Ali Nabwa alitaka:
Zama za kufa zikija
Zije angali yu mtu, hajageuka nguruwe
Hajakuwa nyama mwitu, azaaye na wanawe
Zije bado ana utu, akiondoka aliliwe
Hishima iwe pamoja naye
Navyo ndivyo ‘livyokufa
Sote twalia kwa yeye!
Ali Nabwa alitaka:
Mauti yakimf’ata:
Yamf’ate mapambanoni, apigania nchiye
Yasimfate chumbani, kapakata miguuye
Afe kikondoo kwani, naye ni simba mwenyewe?
Simba hufa kwenye vita
Na ndivyo alivyokufa
Jemedari na shujaa!
Ali Nabwa alitaka:
Siku yake ikifika
Ifike angali chumvi, mithali umuhimuwe
Wamuhitaji wajuvi, wahisi waondokewe
Asife kifo uchimvi, hata tanga ‘siekewe
Kufa huko hakutaka
Naye hakufa ja hivyo
Amekufa akihitajiwa!
Ali Nabwa alitaka:
Safari yake ‘kijiri
Ijiri hayu fakiri, kwamba sanda akopewe
Bali hakutaka kufa tajiri, utajiri kwake kiwe
Hakutaka afe na matajuri, bali na deni asiwe
Deni si mwenza mzuri
Naye hakufa mdaiwa
Labda makala zake!
Ali Nabwa alitaka:
Pumzi ikimuhama
Imuhame sijidani, mauti yamchukuwe
‘Simuhame matungini, kilabuni wala kwenye msewe
Alitaka afe muumini, msala chozi utowe
Uliliye ulitima
Naye amekufa hivyo
Akiwa mchaji Mungu!
Ali Nabwa alitaka:
Buku lake likifungwa
Asiwe katika madhalimu, wa viumbe vya Molawe
Lifungwe watu wangali na hamu, wakitaka lifunuliwe
Afe na wake utamu, ufavyo muwa ufuwe
Asife nikisimangwa
Na Nabwa kafa na hadhi
Na utukufu na jaha!
Mohammed K. Ghassani
17 Februari 2007