Huu ni uhakiki wa kitabu cha khadithi fupi fupi zilizotungwa na Ally Saleh ambapo hii inakuwa ni kazi yake ya pili baada ya ile ya mashairi huru iliyopewa jina la CHANGAMKA. Nimetakiwa niseme mawili matatu katika uzinduzi wa kazi hii adhimu ya Jumba Maro, ambayo ni maoni yangu kwamba imekuja wakati ndio na inazinduliwa pahala ndipo. Nimechagua kuzungumzia hadithi ya Msafiri inayopatikana katika ukurasa wa 10 wa kitabu hiki.
Nitangulize kusema kuwa mimi ni miongoni mwa wanaoamini kuwa jukumu kubwa la mhakiki wa kazi ya fasihi (andishi?) ni kuisafirisha kazi hiyo kutoka kipande chake cha karatasi kwenda kwa watu wenyewe, ambao kila siku wanabakia kuwa walengwa wakuu wa dhamira ya msanii.
Kwa mantiki hiyo, basi naungana na akina Leo Totsloy na Paulo Freira katika imani kwamba kazi za fasihi zinatafsirika na zinaweza kuelezeka kwa muktadha wa jamii iliyopo, hata kama si lazima tafsiri na muktadha huo uwe ni ule uliokuwamo katika mtima wa msanii wakati wa kubuni kazi yake. Si lazima, kwa hivyo, iwe tafsiri yangu ya hadithi hii ni ile aliyoikusudia mwandishi Ally Saleh.
Hadithi hii imeitwa Msafiri ikisimulia mkasa wa mtu anayeliwa na hamu na ghamu ya kurudi kwao baada ya miaka mingi ya kulazimika kuishi ughaibuni. Bwan’ Said, mhusika mkuu, ni msafiri.
Ni msafiri kwa kuwa kwa sasa anaishi pasipo pao, na hivyo kila siku amekuwa akijihisi kuwa ni mgeni wa mahala hapo mithili ya mtu aliye safarini. Hii inakuja hata baada ya kuwa ameshaishi hapo sehemu kubwa ya uhai wake: akaoa na kuzaa. Usimulizi wa hadithi unatupa picha kuwa hisia hii ya ugeni na usafiri imo damuni mwake, ndio maana ameiambukiza hata kwa mwanawe, Kumbukizi, aliyemzaa huku huku ughaibuni.
Mwandishi anatueleza kuwa: “…Kumbukizi…maisha yake yote alikulia ugenini na akizongwa na tamaa na hamu ya kurudi nyumbani. Alisikia kuwa aso kwao ni mtumwa.”
Pia, Bwan’ Said ni msafiri kwa kuwa kwa siku sasa amekuwa na dhamira na matayarisho ya kufunga safari ya kurudi kwao alikotokea. Yeye na mwanawe, wote wamekuwa wakiliwa na hamu na ghamu ya kurudi kwenye asili yao. Swali linalojaribu kujibiwa katika hadithi nzima ni, je nyumbani huko wanakokutamani kurejea, kunarejeleka?
Kipande cha ushairi kinachoifungua hadithi hii kinamraghibisha “Msafiri” wetu aindame safari yake hadi afike akutakako:
“Safari hakika ni safari
Moyo wako ni kuujuburi
Siri uiweke kuwa siri
Kushindwa katu usikukiri
Ujihimu kila mara
Uongozwe na yako ghera
Lisiwepo la kukukera
Hadi kutimu dhamira
Hatua yako ya kwanza
Mwisho ni kuimaliza
Nchi yako maliwaza
Hilo hakika timiza” (Jumba Maro, uk. 10)
Lakini tangu mwanzo, msomaji anapousoma tu ushairi huu, anajiwa na hisia za ugumu wa safari ya Bwan’ Said. Kwamba inahitaji ujuburi na ujasiri wa kutosha na kwamba tajiriba yake ni zaidi ya kujitoa muhanga.
Ndoto tatu, ambazo mwandishi anamuotesha mhusika wake, Bwan’ Said, na kuziwasilisha kwetu kupitia masimulizi yake kwa mwanawe, Kumbukizi, zinamvunja miguu kabisa na kumfanya ashindwe hata kusimama seuze kwenda mbele.
Ndoto mbili zinamuonesha kuwa amefika kwao, lakini akakukuta ku kinyume mbele. Tafauti na ilivyokuwa kabla ya kuondoka kwake, sasa kila kitu kimewekwa mahala si pake. Kuna utando wa khofu na ubiruzi wa mambo. Dhamana zimekabidhiwa wasiokuwa na uwezo wala stahiki nazo. Kuna kiwango cha chini cha maadili na upotevu mkubwa wa staha. Na hivi sivyo Bwan’ Said alivyokuwacha kwao, wala si kwao akutamaniko.
