UCHAMBUZI

Wazanzibari hatulitambui tamko la SMZ

Kuelekea uvamizi wa Uingereza na Marekani dhidi ya Iraq mwaka 2003, waandamanaji waliokuwa wakipinga uvamizi huo jijini London walibeba bango linalosomeka: “No, Blair. Not in our name!” Waandamaji hawa walikuwa wakimkana aliyekuwa Waziri Mkuu wao, Tony Blair, aliyekuwa ameshirikiana na Rais George Bush wa Marekani kushinikiza kwamba uvamizi huo ungelikuwa ni kwa maslahi ya kiulinzi na kiusalama si kwa mataifa yao tu, bali pia kwa dunia. Walikuwa wakipeleka ujumbe wao kwamba wao kama Waingereza hawampi idhini ya kufanya uvamizi huo.

Hata hivyo, Blair hakusikia. Akaiingiza Uingereza vitani, vita ambavyo hadi sasa vinaendelea vikiwa na hasara kubwa ya kijamii. kisiasa na kiuchumi kwa Iraq, Uingereza, Marekani na kwa ulimwengu mzima. Na yeye mwenyewe, Blair, sasa si tena Waziri Mkuu maana alilazimika kuondoka madarakani kabla ya wakati wake kumalizika kwa kile kinachoaminika kuwa ni dhima yake kwenye uvamizi huo. Blair aliiaibisha hishima ya Uingereza!

Mimi leo naandika kama muandamanaji katikati ya kundi la maelfu ya Wazanzibari wenzangu nikiwa nimeshikilia bango linalosomeka: “No, Nahodha, not in our name!” Ndiyo, Wazanzibari tunaandamana; na lengo la maandamano haya ya amani ni kulikana tamko la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) lililotolewa na Waziri Kiongozi wake, Shamsi Vuai Nahodha, kwenye Baraza la Wawakilishi Ijumaa Oktoba 24, 2008. Tunalikana kwa kuwa haliwakilishi mtazamo wetu, Wazanzibari, halina maslahi nasi na, kwa hivyo, tumeamua kutokulitambua. Natazamia kuwa, kama walivyofanya Waingereza, na sisi tutaiadhibu serikali hii kwa kutuendea kinyume!

Katika tamko lake, SMZ kupitia Waziri Kiongozi Nahodha, inasema kwamba inakubaliana moja kwa moja na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Bungeni tarehe 21 Agosti 2008 iliyoitaja Zanzibar kama nchi ndani ya mipaka ya Tanzania, lakini siyo nchi nje ya mipaka hiyo. Tamko linasema pia kwamba, kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, Zanzibar na Tanganyika (tamko linaitaja kama Tanzania Bara, ingawa mwaka huo hakukuwa na nchi yenye jina hilo) zilichanganya utaifa wake katika Muungano wa 1964 na hivyo katika uso wa kimataifa, kuna utambulisho wa Tanzania tu na sio wa Zanzibar wala wa Tanganyika. Tamko linasema, kwa hivyo, kauli hii ya Rais Kikwete inajitosheleza na hakuna haja ya kuongeza la ziada. Hilo ndilo tamko la SMZ!

Lakini, kama nishavyotanguliza kusema, hilo si tamko letu, Wazanzibari. Sisi, kwa wingi na umoja wetu, tunasema kwamba, pamoja na mapungufu ya kimuundo na kikatiba, nchi yetu ni nchi ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nje ya mipaka hiyo kwa yale mambo yote yasiyokuwa ya Muungano. Hili ndilo tamko letu.

Kwa nini hatulitambui tamko la SMZ na kwa nini tutoe tamko letu wenyewe? Kwa uchache, sisi Wazanzibari tuna sababu tatu za kutokulitambua tamko la SMZ. Ya kwanza ni kwa kuwa limedanganya kwa kusema kuwa Zanzibar na Tanganyika  zilisalimisha utaifa wake kwa Jamhuri ya Muungano na hivyo hakuna lolote kati ya mataifa hayo linalotambulika sasa kimataifa. Si kweli kwamba mwaka 1964 Zanzibar ilichanganya utaifa (nationality) wake na Tanganyika. Mkataba wa Muungano, ambao unatajwa na tamko hilo la SMZ kama kigezo cha hoja yake, hausemi hivyo. Badala yake tulichochangiana katika Muungano huu ni uraia (citizenship). Kwa tafsiri ya taifa, utaifa hauwezi kuchanganywa – au angalau tuseme kwa mfano wa kwetu, hatukutaka kuuchanganya.

Taifa ni eneo lenye mipaka inayotambulika na ambayo ndani yake muna watu wanaotambuliwa kwa utamaduni na historia yao kuwa wamoja. Zanzibar ilikuwa, imeendelea kuwa na itaendelea kuwa taifa kwa tafsiri hiyo; na Tanganyika hali kadhalika. Maana watu wa pande zote mbili, wanatambulika na wenyewe wanajitambua kwa tamaduni na historia zao. Wanauhisi uwapo (essence) wao na kuwapo (existence) kwao kama wao.

