BAINA yetu, watawaliwa, na watawala wetu, pana kizingiti cha kimawasiliano. Si sisi raia wala wao viongozi wetu wenye uwezo wa kuingia katika akili na kuisoma fikra ya mwenzake. Na kwa hivyo hawatuelewani.
Huenda, ikawa kwa kuogopa kuonekana watovu wa nidhamu, basi tuko tunaojifanya kuelewa na kukifurahikia kila kinachosemwa na mtawala wetu, hivyo tukapiga makofi na kurukaruka. Na vivyo, kwa kukhofu kuonekana kuwa haungwi mkono, mtawala naye hujifanya kuyajuwa sana maisha yetu. Hivyo sivyo hali halisi ilivyo. Ukweli ni kuwa pana tatizo kubwa la kimawasiliano.

Inawezekana kabisa kwamba ushiriki wa watu katika mikusanyiko yetu hautokani hata kidogo na mvuto wa mtawala kwao. Watu wanaweza kushiriki katika mkutano wa kiongozi fulani, si kwa kuvutiwa na namna anavyozungumza, bali kwa kuwa pana vishawishi vyengine vilivyo muhimu na bora zaidi na tafauti kwao.
Walevi wanaweza kufuata pombe, vijana wa kiume wakafuata wasichana (hasa ikiwa wasichana hao ni hawa wanaovaa mibano na mipasuo), wazee wakafuata kahawa na au kutokana na hali yetu ya maisha ilivyo ngumu, wengi wanaweza kuvutiwa na mlo – pilau, haluwa, n.k.
Hapa tanbihi kwa viongozi wetu wa kisiasa ni kwamba wanapojiona wamewaburuta watu wengi katika mikusanyiko yao, wasilewe sifa. Hawapaswi kudhani kuwa watu wote hao wanawapenda na wana imani nao. Lazima wajihakiki na waone ikiwa kweli wao, wakiwa kama upande mmoja wa mawasiliano, ni wawasilianaji wazuri na ikiwa kweli kile wakiwasilishacho (ujumbe) katika mikutano yao, ndicho hasa kinachowavuta watu karibu yao, wakiwa kama upande wa pili wa mawasiliano haya.
Uzoefu unaonesha kwamba wanasiasa wachovu wana kawaida ya kuyadharau matatizo yanayotokana na mawasiliano na ambayo huyaathiri moja kwa moja mahusiano yaliyopo baina yao na wafuasi wao. Huwa wanakosa uwezo na umakini wa kimawasiliano na, hivyo, kushindwa kuzizingatia hisia na fikra za watu wao.
Matokeo yake ni kuharibika kwa mahusiano baina yao. Wanapofikia hapo, wanasiasa hawa huanza kuchukuwa hatua za kikatili kulazimisha kuwepo kwa mahusiano. Na hata yanapokuja hayo yanayoonekana kuwa mahusiano chanya, basi huwa ni ya kutungwa tu. Hayo hayawasaidii chochote watawala, labda kuwaharibia zaidi.
Hili ni tatizo la kihistoria katika siasa za kutawaliana, lakini kuwa kwake la kihistoria hakulihalalishi. Kiuongozi na kisiasa, tatizo hili lina gharama kubwa sana, nami nadhani kuwa viongozi wetu wanastahili kusaidiwa kujuwa kwa nini pawe na tafauti kubwa za kimawasiliano baina ya watawala na watawaliwa.
Sababu ni nyingi, mojawapo ni hii ya kutokuchimbukia kwao pahala pamoja, yaani kuwa na viongozi wasiotoka migongoni mwa raia wanaowaongoza. Hapa nakusudia kusema kuwa hawa ni viongozi wasiotokana na maisha wanayoyaishi watu wao walio wengi.
Viongozi hawa huwa aidha wamezaliwa katika pepo za dunia na, au, kwa wale waliotokea katika ufukara, wameshayasahau maisha hayo. Sasa wamekuwa hawajuwi chochote kuhusu mambo yetu sisi tuliozaliwa na kukulia katika maisha ya tabu na dhiki. Misamiati, shida na haja zetu si vitu vinavyoeleweka vichwani mwa viongozi hawa. Hawatujuwi.
