UCHAMBUZI

*Kwa heshima ya Socrates Nabwa

Nianze kwa lawama kidogo kwa wanahabari huru wa Tanzania. Kwamba wamelipa kisogo suala la mwanahabari mwenzao, Ali Nabwa, kunyang’anywa uraia, licha ya uzito lilionao. Labda ni kwa kuwa wamezongwa na kinyang’anyiro cha Uraisi kupitia Chama cha Mapainduzi. Labda mazishi ya Papa Yohana Paulo II na uteuzi wa Benedict XVI uliwakosesha wakati wa kufikiria madhila yampatayo mwenzao. Na, labda kikwazo alichokuwa kawekewa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kilikula muda wao mwingi mno kiasi ya kukosa nafasi ya kumsemea mshirika mwenzao.

Marehemu Ali Nabwa: "Zanzibar imekufa dungu msooni. Inaambiwa haimo tena mchezoni na ilokula iziteme." (Dira Zanzibar, 2003)
Mzee Ali Nabwa

Lakini hata baada ya yote hayo, basi angalau mistari michache ya kumdhukuri mwenzao akiwa bado yungali hai? Au ndio wanasubiri afe, waje waandike kurasa kumi za tanzia ya kumsifu na kumtukuza, wakati katika uhai wake walishindwa hata kumpa bega la kulilia ukiwa na mateso yake!?

Kitaaluma, mimi si mwanahabari, lakini nadhani ni wajibu wa wenye taaluma yao kusimama pamoja katika jambo kama hili. Maana kwa kadiri tawala zetu zinavyohusika, hili haliishii kwa Mzee Nabwa tu. Jana ilikuwa ni Jenerali Twaha Ulimwengu, leo ni Ali Nabwa na, kila tunavyoendelea kutawaliwa na watawala wa sampuli hii, basi kesho na keshokutwa itakuwa zamu za wengine.

Nisichupe mstari sana. Ninalokusudia hasa ni hilo la kunyang’anywa uraia kwa Mzee Nabwa. Na, kwa hili, tangu mwanzo niyaweke wazi maoni yangu kwamba, Nabwa anatiwa adabu kisiasa. Kwamba ukiacha virungu vya Polisi, jela na risasi (kama ilivyotokea kwenye maafa ya Januari 2001 na athari zake), njia nyengine inayotumiwa na watawala wetu kuwamaliza raia wanaotafautiana nao kisiasa ni kuwavua uraia na, kwa hilo, kuwafanya watu wasio na kwao (stateless). Ndivyo alivyotaka kugeuzwa Jenerali Ulimwengu.

Kumnyang’anya mtu uraia wake ni kiwango cha juu cha udhalilishaji na uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu. Tarehe 10 Agosti 2002, Jaji wa Mahkama ya Afrika Mashariki, aliyewahi pia kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Waziri wa Sheria, Waziri Mkuu na Makamo wa Kwanza wa Rais, Joseph Sinde Warioba, alizungumzia ubaya wa kumvua mtu uraia katika uzinduzi wa mkutano wa mwaka wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu. Alikuwa na haya ya kusema: “Ni jambo zito kumnyang’anya mtu uraia, kwa sababu ikitokea hali ambayo hakuna uhakika wa uraia wa mtu huyo, basi itakuwa ni mtu asiye na nchi….na hiyo ni kinyume na haki za binaadamu”. (Rai, Agosti 15-21, 2002).

Ndiyo, naiwe kweli kinyume na haki binaadamu, lakini nani kasema kuwa watawala wetu wanazijali haki hizo? Uzoefu wa kesi kama hizi za akina Mzee Nabwa unatupa hoja kuwa, kipimo cha kuwa mwanaadamu mwenye haki kamili mbele ya watawala hawa, ni kuwa kasuku wao. Kinyume chake ni uasi, uhalifu na uhaini. Hapo chochote kibaya hufanywa kuwa ndiyo stahili yako…virungu, jela, risasi, na hilo la kuvuliwa uraia!

Ndio maana tarehe 19 Machi, 2003, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikamtangaza rasmi Ali Mohammed Ali Nabwa, Mtanzania wa Zanzibar, kuwa si raia wa nchi hii na, kwa hatua hiyo, kumfanya kuwa ni mtu asiyekuwa na uraia wowote. Kikwetu husema mja msi kwao. Alianza kupewa stahili yake kutoka kwa mabwana wakubwa!

Kuanzia hapo, Mzee Nabwa alitakiwa kuishi Zanzibar kama mgeni, kufuatana na kifungu cha 9 (1) Jadweli la Sheria No. 6 ya 1995, ambacho kinamtaka mtu wa aina hiyo kuomba ruhusa ya kukaa nchini. Na, kwa kuwa alikuwa ni mwenyekiti wa bodi ya ZIMCO, iliyokuwa ikitoa gazeti la Dira Zanzibar lililokuja kupigwa marufuku na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) baadaye, akatakiwa pia aombe kibali cha kufanyia kazi hapa kama mwekezaji.