Tunajua kuwa pana tafauti katika kuzielezea hisia za utaifa kati ya Watanganyika na Wazanzibari. Kutokana na sababu ambazo sisi Wazanzibari tunazitilia shaka, Watanganyika wengi hawako wazi kuhusu Utanganyika wao. Hata wanapofanya sherehe za Uhuru wa 1961, husema kwamba wanaadhimisha siku ya uhuru wa Tanzania! Lakini Tanzania haikuwapo mwaka 1961. Tanzania haijawahi kutawaliwa na hivyo haijawahi kupata uhuru! Sisi Wazanzibari tuko wazi panapohusika utaifa wetu. Tunazisema waziwazi hisia zetu na hatutafuni maneno kwamba sisi ni Wazanzibari na tunataka tuendelee kubakia hivyo.

Sababu ni kuwa utaifa ni hisia za kujinasibisha na watu na mahala fulani – kile wanachokiita Waingereza feelings of belongingness – na hisia hizo mahala pake ni katika nyoyo za watu. Hazichukuliki wala hazichanganywi kwa mbinu na hila kama hizi zilizomo kwenye Muungano huu, ambao kila ushahidi wa kihistoria unaonesha kuwa kuundwa kwake kulikusudiwa kuidhibiti Zanzibar na sio kushirikiana nayo kama mwenza mwenye haki sawa kwenye Muungano huu.

Dhana ya uraia ni tafauti na ya utaifa maana uraia unaweza kusanifiwa kwa hila za kisiasa na hata kijeshi na mwishowe ukawekewa mipaka ya kikatiba. Watu wa mataifa kadhaa ulimwenguni wameshawahi kutenzwa nguvu ili wakubali kuwa raia wa dola fulani. Historia imejaa mifano ya aina hiyo. Falme nyingi za Ulaya, kwa mfano, kabla ya mwaka 1640, zilijitanua na kulazimisha majirani zao kuzitii tawala zao na hivyo kuwafanya kuwa raia zao. Huo ndio mfano wa zilivyokuwa na kutanuka kwa dola za Ufaransa, Ujerumani, Ureno na Ugiriki kwa kutaja mifano michache. Kwa hivyo, uraia unaweza kulazimishwa – na kwa hakika mara nyingi ndivyo inavyokuwa – na dola yenye nguvu kwa watu wa mataifa dhaifu. Katika mfano unaokaribiana na huo, ndipo nasi tukachangiana uraia kwenye Muungano huu.

Hata hivyo, pamoja na ukungu wa shaka na shukuki uliotawala nia na dhamira iliyopo nyuma ya Muungano huu, sisi Wazanzibari tumeendelea – kwa miaka yote hii 44 – kuuhisi na kuukumbatia utaifa wetu wa Zanzibar, yaani Uzanzibari. Kwa hivyo, kwa mfano, mimi na hawa wenzangu tunaoandamana leo tunajitambulisha kwa utaifa wa Uzanzibari, japokuwa hatukatai kwamba kwa uraia sisi ni Watanzania. Kwa kufupisha maneno ni kwamba Uzanzibari wetu tumepewa na Mungu Muumba nchi na mataifa ya wanaadamu na uraia wetu tumepewa na Mkataba wa Muungano wa Sheikh Abeid Karume na Mwalimu Julius Nyerere kama unavyosomeka katika kifungu chake cha iv (f).

Sababu ya pili ya kutolitambua tamko la SMZ ni vile kujengwa kwake juu ya msingi wa hotuba ya Rais Kikwete ya Agosti 21 Bungeni, ambayo mara tu baada ya kuitoa tulisema kwamba ilikuwa imepotea njia. Kwa mfano, katika hotuba hiyo, Rais Kikwete aliitaja Tanganyika kuwa nayo ni nchi ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano, jambo ambalo si kweli katika udhahiri wake. Tanganyika haipo hata ndani ya mipaka ya Jamhuri hiyo, maana ni bunge la Tanganyika ndilo lililopitisha Azimio la kuifuta (?) mwaka 1964, siku chache tu baada ya kusainiwa kwa Makubaliano ya Muungano.

Kwa hivyo, hadhi ya Zanzibar (nchi iliyo hai) si kama hadhi ya Tanganyika (nchi mfu) katika Muungano huu. Si Mkataba wa Muungano wala Baraza la Mapinduzi, ambalo lilikuwa ndicho chombo cha juu cha kisheria kwa wakati huo kwa upande wa Zanzibar, lililoiua Zanzibar. Kwa hivyo, ikiwa tamko hili limejengwa juu ya msingi uliopotea, ni wazi nalo litakuwa limepotea na sisi hatuwezi kukubali tamko lililopotea liwe ndio mtazamo wetu.

Na sababu ya tatu ya kutokulitambua tamko la SMZ ni njia ambayo limewasilishwa kwetu. Baraza la Wawakilishi ndicho chombo pekee chenye madaraka makubwa ya kisiasa kwa Zanzibar na ambacho kinawakusanya Wazanzibari wa vyama vyote viwili vikubwa katika nchi ya Zanzibar. Kwa lugha ya kisiasa, tunaweza kusema kwamba Barazani humo ndimo Wazanzibari tunamowakilishwa kama Wazanzibari. Tamko hili limesomwa na mkuu wa shughuli za serikali Barazani, Waziri Kiongozi, katika siku ya mwisho na katika saa za mwisho za kikao cha Baraza hilo, ikijuilikana wazi kwamba wawakilishi wetu wasingelipata muda tena wa kulichangia.

