UCHAMBUZI

Bila ya nguvu za dola na vurugu, CCM wepesi

Naandika makala hii refu baada ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, kujitokeza wiki mbii zilizopita kuwaasa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hasa wenyekiti Freeman Mbowe na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, kwamba wachunge kauli zao maana zinaweza kuwaweka pabaya kwa vile zina muelekeo wa kuvunja amani. Amani na utulivu ni misamiati ya kijanja inayotumika na Chama cha Mapinduzi (CCM) na mawakala wake kujijengea taswira kwamba wao ni watu wastaarabu, ilhali ni kinyume chake. Naamini naye DCI Manumba amezungumza zaidi kisiasa kuliko ‘kiulinzi’.

Mimi ni muumini wa kile kinachoitwa non-violence politics, yaani siasa zilizojengwa juu ya msingi kwamba ushindi wa kweli hupatikana kwa kutumia njia za amani. Lakini hapa nahoji kwamba hizo fujo na vurugu anazozizungumzia DCI Manumba ndiyo staili ya utawala ya CCM na serikali zake na kwamba kamwe wapinzani (wawe CHADEMA, CUF au wengineo) hawezi kuwa wazuri hata kidogo katika uwanja huo, hata wakijaribu vipi! Laiti anafanya kweli kazi ya ulinzi, basi Manumba naanze kuzifanyia kazi vurugu na fujo za CCM na pa kuanzia ni hapa kwenye ushahidi wa makala hii.

Asianze na kuwashukia watu wa vyama vya upinzani, maana hawa hawajawahi hata siku moja kujaribu kutumia fujo na vurugu katika kuendesha siasa za nchi hii, na nachelea kwamba siku watakapozijaribu, ndiyo siku ambayo CCM itakuwa imemaliza kazi yake inayotamani sana kuikamilisha, yaani ile ya kuua kabisa upinzani wa kisiasa dhidi yake. Changamoto kwa wapinzani ni kushikilia nafasi waliyonayo sasa na kusonga mbele kuelekea ushindi wa kweli wa umma kwa njia za amani.

Katika kufafanua hoja kwamba CCM inategemea fujo na vurugu kubakia madarakani, tufahamishane kidogo dhana yenyewe ya fujo kwa kuilinganisha pia na dhana za amani na nguvu, maana dhana hizo tatu ni muhimu katika muktadha wa siasa zozote. Tujiuilize, kwa mfano, ni nini fujo, kuna aina ngapi za fujo, ni zipi athari zake, nani anayezisababisha na, mwisho, kwa nini fujo hutumika?

Kwa maneno machache, fujo ni uwepo wa vurugu na ukosefu wa amani. Kimkakati, huu ni utumiaji wa vurugu katika kufikia lengo. Waingereza wanatumia neno violence ambalo linawakilisha dhana pana inayojumuisha kila kile ambacho ungelikiita kiovu. Zenyewe ziko za aina mbili: fujo iliyojificha na fujo ya wazi. Mifano ya fujo zilizojificha ni kama vile ukosefu wa usawa na uadilifu, uwepo wa dhuluma, ubaguzi na ukandamizaji, umasikini na ufisadi. Mifano ya fujo za wazi ni kama vile vita, uripuaji wa mabomu, matukio ya kigaidi, mauaji, na umwagaji damu. Hii ni kusema kwamba baina ya fujo hizi mbili, kiviwango, basi fujo iliyojificha ndiyo kuu zaidi. Kwa hivyo ni sawa kusema kusema kwamba kuna fujo kubwa (zilizojificha) na fujo ndogo (za wazi).

Athari za fujo ni nyingi, kutegemea na aina ya fujo inayohusika. Ulimwengu umekuwa ukishuhudia kila siku maafa yanayotokana na utumiaji wa fujo, kama vile vifo vya raia wasiokuwa na hatia, wakimbizi, kuongezeka kwa umaskini, kupotea kwa heshima ya watu na mataifa na chuki na visasi.