Hayakuishia hapo. Kwa kuwa alishatangazwa si raia tena, alitakiwa papo hapo aikabidhishe paspoti yake Na. A0111824 iliyotolewa Zanzibar tarehe 07/12/1993. Sasa aliambiwa kuwa, eti paspoti ile ilikuwa imetolewa kwake kinyume cha sheria!

Kisingizio (namaanisha hasa kisingizio) kilichotajwa katika amri hiyo ya serikali, kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Uhamiaji Zanzibar, ni kuwa Mzee Nabwa aliupoteza uraia wa Tanzania pale alipochukuwa paspoti ya Komoro. Kwa ufahamu unaotakiwa hapa na watawala ni kuwa, kitendo hicho kilimaanisha kuukana uraia wa Tanzania na kuchukuwa wa Komoro. Hicho kilikuwa kisingizio cha mwanzo.

Lakini, baada ya kufuatilia, Serikali ya Komoro ikakana ikiwa Mzee Nabwa aliwahi kuomba ama kupata uraia wa nchi hiyo. Katika barua ya 13 Machi, 2004, mahakama ya nchi hiyo inathibitisha kuwa: “We do hereby certify, by this letter, as resulting from our public records that: Mr. Ali, born around October, One Thousand Nine Hundred and Thirty Six at Kibokoni (Zanzibar), son of Mohammed bin Ali and Fatma bint Saleh, has never sought nor acquired the Comorian nationality.”

Sasa hapo ndipo serikali ikazuka na kisingizio chengine. Kwamba sio tu yeye peke yake, Mzee Nabwa, asiyekuwa raia wa nchi hii, bali hata wazazi wake hawakuwahi kuwa. Katika barua ya 17 Machi, 2005 kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mzee Nabwa, serikali ya Tanzania inamwambia mtu aliyewahi kuitumikia kwa moyo wake wote na utiifu wa hali ya juu kuwa: “Kuzaliwa kwako Zanzibar hakukupa uraia wa kuzaliwa Zanzibar, (maana) wakati wewe unazaliwa, wazazi wako wote wawili walikuwa na asili ya Komoro na kihistoria nchi ya Komoro ilikuwa chini ya utawala wa Ufaransa na, hivyo, wakaazi wote wa Zanzibar wenye asili ya Komoro walitambuliwa kama raia wa Ufaransa.”

Mimi si mwanasheria, wala siamini kuwa kadhia ya uraia wa Ali Nabwa imechukuliwa kwa muktadha na maslahi ya kisheria. Ikiwa kuna chembe ya ‘usheria’ uliolizunguka jambo hili, basi ni wa hila na mizengwe ya kuwahalalishia watawala kutenda usilifu wao.

Nimetangulia mwanzoni kubainisha maoni yangu kwamba, uraia ni rungu ya kisiasa itumiwayo na watawala kuwaadhibu wale wanaowaona kuwa ni wapinzani wao. Mzee wangu, Ali Nabwa, anakomolewa kwa kuwa amekuwa akiandika mambo yanayowakosoa waliopo madarakani. Makhususi zaidi ni baada ya kuanzishwa kwa gazeti la Dira, ambalo yeye alikuwa ni mhariri mtendaji wake. Na kutoka hapo, Nabwa akawa si tena yule aliyepewa barua ya kumuheshimu kwa utumishi wake uliotukuka kutoka Ofisi ya Makamo wa Raisi. Ghafla-bin-vuu, akageuka na kuwa ‘si mwenzetu’.

Narudia. Ikiwa kuna kosa lolote lililomfanya Mzee Nabwa kuvuliwa uraia wake ni kuwakosoa watawala. Mara moja niliwahi kuandika kuwa “Kuwaambia wakubwa “Hapana” kuna gharama zake (Dira Zanzibar, 2003). Bado ningali na mawazo hayo hayo. Kwamba wetu ni watawala ambao wanamchukulia raia yeyote anayewakosoa au asiyekubaliana na wanayoyafanya kuwa ni muasi, haini na mkosefu wa uzalendo. Kipimo walichonacho watawlaa wetu kwa raia wanayemwita mwema, ni kuwa mfuasi wao. Kinyume chake, chochote kinaweza kutokea, likiwemo hili la kunyang’anywa uraia wa nchi ambayo vitovu vya mabibi na mababu zako vimezikiwa. Ndivyo alivyofanywa Mzee wangu.

Nilisema, na hapa ninarudia, kuwa utawala wetu unafanana sana na ule wa Athens ya zama za mwanafalafa wa Kiyunani, Socrates, miaka 3000 nyuma. Kama ilivyokuwa Athens ya wakati huo, basi na Zanzibar ya leo inatawaliwa na tabaka la watu wanaojiona ma’asumuuna__ wasiokosea na waliotakasika na makosa. Ndani ya vichwa vya watawala hawa mumejengeka imani aliyonayo Majivuno, Waziri Mkuu wa nchi ya Kusadikika, kwamba kidole chake kimoja cha ncha kina akili kuliko vichwa vya Wasadikika wote! (Soma riwaya ya Kusadikika ya Shaaban Robert).