Malkia wa Ufaransa aliwahi kumuuliza mtumishi wake baada ya kuuona umma ukiandamana mbele ya kasri lake: “Kwani wale wanataka nini hasa?” Akaambiwa kuwa wanataka mkate, basi yeye akauliza “kwa nini wasidai keki?”
Malkia hakujuwa kuwa kwa waandamanaji wale, keki si kitu cha kawaida kama vile kilivyo kwake yeye. Wale ni raia waliokuwa na maisha ya dhiki sana kiasi ya kwamba mkate ndio msamiati mkubwa katika maisha yao. Matokeo yake, ufalme wa mumewe ukapinduliwa na raia wanaodai mkate. Mkate tu!
Hivi ndivyo pia walivyo watawala wetu. Hawana uelewa juu ya maisha yetu, watawaliwa. Matokeo yake ni kuwa viongozi hawa wanakuwa wazuri katika majukwaa ya kimataifa, lakini sio katika jukwaa la nyumbani.
Wanazungumza kila lahaja ya Kiingereza, tena vizuri, lakini Kiswahili walichozaliwa nacho kinawapa tabu. Wanapokaa majukwaani hutuvunganyavunganya, la mwanzo wakaliweka mwisho na la mwisho wakaliweka mwanzo. Wanakosa hata misamiati ya kujieleza wao wenyewe mbele yetu.
Wanaujuwa na wanauheshimu sana utandawazi, ndio maana kila siku wanazungumzia umuhimu wa nchi hii kuwamo na kubakia katika mchezo huo wa kilimwengu ulioasisiwa na kusimamiwa na mataifa makubwa.
Lakini, kwa bahati mbaya, wanashindwa kuujuwa umuhimu wa nchi hii kudumu katika Muafaka ambao umeasisiwa na kusimamiwa na watu wa nchi hii wenyewe. Ndio maana wanapata uthubutu wa kuuponda, kuukebehi na kuudharau. Sijuwi huo utandawazi wao utatanda uwazi upi, ikiwa kesho na keshokutwa nchi hii itajaa machafuko yatakayotokana na kuvunjwa kwa Muafaka!?
Wanaijuwa sana historia ya Ulaya na Mapinduzi ya Viwanda na awamu zake zilizoanzia 1750, ndio maana wanayazungumzia kistaarabu na kiuchumi. Lakini hawajuwi chochote kuhusu historia na Mapinduzi ya Zanzibar na awamu zake yaliyodumu kwa miaka 40 tu, na ndio maana wanayazungumzia zaidi kikabila na kijazba.
Wanaweza kuziona kwa urahisi sana athari za ugaidi kwa ulimwengu na maslahi ya mataifa makubwa, lakini ni shida kwao kuziona athari za ukandamizaji ndani ya nchi. Wanaijuwa globalization na athari zake, lakini hawajuwi chochote kuhusu udugunaizesheni na athari zake. Hawaujuwi wala hauwapitikii vichwani mwao.
Wanazijuwa zaidi pudding, hamburger na pizza kwa kuwa ndizo zilizowalea na ndizo walizozizowea. Lakini hawajuwi kitu kuhusu shelisheli, biye, togonya na mtoriro; vyakula vilivyotulea na tunavyoshindia sisi raia wanaoutuongoza. Kwa viongozi wetu, hivi si vyakula vinavyofikirika kuliwa na binadamu.
Wanayajuwa zaidi mabenzi yanayoendeshwa kwa kasi lakini yasiyowaumiza abiria wake hata kama barabara ni za mashimo. Lakini hawajuwi chochote kuhusu bavu za mbwa tunazopanda sisi raia tulio wengi. Hawajuwi kuwa humo watu hubanana na mizigo yao ya makozi na muhogo, na hata wakifika safari yao, wako taabani kwa kudundwadundwa mashimoni. Hawaujuwi usafiri huu.