Kwa nini SMZ ikafanya hivyo? Kwa sababu inajua kuwa hilo si tamko letu Wazanzibari na, hivyo, wawakilishi wetu wangelilipinga kwa nguvu zao zote kama vile walivyoipinga ile kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda iliyoitangaza nchi yetu kuwa si nchi. Ikiwa kuna chochote kilichopatikana kutokana na tamko hili la SMZ, basi, ni muakisiko wa khofu, woga na kutokujiamini ilikonako SMZ na ambako nako hitimisho lake ni kuwa serikali haituwakilishi sisi, Wazanzibari. Sisi tunakataa kuwa sehemu ya khofu na woga huu usiokuwa na maana, na hivyo tunakataa kulitambua tamko hili la SMZ. Tunasema “Not in our name!”

Baada ya kuyataja mapungufu hayo ya tamko la SMZ, sasa tuje kwenye ufafanuzi wa tamko hasa la Wazanzibari wenyewe, ambalo kama nilivyolitanguliza ni kuwa Zanzibar yetu ni nchi ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, kwamba sisi hatukuchanganya utaifa na Tanganyika na kwamba mjadala huu bado haujafungwa, na unaendelea.

Kwa nini Zanzibar iwe ni nchi? Jibu rahisi na la pekee ni kuwa hayo ndiyo matakwa ya sisi wenyewe, Wazanzibari, na ndivyo tulivyoyaeleza kupitia Katiba yetu – ambayo SMZ haina hiari ya kutokuifuata na kuiheshimu, maana viongozi wake waliapa kuilinda – na pia ndiyo matakwa ya msingi wa uhusiano huu baina ya Zanzibar na Tanganyika, yaani Mkataba wa Muungano. Mote muwili humo, Zanzibar inatambuliwa na inasimama kama nchi ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ya mipaka hiyo kwa yale mambo yote yasiyokuwa ya Muungano.

Na, kwa hakika, kimsingi mambo hayo yasiyokuwa ya Muungano ni mengi – au yalitakiwa yawe mengi zaidi – ya hayo ya Muungano. Elimu ya msingi na kati, afya, miundombinu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo, na mengineyo mengi, si ya Muungano; na kwayo Zanzibar ina haki na wajibu wa kuyasimamia na hivyo kujiwakilisha kwenye uso wa kimataifa kama Zanzibar inapoyazungumzia.

Ni bahati mbaya sana ikiwa uongozi wa Zanzibar umeshindwa kufanya hivyo huko nyuma na unashindwa kufanya hivyo sasa, lakini si kwamba ikijiwakilisha kama nchi kwenye masuala hayo Zanzibar itakuwa inakwenda kinyume na Makubaliano ya Muungano, ambayo ndiyo sheria kuu ya Muungano huu!

Kwa hivyo, Zanzibar ni nchi kwa kuwa ina sifa za kuwa nchi kwa maana ya nchi. Kwa kutumia maneno ya Ismail Jussa, nchi ni “eneo ambalo mipaka yake inafahamika, kwa Kiingereza wangeliita geographical area, ambayo ina wananchi wanaofahamika, population, na ina serikali ambayo inafanya kazi, yaani yenye madaraka – tunazungumzia hapa a functioning government.”

Zanzibar ina sifa hizo: ina eneo lake linalofahamika, kama lilivyoelezwa katika Ibara ya 2, kifungu kidogo cha 1 cha Katiba ya Zanzibar: “Eneo la Zanzibar ni eneo lote la visiwa vyote vya Unguja na Pemba na visiwa vidogo vidogo vilivyovizunguka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.” Zanzibar pia ina wananchi wake, ambao ni sisi Wazanzibari tunaoandamana hapa. Sisi tunajitambua kuwa ni wananchi wa nchi ya Zanzibar na tunaunganishwa na historia na utamaduni wetu. Na vile vile Zanzibar ina serikali inayofanya kazi – au ambayo ilitakiwa ifanye kazi – ya kulinda hadhi, heshima na mipaka ya Zanzibar na kuwaendeleza Wazanzibari. Ikiwa serikali iliyopo inatimiza au haitimizi jukumu hilo ni kitu cha mjadala, lakini nguvu hizo inazo na imepewa na Katiba yetu.

La kuwa Zanzibar yetu ni nchi, limo Tamko la Kuitangaza katiba yenyewe (Preamble), ambapo inasemwa: “Na kwa kuwa sisi, wananchi wa Zanzibar, tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katka nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya haki, udugu na amani… tumeunda Katiba hii.”

