UCHAMBUZI

Uhakiki wa Kitabu cha Jumba Maro II

Kwa mara ya pili, Ally Saleh amenipa heshima ya kusema machache katika utambulisho wa kazi yake hii adhimu ya kifasihi, Jumba Maro. Mara ya mwanzo ilikuwa ni katika uzinduzi wa kitabu hiki uliofanyika Zanzibar tarehe 24 Septemba, 2005.

Kama katika mara ile ya kwanza, hapa pia nitangulie kusema kuwa mimi ni miongoni mwa wale wanaoamini kuwa dhima kubwa ya mhakiki/mchambuzi wa kazi ya fasihi ni kuisafirisha kazi hiyo kutoka kwenye kipande chake cha karatasi (au nukuu zake za simulizi) na kuipeleka “watuni”, maana fasihi wenyewe ni watu – ndio inaowalenga, ikawatathmini, ikawaburudisha, ikawafunza, ikawatanabahisha. Ndio inaowasiliana nao. Mchambuzi/mhakiki, kwa hivyo, ana jukumu la kuwasaidia watu wajione kupitia mistari au semi za kazi hiyo ya fasihi.

Basi kama vile ambavyo kazi ya fasihi huweza kusomeka (au kusikika), basi ndivyo pia inavyoweza kupokeleka, kutafsirika na kuchambulika kwa mawanda yoyote ambayo mchambuzi/mhakiki anaweza kujichawanya.

Sababu ni kuwa, katika fasihi neno huwa zaidi ya maneno, na kisa huwa zaidi ya mkasa. Yanayosemwa katika fasihi hayabakii kuwa kama yalivyo tu, bali, ili yakifu lengo la kusemwa kwake, lazima yapimwe, yachambuliwe na yahakikiwe. Ndiyo maana husemwa kuwa, kwa kila kipande kimoja cha kazi ya fasihi, huweza kuzalishwa maelfu ya kurasa.

Ukweli wa nadharia hii, hata hivyo, haulazimishi kwamba pawe na uwiano wa kimawazo baina ya mbunifu wa kazi ya fasihi na mhakiki/mchambuzi. Kwa hivyo, nitakayoyaona mimi katika Jumba Maro huenda yasiwe kabisa yale aliyoyaona Ally Saleh wakati wa kuiandika kazi yake. Naamini kuwa atanistahmilia kwa mawazo yangu kuhusu mawazo yake. Na kwa ufahamu wa hilo hilo, basi uhakiki na uchambuzi huu usihusishwe naye, bali mimi mwenyewe.

Tuje kwenye kazi yenyewe. Imeitwa Jumba Maro, mkusanyiko wa hadithi fupi fupi kumi na mbili na mashairi yenye idadi hiyo hiyo. Katika Yaliyomo, hadithi hizi zimeorodheshwa kwa mfuatano huu: Bi Sakina, Msafiri, Kutaradadi, Utamu wa Wazimu, Kisa Mkasa, Bwana Uwezo, Nyuma ya Pazia, Jumba Maro, Kigego, Vimbizi, Karamu na Gizani. Mashairi pia yametangulizwa kwa kila hadithi kwa mfuatano huu: Himaya Zao, Hakika ya Safari, Hangaiko, Huna Moyo Huo, Uso kwa Uso, Hakika ya Mambo, Usiulize Sababu, Mlevi Tapoleuka, Mdomo Mzito, Kesho ni ya Madhulumu, Mjumbe Kaemewa, Giza Nuruni, Nuru Gizani? (Jumba Maro, iii).

Kwa hivyo ni sawa kusema kuwa Ally Saleh hakuwasilisha mbele yetu kitabu cha hadithi fupi fupi tu, bali pia diwani ya ushairi. Kifani, utangulizaji huu wa ushairi kabla ya hadithi umeipamba kazi yenyewe na kuipa upekee katika historia ya uandishi wa Fasihi ya Kiswahili (nakusudia fasihi inayotumia lugha ya Kiswahili kuzungumzia maisha ya Mswahili).

