaya sana, ikiwa wana-CCM wa Zanzibar waliokuwepo Kibandamaiti siku ile ya tarehe 25 Januari, 2009 hawakumuelewa vyema mwenyekiti wa chama chao. Wao wakadhani kuwa kile kilikuwa ni kitisho dhidi ya Maalim Seif, Duni, Jussa, Bimani, Aboubakar Khamis na Dkt. Juma Muchi tu. Ukweli ni kuwa kile ni kitisho zaidi kwa akina Mansoor, Shamuhuna, Hamza na hata Karume na Shamsi wenyewe kuliko kilivyo kwa viongozi wa CUF.

Mwisho, baada ya maswali na majibu yote hayo, nikajiuliza la mwisho: hivi, ikiwa la ‘kuyachezea Mapinduzi’ ndilo hilo nililoliona, kuna ladha gani zaidi kwa Mzanzibari zaidi ya mchezo huo? Mchezo uchezwao na watu kama Maalim Seif na Shamhuna, Jussa na Hamza, Aboubakar na Mansoor?

Wallahi, fakhari iliyoje kuwa sehemu ya mchezo huo! Mchezo wa kikubwa, mchezo wa kizalendo. Mchezo ambao hauna kupoteza. Maana ikiwa utamalizika kwa Kikwete kufanikiwa ‘kuwashughulikia’ wanaoyachezea Mapinduzi, wachezaji hao watatoka uwanjani mashujaa mbele ya jamii ya Wazanzibari kama alivyokuwa Hayati Abeid Karume. Kwake tulisema: “Kilichozikwa ni kiwiwili chako, bali Roho na Mawazo yako bado ya hai.” Na ukimalizika kwa wachezaji kufanikiwa kuondosha azma, dhamira na mkakati wa Tanganyika kwa Zanzibar, watavikwa nishani za dhahabu, za lulu na yakuti. Majina yao yataandikwa kwa wino wa ajabu kwenye vitabu vya historia ya nchi yao. Kuna mchezo bora zaidi ya huo?

Jibu langu likawa “La, Hakuna!” Na kwa sababu hiyo, nami najiunga nao. Najiunga nao nikizingatia msemo: “Ama unganikeni muwe wamoja, au gawanyikeni muchinjwe mmoja mmoja.” Ni juu ya Amiri Jeshi Mkuu Kikwete kuamua kuanza ‘kunishughulikia’ mcheza mie niyachezeaye Mapinduzi yake. Ila hata akija na vifaru na mizinga, atanikuta ndani ya ardhi ya nchi yangu ninamuimbia Mama yetu Mpendwa, Zanzibar:

Kwa jinalo wewe, neno natamka, na kulikariri
Hitaka ujuwe, ndiwe mtukuka, ndiwe wangu huri
Sina mwenginewe, wala hatazuka, wa kumkubali
Watwani ni wewe, kila kitu wewe, Mama Zinjibari!

Nanisemwe kwawe, sitaadhirika, wala sitajali
Hata nichukiwe, sitababaika, moyo haudhili
Nitakuwa nawe, sitakugeuka, hilo ni muhali
Mimi ni kwa wewe, kwa myaka na kaka, Mama Zinjibari!

Nitukanwe kwawe, sitakukanuka, wala sitabali
Kwa vyovyote uwe, sitakugeuka, nitakukubali
Nimezawa nawe, kwako ‘meleleka, vipi nende mbali?
Mimi bila wewe, sina wa kushika, Mama Zinjibari!

Nipigwe kwa wewe, damu ‘tamwagika, kisha ‘tasubiri
Jela nifungiwe, niwe nadhikika, sitakughairi
Mateso nipewe, ita’wa baraka, na ladha nzuri
Kwa jinalo wewe, mimi nanonoka, Mama Zinjibari!

Wacha nife kwa’we, sitanung’unika, ‘tafurahi bali
Lolote naliwe, ewe mtajika, kwa wewe sijali
Nanilaumiwe, nitwikwe mashaka, na masilisili
Watwani ni wewe, kila kitu wewe, Mama Zinjibari!

Februari 2, 2009

4 thoughts on “Kikwete na Mapinduzi yake, Wazanzibari na ‘mchezo’ wao”

  1. kwa makala hii ndugu yangu Ghassany ninakuvulia kofia!! Keep it up!!
    Ingekuwa Zanzibar kuna waandishi watano tu kama wewe basi Tanganyika wangekibia na huku wauchi bila ya kuona aibu !!

  2. sikubahatika kuisoma mapema nasikitika ila
    makala ni tamu, na wake utamu, itabakia,
    na alie a’limu, hatajidhulumu, kinoendelea,
    sie mahamumu, kwa hizi hatamu, walizotutia,

    1. Tumshukuru Mungu kuwepo watu kama hawa wanaweza kutukumbusha mambo kamahaya muhimu,wengitunajifanya hatuoni wala hatusikii lakini likitota tutazamasote (USIUZE NCHI KWATONGE WAJUKUZAKO WATARISI NINI ?)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.