Kitu cha kuzingatia hapa, hata hivyo, ni ukweli kuwa kila fujo ina msababishaji wake na ni rahisi kumjuwa. Tuje kwenye muktadha wa Tanzania kumgundua msababishaji fujo katika nchi hii. Fikiria kichwani mwako tukio lolote ulilowahi kuliona kupitia chombo cha habari (gazeti, televisheni, mtandao) hapa nchini na ambalo wewe ulilitafsiri kuwa ni fujo. Kibaka anaungua moto? Mapigano ndani ya familia? Majeruhi na au maiti za waandamanaji wa Januari 2001? Chochote tu!

Sasa rudi nyuma kidogo na fikiria kile kilichopelekea kutokea kwa tukio hilo. Kwa mfano, chukulia hizo picha ya majeruhi na maiti za waandamanaji kama kigezo. Huenda ukagundua kuwa waandamanaji hawa walipigwa risasi za moto na vyombo vya dola wakati wakiwa kwenye maandamano, baada ya kukaidi amri ya dola ya kutokuandamana.

Kisha rudi tena nyuma kidogo na jiulize kwa nini waandamanaji hawa waliandamana? Unaweza kupata jibu kuwa waliandamana kupinga hatua ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mshindi mgombea uraisi ambaye, kwa mtazamo wa waandamanaji, hakushinda, kwa hivyo walitaka mshindi halisi atangazwe haraka. Kwa hivyo, nyuma ya picha ile ya majeruhi na maiti ulioiona kwenye chombo cha habari, kuna ‘ukosefu wa uadilifu’ uliofanywa na Tume ya Uchaguzi. Ukosefu wa uadilifu, kama ulivyoona hapo juu, ni katika mifano ya fujo kuu zilizojificha.

Kwa ufupi ni kuwa, nyuma ya kila fujo ya wazi, kuna fujo iliyojificha. Fujo za wazi ni matokeo tu ya fujo hizo zilizojificha. Bila ya kuwepo kwa fujo zilizojificha, hakuna uwezekano wowote wa kutokea kwa fujo za wazi. Katika mfano wa hapo juu, kama Tume ya Uchaguzi ingelikuwa adilifu, basi ingelimtangaza mshindi halali na, kwa hivyo, raia wasingeliandamana na, kwa hivyo, wasingelikabiliana na vyombo vya dola na, kwa hivyo, wasingelijeruhiwa wala kuuliwa na, hatimaye, wewe usingeliiona ile picha ya majeruhi na maiti katika chombo chochote cha habari!

Ufafanuzi wa hapo juu unawaonesha wahusika wa fujo ya wazi (mauaji ya waandamanaji) kuwa ni vyombo vya dola na wahusika wa fujo iliyojificha (ukosefu wa uadilifu) ni Tume ya Uchaguzi. Waandamanaji wenyewe wanajikuta hapa wakiwa ni wahanga tu wa fujo hizo. Ukweli ni kuwa chini ya utawala wa CCM, raia wamejikuta wakiwa wahanga wa fujo zilizoratibiwa, kuendeshwa na kusimamiwa na watawala.

Maana hata katika mfano huu, bado kuna ukweli mwengine uliojificha: kwamba hata nyuma ya fujo hii (ukosefu wa uadilifu) ya Tume ya Uchaguzi, kunaweza kuwepo fujo nyengine pia. Kwa mfano, inawezekana kabisa kuwa Tume ya Uchaguzi ilikosa uadilifu kwa kuwa watendaji wake wakuu wake walihongwa pesa nyingi na mgombea wa chama tawala ili wamtangaze mshindi. Nao watendaji hao walikubali kuhongeka kwa kuwa walikuwa ni maskini, woga na au wana ujinga. Watendaji walikuwa maskini, woga na wajinga kwa kuwa mfumo mzima wa uendeshaji nchi umekuwa ukiwatayarisha watu kuwa wajinga na maskini.

