UCHAMBUZI

Kipanga cha Mohamed Seif, Januari 27 na makinda ya kunguru weusi wa Zanzibar

Nianze kwa kunukuu utungo niliouandika miaka saba nyuma, yaani Januari, 2001, katika wakati ambao mauaji dhidi ya raia wasiokuwa na hatia yakiendelea Unguja na Pemba. Tembelea mtandao wa Shirika la Haki za Binaadamu, Human Rights Watch, http://www.hrw.org/reports/2002/tanzania/zanz0402.htm, kujisomea mwenyewe namna unyama huo ulivyotekelezwa. Niliuita utungo huu ‘Ulipozipata Bunduki,’ na ilikuwa ni suto kwa utungo ‘Nikizipata Bunduki’ ulioandikwa na Muhamed Seif Khatib katika kitabu chake Fungate ya Uhuru. 

Ikumbukwe kwamba wakati nikiandika utungo huo, Muhamed Seif alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania na basi Jeshi la Polisi, ambalo ndilo mtuhumiwa mkubwa wa ukatili huo, lilikuwa chini ya dhamana yake. Kwa nafasi yake angeliweza, kama angelitaka, kuzuia maafa hayo.

Lakini, kama tutakavyoona katika makala hii, hadi katika maandishi yake ya hivi karibuni kabisa, miaka saba baada ya maafa yale, bado kwake Wazanzibari wa aina ile ni sawa na makinda ya kunguru weusi tu, na basi kilichowapata kilikuwa stahili yao au yumkini hata kile kilikuwa hakitoshi!

Na Mohammed Ghassani
Na Mohammed Ghassani

La kuongozea ni kwamba wakati huo Muhamed Seif alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni, chuo nilichokuwa nikisoma, na utungo huu (ambao kutokana na muda kukua, nao sasa umekua kidogo) niliubandika katika ubao wa habari za wanafunzi chuoni hapo kulalamika juu ya kile kilichokuwa kikiendelea dhidi ya Wazanzibari wenzetu (mimi na yeye) sio tu mbele ya macho yake, lakini katika eneo la dhamana yake kabisa. Niliandika:

‘Lipotia mkononi
Bunduki mashine gani
Hukukaa msituni
Bali wekwenda mjini
Kwenye raha na vimwana!

Ulipopata mikuki
Hukuchoma wazandiki
Bali ulipinga haki
Ukawa u mamluki
Wa madhalimu kulinda!

Ulipopata mashoka
Majambazi hukufyeka
Wanyonge ‘lodhalilika
Haki yao wakitaka
‘Kenda kuwachangachanga!

Ulipopata na sime
Ukajiona u dume
Ukasubiri waseme
Wananchi uwachome
Hadi ukarowa damu!

Ulipopata sauti
Ukaanza usaliti
Ukauwacha umati
Kwa bwanao ukaketi
Butile kurambaramba!

Ulipopata uwezo
Ndipo ukaanza bezo
La sizo kuzeta ndizo
Kwamba u kwenye mchezo
Wa ngoma za mkobele!

Ulipata kila kitu
Kukufanya uwe mtu
Bali ada ‘kafurutu
Ukachagua uchatu
Na sasa upewe nini?

Na sasa kipi chengine
Upewe uwe mnene?
Watu wote wakuone
Na chinichini wanene
Kama kweli umepewa!

Ama shipa ukokote
Au makamba uvute
Na makopo uokote
Urande mitaa yote
Ndilo lililobakia!

Dibaji ikomee hapo. Jumapili ya tarehe 20 Januari, 2008, katika safu yake ya Kipanga kwenye gazeti la Mzalendo, Muhammed Seif aliandika kile alichokiita Kunguru Weusi.

