UCHAMBUZI

Spika Kificho waficha nini?

KATIKA siasa, tunaambiwa kuwa ufanisi wa utawala hupatikana kwa kutegemea uongozi na usimamizi madhubuti wa vyombo vinne vikubwa, ambavyo kila kimoja kati yake hutarajiwa kuwa na uhuru usioingiliwa na chengine – chombo cha kuunda sheria, kanuni na taratibu za kuongozana, cha kuzifanyia kazi sheria hizo, cha kuzisimamia sheria hizo kuhakikisha kuwa zinatekelezwa, cha kuzitafsiri na kuzipa maana na chombo cha kuzichambua, kuzifuatilia na kuzihusisha sheria, kanuni na taratibu hizo na maisha ya raia.

kificho
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.

Lakini uhuru pekee hautoshi kukihakikishia kila chombo kati ya hivyo kinatimiza jukumu lake la kuufanya utawala wa umma kuwa utumishi uliotukuka, bali lazima kila chombo kiwe na nguvu za kutosha na ambazo zinalindwa kisheria ili kukizuia chombo chengine kisichupe mpaka wake. Uwepo, mjengeko na ufanyaji kazi wa vyombo hivi huitwa “Unne Mtakatifu!”

Hiki cha mwisho – vyombo vya habari – ndio kwanza kimeingizwa siku za karibuni katika Sayansi ya Siasa, si kwa kuwa ni kipya, bali kwa kuwa mchango wake katika utawala haukuwa ukitambuliwa hapo zamani.
Leo natuzungumzie uongozi na usimamizi wa hiki cha mwanzo hapa petu, yaani Baraza la Wawakilishi, chenye jukumu la kutunga sheria,  na msisitizo wetu hasa upo katika nafasi ya Spika wake, Mhe. Pandu Ameir Kificho, katika kujenga utawala bora na kuifanya kazi yake kuutumikia umma kuwa kweli utumishi uliotukuka.
Kutokana na umuhimu na ulazima wa mhimili anaouongoza, spika anakuwa na nafasi kubwa zaidi katika demokrasia ya uwakilishi, ambayo ndiyo tunayojidai kuwa nayo hapa, maana watu wanaouunda wanatokana moja kwa moja na umma.
Mhe. Kificho anaongoza chombo kinachounda sheria ‘kwa jina la umma’. Maana yake ni kuwa kila kinachofanywa na Baraza la Wawakilishi hutambuliwa kuwa kimefanywa na raia wa nchi hii kwa kuwa wao ndio waliowapeleka wajumbe wao barazani kuwawakilisha katika maamuzi ya kuendesha nchi yao. Tunaweza kusema, kwa nafasi yake ya uspika, yeye ndiye anayeuongoza umma wa Zanzibar katika chombo chao hiki cha kuundia sheria.
Kwa hivyo, kinadharia, hata kama hakupigiwa kura za moja kwa moja jimboni, bado naye anawajibika moja kwa moja kwa umma, kwa kuwa utumishi wake umetokana na unahusiana sana na umma huo. Kwamba hata hao waliompigia kura yeye, kwanza walipigiwa kura na umma.
Kwake yeye ndiko kuliko na makutano ya raia na serikali yao kuzungumzia ustawi wa maisha yao na mustaqbal wa nchi yao. Kupitia kwa wawakilishi wao, raia hutumia vikao hivi kuangalia wapi na wapi serikali imetenda kama ilivyowaahidi wakati wa kuomba dhamana ya kuwatawala, na wapi na wapi imetenda sivyo kwa mujibu wa makubaliano yao katika kuombana na kupeana kwao kura.
Ni kutokana na hilo, ndio maana kunakuwa na maswali, hoja, ushauri na changamoto kwa serikali huku ikitakiwa na umma iwajibike kutekeleza dhamana na ahadi zake. Hivyo ndivyo ilivyo.
Kwa hivyo basi, katika hali yoyote ile spika si sehemu ya serikali inayoulizwa maswali, ikajengewa hoja au ikapewa ushauri na changamoto. Spika ni mwangalizi na msimamizi tu wa vikao hivi baina ya serikali, inayowakilishwa na mawaziri, na umma, unaowakilishwa na wawakilishi wao.
Maswali, hoja, ushauri na changamoto huwa havielekezwi kwake yeye, bali kwa serikali. Spika haijibii, haitetei wala haifichii kitu serikali, zaidi ya kuhakikisha kuwa sheria na kanuni za Baraza zinafuatwa katika kila kikao. Hivyo ndivyo inavyotakiwa iwe.
Si stahili, na haifai hata kidogo, kwa spika kujaribu kuikingia kifua serikali kwa hali yoyote ile. Ni sawa kwamba yeye ndiye anayepaswa kuweka nidhamu ya Baraza, kwa kuwa yeye ndiye kiongozi wake. Lakini kuweka huko nidhamu hakuna uwiano wowote na kuinusuru serikali na maswali, hoja au changamoto litokalo kwa wawakilishi wa watu, litokalo kwa umma.