Kwa hakika, hata katika waandishi wa fasihi za lugha nyengine, si wengi sana waliowahi kujitokeza na mbinu hii. Kwa wingi, nakumbukia kazi za Ngugi O’Thiong’o ambazo huanza na aya za Biblia (angalia The River Between). Katika Kiswahili, kumbukumbu zangu zinanionesha kuwa Ally Saleh amekuwa mwandishi wa mwanzo kutumia mbinu hii. Nakubali masahihisho ikiwa kumbukumbu zangu haziko sawa.

Lakini utangulizaji huu wa ushairi haubakii kuwa urembo wa kufurahisha macho ya msomaji wa kazi hii tu, bali unakwenda mbali zaidi na kuwa kisaidizi chake cha kuifahamu hadithi inayofuatia. Vipande vya ushairi vilivyotangulizwa kabla ya kila hadithi vinasimama kama ufupisho wa hadithi yenyewe na katika baadhi ya mifano vinakuwa kama changamoto kwa msomaji linalomsisimua agunduwe majibu ambayo huenda akayakuta katika hadithi yenyewe.

Katika ukurasa wa 39, kwa mfano, kuna ushairi Uso kwa Uso ambao unaitangulia hadithi Kisa Mkasa. Kipande cha mwisho cha ushairi huu kinasisimua hivi:

Na siku ayami kupita, mmoja akikataa kusamehe
Mwengine akidhani ndio yamekwisha kabisa
Loh, kumbe inawezekana kukutana
Ama kweli vilima kwa vilima…
Nani angedhani uso kwa uso ingekuwa?

Ukiisoma hadithi yenyewe ya Kisa Mkasa, utakuta kuwa ni simulizi ya kulipiziana baina ya watendwa na mtenda: visasi vya unyumba ambavyo vinaishia kwa kuvunja heshima na stara ya ndoa ya Zahrani.

Ndivyo pia unavyobashiri ushairi wenyewe, kwamba maisha ni mzunguko, na wanaadamu ni ‘waja-kwenenda’, kuna siku moja wale waliotendana na kukimbiana, watakuja kuonana na kutazamana Uso kwa Uso, lakini uso mmoja ukiangalia kwa haya na kujishuku: “Loh, kumbe angali hai!” na mwengine kwa suto na udadisi: “Kwani we’ siye mbaya wangu!”

Kwa wenye uweledi wa sanaa ya ushairi watakubaliana nami kuwa katika baadhi ya sehemu, Ally Saleh amevipa vipande hivi vya ushairi kiwango cha juu zaidi cha tafkira kuliko hadithi zenyewe. Angalia kwa mfano hadithi Msafiri (uk. 10) inayotanguliwa na ushairi Hakika ya Safari unaosomeka hivi:

Safari hakika ni safari
Moyo wako kuujuburi
Siri uiweke kuwa siri
Kushindwa katu usikukiri.

Ujihimu kila mara
Uongozwe na yako ghera
Lisiwepo la kukukera
Hadi kutimu dhamira.

Hatua yako ya kwanza
Mwisho ni kuimaliza

Nchi yako Maliwaza
Hilo hakika timiza. (uk. 9)

Dhati ya shairi huu inamtia moyo msafiri kwamba aiandame njia hadi awasili katika nchi yake ya Maliwaza. Lakini katika hadithi yenyewe, Bwan’ Said (huyo msafiri wenyewe) anashindwa kuinua mguu hapa na hapo, maana ndoto alizooteshwa na mwandishi zinambainishia kuwa, akutakako kwenda hakwendeki!