Kwa hivyo, ikiwa tamko la SMZ linakubaliana na Rais Kikwete ambaye naye alikubaliana na Waziri Mkuu Pinda, basi sisi tunachukulia kuwa wote watatu (Pinda, Kikwete na SMZ) wamekosea. Alianza kukosea Pinda kwa kuitangaza Zanzibar si nchi akitumia Kifungu cha 1 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambacho kinasema kwamba “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” bila ya kuzingatia Katiba ya Zanzibar, ambayo inaitangaza Zanzibar kuwa nchi yenye sifa zote za unchi. Akafuatia kukosea Kikwete kwa kumuunga mkono Pinda na kushadidia kuwa Zanzibar ni nchi kwa ndani na si nchi kwa nje. Na sasa imefuatia kukosea SMZ kwa kumuunga mkono Kikwete na kutokuheshimu Katiba yake yenyewe. Wote kwa pamoja, hoja yao inaporomoka kama mlima wa karata; na sisi tunakataa kuwa sehemu ya kuporomoka huko.

Tunasikitika sana kwamba SMZ, serikali yetu tuliyoipa dhamana ya kuilinda nchi yetu ya Zanzibar na katiba yake, imekubaliana na hoja ya Waziri Mkuu Pinda kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano iko juu ya Katiba ya Zanzibar. Tunasikitika kwa kuwa hivyo si kweli. Ukweli ni kuwa Katiba zote mbili ziko sawa sawa, kila moja ikiongoza taasisi zake katika eneo lake na kwa mamlaka yake. Na juu ya yote, Muungano huu hautawaliwi na katiba hizi mbili, bali Mkataba. Kilichotakiwa kufanywa na Katiba hizi, kwa hivyo, kilikuwa ni kuutafsiri tu Mkataba wa Muungano na sio kuukosoa ama kuurekebisha. Na Mkataba wa Muungano umetangaza kuwepo kwa Jamhuri (republic) moja na sio nchi (country) moja. Kinachoifanya jamhuri kuwa jamhuri hakiizuii nchi kuwa nchi.

Mkataba haukuzifuta nchi za Zanzibar wala Tanganyika; na wala haziwezi kufutwa na Pinda, Kikwete wala Nahodha, maana kwa kuwa huu ni Mkataba wa Kimataifa, wanahitajika kuwepo wale wale waliokubaliana, ndio waufanyie marekebisho. Katika hali ya sasa ambapo Serikali ya Tanganyika inaambiwa kuwa haipo, maana yake ni kuwa tayari mwenza mmoja wa Mkataba huu hayupo na hivyo mabadiliko hayawezekani – kwa lugha ya kisheria.

Ikiwa hivyo ndivyo, basi ilivyovisema SMZ katika tamko lake sivyo na wala haviwakilishi ukweli unaotambuliwa na sisi, Wazanzibari, na basi tunakataa kujinasibisha na kosa lililofanywa na serikali iliyopo madarakani hivi sasa Zanzibar. Hatulitambuwi tamko la SMZ kwa kuwa si letu!

Nimalizie maandamano haya kwa kusisitiza mambo matatu. Kwanza, viongozi wa sasa wa SMZ wamejidhihirisha kwamba hawapo kwa maslahi ya Wazanzibari. Wamefeli kuilinda na kuitetea Katiba ya Zanzibar na hatima ya Uzanzibari. Kufeli huko, kwa hivyo, kunatupa Wazanzibari sababu ya kutosha ya kudhamiria kuwaondoa madarakani kwa kutumia njia tulizokubaliana katika taratibu na sheria zetu, yaani kura. Itakuwa aibu kwa Wazanzibari kuwarudisha tena viongozi hawa hawa katika uchaguzi wowote utakaofanyika kuanzia sasa. Badala yake tuwaweke madarakani watu ambao wana bwana mmoja tu wa kumtumikia, na bwana huyo awe ni sisi Wazanzibari. Tutafanya kosa la makusudi kuwaweka madarakani watu ambao wanaonekana kutumikia mabwana zaidi ya mmoja!

Pili, kwa kuwa hao waliopo sasa madarakani wametusaliti na wamezisaliti nguvu tulizowapa kusimama kwa ajili yetu na badala yake wamejawa na woga matumboni mwao, basi sisi Wazanzibari wenyewe tunapaswa kuwa imara zaidi sasa kuliko wakati mwengine wowote ule kuilinda na kuitetea Zanzibar yetu. Wakati umefika kwa Mzanzibari kujinasibisha na kujilindia kwa Uzanzibari wake. Tuungane pamoja na tusimruhusu tena adui kusimama katikati yetu na kutuchagulia namna ya kuangaliana wenyewe kwa wenyewe. Mpemba na Muunguja ndiye mmiliki wa Zanzibar na wasifitinishwe tena.

Na tatu, kwa kuwa tunapaswa kujilinda wenyewe kama Wazanzibari – bila kutegemea serikali iliyopo sasa madarakani – basi tusikubali hata kidogo kuuwa mjadala huu unaondelea wa hadhi na nafasi ya Zanzibar ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Licha ya kuwa Waziri Kiongozi amechagua kuibwaga mada hii kavu kavu na kuepuka kujadiliwa na wawakilishi wetu Barazani, sisi Wazanzibari huku nje ya Baraza tusikubali kufungwa kwa mjadala huu.

