UCHAMBUZI

Tume ya ‘Zitto’ ni kupapasa au kupotea njia?

Na Mohammed Ghassani

Baada ya kufuatilia taarifa na chambuzi mbali mbali kwenye vyombo vyetu vya habari kuhusiana na tendo la Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya kuangalia matatizo yaliyomo kwenye sekta ya madini na kumteua mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zuberi Zitto Kabwe, kuwa mjumbe wa kamati hiyo, nimegundua kuwa kuna angalau nadharia nne za kulielezea suala hili. Nitazielezea moja baada ya nyengine na kuonesha ile ambayo mimi ninasimamia.

Nadharia ya kwanza ni kwamba Kikwete ameunda tume hiyo kwa dhamira ya kurekebisha mapungufu makubwa yaliyomo kwenye sheria za madini. Hili lilikuwamo kwenye ahadi zake za mwanzoni kabisa alipoingia madarakani. Hata msingi wa hoja ya Zitto siku zile alipokuwa akitaka mkataba wa Buzwagi uliosainiwa na Nazir Karamagi uchunguzwe, ilitokana na hofu yake kuwa umesainiwa bila ya kuzingatia na ahadi hiyo ya Rais Kikwete.

Wenye nadharia hii wanamuona Kikwete kama shujaa kwa sababu zaidi ya moja. Kwanza, anaunda tume kuchunguza matatizo yaliyomo kwenye sekta ambayo ilishatajwa na kambi ya upinzani Bungeni kwamba imeoza. Bunge lenyewe likakataa kufanya kufanya chochote dhidi ya hilo, na badala yake Zitto aliyewasilisha ombi la kuundwa kwa tume kuuchunguza mkataba wa Buzwagi, sio tu kwamba alikataliwa, bali baya zaidi ni kuwa ‘aligeuziwa’ kibao na Bunge hilo na kutiwa hatiani.

Sasa, katika wakati ambao Zitto huyo huyo anamalizia adhabu aliyopewa na Bunge kwa kuomba tu kuundwa kwa tume, Rais wa nchi anamteua kuingia kwenye tume ambayo ‘aliililia’ iundwe. Tulioliangalia tukio lile la kuadhibiwa kwa Zitto katika kikao cha bajeti kilichopita, tunakumbuka kauli yake ya mwisho: “Unaweza kumuua mtu, bali huwezi kuua fikra.” Rais Kikwete amemsaidia Zitto, kwa hivyo, kuthibitisha kwamba fikra zake zilikuwa sahihi, na huko ni kumsaidia shujaa, ambako kwenyewe ni ushujaa; nadharia hiyo inasema.

Pia ushujaa wa Rais Kikwete hapa unaonekana kwa sura ya kuthubutu kutofautiana na vyombo vikuu ambavyo yeye ni sehemu yake. Hapa inakusudiwa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) na Baraza lake la Mawaziri. Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kuwa adhabu dhidi ya Zitto ilitolewa kwa kuzingatia chochote kilicho tafauti na utamaduni wa kulindana na kukomoana uliojengeka ndani ya CCM na serikali.

Kwa nadharia hii, japokuwa ndiye mwenyekiti wa CCM na mkuu wa Baraza la Mawaziri, Kikwete amejipapatua kutoka kundi la watu wa chama na serikali yake wenye fikra ndogo (ambao hawawezi kufikiri nje ya boksi lao), na kuwaonesha kuwa wamekosea. Kwa maneno machache ni kwamba, Kikwete amechukua nafasi kama kiongozi wa Taifa kutoa muongozo kwa mambo tata, ndio maana hata baada ya Bunge linalomilikiwa na chama chake kukosea, yeye amelisuta kiaina.

Hapa nataasafu kusema kwamba, kama Zitto aliadhibiwa kwa kumdhalilisha Karamagi, basi Kikwete amelidhalilisha Bunge zima. Amelitoa maana na kuliona halifai. Hii ndiyo tafsiri nyepesi ya kitendo chake cha kuunda tume na kumteua Zitto kwenye tume hiyo. Kwamba kama Bunge liliziona hoja za Zitto nyepesi na za kisiasa tu, yeye ameziona nzito na zenye mashiko!

Lakini nadharia hii ina tatizo ambalo linasababisha kuibuka nadharia nyengine, nalo ni suala la wakati. Kwamba kama kweli dhamira ya Rais Kikwete ni njema katika suala hili, kwa nini amesubiri hadi leo kuchukua hatua alizochukua. Inakumbukwa kwamba hatua hii ya sasa imekuja siku za mwisho mwisho kabisa za adhabu ya Zitto aliyopewa na Bunge. Imekuja baada ya viongozi kadhaa wa serikali na chama chake kujitokeza hadharani kutetea kila kitu walichomfanyia Zitto kule Bungeni, ikiwa ni pamoja na kuitetea mikataba ya madini, ukiwemo huo wa Buzwagi. Bali itakumbukwa zaidi kwamba hata yeye mwenyewe, Rais Kikwete, amekuwa akionesha kuilinda serikali yake na msimamo wa Bunge katika hili. Sasa, kwa nini sasa?