Ukiacha mtindo huu wa kuitangulizia kila hadithi kipande cha ushairi, kazi hii inaweza pia kutukuzwa kwa matumizi yake ya lugha na uumbaji wa wahusika. Haitoshi tu kusema kuwa kimetumika Kiswahili fasaha, bali pia kimetumika kama kinavyotakiwa kitumike. Haitoshi tu kusema kuwa muna wahusika wa kila aina, bali pia muna wahusika halisi katika maisha.

Ally Saleh amejitahidi kuteua maneno yake na kumpa kila muhusika lugha, mavazi na vitendo kwa mujibu wa nafasi aliyokusudia kuiwakilisha. Hebu msikilize Vituko, kwa mfano, katika hadithi ya Jumba Maro yenyewe, ambaye mwandishi anasema kuwa, huwa anatumia mwamvuli wake wa ulevi kuwapasha wale wote waliomtenda, wakiwamo waliomkamata, waliomchongea, waliomshitaki na waliomtesa:

“Ati wanasema nimeripua bomu…ati mimi Vituko naweza kulipata bomu. Kama kweli hasa mie…mie Vituko nilipate bomu, basi sipajui kweli pa kwenda kulitupa…nikalitie kwenye kile kibanda cha kufugwa mabata…na…na kuku ambao kwa vyovyote tu watachinjwa…” (uk. 65).

Vituko ni mtu wa vituko kwelikweli. Mtaa mzima huwatukana usiku, asubuhi akawaamkia. Anaishi katika vituko, maana Jumba Maro lenyewe limejaa vituko. Bahati nzuri ni kwamba mimi binafsi niliwahi kuishi jirani ya jumba hilo, katika mtaa wa Mtendeni, Mjini Unguja, na nilikuwa sehemu ya yatokeayo hapo kwa mwaka mzima, takribani miaka 10 iliyopita.

Mfumo wa Vituko wa maisha ni wa vituko vitupu, maana, kwa mfano, siku aliyotolewa jela tu, breki yake ya mwanzo aliifunga kwa muuza pombe, ‘alikopasha’ kabla hajawashukia mtaani. Na anachosema pia ni vituko, lakini huwa kiko fasaha na ujumbe mweupe!

Katika matumizi ya lugha kuna pia utamu wa kuibua picha kutokana na upangaji wa maneno. Kwa mfano, katika hadithi Bwana Uwezo kuna mpangilio huu wa maneno:

“Iko siku anapoamka tu, Bwana Uwezo na kujisikia, basi huuita upepo ofisini kwake. Kimya kimya, ndani kwa ndani. Chemba hiyo ikitoka, limezuka jambo. Upepo ukaonekana unatekeleza amri…Nyumba zikachukuliwa, seuze vibanda. Nguo zikavuliwa seuze kupeperushwa. Watu wakawa nje, wakawa uchi” (uk. 50).

Ujengaji huu wa taswira unatusaidia kutupa mantiki ya uhusika wa akina Bwana Uwezo, Upepo, Jua na Mvua. Ni utiaji chumvi wenye lengo la kuibua maana ndani ya maana. Unaoufanya upepo uwe zaidi ya upepo na jua liwe zaidi ya jua.

Ni bahati mbaya kwamba hatuna muda wa kutosha kuweza kukichambua kila kipengele cha fani katika hadhara hii, lakini itoshe kusema kwamba Jumba Maro ni kazi iliyopikwa ikapikika kifani. Ni kazi inayomfanya msomaji ambaye ni Mswahili aihisi ile fahari ya kuwa Mswahili.

Basi naomba tukomee hapo katika fani na sasa tugeukie kidogo katika maudhui. Kutokana na ukweli kwamba hii si riwaya yenye hadithi moja tu refu, bali mkusanyiko wa hadithi nyingi fupi fupi, basi nitachambua moja tu kati ya hadithi hizi kumi na mbili za Jumba Maro, nikiamini kuwa kwa kufanya hivyo sitakuwa nimemdhulumu mwandishi bali nitakuwa nimeisaidia hadhira kuuona undani wa ‘jumba‘ lote. Hadithi niliyoichagua ni Karamu inayopatikana katika ukurasa wa 90 wa kitabu hiki.

