UCHAMBUZI

Bendera kama ishara ya unchi wa Zanzibar

Na Mohammed Khelef Ghassani

12 Novemba, 2008

Rais wa Zanzibar, Amani Karume, akizindua bendera ya Zanzibar, mwaka 2005
Rais wa Zanzibar, Amani Karume, akizindua bendera ya Zanzibar, mwaka 2005

Peter Kisumo, mbunge kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema katika kikao cha Bunge la Bajeti la mwaka huu, 2008/2009, kwamba Zanzibar kuwa na bendera haimaanishi kuwa Zanzibar ni nchi, kwani bendera hiyo ni sawa na ile ya klabu ya mpira ya Yanga. Bila ya shaka, kauli hii ilitukera Wazanzibari na kuamini kwamba tumedhalilishwa. Licha ya kusema maneno hayo katika Bunge na sisi kudai kwamba aombe radhi na achukuliwe hatua kwa kuikosea adabu Zanzibar, hakuna chochote kilichofanywa hadi sasa, na hakuna dalili kama kitu hicho kitafanywa.

Sisi Wazanzibari hatuoni ikiwa kuna la kubishania ikiwa Zanzibar ni nchi ama la, maana ni kinyume cha mantiki kuuliza ikiwa jua linatoka mashariki ama la. Nakusudia kuwa ukweli haubishaniwi, yanayobishaniwa ni maoni ya mtu binafsi. Kwetu si suala la maoni ya mtu binafsi kwamba Zanzibar ni nchi, bali ni ukweli ulio wazi na usiopingika.

Makala hii, hata hivyo, haijikiti sana huko, bali inakusudia kuonesha historia ya bendera nchini Zanzibar kwa miaka 44 iliyopita na ikiwa historia hiyo inamaanisha lolote kwa hadhi na heshima ya Zanzibar.

Bendera ya Zanzibar baada ya Uhuru wa Disemba 1963 na kabla ya Mapinduzi ya Januari 1964
Bendera ya Zanzibar baada ya Uhuru wa Disemba 1963 na kabla ya Mapinduzi ya Januari 1964

Tarehe 10 Disemba, 1963 Zanzibar ilipata uhuru wake kutoka ukoloni wa miaka 73 wa Uingereza. Kuashiria uhuru kamili, Zanzibar ilipandisha bendera yenye mji mwekundu ikiwa na alama ya karafuu mbili katikati. Karafuu limekuwa zao la kibiashara kwa visiwa hivi kwa takriban karne mbili sasa.

Bendera ya kwanza ya Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 1964
Bendera ya kwanza ya Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 1964

Bendera hii ya uhuru ilipepea kwa muda usiozidi mwezi mmoja, kwani Januari 12, 1964 palifanyika mapinduzi yaliyoitangaza Zanzibar kuwa Jamhuri na kupandishwa kwa bendera mpya. Hii ilikuwa na rangi tatu: nyeusi juu, katikati manjano na chini buluu, ambayo nayo ikaja ikachukuliwa nafasi yake na bendera nyengine yenye rangi tatu pia, lakini zikiwa kwa mtiririko huu: buluu juu, nyeusi katikati na kijani chini. Kuondoka kwa bendera moja kwenda nyengine baina ya mbili hizi hakukuchukua muda mrefu. Labda ni chini ya mwezi mmoja.

Bendera ya pili ya Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 1964
Bendera ya pili ya Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 1964

Mapinduzi ya Januari 1964 nayo yakafuatiwa na Muungano wa Aprili 1964 na Jamhuri ya Tanganyika. Kwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar, Julius Nyerere, alama zote zilizokuwa zikitunika kuitambulisha Jamhuri ya Tanganyika sasa zikaidhinishwa kuitambulisha Jamhuri hiyo mpya iliyotokana na Muungano huu. Kwa hivyo, kuanzia hapo, Zanzibar ikawa nayo inapepea bendera ile ile inayopeperushwa Tanganyika.

Bendera hii inaunganisha karibuni rangi zote ambazo zilitumiwa na bendera mbili za Zanzibar baada ya Mapinduzi (ingawa hiyo haisemi kwamba ilifanyika kwa makusudi ya kuonesha uwepo wa Zanzibar ndani ya Muungano), isipokuwa zimepangwa kwa staili tafauti. Katika muundo wa pembe tatu, juu kuna rangi ya kijani, katikati kuna utepe mweusi unaozungukwa na tepe za kijani na chini kuna rangi buluu. Katika mtandao wa www.swimport.com/flags/unmemberflags.html, ambao una orodha ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na bendera zao, bendera hii ipo kwenye kiungo cha Tanzania – Zanzibar. Hii inaweza, pengine, kuhalalisha ile hoja ya Wazanzibari kwamba Zanzibar bado ni mwanachama wa Umoja huo, kwani haijawahi kujiondoa wala kupeleka ombi la kubadilisha uanachama wake. Hili, hata hivyo, ni suala la mjadala maana ni maoni tu.

