UCHAMBUZI

Shujaa Nabwa anapambana, tumuunge mkono

Kwa wiki ya pili sasa, mwandishi mkongwe wa habari nchini Tanzania, Ali Mohammed Ali (Nabwa), amelazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, mjini Zanzibar, akiugua ugonjwa wa pumzi unaosababishwa na mapafu kujaa maji. Hali yake inakwenda ikibadilika baina ya mbaya kidogo na nzuri kiasi.

Nabwa ni mwandishi wa kudumu wa gazeti hili katika safu yake, Tafakuri za Mzee Nabwa, ambamo amekuwa akichangiana uzoefu wa historia ya maisha yake na wasomaji wake, ambao lazima tuseme kwamba ni wengi mno. Umahiri wa Nabwa katika uandishi hauhitaji kuongezewa chumvi, na wasomaji wenzangu wa makala zake ni mashahidi wa hilo.

Kwa sisi wengine tunaojaribu kufuata nyayo zake, Nabwa anaendelea kubakia zaidi ya mzee kwetu. Huyu ni mwalimu na kiongozi wetu. Kwamba kila fani ina shujaa wake kwa mujibu wa maeneo yake. Katika eneo letu hili, Nabwa ndiye shujaa wa fani hii ya habari. Wanayemkumbukia zama za Dira Zanzibar, wanaweza kulithibitisha hili pasina shaka.

Wasiolikumbuka, Dira lilikuwa gazeti huru la kila wiki la Zanzibar lililokuwa likiongozwa naye. Mafanikio ya Dira pia hayahitaji kutiliwa chumvi. Lilizoa ufuasi wa kutosha na kutisha. Ulitosha kwa waendeshaji gazeti, lakini ulitisha kwa serikali. Ndani ya kipindi kifupi cha uhai wake, liliweza kuinua, kwa kiasi kikubwa, kiwango cha uelewa na mwamko wa Wazanzibari katika nyanja zote za maisha – uchumi, siasa, historia na utamaduni.

Tuko tunaokwenda umbali wa kusema kwamba, hata kile kitendo cha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kulisakama gazeti hilo kwa kesi na hatimaye kulifungia na kumpokonya uraia Nabwa, ni katika mafanikio hayo makubwa ya Dira. Kwamba kwa kukataa kwake kuramba buti la watawala, Dira ilikuwa imejipambanua kutoka kundi la vyombo vya habari vinavyochunga maslahi ya mabwana tu, na kujidhihirisha kuwa chombo cha kweli cha kuleta mabadiliko na kinachochea ari ya maendeleo miongoni mwa jamii kama lilivyo jukumu la taaluma hii. Ikajijengea heshima.

Tukitaka kuwa wakweli wa nafsi zetu, basi tuko ambao hadi leo hii tunaendelea kufaidi heshima iliyojengwa kwetu na Dira. Na kwa kusema hivyo, sioni namna ambayo tunaweza kuizungumzia heshima hiyo, bila ya kumtaja na kumnasibisha Ali Nabwa. Binafsi naona fahari kubwa mno kunasibishwa naye. Naona fahari kunasibishwa na mtu ambaye alipambana na kusimamia kilichochapishwa na gazeti hilo hadi ukomo wa jitihada zake. Nampigia saluti mtu ambaye alipambana kwa ajili ya uhuru wangu wa kuandika na kupokea maoni.

Nakumbuka alipolumbana na Jaji Joseph Warioba, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) wakati huo, kuhusiana na madai ya SMZ kwamba Dira ilikuwa ikikiuka maadili ya uandishi wa habari. Ilivyoonekana Jaji Warioba alishaamua kusimama zaidi upande wa SMZ kuliko wa usuluhishi. Na kwa kuwa Nabwa alikuwa na hoja, akachanganya kujiamini kwake na ukali kidogo kuisimamia heshima ya Dira.

Hata kabla ya Dira kufungiwa, wengi wetu tulishajuwa kuwa hilo lingelitokezea tu. Tabia ya serikali yetu ya ukosefu wa ustahmilivu kwa hoja inayokinzana na mtazamo wake, haikuwa kitu cha ajabu. Mara nyingi, nakumbuka, tulikuwa tunajadiliana kabla ya kuchapa habari au makala ambayo tulishaiona kwamba ingeliigusa mishipa ya fahamu ya watawala. Lakini inapotokea tumekubaliana, ni Nabwa aliyekuwa akisema, “Mimi ndiye Mhariri Mtendaji. Ichapwe, liwalo naliwe!” Akatupa nguvu, tukasimama na kuingia mzigoni.

Huyu ndiye Nabwa aliyelala kitandani sasa katika wodi ya wagonjwa mahututi. Hadi SMZ ilipoamua kulifungia gazeti la Dira, ilikuwa ‘imeshaipata fresh’ na haikuwa tena na fahari ya kujigamba kumiliki habari zote za nchi hii. Tayari milango ya habari ilikwishafunguka, na tangu hapo haijapata kufungika tena. Ni Nabwa na Dira ndio waliokuwa wameifungua milango hiyo. Fahari iliyoje!