Kama zilivyo nyengine, hadithi hii nayo inaanza na ushairi ulioitwa Mjumbe Kaemewa, ambao unasimulia masaibu yaliyompata mjumbe aliyetumia kalamu yake kuandika mambo ambayo aliamini kuwa ni ya kweli kwa kusudi la kuwafanya watu wake waelewe kile hasa kilichotokea, lakini kumbe hakujuwa kwa kufanya hivyo alikuwa anakosana na wakubwa. Matokeo yake, mjumbe huyu akaadhibiwa kwa kuwekwa jela na ‘kukatwa kidomodomo’ chake.

Kule kwetu Zanzibar kulikuwa na mjumbe kama huyu ambaye naye aliamini kuwa, kwa kuandika ukweli alikuwa anaisaidia jamii yake kufahamu mambo na hivyo kuifanya isimamie ukweli siku zote. Lakini naye pia alikuwa anawakera wakubwa. Matokeo yake yakawa ni yale yale ya mjumbe huyu wa Jumba Maro.

Mjumbe aliyekuwepo Zanzibar alikuwa ni gazeti la Dira, ambalo lilikuwa limejitolea kuandika na kuchambua ukweli kuhusu masuala mbali mbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo yalihusu hatima ya Zanzibar. Lakini hilo halikuwafurahisha mabwana wa Zanzibar, na matokeo yake ni kuwa liliandamwa hadi likafungiwa moja kwa moja, huku wahusika wake wakitangazwa kuwa si raia wa nchi hii.

Hapa nazungumzia Mzee wangu, Ali Nabwa, ambaye amegeuzwa mkimbizi katika nchi ya mababu na mabibi zake. Ni huzuni iliyoje kwamba hata alipokuwa anakiwekea utangulizi kitabu hiki tunachokichambua hapa, alilazimika kusaini kama TX, yaani mfanyakazi kutoka nje ya nchi. Mjumbe kaemewa!

Baada ya ushairi huo kuifungua hadithi, mwandishi ameianza Karamu ya Jumba Maro kwa kitendawili cha kuingia nyoka katika chumba cha Bwan’ Tajir, ambacho kwa namna kilivyojengwa hakukuwa na uwezekano wowote wa kawaida wa nyoka huyo kufika huko. Kuingia kwa nyoka huyu kulimshtua sana Bwan’ Tajir kiasi ya kwamba alimvua kazi nokoa wake mkuu kwa kuwa uchunguzi wa barza aliyoiunda kuchunguza mkasa wenyewe ulibaini kuwa nyoka aliingia kwa uzembe wa nokoa huyo.

Tafrani ya kuingia kwa nyoka katika chumba cha Bwan’ Tajir ndiyo inayotuunganisha na kiini cha hadithi yenyewe. Kwamba sio tu kuwa Bwan’ Tajir alikuwa akimuogopa nyoka huyu binafsi, lakini pia alikuwa amekusudia kupika karamu kubwa na kuwaalika watu wazima wote wa mji kuja kula kwake, katika kasri lake.

Kujitokeza kwa habari hii, kwa hivyo, kungelisababisha watu wengi kusita kuja katika karamu hiyo kwa kuhofia usalama wao, kwa upande mmoja, na pia kuwapa picha halisi kwamba naye Bwan’ Tajir ni mwoga na kwamba kwake kunapenyeka, kwa upande mwengine. Na fahari ya Bwan’ Tajir ni “kuwa watu wote kabisa washiriki katika karamu yake, wale wanywe fadhila zake” (uk. 92), bila ya kuushuku woga wake na ugoigoi wa himaya yake.