Kwa hivyo basi, mfumo wa uendeshaji nchi ndio kiini cha fujo zilizo wazi na zilizojificha. Wanaoendesha nchi ni watawala na mawakala wao (vyombo vya dola, mahkama, bunge, usalama wa taifa na mataifa yanayowaunga mkono watawala hao kwa maslahi yao). Na basi, mwisho wa yote, utakuta kuwa kiuhalisia, hapa tunazungumzia CCM kama watawala na waliobakia kama mawakala wake, kwamba ndio wasababishaji wa fujo. Mfano wa karibuni wa Bunge kumsimamisha Zitto Kabwe ni katika fujo hizo, ambazo zinapokuwa zimezoeleka kama ilivyo petu, basi huwa ‘zimehalalishwa’ kwa kutumia kanuni, sheria na hata kulindwa na katiba.

Ninachokusudia hasa kusema ni kuwa kwa kipindi chote cha uhai wake ndani ya mfumo wa vyama vingi, CCM imekuwa ikitawala kwa kutumia mfumo unaolea na kuendeleza fujo. Fujo, kwa CCM, ni msamiati unaofahamika vyema, maana ndiyo mkakati ambao imekuwa ikiutumia kutawala. Ni bahati mbaya inajificha nyuma ya kaulimbiu ya ‘amani na utulivu’ na baadhi ya watu wamezugwa mno kuweza kuung’amua unafiki huu.

Tangu kurudi kwa mfumo wa vyama vingi, CCM imejenga mduara wa papo kwa papo wa fujo na vurugu (vacious circle of violence). Kwa mfano, Zanzibar kuna kundi maarufu la Janjaweed ambalo hata kama Serikali ya Mapinduzi (SMZ) iliyo chini ya CCM inalikana, ni siri iliyo wazi kwamba limeundwa na linaratibiwa nao. Hiyo ni fujo. Katika mkasa mmoja wakati wa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, Janjaweed walivamia eneo la Kinuni, Magharibi ya Unguja, wakawapiga na kuwatesa wakaazi wa huko kusudi wasijitokeze kujiandikisha. Hiyo ni fujo. Wakaazi walipokakamaa kupambana nao, polisi ikaja kuwakamata na kuwapiga wakaazi hao. Hiyo ni fujo. Viongozi wa CUF walipolisema hilo kwenye mikutano ya hadhara na kuwataka wananchi wajihami wenyewe kwani polisi imeshindwa kuwalinda, SMZ ikawa inasema CUF inachochea vurugu na viongozi hao wakaitwa kuhojiwa na polisi. Huu ndio mduara wa papo kwa papo wa vurugu na fujo na hivyo ndivyo CCM inavyofanya kazi.

Lakini kwa nini CCM inaamini na kutumia fujo na vurugu? Ni kwa kuwa haijiamini kuwa inaweza kuishi nje ya wigo huo. Fujo ni njia ya mwoga kuhakikisha uwepo wake na CCM ni woga kweli kweli. Woga wa CCM unatokana na kushindwa kwake kuwatumikia raia wa nchi hii kama vile ambavyo imekuwa ikiahidi. CCM imekuwa chama cha viongozi wanaopigania madaraka kwa gharama yoyote ile ili wapate wasaa wa kujinufaisha wao, familia zao, marafiki na mawakala wao. CCM imeusaliti umma wa Watanzania na inaijuwa nafasi yake katika vichwa vya wapiga kura walio wengi wa nchi hii. Kwamba umma umepoteza imani kwayo na unataka mabadiliko.

Wapinzani wako tafauti: hawana woga ilionao CCM. Wanajiamini kiwango ambacho CCM haiwezi. Hawajawahi kushika madaraka wakaboronga, kwa hivyo wana satwa ya kuongea na kusikilizwa na umma. Hao wachache waliowahi kuwa sehemu ya CCM hapo zamani, waliondoka huko wakiwa na rikodi nzuri mbele ya macho ya umma na, kwa hivyo, hawana sababu ya kutumia njia mbovu ili kuungwa mkono na umma huo.