Baada ya Muungano wa Aprili 1964, Zanzibar ilianza kutumia bendera hii ambayo pia ni ya Jamhuri ya Muungano hadi Agosti 2005
Baada ya Muungano wa Aprili 1964, Zanzibar ilianza kutumia bendera hii ambayo pia ni ya Jamhuri ya Muungano hadi Agosti 2005

Zanzibar imeendelea kutumia bendera ya Jamhuri ya Muungano kama alama yake hadi mwaka 2005, ambapo Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha azimio la kuanzishwa kwa bendera ya Zanzibar, baada ya shinikizo la siku nyingi kutoka kwa Wazanzibari wenyewe. Kwa hivyo kuanzia mwaka huo hadi sasa, bendera ya Zanzibar imekuwa ni tafauti na ile ya Muungano, japo kwa umbile zinafanana sana. Bendera ya sasa ya Zanzibar ina rangi tatu: juu buluu, katikati nyeusi na chini kijani na ndani yake – upande wa kushoto juu – kuna bendera ndogo ya Jamhuri ya Muungano.

Bendera ya Zanzibar kuanzia Septemba 1, 2005 hadi sasa
Bendera ya Zanzibar kuanzia Septemba 1, 2005 hadi sasa

Pamoja na kuwa na bendera hii, Zanzibar pia ina bendera ya Rais, ambayo ina mji wa kijani, muhuri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar uliozungushwa kwenye duara lenye maandishi “Rais wa Zanzibar” na juu ya muhuri pameweka herufi “R” inayosimama kwa neno Rais.

Kama nilivyosema, Zanzibar pia ina muhuri wake ambao una michoro ya visiwa vya Unguja na Pemba, bahari, miti ya mnazi na mkarafuu na umeegemea kwenye panga na shoka. Huu ni tafauti na muhuri wa Adam na Hawa, ambao mwanzoni ulikuwa ukitumika na Serikali ya Tanganyika kabla ya kuhamishiwa kwenye Serikali ya Muungano.

Bendera ya Rais wa Zanzibar
Bendera ya Rais wa Zanzibar

Bila ya kutaja, bila ya shaka, kwamba wimbo wa Taifa wa Zanzibar ni tafauti sana na ule wimbo mrefu wa Taifa wa Jamhuri ya Muungano, ambao nao kama ilivyokuwa kwa alama nyengine za Muungano, ulikuwa wimbo wa Jamhuri ya Tanganyika. Wimbo wa Taifa wa Zanzibar ni mfupi:

“Mungu amtubarikia

Unguja na Pemba yote

Sote tunashangiria

Jamhuri kutuletea.”

Muhuri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Muhuri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

“Jamhuri” ndilo neno lililomo kwenye Wimbo wa Taifa wa Zanzibar. Tunahitajika kusema zaidi ya hapa?

Kwa maelezo ya ziada kuhusu bendera Zanzibar tembelea www.allstates-flag.com/fotw/flags/tz-zan.html

1 thought on “Bendera kama ishara ya unchi wa Zanzibar”

  1. kikawaida nchi hutambiliwa kama nchi inapokuwa na mambo makuu 3.eneola ardhi ambalo zanzibar ni visiwa,raiya ambapo sisi wenyewe tupo wazanzibari pia kuwa na serikali ambapo tunayo sasa hii inakuwaje leo kuna mjadala kuwa zanzibar ni nchi au la ?je hayo mambo tunayo au hatunayo ?naserikali hutambuliwa ikiwa na mambo makuu 3,bunge au baraza la kutunga sheria,mahakama na baraza la uongozi au la mawaziri,na hayo yote zanzibar yapo je tutakataa kuwa si nchi ?nchi hutofautiana kwani kuna kubwa na ndogo au kuna nyengine kutokana na udogo wao hutoa baadhi ya madaraka kwa nchi kubwa ili wasaidiane mfano MONAKO ambayo kuna mfalme na imetoa baadhi ya mambo kwa nchi ya ufaransa ila hatuwezi kusema kuwa monako ni ufaransa pia kuna nchi inayoiwa ANDORRA ambayo baadhi ya madaraka yanashikwa kwa pamoja baina ya hispania na ufaransa au SAN MARINO ambayo baadhi ya mambo hufanyiwa na italia au LIECHSTENSTEIN ambayo baadhi ya mabo yanashikwa na uswisi ila kuna mengine hujiamulia wenyewe kwani hawa pesa yao inaitwa frak ambayo tofauti na frank ya uswisi ilhali ANDORRA,MONAKO na SAN MARINO hutumia euro ingawa sio wanachama wa jumuiya ya ulaya kabla ya euro kila 1 ilikuwa na pesa yake sio za nchi walozikabidhi madaraka.hii ni kuonesha kuwa nchi inaweza kuikabidhi baadhi ya madaraka nchi nyengine kwa makubaliano tu na kama wenyewe hawataki basi kwenda kivyao na hamna lolote litakalotokea kwani zama za kutishana zimekwisha.mfano mwengine ni aple kampuni ya simu ya sudani ya kusini GEMTEL kutumia namba ya muito wa kimataifa ya uganda +256 na hii hatuwezi kusema kuwa kampuni hii ni ya uganda bali ni makubaliano yao na serikali ya uganda.tutizameni mambo yalivyo na sio kutokana nautashi wa kisiasa

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.