Kwa mfano, katika ndoto ya kwanza, Bwan’ Said anawakuta mbwa wakiwa wamo msikitini lakini waswalihina wako nje. Na hata hao waswalihina wenyewe wako shaghala baghala – kila mmoja kivyake. Imamu wao yuko katikati, badala ya kuwa mbele kama ilivyo kawaida. Na kivazi alichovaa hakifai hata kuvaliwa msikitini, seuze na imamu kama yeye.
“Kila mtu alikuwa ameelekea upande wake na… alisoma sura aitakayo… imamu alikuwa katikati… amevaa suruali kipande iliyovuka magoti yake, sio kwenda chini, la ilivuka magoti kwendea juu.”
Ndoto ya tatu inaonesha kuporomoka hadi kiwango cha chini kabisa kwa maadili aliyoyawacha. “Biashara ya tupu ilikuwa imetandazwa kama biashara nyengine. Za rangi hii na ile, za ukubwa huu na ule, za nchi hii na ile…”
Nimetangulia mwanzo kuutaja msimamo wangu katika uhakiki wa kazi za fasihi, kwamba ni lazima mhakiki airejeshe kazi hii “watuni.” Naomba sasa nilirudishe Jumba Maro kwa watu.
Kwangu mimi, nyumbani huku anakotaka kurudi Bwan’ Said hakuna tafauti kubwa na kulivyo hapa nyumbani, Zanzibar.
Zanzibar ya sasa ina mambo yako shaghala baghala kama yalivyo ndotoni kwa Bwan’ Said. Maadili yanaporomoka kwa kasi kubwa mno na, ninaposoma hadithi hii ya “Msafiri”, nashindwa kuzizuia fikira zangu zisizivute picha za Kibanda Ugali (Kiwengwa), New Happy Lodge (Mji Mkongwe) au hata maeneo ya Golf, ambako kuna biashara ya tupu inayoendeshwa kwa siri ya wazi.
Nashindwa kutokuoanisha na hali ya petu ya ‘usiasishwaji’ wa kila jambo, ambapo utaalamu unapuuzwa na ukereketwa wa kisiasa unatukuzwa. Ni petu Zanzibar ambapo inawezekana, kwa mfano, watu kupewa dhamana za uendeshaji wa ufuasi wao kwa chama tawala na sio kwa uwezo wao wa kitaalamu.
Kufeli tunakofeli ni kwa kuwa mfumo mzima unatufelisha. Kuondoka kwa nidhamu makazini na kuanguka kwa pato letu kunatokana na hilo la waliopewa dhamana kutokuwa na uwezo kama vile imamu wa kwenye ndoto ya Bwan’ Said anavyoshindwa kuiongoza sala, maana yeye mwenyewe hajijuwi hajitambuwi. Ndipo akaingia kuswalisha na kaptula!
Lakini kwa nini mambo yakafika hapa? Ndoto ya pili inampa jibu Bwan’ Said na inatusaidia sisi kuujuwa ukosefu wetu. Kwamba katika nchi yake anayotaka kurejea kuna unyanyasaji mkubwa wa haki za watu, kuna uhuru finyu wa kisiasa na kuna kiwango cha hali ya juu cha kutokujiamini miongoni mwa wakandamizwaji.
Yumkini ni kukaa kwao kwa miaka na kaka chini ya mfumo huu kandamizi, ndiko kunakowafanya wakandamikzwaji wakose hata uthubutu wa kuhoji madhila juu yao na, baya zaidi, wadiriki hata kumsaliti yule anayehoji kwa shufaa yao.
Anapojitokeza mtu wa kuwaamsha ili wapambane na udhalimu dhidi yao, nidhamu ya woga huwatanda na khofu kuwageuza wahanga wa milele. Matokeo yake, badala ya kusaidiana naye, humkengeuka na kurudi kule kule chini ya himaya ya dhuluma.
Pahala pamoja katika ndoto hii ya pili, Bwan’ Said anatusimulia hivi: “Mmoja wa watu hao…alilivuta sikio lake na kumuambia kama walichokuwa wakiambiwa… wengine, “Wakati. Mapambano. Mwisho.Tuungane”. Lakini “Mara kelele zikazuka kila kipembe…. “Wasaliti. Wauwawe hao wasaliti,” na punde si punde wale wahamasishaji wa yale maneno manne wakabebwa juu juu, hobela hobela, kiti kiti na kukabidhiwa kwa walinzi. Wakatiwa kwenye makucha ya walinzi. Umma kimya, haukusema kitu.”