Mwandishi anatuonesha kuwa, hata hivyo, Bwan’ Tajir si mtu wa fadhila kiasi hicho. Hana ukarimu jambo. Kupitia nong’ono za watu, tunajifunza kuwa huyu ni mtu bakhili na mwenye tabia ya uchoyo mno kiasi ya kwamba hutia ndizi na dagaa katika mifuko yake ya suruali kuepuka asiombwe. Suali ambalo watu walikuwa wakijiuliza ni vipi angeliweza kuwakirimu watu wa mji mzima?

Hatimaye karamu inapikwa na kuliwa, lakini, kama ilivyohofiwa tangu mwanzo, ilikuwa na mapungufu kibao kiasi ya kwamba haikuwa halali hata kidogo kuuita kuwa ilikuwa ‘karamu ya mji’. Kwamba wengi wa watu ni wale waliokosa hata tonge moja ya biriani huku wachache wakiwa wamekula zaidi ya sahani moja. Na hata hao waliopata kula hiyo karamu, wengi wao ni watoto na sio watu wazima wa mji kama ilivyokuwa imeahidiwa tangu mwanzo.

Hao watu wazima waliokoseshwa, walikuwa wamekoseshwa katika mazingira ya kutatanisha na kusikitisha kabisa. Kwa mfano, mwandishi anatwambia kuwa kuna wengi waliokataliwa kuingia katika ukumbi wa dhifa kwa kuwa bawabu hakuzitambua kadi zao za mwaliko. Ati zilikuwa na rangi tafauti na kadi alizoagizwa kupokea.

Kuna wengine walikuwa na kadi zenye rangi ndizo, lakini walikataliwa kuingia kwa kuwa herufi za majina yao ni tafauti na wanavyoyatamka. Katika ukurasa wa 93, bawabu anamuuliza mwenye kadi:

“Mbona umeniambia jina lako Ahmed na humu limeandikwa Ahmad?”

Mwenye kadi anajitetea kuwa si yeye aliyeandika kadi hiyo, bali ni karani wa Bwan’ Tajir. Anasema kwamba hata yeye alimuambia na mapema karani huyo juu ya ukosewaji huo wa herufi moja kwenye jina lake, lakini karani akawa amemuhakikishia Ahmed kuwa pasingelikuwa na tabu yoyote ile: siku ya karamu, angelikula tu.

Lakini leo hii bawabu anamwambia Ahmed: “…hutaramba karamu….saa ya kutazama makosa imekwisha. Kazi yangu ni kutazama kadi sahihi. Asiyekuwa nayo haingii”. Na kweli Ahmed, na wenziwe wa mfano wake, hawakuruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa karamu.

Kwa hali hii watu wazima wengi wa mji wakakosa kula karamu iliyoandaliwa na Bwan’ Tajir kwa ajili yao. Ilikuwa imeonekana kana kwamba huu ulikuwa ni mpango uliofanywa makusudi na Bwan’ Tajir na wasaidizi wake, maana hata watu hawa walipolalamika kuwa wamekoseshwa karamu, hakuna mwenye mamlaka aliyewasikiliza. Hata Shawishi Mkuu, ambaye ndiye aliyekabidhiwa jukumu la uandazi, alipoambiwa kuhusu hilo, alipinga kwamba haiwezekani kuwe na watu waliokosa chakula ilhali biriani ilikuwa ya ‘kupigia mbwa’ huko ndani.

Watu walipomuapia kuwa wao hawajaramba kitu, aliwanuka viganja vyao. Alipoona ni kweli havinukii harufu yoyote ya machopochopo, akawaruka hapo hapo:

“Waongo hawa. Wamekula kisha wakaenda kunawa na wanataka kudanganya kula mara mbili”. (uk. 94).

Masikini watu wazima wale, wakasawijika kwa kuambiwa kuwa wanazua ili wajilie mara mbili ilhali hata hiyo moja hawakuipata. Hivi ndivyo karamu ya Bwan’ Tajir ilivyoishia.