Wito wangu ni kwamba waendelee na tabia hiyo ya kutumia njia za amani na kamwe wasije wakaangukia katika mtego wa fujo na vurugu, maana watapoteza kila kitu. Wanaweza wakajidhani wanachelewa, kwani sasa zimepita chaguzi tatu (1995, 2000 na 2005) na bado vyama hivyo vya upinzani vimekuwa vikitumia njia zile zile za amani kudai haki yao na havijafanikiwa. Hiyo ni hata baada ya kuwepo kwa matukio ambayo yanaonesha wazi kwamba vyama hivyo vinakubakika na wapiga kura (angalau kwa kigezo cha chaguzi za Zanzibar). Hiyo ni hata baada ya matukio kadhaa ya kuchokozwa na vikosi vya ulinzi na usalama vinavyoitumikia CCM (rejea mkasa wa 2005 ambapo polisi wa Zanzibar kwa matakwa yao tu waliizuia CUF isifanye kampeni katika eneo la Donge, Unguja, na kuwajeruhi watu kwa risasi za moto pale wapinzani walipojaribu kwenda huko).

Kwa hivyo, tukirudi pale makala hii ilipoanzia, kaulimbiu ya ‘amani na utulivu’ inatekelezwa zaidi kivitendo wa wapinzani na ile ya vurugu, fujo na chuki inatekelezwa na CCM. Wako watakaohoji kwamba hilo ndilo ambalo limekuwa kosa la wapinzani na ndio maana hadi leo wameshindwa kuchukua hatamu za nchi hata baada ya kudai kuwa wanapigiwa kura, kama ilivyo kwa mfano wa chama cha CUF, Zanzibar.

Lakini hebu tuliangalie suala hili katika upana wake. Tufanye tena tajiriba hii: chukuwa karatasi na penseli. Chora duara dogo na ndani ya duara hilo andika neno ‘amani.’ Kisha toa mishale minne au zaidi kutoka kila upande wa duara hilo. Mwisho wa kila mshale, andika neno ambalo wewe ungelilitumia kutafsiri neno amani. Bila ya shaka, maneno hayo yangelijumuisha furaha, imani, umoja, mshikamano, upendo, shibe na mengi mengineyo yenye sifa nzuri kama hizo.

Kwa hivyo utaona kuwa, tafauti na fujo, ambayo imezungukwa na mambo mabaya, amani imezungukwa na mambo mema. Fujo inachimbukia kunako dhuluma, ubaguzi, unyanyasaji, ufisadi, woga na utoadilifu. Amani inachimbukia kunako imani, upendo, utangamano, kuridhika na kujiamini. Matokeo ya fujo ni vifo, njaa, umasikini, wakimbizi, chuki na visasi. Matokeo ya amani ni uhai, shibe, hali nzuri ya maisha, kustahamiliana na kuvumiliana.

Katika harakati za kidemokrasia, kwa maana ya harakati za kusimamisha serikali ya watu inayotokana na watu na iliyopo kwa ajili ya watu, amani inamaanisha kila kitu. Ndio njia na ndilo lengo. Mwanademokrasia wa kweli hutumia njia za amani kufikia uundaji wa serikali itakayodumisha amani katika maana yake halisi.

Mwanademokrasia wa kweli ni lazima aoanishe baina ya njia anazopitia na lengo analotaka kulifikia. Hakuna uhusiano wowote ule baina ya azma ya kusimamisha, kwa mfano, utawala unaochunga haki za binaadamu na kuzivunja haki hizo katika kuelekea kwenye utawala huo. Leo hii tunalilia ufisadi na utawala unaovunja haki za watu, lakini hayo yapo kwa kuwa waliopo madarakani wameingia kwa kutumia njia ya fujo na vurugu.