Hata sasa ambapo amekuwa na safu ya kudumu katika gazeti hili, ule mwangwi wa sauti za milango kufunguka unaendelea kusikika. Binafsi, mara nyingi napokea salamu za kumsifu Nabwa kwa simulizi zake zilizomo kwenye safu hiyo. Inafahamika kwamba, kuna wasomaji wengi ambao, baada ya kununua tu gazeti hili, hukimbilia kusoma ukurasa wa nne, kwenye Siku Moja Itakuwa Kweli, kabla ya hata kusoma ukurasa wa kwanza.

Naamini uongozi wa gazeti hili unapata heshima kuona kwamba miongoni mwa vitu vinavyolifanya gazeti hili la Fahamu Mwananchi kuwa hasa Fahamu ni yeye, Ali Nabwa. Fahamu nalo, kama lilivyokuwa Dira, linazidi kupata ufuasi kila kukicha na, miongoni mwa sababu nyengine zote, ni kwa kuwa muna Nabwa. Nabwa amekuwa kama ishara ya habari na mawasiliano katika nchi hii, na hasa Zanzibar ambako ameamua kuikita mantiki ya uandishi wake. Ni majaaliwa yake Mungu kwamba ishara hii hivi sasa imelala kitandani Mnazi Mmoja ikipambana na maradhi.

Kitu kimoja cha ziada, ambacho pengine hakijuilikani na wengi wetu, ni kwamba Nabwa anaamini mno juu ya kuwasiliana na watu. Ukimya na upweke si katika misamiati anayoipendelea maishani mwake ingawa, kwa mujibu wa simulizi zake, kuna mara nyingi alizolazimishwa kuwa katika hali hiyo na mfumo. Hata hivyo, hajapata kuuruhusu ukimya na upweke umlemee. Hata katika siku hizi za karibuni ambapo maradhi yamekuwa yakimpa tabu na akawa hawezi kuandika moja kwa moja kwa mkono wake, basi bado huagiza mtu aende na kompyuta nyumbani kwake ili amkaririe naye aandike.

Najua kuwa hakuna kitu kinachomkera Nabwa kama gazeti kutoka hali yeye hayupo kwenye safu yake. Ni mtu anayekerwa na hali ya kutokuwasiliana, incommunicado. Anataka kuwasiliana na kuendelea kuwasiliana hata pale kitandani alipo. Anataka kuendeleza mapambano na kuuvuja upweke na ukimya uliomo kwenye maradhi. Alifanya hivyo hata alipokuwa amefungwa jela pale Keko na Mwalimu Julius Nyerere. Aliwasiliana na wafungwa wenzake kwa ishara na hata kwa miguno na mipigo ya viambaza. Huyu ndiye Ali Nabwa aliye kwenye chumba cha wagonjwa mahututi akipambana na jaala yake.

Kama yeye aliyepo kitandani anapambana hivyo, sisi tulio nje tuna jukumu gani? Kwanza tuna jukumu la kibinaadamu. Kwamba huyu ni mja mwenzetu aliyepatwa na masaibu kama ambavyo yangelimpata yeyote kati yetu. Ugonjwa ni kinyume tu cha uzima, na vyote viwili ni dhati kuhusu maisha. Tunapaswa kumuombea kwa Mungu ampe afya ya haraka ili arudi nyumbani kuunganika na familia yake kuyafurahia maisha. Msaada huu uwe ni wa hali na mali. Hali ya kiuchumi ni mbaya kwetu sote, lakini penye dharura kama hii, waungwana huchangizana ili kukidhi haja.

Pili, tuna wajibu kama wanahabari wenzake. Kuwa mwanahabari hakumaanishi mwandishi wa habari tu, bali wote ambao mfumo wa habari unawahusu, na hao ni wengi. Tunapaswa kumuunga mkono katika mapambano haya. Tuwasiliane naye, maana sote tunajuwa kuwa pamoja na kuvuta hewa, uhai wa mwanaadamu huhuishwa na kuwasiliana. Pasipo mawasiliano, maisha huwa chapwa, yakakosa ladha na yasiwe na thamani.

Alipo Nabwa ni kitandani hospitalini – mahala pakimya, papweke na palitima. Si mahala pa kukaa hata sekunde chache kwa mtu mwenye furaha na afya. Tuwasiliane naye, auhisi umoja na mshikamano wetu. Ayaone mapenzi na huruma zetu kwake. Ajuwe kuwa, hata kama yuko peke yake humo chumbani kimwili, kiakili na kiroho sisi sote tuko naye.

Tusisahau kwamba, Nabwa amekuwa akiwasiliana nasi siku zote kuuondoa ukimya na upweke wetu. Tangu akiwa kwenye Dira kisha An-Nur na sasa Fahamu, huyu ni mtu ambaye hajapata kuacha kuwa karimu kwetu, akitunywesha maji ya fikira kutoka kisima chake kisichokauka cha kumbukizi. Kwamba amekuwa akitufanya tuione dunia ya miaka 50 nyuma kana kwamba iko mbele ya macho yetu hivi sasa. Kwamba amekuwa nasi kutufumbua macho kuhusiana na historia yetu, akiupambanua ukweli kutoka giza la uongo.

Nabwa anapambana. Tumsaidie katika mapambano hayo kwa kuwasiliana naye na kuwasiliana na Mungu Muumba wetu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.