Makala hii ilikumbana na sadfa nne: sadfa ya kwanza ni kwamba, ndani ya toleo hilo hilo mulikuwa na tangazo la Wizara ya Maliasili na Utalii lililokuwa likiuarifu umma juu ya “zoezi la kudhibiti kunguru weusi jijini Dar es Salaam” kwa lengo la “kulinda afya, mazingira na kuondoa kero kwa wananchi.” Panatajwa njia tatu za kutimiza hilo: matumizi ya sumu maalum ya kuua kunguru aina ya DRC 1339, ukamataji kwa kutumia mitego maalum na, tatu, “uharibifu wa viota, makinda na mayai ya kunguru.” (Mzalendo, Na. 1912, Uk. 26).

Sadfa ya pili ni kwamba makala hii imetoka mwezi ule ule ambao mauaji dhidi ya Wazanzibari yalitokea (kwa hakika wiki moja tu kabla) na ambayo chimbuko lake ni kuharibiwa kwa uchaguzi wa 2000 na sasa wiki hii, Chama cha Wananchi (CUF) (kama tutakavyoona mbele kwamba hawa ndio miongoni mwa hao kunguru weusi na makinda yao?) wanafanya maandamano ya kuyakumbuka.

Nyongeza ni kuwa, katika kipindi hiki hiki na kwa sababu zile zile, ndugu zetu wa Kenya wanapatwa na yale yale.Sadfa ya tatu ni kwamba, kutokana na kuchafuliwa tena kwa uchaguzi wa 2005, hivi sasa Chama cha Mapinduzi (CCM) na CUF tunaambiwa vimo katika ‘hatua za mwisho’ za mazungumzo ya suluhu. Muhammed Seif ni mwana CCM (kwa tafsiri ya makala yake hiyo, ndiye Mswahili safi wa Zanzibar) na CUF ni kunguru weusi na makinda yao (rejea maandishi na kauli kadhaa za CCM ambazo huwahusisha CUF na Hizbu na Waarabu).

Na sadfa ya nne ni kwamba, mwisho wa makala yake, Muhammed Seif anaandika hivi: “Nasikia makinda ya ‘kunguru weusi’ sasa yanaota mbawa, yanajifundisha kuruka. Tunasubiri. Mitego yao bado ipo. Viota vyao tunavijua. Makinda yao tutayadhibiti na mayai yao tutayaharibu. Tunawasubiri.” Husemi ila wamekopiriana na mwandishi wa tangazo la Wizara ya Maliasili na Utalii!

Ni sadfa hii ndiyo inayoshawishi mjadala. Makala ya Muhammed Seif inazungumzia asili ya kuja na kuzagaa kwa kunguru weusi katika visiwa vya Zanzibar: waliletwa kutoka India kuja kusaidia kuondoa mizoga, kisha wakaselelea na kuanza kuwa adha kwa wakaazi kutokana na khulka zao chafu ikiwemo ya wizi.

Anasema: “Kunguru ana hila nyingine ya wizi. Huiba kitu chochote, pahali popote na saa yoyote…..Vitoweo jikoni havisalimiki. Vyakula kama ndizi, mihogo, maboga ama wali hukwapuliwa na ndege hawa. Sigha za akinamama tokea vidani, pete, hazamu, mikufu, timbi, kekee ama kikukuu huchukuliwa na kunguru hawa wezi.”

Ni kweli hii ndiyo khulka ya kunguru, lakini yeye hakusudii hasa kuwazungumzia kunguru ndege, bali wale wote wanaopingana na CCM, Zanzibar. Lakini, kwa kuwa chuki za ugozi (racism hatred) hufunika uwezo wa kufikiri, basi anajenga tashbiha ya majilio ya kunguru weusi Zanzibar kwa majilio wa Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu ili apate kianzio.

Anasema Waomani waliitwa Zanzibar na Waswahili (kwake tafsiri ya Mswahili ni mtu mweusi tu, peke yake, na ndiye mwenyeji hasa wa Zanzibar), kuja kuwasaidia kumuondoa Mreno aliyekuwa anawatawala. Lakini kisha “Waarabu hawa hawakuondoka tena Zanzibar tokea mwaka 1832 hadi Januari mwaka 1964 walipopinduliwa na Waswahili wenye hasira ya kutawaliwa.”