Amani ni matokeo ya kuwa na jamii ya watu wenye kujiamini, wasio na woga na hivyo wenye uwezo wa kushiriki kwa umoja wao na kwa uhuru wao katika shughuli za kujiletea maendeleo. Watu wanapokuwa wamefunikwa na woga, wanapokosa kujiamini katika nchi yao ya uzawa, hapo hapana amani. Na hapo hapawezi kutandikwa misingi ya demokrasia na daima hapatakuwa na maendeleo. Ndipo ilipofikishwa Tanzania ya leo.

Amani ni matokeo ya kushibana na kuaminiana kwa watu. Ni upeo wa imani iliyopo katika jamii na kiwango cha juu cha ustaarabu wa watu hao. Penye amani, pana maisha. Penye fujo, pana mauti. Penye amani pana matumaini na matarajio. Penye fujo pana kuvunjika moyo na kukata tamaa.

Kwa hivyo, anayependa amani na akapitia njia za amani kufikia malengo aliyojipangia, ana nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa kuliko yule anayependa fujo na kutumia njia hizo kuelekea malengo yake. Na hapo ndipo penye tafauti ya upinzani na CCM. Na hiyo ndiyo hoja ya CUF, kwa mfano, kuendelea kutumia njia za amani, Zanzibar. Ili kuja kupata nchi inayotawalika na kuendesheka ni muhimu kwa wapinzani kuendelea kutumia njia za amani.

Na ili kuishinda CCM ni lazima kwa wapinzani kutumia njia ambayo CCM haiwezi kuitumia. Ufafanuzi uliotangulia kuhusu fujo umeonesha CCM inasimama wapi. Kwamba fujo ndio nguzo pekee inayotegemewa na CCM, kwamba CCM si kiumbe kinachoweza kuishi katika mazingira ya kidemokrasia na ya amani na kwamba jeuri ya CCM imo katika wigo wa fujo kama vile jeuri na ujuba wa papa mla watu inavyotegemea kuwamo kwake baharini. Nje ya maji, papa huyu hana matao yoyote. Ni dhaifu, dhalili na madhulumu. Basi nje ya wigo wa fujo na vurugu, hakuna jeuri wala hakuna uhai wa CCM. Ni nyepesi kama usufi.

Kwa macho yangu madogo naweza kuona kwamba upinzani unaanza kufanikiwa nchini mwetu. Kwa siku za karibuni umeweza kujijengea sifa ya kuwa kundi la matumaini na matarajio mapya ya kujenga mustakabali mwema wa nchi hii. Umekuwa ukipaza sauti inayonukia maisha, na kuishinda ile ya CCM inayonukia mauti. Nauona kuwa una nafasi nzuri zaidi ya kufikia malengo yake kwa kuwa umekuwa ukiamini na ukitumia njia za amani, ambapo CCM ina wakati mgumu kwa kuwa imekuwa ikiamini na ikitumia njia za fujo.

Fujo ina khatima yake, nayo ni pale watenzwa wanapoijuwa nafasi yao na kujiaminisha kuwa, kwa wingi wao na kwa umoja wao, wanaweza kuchukuwa hatua za amani na za kistaarabu dhidi ya fujo hiyo. Na hilo ndilo linalofanyika sasa, ninavyoona, ambapo upinzani unaranda nchi nzima ukiihemua nguvu ya kweli ya umma iiadabishe CCM. Hilo liliwezekana kwengineko duniani, hakuna sababu ya kushindikana hapa.

Lakini hapa napo tuwekane sawa neno ‘nguvu’ maana nalo pia linapotoshwa. Kwa mfano, kama ungetakiwa utaje vitu unavyovihusisha na nguvu, kwa haraka sana ungerukia kutaja vyombo vya dola. Ungetakiwa kufafanua sababu zako, ungelisema kuwa vyombo hivyo ndivyo vinavyomiliki silaha kama bunduki, mizinga, vifaru, mabomu, jela na mengineyo. Kwako wewe, hivyo ndivyo viashiria vya nguvu!