Mjadala upo wazi na tuendelee kuuchangia kwa maslahi ya Zanzibar yetu. Kwamba hatuwezi kuwa na Tanzania imara, kama tuna Zanzibar dhaifu. Mzanzibari hawezi kuipenda Tanzania ikiwa mapenzi yake kwa Zanzibar ni mapungufu. Zanzibar ndipo petu, wala hatuna pengine, katu asitudanganye mtu!

Hili ndilo tamko la Wazanzibari. Zanzibar itakuwa Zanzibar daima, kama ilivyokuwa jana, ilivyo leo na itakavyokuwa kesho.

23 thoughts on “Wazanzibari hatulitambui tamko la SMZ”

 1. Heko Ghasaany kwa msimamo huu, tuko pamoja na Wazanzibari wenzetu hili moja kwa moja!!
  Idumu Zanzibar !! leo na kesho na daima!!

 2. Mimi nakuunga mkono kabisa. Sisi tamko la CCM, halikubaliki. Kama azanzibari iko haja kuulizwa tunachokitaka. Haya yalipo ni kuburuzana kwa hali ya juu. Ni nchi ndani lakini si nchi nje bado hamujatueleza. Kama munataka kufanya kama Scotland, kuna njia zake na kanuni zake. Hapa kwetu usanii tu umezidi.

 3. Idumu Zanzibar hakuna wa kuimeza Zanzibar tutailinda nchi yetu kwa bei yoyote hata ikibidi damu imwagike tena ila hatutomezwa na majambazi yaliopandikizwa na Tanzania Bara time will tell muangalieni Mugabe achechemea sijui CCM inafikiri nini inajichimbia kaburi uchaguzi ujao.
  Aluta continua GH
  From Toronto

 4. nimo kwenye maandamano!!
  natoka nyuma nakimbilia mbele, nakushika mkono na tunalinyanyua kwa pamoja bango letu:-
  Zanzibar ni nchi ndani na nje ya Tanzania
  Hatukuchangaya utaifa bali uraia
  Mjadala haujafungwa, bado unaendelea
  Zanzibar daima…jana, leo na kesho ,

 5. Tanzania idumu daima mbinguni na duniani,umoja ni nguvu utengano ni udhaifu …Mungu ibariki Tanzania na watu wake.. amen

 6. tuko pamoja kenye maandamano zanzibar ni nchi kimataifa na itabaki kua nchi kimataifa mungu ibariki zanzibar na wanzanzibari wake

 7. Al Haji Ameir, Virus99 na Atoya, nyote nawashukuruni kwa maoni yenu. Kwa Al Haji, bado wakati tunao kufanya mema kwa Mama yetu Zanzibar. It’s never too late. We have just to believe that we can and YES WE CAN. Kwa Virus, nashukuru kwa msimamo mmoja. Zanzibar Daima. Kwa Atoya, ahsante kwa kuwa pamoja nami kwenye maandamano haya ya amani. Kwa pamoja tutashinda na Zanzibar itadumu.

 8. Maneno yako haya Ghassani yasiishie kwenye mtandao tu. Yachapishwe kwenye vitini na kusambazwa nyumba hadi nyumba ya Unguja na Pemba na kusomwa na Wazanzibari hasa wa kizazi cha vijana ambao nyoyo zao zina kiu ya kujua ukweli na huwa rahisi kuukubali. Lifanywe hili kwa makala yako hii adhimu na zilizo mfano wa hizi. ZANZIBAR NI NCHI HATA NJE YA TANZANIA iwe ndiyo MOTTO ya uchaguzi mkuu wa 2010!!!