Sasa, kama ni hivyo, ni vipi raia wajinga na wavivu wa kufikiri kama sisi tunathubutu kuwahoji na kuwakosoa watawala waswafii kama hawa? Hili ndilo lililowakuna na kuwakereketa mabwana wakubwa hawa hata wakafikia pahala pa kuona kuwa adhabu itoshayo kumkomoa raia huyu, mzee, masikini na dhalili ni kumnyang’anya uraia wake. Kwangu mimi, hii ni adhabu kubwa zaidi kuliko virungu, jela na hata risasi!

Wenzao wa Athens walipokabiliwa na ‘tatizo’ kama hili la kujitokeza kwa Socrates aliyekuwa mzee, masikini na dhalili lakini mwenye akili inayochaji vyema kama alivyo Mzee Nabwa, waliamua kumkamata na kumfungulia mashtaka ya kuwapotoa vijana kwa kuwapa elimu inayopingana na uungu na inayochochea uasi dhidi ya serikali.

Kwa hakika, kosa hasa la Socrates lilikuwa ni kama hili la Mzee Nabwa, yaani kuihakiki upya mitazamo na misimamo iliyojengwa kulitukuza tabaka moja (watawala) dhidi ya jengine (raia) kwa miaka nenda-rudi na kupewa baraka hizo za uungu, elimu na nyenginezo zote zilizomfanya mnyonge atwazike na asiulize ilipo haki yake. Msimamo wa Socrates ulikuwa: “The unexamined life is not worth living”.

Kwa kadiri nimjuavyo Mzee Nabwa, hivyo ndivyo pia anavyoamini yeye. Kupitia maandishi yake, sio tu kwamba anayahikii upya maisha yake binafsi kuungama alimokosea na hivyo ‘kujizaa upya’, bali pia anawaonesha watawala (ambao kuna wakati alikuwa sehemu yao) pale walipokosea na jinsi ya kujirekebisha. Amekuwa akifanya hivyo kwa kuyajadili upya, mambo yanayohusu nchi hii, kizazi chake na khatima yao.

Maandishi yake yamekuwa yakihakiki upya, kwa mfano, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uadilifu wa watawala, misingi ya utawlaa bora na haki za binaadamu na mengineyo mfano wa hayo. Na kwa kuwa katika kila moja kati ya hayo muna kukosea kwa watawala, basi kuhakiki kwake kunaelekeka kuwakosoa. Na hakuna jambo baya na gumu kwa watawala kama hilo la kukosolewa.

Wa Athens walimuua Socrates kwa kumlazimisha kunywa kinywaji cha sumu, wetu wanamuua Mzee Nabwa kidogo kidogo kwa kumvua uraia, maana wanajuwa kuwa kwa njia hiyo wanamnyima uwezo wa kufanya kazi na, hivyo, kwa makusudi wanaziziba tundu zake za riziki. Kubwa zaidi ni kuwa, katika umri alionao wa miaka 70, wanampiga pigo la mwisho la kisaikolojia na kumfanya amalizie maisha yake katika upweke, simanzi na sononeko.

Basi, dhaifu mimi kama nilivyo, naandika hapa kuthamini mchango wa Nabwa, Mtanzania wa Zanzibar, ambaye baada ya kuitumikia nchi hii kwa utiifu na kwa moyo wake wote, serikali iliyopoewa dhamana ya kuongoza raia imeamua kumtangaza kuwa yeye na wazazi wake hawajapata kuwa raia halali wa nchi hii.

Naandika kumfariji kuwa, hata kama kuna hicho kikundi kidogo cha watu wachache (wao, serikali) katika kundi kubwa la watu milioni 30 (sisi, raia) wa nchi hii kilichoamua kutumia nguvu yake kumdhalilidha hivi, basi bado tuko raia wa nchi hii tunaomuona kuwa yeye ni mwenzetu na mwenye kustahiki heshima ya kiwango cha juu kabisa. Tunamuheshimu kwa kuwa mchango wake kwa nchi hii ni mkubwa mno kiasi ya kwamba wengi wa hao waliompokonya uraia, hawajapata kuuchangia.

Nasisitiza tena maoni yangu katika hili: Ali Mohammed Ali Nabwa ametangazwa si raia na watawala kutokana na maandishi yake yanayowakosoa. Lau Nabwa angelijikubalisha kuwa kasuku wa kuitikia kila kiimbwacho na watawala, akakubali kuwa mramba buti lao, basi suala la uraia wake lisingelitajwa hata siku moja. Maana, hakuna watu wapendao kusifiwa na kutiiwa kama watawala wetu.

*Kwa mara ya mwanzo makala hii ilichapishwa katika gazeti la Rai, Mei 2004

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.