Nimetangulia kusema kuwa dhima ya mchambuzi/mhakiki wa kazi ya fasihi ni kuirejesha kazi ‘watuni’, yaani kuisaidia jamii kujisoma baina ya mistari ya msanii. Na hili ndilo nitalolifanya sasa kwa kuwasaidia wenzangu kujiona walivyo kupitia mistari hii michache ya Ally Saleh katika Karamu.

Natokea Zanzibar kama alivyo mwandishi wa Jumba Maro na ni maoni yangu kwamba Karamu hii aliyoiwasilisha Ally Saleh inaakisi moja kwa moja chaguzi zetu katika mfumo wa vyama vingi.

Ninaamini pana mfanano mkubwa baina ya maandalizi, uendeshaji na matokeo ya chaguzi zetu ndani ya mfumo huu wa vyama vingi na karamu hii ya Bwan’ Tajir (ambaye kwa tafsiri yangu ni serikali ya chama tawala).

Ule mkasa wa kuingia kwa nyoka katika chumba cha Bwan’ Tajir naufananisha na kuja kwa siasa za vyama vingi katika nchi, ambazo zilijipenyeza bila ya ridhaa ya watawala. Siku zote watawala wamekuwa wakiogopa kuwa upinzani unahatarisha maslahi yao, kama vile Bwan’ Tajir anavyoogopa kuwa nyoka angelimfichulia aibu zake za woga na ugoigoi.

Kupitia mdomo wa Bwan’ Tajir, serikali ya chama tawala inamkaripia mtu inayedhani kuwa amechangia kurudi kwa vyama vingi:

“Usiniambie mie habari ya (nyoka) kutoka wapi…mie nilikwambia naogopa nyoka. Nilikukabidhi kazi ya kuhakikisha nyoka sio tu hawaonekani, lakini pia wasikaribie nilipo”. (Uk. 91)

Ukweli ni kuwa, laiti serikali ya chama tawala ingelikuwa na uwezo wa kuzuia vyama vingi visije, ingelifanya hivyo. Lakini kilichotokea ni kuwa wakati ulikuwa umeshafika, na hakuna ambaye angelikinzana na matakwa ya wakati, kama vile anavyosema Nokoa Mkuu, ambaye alituhumiwa na kuhukumiwa kwa kumruhusu nyoka kupita hadi chumbani kwa Bwan’ Tajir, kwamba: “Sina uwezo wa kuzuia kudra”. (uk. 91)

Wasemavyo wamalenga: “Muda na kudura hazina zisubirio,” ndivyo ambavyo wakati ulivyolazimisha kuja kwa vyama vingi hata kama wakubwa walikuwa hawavitaki. Kwa hivyo, nyoka (siasa za vyama vingi) hakuweza kuzuilika kuingia katika chumba cha Bwan’ Tajir (nchini). Watawala na mawakala wao katika vyombo vya habari, vyombo vya dola, taasisi za kijamii na kwengineko, hawakuwa na uwezo wa kuvizuia vyama vingi visirudi Tanzania, kwa kuwa hayo yalikuwa ni matakwa ya wakati.

Lakini ikiwa walishindwa na hicho, kuna chengine ambacho waliweza kukifanya, nacho ni kuandaa mikakati na mbinu za kuvizuia vyama hivi kuwaondoa wao madarakani. Na karamu (chaguzi) za magube na varange ndiyo ikawa njia ya wao kujihalalishia kuendelea kubakia madarakani huku wakiudanganya ulimwengu kuwa na wao wana demokrasia ya vyama vingi.

Ndivyo karamu ilivyoandaliwa katika Jumba Maro. Bwan’ Tajir alimtafuta Shawishi Mkuu kuwa muandaaji na mpishi wake. Shawishi huyu akawa na jukumu moja tu: kwa upande mmoja, kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wenye haki ya kula karamu hiyo hawapati fursa na, kwa upande mwengine, wale wasio na haki hiyo, lakini ambao kula kwao kutakuwa kwa faida ya Bwan’ Tajir, wanaila kwa matonge na hata kwa ‘kufuta’ sinia mbili mbili. Kwa ufupi, Shawishi Mkuu alikuwa na dhima ya kuifuja karamu.