Lau baada ya hapo ungetakiwa utoe mfano ambapo nguvu ilitumika, basi ingekuwa rahisi kutaja tukio ambapo askari polisi waliwavamia raia, wakawapiga kwa marungu na hata kuwafyatulia risasi kisha wakawasweka rumande. Labda utastaajabu ukiambiwa kuwa wewe ulikuwa huzungumzii nguvu, bali ulikuwa unazungumzia utumiaji wa mabavu. Na kwamba hivyo ulivyovitaja kuwa ni viashiria vya nguvu, kwa hakika hasa vinaashiria woga!

Kwamba pamoja na kuwa haya ndiyo mazoea yetu katika kuifasiri nguvu, hayo ndiyo pia makosa yetu. Nguvu, katika maana yake halisi, haihusiani kabisa na utumiaji wa mabavu. Nguvu ni dhana ya kisaikolojia zaidi kuliko ilivyo ya kifizikia, yaani ni uwezo wa kuwashawishi wengine kuamini, kuridhia, kutii na au kutenda vile unavyotaka.

Utumiaji wa mabavu, kama wa CCM, ni jitihada pofu ya kuwafanya watu watii bila ya ridhaa zao. Inawezekana kulazimisha ‘utii wa uongo’ kutoka kwa watu katika ule wakati ambao tu mabavu yanatumika, lakini ama utumiaji huo wa mabavu uongezeke au upunguwe, haiwezekani kuwafanya watu hao wawe watiifu wa kweli na wa muda wote.

Kujaribu kumdhibiti mtu kwa kutumia mabavu kunahitaji uangalizi wa hali ya juu na wenye gharama kubwa. Kwamba unapotumia kiwango cha chini cha mabavu, basi kunakuwa hakuna mafanikio, na unapotumia kiwango cha juu cha mabavu, basi unachochea uasi wa wazi dhidi yako. Angalia, kwa mfano, operesheni ya kijeshi inayofanywa na Serikali ya Muungano kila wakati wa uchaguzi Zanzibar na kisia gharama zake kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Lakini mabavu ndiyo silaha ya woga na watu wasiojiamini, na nimeshaonesha namna gani CCM isivyojiamini. Wale wasiokuwa na nguvu za kutosha kushawishi au kudhibiti mambo, hutumia mabavu ili kuonesha uwepo wao. Ubaya zaidi ni kuwa kila mabavu yanapotumika ndipo yanapoiondosha hata ile chembe ya nguvu ambayo yumkini mtumiaji mabavu aliwahi kuwa nayo hapo kabla.

Kwa mfano, pale serikali zinapogeuka na kuwa watumiaji wa mabavu na sio ushawishi wake katika kuongoza na kudhibiti mambo, huwa zimeanza au zimekwisha kupoteza nguvu zake kwa raia zinaowatawala. Watawala wa kidikteta hulazimika kila siku kutumia mabavu dhidi ya raia wao ili kufidia ukosefu wao wa nguvu juu ya raia hao. Na kwa kufanya hivyo hakuwafalii chochote zaidi ya kuimomonyoa ile chembe ya nguvu waliyokuwa wamebakia nayo. Siasa za Zanzibar kwa ujumla wake ni shahidi wa namna ambavyo Dodoma imekuwa ikitumia mabavu mengi lakini ikishindwa kuwashawishi Wazanzibari waikubali moja kwa moja.