Wanaujuwa usafiri wa Boeing wanaopanda wakapewa chai na vyakula vizuri vinavyotolewa na wahudumu warembo na watanashati, mara tatu kabla hawajafika safari ya robo siku. Hawaujuwi usafiri wa majahazi tunayoyapanda sisi na njaa tokea asubuhi ya siku moja hadi usiku wa siku ya pili.
Hawaujuwi wala hawaujali upepo huu wa Kusi ambao huangamiza mamia ya roho za raia wao wanaotumia usafiri huo. Ndio maana wanashindwa hata kwenda kuwapa mkono wa pole walioondokewa na ndugu na jamaa zao!
Kwa hivyo, chanzo ni huku kutoka na kuishi dunia tafauti kati yetu sisi raia na hao wanaoitwa kuwa ni viongozi wetu. Unaweza kumsikia kiongozi anahutubia katika mkutano wa hadhara huko kwetu kijijini, huku anazungumzia ubinafsishaji, utandawazi, ugaidi, kupunguziwa madeni, nafasi ya kodi katika ukuwaji wa uchumi, na vitu vyengine kama hivyo.
Bila ya shaka, si vibaya kuvizungumzia vitu hivi, lakini suali ni wapi, wakati gani na kwa nani? Busara ya tendo ndilo ni kutendwa pahala ndipo na wakati ndio. Likiepuka mipaka hiyo, tendo hilo huwa halina chembe ya busara, na huwa hasara tupu!
Karibuni Rais Amani Abeid Karume alikuwa akizungumza na wana-CCM wa mikoa mitatu ya Unguja katika kijiji cha Mtende, kusini ya kisiwa cha Unguja. Yale yale tunayoyazungumzia hapa ya ukosefu wa uwiano baina ya kile kilichomo katika fikra za mtawala na za watawaliwa, ndiyo yaliyodhihirika.
Pamoja na mengine, Rais alitutaka vijana wa Zanzibar tusikubali hata siku moja kupokonywa uhuru wetu ulioletwa na Mapinduzi ya 1964, maana uhuru una utamu wake. Sadakta kabisa!
Si wakati tena huu wa kuzungumzia uhalali na uharamu wa Uhuru wa 1963 na Mapinduzi ya 1964, lakini itoshe kukubaliana kuwa wazee wetu walipigania uhuru wa nchi hii. Hapo sote tunakubaliana, na ndio maana nikasadikisha maneno ya Rais kututaka vijana tuutambuwe utamu wa uhuru.
Lakini nina hakika kuwa baina yake Rais Karume na sisi vijana wake, pana tafauti kubwa sana ya kuupata uhuru huo. Niseme kuwa ‘uhuru’ wake si ‘uhuru’ wetu. Wake yeye una kila sababu ya kulindwa na kutukuzwa, wa kwetu ni hasara. Wetu ni uhuru-njaa!
Kwamba uhuru uliopo Mazizini sio uhuru uliopo Mtende, na wala haufanani kabisa. Wa Mazizini ni uhuru kwa maana yake hasa – ni uwezo wa kuamua, kuchagua na nguvu za kupata. Ni uhuru wa kuamka asubuhi na kukuta kila kitu kipo tayari kwa ajili yake. Bafuni kuna maji ya kukoga katika mabeseni makubwa makubwa na mifereji inayotowa kila aina ya maji – ya moto, vuguvugu, au baridi kwa mujibu wa hali ya hewa na mahitaji ya muogaji.
Mazizini kuna uhuru wa kuwa na umeme kila wakati. Hata TANESCO wafanye tajriba yao ya kuizimia umeme Unguja nzima, basi huko majenereta yanajiwasha yenyewe. Huko ndiko kwenye uhuru wa kula chakula unachokitaka na kwa wakati unaoutaka mwenyewe.
Kuna uhuru wa kupata maji safi na salama, wa kuwa na makazi ya kuridhisha, wa kuvaa nguo za kupendeza. Kuna uhuru wa kuumwa na kupata matibabu mazuri na ya kuridhisha, na mara nyingi nje ya nchi. Huo ndio uhuru wa kulindwa na kumfanya mtu awe ‘mzalendo’. Uhuru wa aina hiyo ukikhatarishwa, lazima aliyenao atokwe na machozi na apigane kwa kucha na meno kuurejesha. Kwamba huo ni uhuru-shibe.