 9. kwanza umeshajaribu kujichunguza huwenda wewe wala sio mzanzibari huna damu ya kijerumani kweli wewe ninawasiwasi umeona jinsi wanzanzibari walivyodhaifu ndio unataka kuchukua mwanya huo kujipatia umaharufu kupitia udhaifu wao maana nao sijui wana chuki na nini badal aya kujifanyia kazi zao wajipatie maendela wameshindwa sasa wanafikiri muungano ndio utakaowaletea maendela hakuna maendela kama kila mmoja hatafanya kazi leo hii maisha yamewashinda wanatafuta wa kumsingizia hakuna mganga mganga wenu ni nyie wenyewe kama hamfanyi kazi hakuna atakayewaleata helka nyumbani ndio muone kuwa eti muungano una faida nahisi unajitafutia maarufu baada ya muda tutasikia umeanzisha chama cha kutete maslai ya wanzanzibari utapata wafuasi wapuuzi na pengine ukajidanganya na kuanzisha chama cha siasa utaishia kama mwenzio maalimu saif kwanza hata kwetu sisi wabara huo muungano ni kero tu na ole wenu mlilie kujitenga mtaona makali ya maisha mtakayoyapata nyie wanzanzibari mtaishia kujitenga tu mpaka muishie kutawaliwa tena na kuwa watumwa kwenye nchi yenu hamjui hata hostoria na wala hamjui mnachokitaka hata sasa ukiitisha maandamano watajitokeza wengi tu ukifikiri wanasapoti hizo hoja zako wengone kiukweli watakuwa wanaingia tu kwenye hayo maandamano yoko kwavile hawana kazi, wengine wana matatizo na fanmilia yao yaani kwaujumla wanzanibar wanamatatizo ya kisaikolojia tumewabeba sana nana sasa mmekuwa mnamtukana mzazi wenu tanganyika , napenda niwahakikishie kwamba kwahakika maendeleo hayaletwi na muungano bali na mtu binafsi kila mmoja kwa nafasi yake na kuuacha kulalamika na kuridhika ndipo mtakapoyaona hata mema mengi yaliyoyofanywa na muungano vinginevyo mmefunga macho na hamuwezi kuona maana dhamira zenu zimekataa kuona na mnatazama mambo kwa chuki binafsi mliyo nayo hata muungano ukivunjika leo hii hamtakuwa na nafuu yoyote ya kimaisha mtaendelea kulalamika na kulaumiana wenyewe kwa wenyewe nchi ngapi za afrika tunaziona hazijaungana na hazina maendelo kuwa na maendeleo au kutokuwa nayo hakuletwi na muungano kuwepo au kutokuwepo mnakaa kujadili muungano na kusahau kufanya kazi mnarithisa chuki tu kwa kizazi kijacho na wote wanaozaliwa sasa wanashindwa kujikwamua kutokana na ugumu wa maisha kwa fikra kuwa muungano nio kiwako vijana wanakaa vijiweni wanasema muungano ndio umewaweka vijiweni? wazee kushinda vibarazani kucheza bao nayo inasababuishwa na muungano wakinamama kushinda na kanga nayo ni muungano jaribu njia nyingine ya kujitafutia umaarufu hapa tumekustukia unasema mwenye mapenzi mema na zanzibar ni yule anayewauinganisha nakuona wewe kama unayezidishwa kuwjaza chukli wanzibari wenzio na kutafutana namna ya kuwagawa waune muungano kama kikwazo kwa maendeloe yao hivyo wewe ndiye adui namba moja wa zanzibari, MTAZAMO WANGU NI KUWA ZANZIBAR NI CHI NDANI NA NJE YA MIPAKA TA TANZANIA NA INATUMIA BENDERA YA TANZANIA HAKUNA BENDERA YA ZANZNIBAR WALA YA TANGANYIKA HIVYO KWA YEYETE YULE ANAPOTOKA NJE YA TANZANIA IWE AMETOKEA BARA AU ZANZIBAR AKIENDE NJE YA NCHI ATASEMA AMETOKA TANZANIA AU TANZANIA ZANZIBAR AU TANZANIA MBEYA, IRINGA, DODOMA, ARUSHA, MWANZA, HAYA NI MAJIMBO TU .
  kwa wenye akili wachukulie mfano wa Marekani iwe umetokea jimbo lolote lile ukienda nje ya usa unasema umetoka marekani hao ndio watu wenye akili sasa wametulia wanajadili mambo ya maendelo na sio muunganiko wao (au hujui maana ya U.S.A) sasa wewe jiulize muungano umekuzuije kujipatia maendeleo yako binafsi na kama ukiwa haupo utapataje maendeleo yako binafsi.
  NATUMAINI SIJAMKWAZA YEYEYO KATIKA HILI KAMA NIMECHEMKA TUKOSOANE KWA HEKIMA KATIKA KUAIDIANA LAKININAOMBA NIMALIZI KWA KUSEMA TUWEMAKINI NA WATU WANAONATAKA KUTUMIA KUTOKUJUA KWETU AU UJINGA WETU KWA MASLAI YA KUJIPATIA UMAARUFU.

  NAOMBA KUWAKILISHA.

  MUNGU WA MBINGUNI AWAPE AMANI NA MISTARI HII IZIDI KUWAUNGANISHA NA KUWAONGEZEA UPENDO

  MUNGU LIBARIKI TAIFA LA ZANZIBAR MUNGU LIBARIKI TAIFA LA TANZANIA MUNGUI IBARIKI AFRIKA NA WATU WAKE DUMISHA UHURU, UMOJA , AMANI NA MSHIKAMANO

 10. Hata mkiambiwa nyinyi ni DUNIA ukweli unabaki palepale nyinyi ni mkoa wa Tanganyika Rais wenu sawa na Tenga, baraza la wawakilishi sawa na mabaraza ya kata huku Tanganyika.

  Nchi gani haina kiti UN?
  Nchi gani haina hata jeshi? hamuwezi hata kupigana vita na ukerewe?
  Mlikubali kuwa koloni letu na mtaendelea hivyo. Tena mkifanya mchezo baada ya uchaguzi 2010 tutaunda serikali moja na kuifanya ZNZ Kanda kama zilivyo kanda ya mashariki, kati, nyanda za juu, ziwa etc yenye mikoa 5.

  Hatukubali kuachia hayo mafuta yanayosemekana yapo ktk mwambao wa ZNZ. Yaani tumewalisha siku zote sasa KIMWANA wetu ZNZ umependeza unataka talaka thubuti! HABARI NDIO HIYO.