Jibu la swali hilo ni hii nadharia ya pili inayosema kuwa Rais Kikwete ameunda tume hii kuitikia shinikizo la nchi wafadhili, ambao kwa kipindi cha karibuni wamekuwa wazi sana panapohusika msimamo wao kwa serikali yake. La matatizo yaliyomo kwenye sekta ya madini ni miongoni tu mwa mambo yanayowatatiza. Kwa hivyo, Kikwete anachukua hatua sasa, na si wakati ule, kwa kuwa hadi pale wafadhili hawakuwa wameshinikiza lolote.

Hili, kwa hivyo, linaivunja nadharia ya ushujaa na dhamira njema. Haikuwa dhamira njema, maana imesukumwa na shinikizo la wanaotufadhili, vyenginevyo hakikuwa kitu kilichomo kwenye nafsi. Inawezekana kwamba, kama wafadhili hawakushinikiza, hakuna siku Rais Kikwete angelikumbuka kutimiza ahadi yake ya kuishughulikia mikataba ya madini. Angelijisahaulisha mpaka akaondoka madarakani, kama ambavyo mwenzake Benjamin Mkapa alijisahaulisha kutatua kero za Muungano.

Nadharia ya shinikizo pia inawajumuisha wapinzani, kwamba tume hii imeundwa kwa ‘kelele’ zao ili kuwanyamazisha. Kwamba Zitto, kijana machachari kutoka kambi hiyo yumo, ni hizo jitihada tu za kuwanyamazisha, maana baada ya yote tume hiyo itatoa taarifa ambayo hata kama Zitto hataikubali, hatakuwa na jinsi ya kujitenga nayo.

Tuna mfano hai Zanzibar, ambapo katika Tume ya Uchaguzi (ZEC), kuna wajumbe wawili kutoka chama cha upinzani, yaani CUF. Mara zote ZEC ilipokuwa ikifanya maamuzi makubwa na yenye gharama kwa taifa, wajumbe hao walipinga, lakini upinzani wao haukuzuia maamuzi hayo kufikiwa. Miongoni mwao ni ile kesi ya kuwazuilia wagombea wa CUF kutogombea kwenye uchaguzi mdogo wa Pemba wa 2003 (maarufu kama Uchaguzi wa Maruhani) na kugawa upya majimbo ya uchaguzi ya Zanzibar.

Leo hii, tukifanya marejeo ya mwenendo wa uchaguzi, bila ya shaka rejea kubwa ni ZEC yenyewe ambayo kimsingi ni tume iliyoundwa na wajumbe kutoka pande zote mbili zinazovutana kisiasa Zanzibar, yaani CCM na CUF. Wafadhili wanamwaga mapesa kwenye tume hiyo, maana msingi wa sheria za nchi unaitambua kuwa iko hivyo na wao hawawezi kufanya kinyume chake.

Lakini sote tunajuwa kuwa wale wajumbe wawili wa CUF hawakuwa na nguvu wala uwezo wa kubadilisha chochote kile na badala yake kuwepo kwao kwenye tume kulitumika kuhalalisha matendo yote ya ZEC kwa jina la tume huru. Kwamba, kitaasisi huwezi kuwa sehemu ya tume fulani inayokulipa mshahara wake, halafu ukajitenga na maamuzi yake. Hilo haliwezi kufahamika, kitaratibu. Ama uwemo na uwe sehemu yake, au usiwemo kabisa. Akina Zitto, kwa hivyo, wameitwa kwenye tume ili kwenda ‘kuisaifisha’ mikataba ya madini na sio kwenda kuichunguza, kama vile ambavyo akina Nassor Seif waliitwa kwenye ZEC kwenda kuhalalisha na sio kusimamia uchaguzi wa Zanzibar.

Bado kuna nadharia nyengine ya tatu, kwamba Rais Kikwete anakusudia kuunyamazisha upinzani. Kwa mujibu wa nadharia hii, Rais Kikwete hana dhamira hasa ya kulishughulikia tatizo lililomo kwenye sekta ya madini, bali ana dhamira kubwa ya kumshughulikia Zitto au watu wa aina yake. Kwamba Kikwete hawezi kusahau jukumu lake la kuilinda serikali na chama chake kwa gharama yoyote ile, na kwamba kama alivyowahi kusema Mbunge wa Mtera na Makamo Mwenyekiti wa CCM Bara aliyemaliza muda wake, John Malecela, akina “Zito ni jipu….na mdharau jipu, mguu huota tende.” Kwa hivyo, kumleta Zitto karibu ya tume zenye ulaji kama hizi ni kumtia kwenye mtihani, ambao mwisho wa siku ataufeli na kumuua kabisa kisiasa.