Haya ndiyo yale ya mkasa wa Allegory of the Cave unaosimuliwa na Plato katika Phaedo ambapo mfungwa mmoja wa pangoni aliyefanikiwa kuja nje na kuyaona mambo yalivyo tafauti na vile wanavyosimuliwa na kuoneshwa na mabwana jela kule pangoni, alijikusuru kurudi kwa wafungwa wenziwe na kuwahadithia uhalisia ulivyo.
Lakini kwa kuwa wafungwa hawa walikuwa wameshalevywa na ilimu ya uongo kwa miaka kadha wa kadha, sio tu kwamba walikanusha alichowambia, bali pia walimuua mwenzao aliyekuja kuwapa ilimu hii mpya.
Nataka hapa nipate uthubutu wa kuihusisha ndoto hii ya Bwan’ Said na kadhia ya kufungiwa kwa gazeti huru la Dira karibuni miaka miwili iliyopita. Nataka nijuburi kuihusisha na kutangazwa kwa Mzee wangu, Sheikh AliNabwa, kuwa si raia wa nchi hii. Yote ni kwa kuwa Dira na Mzee Nabwa walipaza ile sauti, “Wakati. Mapambano.Mwisho. Tuungane.” Afanaalek! “Wakabebwa juu juu, hobela hobela, kiti kiti na kukabidhiwa kwa walinzi…Umma kimya, haukusema kitu.”
Umma wa Wazanzibari ambao ulijiwa na ilimu mpya ya kuoneshwa uhalisia wa kile hasa kilichomo ulimwenguni, badala ya kusimama pamoja na Dira na Mzee Nabwa katika wakati ule wa kubebwa hobela hobela, ulikaa kimya na kuyaacha makucha ya walinzi wachache yairarue Dira na yaivujishe damu ya Mzee wangu, Nabwa.
Lakini hivyo ndivyo kulivyo kwao Bwan’ Said. Hivyo ndivyo ilivyo Zanzibar yetu pia. Ndivyo ndoto ya tatu imwambiavyo “Msafiri” wetu anayeishi ndani ya kitabu hiki, na ndivyo uhalisia utwambiavyo sisi tuishio nje ya kitabu. Umma wote uliopo pale uwanjani, pamoja na wingi wao, hawana umoja. Na wingi usio umoja haufalii chochote kuwa nao. Ni wingi wa nzi.
Swali bado linabakia kuwa ni lile lile, je nyumbani kunarudika?
Kikwetu husemwa kuwa msafiri kafiri. Busara moja ya msemo huu ni kwamba safari ina visa na vitimbi, mikasa na vioja. Na basi mwenye kusafiri hulazimika hata kuzipinda ada na mila zilizotukuza na kutulea, alimradi tu tutimize safari yetu.
Kwa sisi tuliolelewa katika utamaduni huu adhimu wa Kiswahili, kuzivunja ada hizo ni pamoja na, kwa mfano, kula vilivyoharamishwa, kunywa vilivyokatazwa, kusema yasiyoridhisha na kutenda visivyoruhusiwa.
Lakini si kila wakati busara hii inafanya kazi, inategemeana sana na aina ya safari ifanywayo na dhamira ya huyo msafiri mwenyewe. Safari ya “Msafiri” wetu katika hadithi hii haimjuburishi hata kidogo kuzivunja mila na ada za kikwao, maana baada ya yote yeye hafungi safari kutoka uwenyejini kwenda ugenini, bali anatoka ugenini kwenda uwenyejini.
Haimpi kuwa msafiri kafiri, maana wetu ni msafiri aliyekuhama kwao zamani, na sasa baada ya kuishi sana ugenini, akaona kuwa hana pengine pa kustaaladhi ila kwao kulikozi kwa kitovu chake na vya wazazi wake. Huyu lazima aoanishe baina ya safari kama njia ya kufika atakako na safari kama kwa hali anakokwenda.Vyenginevyo kwenda kwake hakutakuwa na maana yoyote!
Ndio maana tangu pale mwanzo wa hadithi tunaelezwa na mwandishi kuwa: “Tokea ahamie ughaibuni, Bwan’ Said amempoteza mkewe, Bi Imani…”
Hapa ndipo lilipo jawabu la ndoto zake zote, ambazo hata hivyo mwandishi anasema kwamba hakuwa nalo. Kwamba kumpoteza Bi Imani, hakukuwa tu kumpoteza mke, bali ilikuwa ishara ya kupoteza imani hasa aliyokuwa nayo na kwao. Na je, mtu asiko na imani nako, kunakwendeka?
Mohammed Ghassani
24 Septemba 2005
Bwawani
Zanzibar