Hapa ni baina ya umma na serikali tu. Wala sio baina ya umma, kwa upande mmoja, na serikali na spika, kwa upande wa pili. Hivyo haitakiwi iwe.
Pamekuwa na matukio mawili matatu ambayo yanamuonesha Mhe. Kificho akicheza nafasi mbili anapokuwa Barazani; moja kama Spika, kwa maana ya msimamizi wa chombo cha uundiaji sheria, na ya pili kama ‘mtetezi’ wa Baraza la Mawaziri.
Ingawa hii ya pili haichezi kwa kujibu maswali au hoja zinazotolewa kwa mawaziri wa serikali, lakini hufanya hivyo kwa kuyazimua maswali, au kuzikwepesha hoja zinazoelekezwa kwao. Hiyo haipendezi, haivutii na inakirihisha. Inatafsirika kuwa Mhe. Kificho anawakingia kifua mawaziri hao kila pale anapoona kuwa kuna hatari ya kukwamishwa na kuwajibishwa na sauti ya wawakilishi wa watu – sauti ya umma.
Tukio la karibuni zaidi lilitokea wiki iliyopita. Inakumbukwa kuwa si zamani sana tokea Mhe. Hafidh Ali Tahir, mwakilishi wa watu wa jimbo la Rahaleo na ambaye yasemwa kuwa kitaaluma ni mwanakhabari, atake gazeti hili la Dira lifungiwe. Hilo lilikuwa limetanguliwa na kauli ya Mhe. Salim Juma Othman, Waziri katika ofisi ya Waziri Kiongozi anayeshughulikia khabari, kwamba serikali inakusudia kulishitaki Dira katika Baraza la Habari kwa kukiuka kwake maadili ya uandishi.
Suala la kulifungia Dira linapingana, bila ya shaka, na dhana nzima ya utanuzi wa sekta binafsi. Sasa kwa kuwa aliyewahi kulizusha suala hili ni Waziri Salim katika mazungumzo na waandishi wa khabari huko Pemba na kufuatiwa na Mwakilishi Hafidh katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, pakaonesha kuwa hapa pana shaka na shukuki.
Kama tulivyo sisi raia tulio nje ya Baraza, na ambao tunaliangalia Dira sio tu kama gazeti, bali pia kama taasisi ya umma, hata Mhe. Abbas Juma Muhunzi, mwakilishi wa watu wa jimbo la Chambani, naye akawa anataka kujuwa kulikoni. Serikali imesimama wapi na Dira?
Kwamba huko nyuma Waziri Salim alisema kuwa serikali italishitaki gazeti hili, kisha akazuka na Mhe. Hafidh akataka gazeti lifungiwe, tena leo katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri huyo huyo anazungumzia utanuzi wa sekta binafsi. Mhe. Muhunzi akataka kujuwa serikali imelichukulia vipi ombi la Mhe. Hafidh na ni kwa kiasi gani inalihusisha jambo hilo na utanuzi wa sekta binafsi? Hilo ndilo lililokuwa swali lililohitaji jawabu.
Unajuwa nini kilitokea? Mhe. Kificho akasema kuwa hilo la Dira si swali, kwa hivyo Waziri alitakiwa kujibu tu utanuzi wa sekta binafsi.
Afanaalek! Hivi kama la Dira si swali, huo uhalali wa utanuzi wa sekta binafsi kuwa swali ni upi? Wananchi huku nje walikuwa na sababu na hamu ya kuijuwa kauli ya serikali kuhusiana na Dira hivi sasa. Na hiyo ni kwa sababu zilizotangulia kutajwa huko nyuma.
Kwanza, waliona kuwa uwezekano wa kulishitaki Dira kwenye Baraza la Habari ni finyu sana kwa kuwa khabari si jambo la Muungano, na baraza hilo ni chombo kinachofanya kazi kwa sura ya Muungano. Kwa kuwa hapo, serikali ingelishindwa, basi uwezekano ni kwamba, badala yake, ingelitumia njia nyengine kujenga hoja ya kulifungia.
Pengine ingeliwashawishi watu wake walio nje ya serikali kutoa shinikizo hilo kupitia maandamano au njia yoyote ile na, au, hata kwa kupitia Mwakilishi kuwasilisha hoja binafsi na kupitishwa Barazani. Sasa, hadi hapo watu wakataka kuijuwa nafasi ya Dira, gazeti lao, iko wapi!
Sababu ya pili ni ule uwiano uliopo baina ya hatua za kuliandama gazeti hili –  kitu ambacho hivi sasa kimezoeleka – na dhana nzima ya kutanua sekta binafsi katika khabari. Ama ikiwa andamo hilo linatokana na serikali, wawakilishi, au watu wa kawaida, Dira ni chombo halali kwa mujibu wa sheria, basi ni kwa vipi serikali inakilinda kama ilivyoapa kulinda na kusimamia sheria za nchi hii?