 11. Mada nzuri nakubali kuwa ZnZ ni nchi kwa maana ya eneo ila katika sifa za nchi Zanzibar imepokwa baadhi ya sifa hizo hivyo kupoteza sifa za kuwa Taifa.
  Zanzibar ina sifa zote za utaifa ila haina nguvu za dola. Haina Polisi wala Jeshi hivyo kupoteze sifa muhimu. Mkubali msikubali, Zanzibar ni sehemu ya Jamuhuri Ya Muungano wa Tanzania and this is a fact.

 12. Huko mnakotaka kuipeleka Zanzibar hatufiki!! mtalazimisha punda kwenda mtoni, lakini hamwezi kumlazimisha punda huyo kunywa maji !! Si leo , si kesho ,si keshokutwa !!

  Zanzibar milele!!

 13. Mimi nadhani ni upumbavu kuamini kuwa Zanzibar haiwezi kusimama yenyewe bila ya Tanganyika na ati Tanganyika ndiyo iliyoifanya Zanzibar isiwe na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe. Mimi mwenyewe ni Mtanganyika, lakini najua kwamba ile Zanzibar tumeitawala na kuikalia kijeshi tu. Unajua kuna kambi ngapi za kijeshi katika kisiwa cha Unguja tu? Zaidi ya 10 katika eneo lenye wakaazi wasiozidi 600,000, yaani kama vile sehemu ndogo tu ya wilaya ya Temeke kuwa na makambi yote hayo.

  Hebu kama wanataka kujitawala na kujiendesha wenyewe, tuwaachieni Wazanzibari wafanye hivyo. Kwani hivi kuna dhambi gani wakisema hawataki tena Muungano? Kwani Muungano huu ni wa maumbile? Si ulibuniwa tu na watu wawili, Nyerere na Karume? Tuwache kuwatisha kwa mizinga na chuki za usultani na utumwa kama kwamba hapa Tanganyika hapakuwa na utumwa na usultani mbaya zaidi wa uchifu.

  Zanzibar ni ya Wazanzibari. Tanganyika ni ya Watanganyika. Halafu wenyewe wakiamua ndio wataungana.

 14. zanzibar ni mkoa tuu …………..tuko tayari kuitetea nchi yetu mpaka …………..na damu zetu zitaonekana siku ya ushindi tunakoenda kutakuwa na mkuu wa mkoa tu zanzibar ………..jifunze kwa amin na wajinga wengine ndio utaijuwa tanzania vizuri……….au ujaona comoro mazoezi ya makuruta…………….na mwambie jamaa aache sifa za kijinga ………kwa sababu ataishia shimo…………….kuna kijama kina sema kitatoka nyuma na kuja mbele mzee wangu alie mfesi nduli ananyambia jamaa ni wachovu balaaa porojo nyingi (umwinyi) kwenye mapambano ni aibu tu kijana wake niko sasa kwa msovieti kuna ninni tena kama sio balaa ………….mnabahati mbaya hii ni tanzania ingekuwa kenya sawa ……….sababu tunayo , nguvu tunayo yakutosha tena……,na uwezo tunayo ni amri tu…………….discusss maja za maendeleo ……………..kuwajaza wenzio ujinga kwa sababu elimu ndogo kibaraka mkubwa wa koloni rudi nyuma……….she

 15. ni amri tuu ……tunasubiria kwa muda mrefu endeleza tuuuu chokochoko huijui tz mwana mi mwenyewe ndio niko bado na moto………..ndio tukamilishe vizuri nimkuu wa mkoa tuu unapima moto wa tanuri hujui kagame , museveni joakim ch kabila na nk…………………. unakopitia watu wamemka zamani……………kwan si porojo tunataka…………

 16. Na mimi nashauri sana mawazo haya wapelekewe wawakilishi ili nao wajitayarishe kurudisha hoja hii muhimu sana kwenye kikao cha Baraza kinachofuata. Vile vile ni muhimu mwandishi akatafuta msaada wa kutoa nakala nyingi za maoni haya ili wananchi wengi wakapata nao faida ya kujua haya.

 17. kumaoni yangu ingetumika hii blogi kufundishia masomo ya sayansi na hisabati ambako taifa kama letu masikini linahitaji sana na pia wapitia nafasi wa wakulima na sio wakulima jinsi ya kupata masoko ujerumani na maeneo mengine , nafasi za wanafunzi za kielimu na jinsi ya kujikomboa na umasikini nazani ingekuwa inafaa zaidi kuliko kueneza siasa za chuki ……..usiombe izae sikia tuu ombaa Mungu ..uliza uambiwe utaomba ardhi ipasuke ..na kwa njia hii tutafika kweli afrika mpaka wahindi watuzarau tutakuwa watumwa mpaka lini?tutatengeza mamitambo kama ya ujerumani kwa namna hii ya kubomo a inabidi tutafakari?kunavitu katika maisha inabidi ukubali tu kupoteza hakuna maisha bila sadaka Mungu wabariki hawa watu na Tanzania na Afrika yao ili wawe na hekima ya maendeleo na umoja,.