Kwa nini hasira ya kutawaliwa? Jibu ni kwamba: “Watawala hawa kama ilivyokuwa kwa kunguru weusi, badala ya kusaidia kuondosha uchafu na uoza, wao wakageuka malaghai na wezi…wakaanza kusomba kila kitu kwa manufaa yao…mashamba makubwa yote yenye rutuba. Mazao ya biashara na minazi na mikarafuu…..! Wakwezi wa minazi wakawa Waswahili. Wachumaji karafuu wakawa Wapemba na Wahadimu. Manokoa wakadamu na manamba wa mashamba ya Masultani hawa wakawa Waswahili…..”

Anaendelea kuonesha kuwa maovu ya ‘kunguru weusi’ hawa hayakuishia kwa kuwakamua wenyeji kiuchumi tu, bali hata kuwadhalilisha utu wao, maana “(Masultani) Walipenda starehe za mwili na akili. Majahazi yao kutoka Omani hayakuja na wanawari, vigori na mabinti. Hivyo mijanajike na mifanyakazi ya Kiswahili ikawa ndio kimbilio lao Masultani hawa walioshiba. Majumba yao pia yalijaa masuria. Hakuna mwanamke mzuri wa Kihadimu, Kipemba au Kitumbatu aliyenusurika katika matamanio ya Sultani hawa au watoto wao.”

Katika kilele cha machungu hayo, Muhammed Seif anataka tuamini, ndipo ‘Waswahili’ wakafanya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, kuvunja minyororo ya dhiki na dhuluma (kwa kutumia maneno ya Kanali Seif Bakari).

Kwa wenzetu walio Tanganyika, na hata baadhi ya Wazanzibari, hii ndiyo ‘historia rasmi’ ya Zanzibar. Hii ndiyo pia ‘taswira rasmi’ ya, kwanza, ukoo wa Busaidi uliokuwa ukitawala Zanzibar, pili, ya kila Mzanzibari mwenye japo tone la Kiarabu katika damu yake hata ajifanye kuipenda na kuitumikia CCM na serikali zake (rejea mkasa wa Dk. Salim Ahmed Salim katika kinyang’anyiro cha tiketi ya uraisi kupitia CCM, mwaka 2005), tatu, ya wale wote ambao wao au wazee wao hawakuwa wafuasi wa chama cha Afro Shirazi (ASP) kinachodaiwa kufanya hayo Mapinduzi ya 1964, na tano wale wote ambao baada ya kurudi tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa waliamua kukiunga mkono chama cha CUF. Hawa ndio kunguru weusi na makinda yao!

Ukiwajumuisha hao, utapata zaidi ya nusu ya Wazanzibari. Sina hakika sana, ikiwa Muhammed Seif mwenyewe anaingia humo au la, maana kuna ndumondumo kuwa naye aliwahi kuwa mwanachama wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP au Hizbu) kama alivyowahi kuwa Dk. Salim, mmoja akipiga goma la vijana wa chama hicho kutokea Kikwajuni na mwengine akipuliza tarumbeta lake, lakini nina hakika tumo wengi, wengi sana, ambao tunatukanwa tusi hili.

Nimesema chuki za ugozi huzuia mantiki. Kwa mfano, hailekei kuwa mwandishi mwenye shahada ya Uzamili kama alivyo huyu hana rekodi sahihi ya historia ya nchi za Uswahilini, kwao mwenyewe, ambako majilio ya watu kutoka Bara Arabu, hasa Yaman na Syria, yalianzia tangu karne ya kwanza na mahamizi rasmi (hata kwa rekodi za karibuni zaidi) yalikuwa karne ya 10 na 11!