Maana kulinda na kusimamia sheria ni pamoja na vile vilivyopo kwa mujibu wa sheria hizo. Mwakilishi wa watu alitaka serikali iseme ina msimamo gani juu ya hilo. Kwa maneno mingine, chombo cha kutunga sheria kilitaka kujuwa vipi chombo cha kutekeleza sheria kinakitendea chombo cha uchambuzi wa sheria?
Lakini, kwa Mhe. Kificho, hili lilikuwa ni swali linaloujengea hoja na kuupa changamoto uadilifu wa serikali iliyokamia kusimamisha utawala wa sheria. Na kwa kuwa Spika ni ‘mtetezi wa serikali’ barazani, basi akaikingia kifua: “Swali ni utanuzi wa sekta binafsi”. Kwa hivyo, Waziri akatakiwa kujibu tu serikali inajishugulishaje na utanuzi wa sekta binafsi katika khabari. Akabororowa bwerere, papai kwa kijiko!
Mwenye kuzingatia anaweza kujiuliza: hivi utanuzi huu wa sekta binafsi kwa kuuhusisha na nini? Kwamba chimbuko la swali halikuwa utanuzi wa sekta binafsi, na hilo Mhe. Kificho analijuwa kuliko ninavyolijuwa mimi. Anajuwa kuwa chimbuko lake lilikuwa ni uhusiano wa utanuzi huo na kauli za wahishimiwa Salim na Hafidh juu ya kufungiwa kwa Dira. Hapo, na hapo tu, ndipo umma unapotaka ujibiwe.
Kwa nini Mhe. Spika Kificho afanye hivi? Anaficha kitu gani hasa, kisijuilikane? Anamficha nani, asijuwe? Anamfichia nani, asifahamike? Kwa kufanya hivi, Mhe. Spika anatujengea dhana nyingi vichwani mwetu na kutufanya tuhoji hata uadilifu wake yeye binafsi, akiwa kama kiongozi wa chombo cha umma. Tuhoji huo utumishi wake wa umma uliotukuka.
Ni kana kwamba anajenga picha kuwa serikali iliyopo madarakani haina dhamira nzuri na utawala wa sheria, na hivyo analificha hilo lisijuilikane. Ni kana kwamba anatuficha sisi raia tuliowapeleka wawakilishi wetu barazani kutuundia sheria na kuangalia utendaji kazi wa watawala tuliowapa dhamana ya kutuongoza, tusijuwe kile kilichopo nyuma ya pazia. Ni kana kwamba anawafichia mawaziri ‘wake’ na kuwasitiri wasibwagwe kwa hoja.
Yumkini, Mhe. Kificho ana khofu zake zinazomfanya afiche, hata kama hazina uhalali. Pengine, sababu moja ni kuwa amezoea kuongoza vikao vyenye wajumbe kutoka upande mmoja tu wa kimawazo na, au, kichama, hivyo hana uzoefu wa migongano ya hoja vikaoni. Huwa anadhani vile watu wakigongana kihoja, huenda wakamalizia kwa kuvunja kanuni za Baraza. Hivyo, ili kulinusuru hilo, huamua kuingilia kati.
Au, pengine, Mhe. Spika huamua kuingilia kati kwa kuwa hawa mawaziri wanaopewa changamoto ni mawaziri kutoka chama chake. Kwa hivyo, anaona kuwa wakikwamishwa wao, ndio kama kimekwamishwa chama chake. Kwamba ikiwa mawaziri hawa wanaonekana kuwa na udhaifu mkubwa kama huo, basi itachukuliwa kuwa hivyo ndivyo ilivyo serikali, na vivyo chama kilichoiunda. Naye, Spika, akiwa mmoja kati ya watu muhimu katika chama, basi ndivyo alivyo!
Lakini, kama nilivyotangulia kusema, khofu hizi hazina uhalali. Spika anatakiwa kuwa jasiri na muadilifu. Awe jasiri kwa kuwa wanaojengeana na kuvunjiana hoja ni watu wazima, tena wastaarabu. Hakuna hasara yoyote kwa mgongano wao wa hoja. Bali, kinyume chake, kuna manufaa mengi yatakayopatikana kupitia mijadala ya aina hii.
Na awe muadilifu kwa kuwa yeye anaongoza mhimili muhimu wa utawala. Lazima ajijengee utumishi unaohishimika. Kama nilivyosema huko nyuma, kinadharia huyu ni sehemu ya watu wanaowakilishwa barazani, na kiutendaji angelitakiwa kusimama baina ya pande hizi mbili, yaani serikali inayotawala na umma unaotawaliwa. Serikali inawakilishwa humu Barazani na mawaziri wake kama vile umma unavyowakilishwa na wawakilishi wao. Hiyo ndiyo mizania iliyopo!
Yeye ni refa tu na anatakiwa kuufanya mchezo huu kuwa fair play. Haipendezi, haikhalisi na inachefua mno kumuona refa anapuliza kipenga na wakati huo huo anapiga shuti kuuondosha mpira kutoka eneo la goli la timu moja. Sasa yeye atakuwa nani? Muamuzi au mchezaji? Akifanya hivyo, si bora akawacha kipenga na kuvaa jezi?
Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Dira Zanzibar, Toleo Na. 33,la tarehe 16-24 Julai 2003.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.