 18. niko pembeni yako katika maandamano ya kupinga kauli ya vibara vya makafiri wa tz bara,ambao wapo tayari kuua kwa minaajili ya pesa Nahodha anatamka hayo kwa sababu anamaliza muda labda keshahaidiwa nyeye kuwa Rais,kumbe hajuwi masikini kizazi cha makunduchi kuukata uzanzibar ni kukataa uislam na kumkataa Mtume wa M/Mungu na kuukubalisa Utz ni kuukubali Ukatoliki wa Nyerere,Mungu ibariki Zanzibar na wabariki watu wake,Mungu mbariki Maalim Seif Sharif Hamad Amin.

 19. Mi nawashangaa Wazanzibar wanang’ang’ania ati Zanzibar ilitawala bara kipindi cha mwarabu na hawasemi Kilwa pia iliitawala Zanzibar 100-1500 AC wakati wa utawala wa kiafrika kabla ya wakoloni hawajaja EA, hizi fikra za ubinafsi nauarabu zinatoka wapi sio nyie mlipigana kumuondoa mwarabu? sasa inakuwaje miaka 44 ya Muungano sasa tunataka mwarabu arudi? hizo porojo za kutaka kuwa nchi sioni mantiki yake mi natokea kilwa na nina ndugu zanzibar mnaponiambia ati sina haki Zanzibar hamnitendei haki ati ! na mnamshabikia Maalim Seif wakati mnajua rohoni hamtaki kabisa awe raisi wenu na anaomba sana Zanzibar ijitenge ili apate fursa ya kuwagawa na kuwatawala na akishindwa atatangaza serikali ya Pemba! Kuweni werevu jamani nakuja salimia bibi yangu Kojani msininyanyapae na kunkera mie.

 20. maisha yote jaribu kutawala roho za watu na sio viwiliwili vyao kwani angalia mataifa ya ulaya mashariki urusi,chekslovakia ya yugoslavia ya zamani yako wapi ?wao waliona mtutu ndio nguvu ya kutawala watu sasa leo yaguju.pia khaji fatilia historia walotawala kilwa enzi zile walikuwa ni WABAZRANGID watu waliotoka shirazi/irani ya leo (soma historia ya kweli sio ya nyerere) kwa hiyo zanzibar ilitawaliwa na hawa watu walioweka makao makuu yao hapo kilwa.

 21. hongera mwandishi wa nakala hii.
  tunaunga mkono maelezo yako kwa asilimia mia.
  Idumu jamhuri ya watu wa ZANZIBAR.

 22. NIMEFURAHI SANA KWA KUWA SIO MIMI TU TUNAOTAKA ZANZIBARI YETU IWEPO KATIKA PAHALA AMBAPO PAZURI KWA ZANZIBAR WOTE.

  KWANI NI SHIDA NA KUKOSA FURAHA TANGU VILIPO ANZA VYAMA VYA KISIASA YANAYOTOKEA ZANZIBAR INCHI YA AMANI NA YA WASILAMU, NI MAMBO AMBAOYO HAYANAFIKIRA YA KIAKILI NA WALA YA UBINADAMU. WATU KUWAWA, WATOTO, WANAWAKE MAMA ZETU BABA ZETU KWA KITU FEDHA, NINI FEDHA ? AMBAPO NCHI HAINA SALAMA WALA UHURU WA WA RAYA ZAKE.

  NINI MUNGANO ? NI KUTIA KATIKA BALAA NA FITNA NDANI YA UDUNGU WA ZANZIBAR, ETE ITAPO FIKA UCHAGUZI PELEKA JESHI KUUWA WATU NDIPO WATATULI. KWA MTAZAMO WA FILOSOFIA NI SAWASAWA NA KUSEMA KWAMBA KUZIMA MOTO NA PETROLI.

  KWANI KILA UTAPOWAPIGA WATU AU UWA WATU NDIPO WATAJITARISHA KIVITA, NA UTAPO FANYA KI UBINADAMU NDIPO WATAKUKARIBISHA. JE HAMUONI BAADHI YA NCHI ZA KIARABU NANI ANAOGOPA RISASI AU BOMBA AU JESHI NI UPUZI TU UMEKUWA, KWANI SERIKALI YAO ILICHEZA NA MAISHA YA WANANCHI NDIPO SASA HAMNA HATA MUNGALIAO WA FUTURE. JE MNATAKA IFIKEHIVYO AU TUNATAKA AMANI.

  KUTUMIA JESHI KUAWATU KUNA WATU WAJUA KUFANYA MAMBO KULIKO MAJESHI YENU. NDANI NCHI HIHI. BASI JIHAZARINI NA HATU MNAZO CHUKUA HAKUNA HATA MMOJA ATAKUBALI ALIWE MAMA AKE HATA BABA AKE YEYOTE YULE KATIKE DAMU YAKE.

  NDANI YA RAIA KUNA WATU WANA FIKIRA ZA KULETA MANDELEO KULIKO RAIS.

  SINA MENGI NI ISPOKUWA ZANZIBAR HATO KUFA MAISHA.

Leave a Reply to THINK BEFORE YOU DONE Cancel reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.