Haijuzu kama hajui kuwa hao watawala wa Kireno waliokuja kuzitawala nchi za Uswahilini, hata ikawabidi wahenga wetu (wake na wangu) kwenda kutaka usaidizi wa ’kunguru mweusi’ wa Oman, walikuja mwanzoni mwa miaka ya 1500, zaidi ya miaka 500 baadaye! Angalau naasome kiungo hiki: http://en.wikipedia.org/wiki/Zanzibar. Ndio maana haielekei ikiwa hajui kwa hivyo, hao wazee wa Kiswahili anaotaka tuamini yeye kuwa ndiyo Waswahili hasa, tena peke yao, yaani Wabantu, kwamba walifika katika maeneo haya ya Uswahilini kuanzia karne ya 16!

Naajipe tabu kidogo msomi huyu ya kupitia hapa: http://en.wikipedia.org/wiki/Bantu, asaa akapata uelewa. Kama hajuwi kuwa wakati huo hata msikiti maarufu wa kwao, Kusini Unguja, Kizimkazi, ulishajengwa tangu mwaka 1107! Kwa hivyo, hao wazee wetu wa ’Kiswahili’ anaosema kwamba walikwenda kuomba msaada wa kumuondoa Mreno, ama hawakuwa hawa anaowaita yeye Wabantu, au walikuwa ni mchanganyiko wa Wabantu na hao waliokuwepo kabla yao.

Hii ni mantiki rahisi kuifahamu, lakini shuti ubongo usiwe umetandwa chuki za ugozi.Sina hakika ikiwa hajui kuwa kiongozi wa Oman aliyeshirikiana na wazee hao kumuondoa Mreno, alikuwa ni Imamu Seif Al Orobi, ambaye, kwanza, hakuwa mfalme bali imamu anayeendesha dola ya Kiislam na, pili, zoezi la kumtoa Mreno lilimalizika mwaka 1698; lakini utawala wa kifalme, tena kutoka ukoo tafauti, ukaja nchi za Uswahilini zaidi ya miaka 142 baadaye, yaani 1840.

Akijua hili, Muhammed Seif atajua kuwa hisabu hii inamaanisha kuwa yule ‘kunguru mweusi’ wa mwanzo aliyekuja kuwasaidia wazee wetu wa Kiswahili kuondoa uchafu wa Mreno, siye aliyekuja kutawala. Kwamba baina yao pana masafa ya takribani karne moja na nusu, kipindi ambacho mnyumbuliko wa historia ya mwanaadamu unadai mengi yawe yameshatokea, kiasi ya kwamba hata kama ni kweli Waarabu wale wa mwanzo hawakuja na wake zao na walioa hapa hapa Uswahilini, basi ni kinyume cha mantiki kukiita kizazi kilichokwishakaa muda wote huo kwamba hapa si pao na ni makinda tu ya kunguru weusi yanayostahiki kudhibitiwa, na mayai na viota vyao kuharibiwa!

Ikiwa yote hayo hapo juu Muhammed Seif hayajuwi, nina hakika jambo moja atakuwa analijuwa kwa yakini: kwamba wanawake wa Kiswahili (kama alivyowataja wa Kihadimu, Kitumbatu na Kipemba) ni warembo sana. Mama yangu na mama yake na mama wa mama zetu ni miongoni mwao. Sasa ikiwa hakuna mwanamke wa Kiswahili, kwa maneno yake mwenyewe, “aliyenusurika na matamanio ya Sultani hawa au watoto wao,“ basi mimi naye hatuna sitara, maana tutakuwa tu mabotea, tena ya haramu, ya Masultani hao!

Vyenginevyo, akanushe kwamba aidha alilolisema si la kweli, ni uzushi tu, au ajisalimishe kwamba yeye hakukaa miezi tisa katika matumbo ya mmoja kati ya hao wanawake wa Kipemba, Kihadimu na Kitumbatu na hivyo basi si Mswahili wa Zanzibar. Akikiri hilo, hata hivyo, atatufanya sisi Waswahili wa Zanzibar tung’amue kwamba kumbe huyu ni mkando na ndiyo maana akapata sauti ya kututukana hivi!