Nadharia hii ina mifano katika historia ya siasa za vyama vingi tangu zianze tena 1992. Tanzania inawakumbuka vijana machachari na wasomi wakubwa kuliko hata Zitto lakini ambao hivi sasa aidha wameshamezwa na ‘mfumo’ waliokuwa wakiupinga kwa nguvu zao zote au ‘wameshapigwa na chini’ baada ya kutumiliwa na ‘mfumo’ huo.

Kwenye orodha hiyo, wamo akina Dk. Masumbuko Lamwai, Dk. Walid Kabourou na Salim Msabah. Nadharia hii inamuona Zitto mwenyewe kuwa si mzito sana kuweza kuvinyanyua juu vishawishi vya ‘mfumo’ kwenye mizani. Inaonekana jamaa wa Intelligence wamecheza karata yao katika namna ambayo wanadhani kwamba ile ile ndoana iliyowanasa akina Lamwai, Kabourou na Msabah, inaweza kubadilishwa chambo na kumnasa Zitto, kisha wakampelekea Rais Kikwete ‘package’ yenyewe.

Sina ubishani sana na nadharia hiyo, maana nimekulia katika mazingira yanayonieleza nguvu za mfumo zilivyo. Lakini pia nina imani kwamba Zitto ni mtu makini sana kuweza kuyumbishwa na ahadi za vinoo vya dhahabu, wanawake warembo, akaunti ya dola milioni moja, ubalozi au hata vitisho dhidi yake na familia. Nikiwa kama kijana wa umri wake, namuonea fahari na najigambia yeye, na naamini hatoniangusha. Hiyo, hata hivyo, ni imani tu. Kuthibitika kwake kunahitaji matendo ambayo si yeyote mwengine, isipokuwa Zitto mwenyewe, atakayeyasimamisha.

Lakini mimi nasimamia nadharia ya nne, kwamba Rais Kikwete anapapasa tu, kubahatisha kitu cha kumtoa kutoka rundo la kashfa linaloiandama serikali yake. Siutenganishi uundaji wa tume hii na lile wingu la tuhuma za ufisadi lilioitanda serikali yake kwa siku nyingi sasa. Wingu hili, bila ya shaka, liliibuliwa na wapinzani na mkasa wa kufukuzwa kwa Zitto Bungeni ukaongeza tu uzito wa jambo lenyewe.

Tangu hapo, Rais Kikwete hajawahi kukaa kitako, ingawa ilikuwa tumefanywa tuamini kwamba amekuwa mtulivu akisubiri kuchukuwa hatua muafaka kwa wakati sahihi. Ukweli ni kuwa amejikuta na dhima ya kufanya ‘kitu fulani,’ chochote tu, ambacho kinaweza kulilainisha suala lenyewe zima na ikibidi hata kupindisha hoja na makini ya wananchi katika kadhia hii. Naye amekuwa akikifanya kitu hicho.

Kwa mfano, mwanzoni alikuwa amejaribu kuwatumia watendaji wake serikalini, kama akina Kingunge-Ngombale Mwiru, Mohammed Seif Khatib na Benard Membe, kwa namna moja ama nyengine, kufanya kitu cha kupunguza makali. Ulikuwa ni upumbavu kuamini kuwa mawaziri hao walikurupuka tu kujibu tuhuma za ufisadi bila ya kushauriana na serikali nzima, bila ya Kikwete kuhusika! Kama majibu yao yalikuwa hayatoshi, ni kwa kuwa majibu ya Kikwete mwenyewe hayakutosha.

Nje ya serikali, akina Jaji Mark Bomani na Jaji Joseph Warioba nao wakafanya kitu cha kupunguza makali. Hata hawa nao, kuna kitu nyuma ya ubongo wangu kinaniambia kuwa walikuwa wamepangwa. Siamini kwamba walizungumza kama wao, nje ya mfumo. Bahati mbaya nao wakabwagwa kitakotako.

Wakati huo huo baraza lake zima la mawaziri likajimwaga mikoani kufanya kitu cha kujinasua matopeni. Hata yeye mwenyewe, aliporudi safari zake za Marekani akaamua kutumia sherehe za kuzima mwenge wa uhuru huko Arusha kusema kitu cha kuzima moto wa ufisadi pia. Alipoona yote hayo hayafai, akazungumza Rome, Italia, kutisha kuwa sasa atachukuwa hatua za ziada dhidi ya watoa tuhuma za ufisadi.

Alimradi Rais Kikwete alikuwa anachacharika, akishika hiki na kile kutaka kuzima moto. Ile taswira anayojidhihirisha kwetu kwamba ni mtu aliyetulia sana katika kufanya maamuzi, mimi siiamini. Naamini, badala yake, kwamba ni mchakarikaji kweli anapopatwa na jambo linalomkera. Hakai kitako, hali wala hanywi mpaka ajuwe kuwa limefikia mfundo. Na hili limemuhangaisha sana nab ado linazidi kumuhangaisha Rais Kikwete.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.