Ndivyo ilivyo katika uhalisia. Kwamba katika kuandaa mazingira ya kuendelea kubakia madarakani, watawala waliwatafuta akina mashawishi wakuu na kuwafanya wawe na mamlaka ya kuandaa na kusimamia chaguzi ziitwazo za vyama vingi. Kwa maana nyengine ni kuwa watawala walijiundia mtandao utakaohakikishia uwepo wao madarakani dumu daima, hata pale umma (watu wazima wa mji) utakapokuwa umeshawakataa.

Hiki ndicho kilichofanyika Zanzibar, kwa mfano, ambapo mtandao madhubuti wa masheha, vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi, ulihakikisha kuwa Wazanzibari wengi wenye haki ya kupiga kura hawaandikishwi kuwa wapiga kura, kwa upande mmoja na, kwa upande mwengine, wale wasiokuwa na sifa, lakini ambao watatumiwa kukipigia kura chama tawala wanaandikishwa ikibidi hata zaidi ya mara moja. (Rejea ripoti ya TEMCO/REDET: The Politics of the PVR, 2005).

Mkasa wa Karamu ya Jumba Maro kuliwa na watoto wadogo huku watu wazima wakitazama macho tu, ndio mkasa wa kura za Donge zilizoambiwa zimemchagua Ali Juma Shamhuna kupigwa na watu wasiotimia umri huku wale waliokwishatimia wakilia machozi.

Mkasa wa watu wachache kula sahani mbili mbili za biriani huku wengine wakienda miayo kwa njaa, ndiyo mkasa wa upigaji kura zaidi ya mara moja katika maeneo kadhaa ya Zanzibar, huku zaidi ya Wazanzibari 13,000 wakiwa wamepingwa na masheha kuwa wapiga kura. (Pitia ripoti ya National Democracy Institute-NDI).

Mkasa wa akina Ahmed kukataliwa kuingia kwenye chumba cha karamu kwa kuwa kadi zao zimeandikwa Ahmad, ndio mkasa wa Wazanzibari waliojikuta ama majina yao yameshapigiwa kura au wanaambiwa hawamo katika orodha ya wapiga kura katika siku yenyewe ya kupiga kura. (Rejea makala za Christian Science Monitor) .

Kwa hivyo, kwa kila hali, karamu ya Jumba Maro inafanana sana na chaguzi zetu ziitwazo za kidemokrasia. Ni njia ya akina Bwan’ Tajir kuutangazia ulimwengu kuwa na wao wana ukarimu wa kutosha wa kualika watu kuja kula katika makasri yao, lakini kumbe hawana uhodari huo. Kutoa na kujitolea kwataka moyo, na moyo huo akina Bwan’ Tajir (watawala wetu) hawanao.

Watawala wetu, kama alivyo Bwan’ Tajir, huomba pesa za kugharamikia chaguzi kutoka kwa wafadhili ati kuwapa fursa raia kuweka madarakani viongozi wawatakao, lakini kwa hakika huwa ni kwa kujionesha tu. Katika vyembe vya nafsi zao, huwa wameshajiwekea kabisa, kwamba hawataondoka madarakani kwa vyovyote vile, ikibidi hata kwa kutumia mtutu wa bunduki ili waendelee kusalia pale walipo. Hufanya mbinu, visa na mikasa, alimradi tu utimu muradi wao. Ndio maana hunukuliwa wakisema kuwa mapanga na mashoka ya 1964 bado yangalipo.

Ya Zanzibar na ya Jumba Maro ni mama mmoja, baba mmoja.

Mohammed Ghassani,
Dar es Salaam,
02 Disemba 2005