Lakini huo sio uhuru tulionao sisi vijana wake tuliojitia kwenye magari kumfuata yeye kutoka Sogea na Mikunguni. Huku, asubuhi ukiamka, lazima kwanza uwe na shilingi mia ya kununua dumu la maji pale Mwembe Beni, maana mifereji yetu haitoki maji kwa karne sasa.
Ukikosa mia ya kununulia maji, basi itabidi uende kazini na tongo zako, ikiwa hiyo kazi unayo. Ikiwa kazi huna, kama tulivyo wengi wetu, basi utaishia maskani kumsubiri wa ‘kumpiga kirungu’. Tunatakiwa tuulinde na tuutetee uhuru huu, sio kuupinga na kuuondowa?
Utamwambiaje kijana wa Pandani kuwa huu ndio uhuru uliopiganiwa na wazee wake na hivyo aulinde? Uhuru wa kuamka asubuhi na kukimbilia Msaani kwenda kukunguzuwa shina la muhogo, ndiyo chai inywewe nyumbani. Na muhogo wenyewe ni hilo hogo tu. Halina nazi, halina kitoweo. Huu ni uhuru-njaa na basi hauwezi kuwa wa kung’ang’aniwa na vijana wako, mtukufu Rais. Utamwambiaje kijana wako wa Msuka kwamba yuko huru na ajifakharishe, ilhali ndio kwanza anarudi kumzika ndugu yake barobaro zima? Unajuwa alikufa kwa nini?
Alianguka mkarafuu, akaumia vibaya. Hospitali ya Wete wakasema hawana uwezo wa kumtibu hapo, lazima apelekwe Mkoani. Mkoani akaambiwa hadi Mnazi Mmoja, nako akaambiwa hadi KCMC, Moshi. Akafa hajapata matibabu. Huo ndio uhuru wa kujivunia, wa kuumwa bila matibabu?
Kwa nini asijisifu kwa ule ‘uhuru’ wa Mazizini, ambao kijana wake akiumwa hupanda ndege hadi kwa Mtakatifu Thomas, London, hata kama maradhi yake yangeliwezekana kutibiwa Mnazi Mmoja tu?
Nadhani umefika wakati wa viongozi wetu kujifunza lugha ya kuwasiliana na raia ili kuyafanya mahusiano baina ya watawala na watawaliwa kuwa makini na ya kweli zaidi.
Vyenginevyo, kuna uwezekano wa kiongozi kuwaona kila siku raia wanajaa mikutanoni kwake, naye akadhani kuwa wanamfuata na wanavutiwa naye, na kumbe wanafuata mambo yao: pombe, wanawake, ngoma. Na siku ya siku ikafika, akajikuta wale wale waliokuwa wakiitikia “Ndiyo mzee”, sasa wanasema “Sio mzee.”
Katika Communication Works (McGraw-Hill Companies, Inc., 1999), Michael Gamble na Teri Kwal Gamble wanasema kuwa, katika wote, wanasiasa ni watu wanaotegemea zaidi mawasiliano kujijenga na kulinda nafasi zao za kisiasa. Na ili kuendelea kuwa hai kisiasa, basi lazima mwanasiasa aweze kuyajibu ndivyo maswali haya matatu.
La kwanza ni kwa vipi na kwa nini anayaona mambo kama anavyoyaona na raia wanayaona mambo kama wanavyoyaona? Pili, ana uwezo gani wa kusikiliza na kuratibu ujumbe anaoupokea? Na, tatu, anaifahamuje nafasi ya mazingira – kiuchumi, kisiasa na kiitikadi – katika kujenga fikra ya watu?
Sijuwi ikiwa Rais Karume ana majibu kwa maswali haya, na kama anayo, sijuwi ni yapi!
Chanzo: Gazeti la Dira, Na. 36, Agosti 8-14, 2003