Kwa hivyo, hakuna uwiano baina ya kuwa na nguvu na kutumia mabavu. Hakuna popote ambapo utumiaji mabavu umempelekea mtumiaji kuwa na nguvu. Dola ya Kisovieti ilikuwa inalingana na dola ya Marekani kwa uwezo wa kijeshi na kiuchumi duniani. Lakini watawala wa Usovieti walikuwa wakitumia mabavu kuwatawala raia wao, na kwa hivyo kujenga udhibiti wa mambo katika dola yao. Siku umma ulipoamua kikweli kweli kwamba unataka mabadiliko, mabavu ya dola hii hayakusaidia kitu. Hatimaye iliporomoka vipande vipande kama mlima wa makaratasi. Hali ilikuwa sawa kwa tawala za kidikteta kama za Yugoslavia, Ukraine, Krygistan, Indonesia na Kenya kwa kutaja mifano michache.

Hapa petu, kuporomoka kwa kiwango cha utii wa watu wa Pemba, kwa mfano, mbele ya CCM na serikali zake ni ushahidi unaotosha kuelezea ubaya wa kutumia mabavu katika kuwadhibiti watu. Vivyo, kupanda kwa kiwango cha ufuasi wa watu hao kwa chama cha upinzani, CUF, ni ushahidi unaotosha kuelezea uzuri wa kutumia ushawishi katika kuwafanya watu waamini na watende.

Nimalizie kwa kukumbusha kuwa tunazungumzia uhusiano wa CCM na vurugu tukionesha kwamba chama hiki hakina uthubutu wa kubakia madarakani bila ya fujo na vurugu. Tunazungumzia kwamba kauli ya DCI Manumba dhidi ya viongozi wa CHADEMA, Mbowe na Zitto, kwamba waache na kauli zinazoweza kuleta fujo na kuvunjika kwa amani ni msamiati wa kisiasa tu, kwani kwa hakika CCM ingependelea sana kuona vyama vya upinzani vinacheza katika uwanja huo (wa fujo na vurugu) ambao kwa CCM ni uwanja wa nyumbani, ili ipate kuvibamiza.

Nikukumbushe pia kuwa, katika kiwango cha mazungumzo haya, tunalitumia neno nguvu katika mahala ambapo maneno nguvu ya umma na madaraka yangeliweza kutumika. Neno ‘madaraka’ lina mahadhi zaidi ya kisiasa, wakati neno ‘nguvu ya umma’ linahisika zaidi kuwa la kimapinduzi. Neno nguvu, kwa hivyo, lina wigo mpana zaidi.

Mwenye nguvu, kama tulivyotangulia kusema, ana uwezo wa kuwashawishi wengine kuamini au kutenda vile anavyotaka yeye. Mwenye nguvu, kwa hivyo, ana uthubutu wa kufanya maamuzi na kisha kuyawasilisha maamuzi hayo kwa watu, akawashawishi wakubaliane nayo, nao wakamtii. Mwenye nguvu, hata hivyo, hafanyi maamuzi kibubusa tu, bali huwa makini katika maamuzi hayo maana atahitaji umoja na mshikamano wa wenzake katika kuyafanikisha. Kisha, baada ya yote, mwenye nguvu atakuwa mvumilivu na msikivu kwa wenzake, maana bila ya hao anaelewa kuwa hizo nguvu zake hazipo.

Kwa hivyo, kwa kuangalia haya mambo yanayohusiana na nguvu na yale yanayohusiana na fujo na amani, utapata jawabu kuwa pana uhusiano wa moja kwa moja baina ya nguvu na amani na hapana uhusiano wowote ule baina ya nguvu na fujo. Kwamba kuna uwezekano wa kupata nguvu kwa kutumia njia za amani; na haiwezekani kuwa na nguvu kwa kutumia fujo.

Kadiri vyama vya upinzani vinavyozidi kutumia njia za amani katika kuendesha siasa za nchi hii, ndivyo vinavyozidi kupata nguvu, na kadiri CCM inavyoendelea kutumia mabavu, ndivyo inavyopoteza nguvu. Siku si nyingi, kwa hivyo, upinzani utakuwa madhubuti kama mwamba, ilhali CCM itakuwa nyepesi kama usufi!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.