Na ikiwa hivyo ndivyo, tutapata shaka: ilikuwaje huyu basi akawa mbunge wa kuchaguliwa na wananchi, Waswahili wa Kizanzibari, waliozaliwa na ama Wahadimu, Watumbatu au Wapemba wanaoishi Uzi? Tukifika hapo, tutakuwa tunaushuku si tu Uzanzibari wake, bali pia Uswahili wake na uhalali wa yeye kuwa hapo alipo kwa kutumia migongo yetu!

Nilisema kwamba kwa hisabu ya wanaoingia kwenye idadi ya kunguru weusi na makinda yao, basi tumo wengi wetu miongoni mwa Wazanzibari. Tumo wengi ambao ni ’halali’ kuharibiwa viota vyetu (nyumba zetu na miji yetu) kama ilivyotokea kwa Piki (Pemba) na Kianga na Bububu (Unguja) katika uchaguzi wa 2005.Tumo wengi ambao ni stahili kuharibiwa mayai yetu (kuuliwa kwa watoto wetu, kubakiwa wake na watoto wetu) kama ilivyotokezea kwa Pemba na Unguja Januari 2001, Kizimbani-Wete 2005, Piki 2005 na Dole 2005.

Tumo wengi ambao ni sawa tukidhibitiwa kila tunapoonesha dalili za kuota mabawa (kufukuzwa kazi kiholela, kuvunjiwa biashara, kunyimwa nafasi za masomo na ajira), kama ilivyotokezea katika kipindi cha pili cha awamu ya nne na inavyotokezea sasa katika awamu ya sita ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Alimradi tupo wengi.

Ubaya wa mambo kwa hao wanaofanya (na sio kwa sisi tunaofanyiwa), ni kwamba sisi, kunguru weusi na makinda yetu, tunazidi kuongezeka na tunazidi kuimarika. Kila wakikiharibu kiota kimoja, basi kwa wingi na kwa umoja wetu huo hujenga viota vyengine madhubuti na imara zaidi. Wakiliharibu yai moja, huingia chumbani tukataga mengine. Wakilidhibiti kinda moja, sisi huwabwerusha wengine kumi na moja.

Na sababu ni hiyo moja tu. Wingi wetu na usafi wa dhamira yetu. Tumo mote. Pemba na Unguja. CUF na CCM. Donge na Mtambwe. Bali hadi Umbuji na Msuka. Ndani na nje ya Zanzibar. Tuko wengi tunaojinasibisha na Uzanzibari wetu na tunaosema Zanzibar Daima. Zanzibar ni yetu sote. Zanzibar ndipo petu. Kwa ajili yake tutaishi, na kwa ajili yake tutakufa!

Kwa hivyo, niruhusuni waungwana, nimalizie kama nilivyoanza: kwa utungo mwengine ambao niliutunga katika kipindi hicho hicho cha dhuluma ya Januari 2001, cha kudhibitiwa kwa kunguru weusi, viota vyetu vilipoharibiwa na mayai yetu kuvunjwavunjwa. Kwa muktadha wa sasa na wa makala hii, hiki ni kiapo kwa wale ambao chuki zimeziba uwezo wao wa kutumia mantiki hata kufika mahala pa kuwafananisha Wazanzibari wenzao na kunguru weusi.

Nawajuwe kwamba sisi, makinda wa kunguru hao, hatujavunjwa moyo na vigaro vyao dhidi ya Mama yetu Zanzibar. Kwamba Zanzibar ndipo petu, hatuna pengine, wala hatudanganyiki na mtu. Kama kweli wanaamini kuwa Zanzibar ni nchi ya Waswahili, basi sisi ndio hao Waswahili wenyewe.