UCHAMBUZI

SMZ, mpaka tusukumane ndio twende?

KAMA bado unaishi chini ya utawala ambao wale waliopewa madaraka wameamua ‘kujibinafsishia’ ofisi za umma na kuzifanya milki yao, usijihisabu kuwa wewe ni raia huru. Ikiwa mpaka sasa ungali unaishi katika mfumo ambao kuipata haki yako mwenyewe, inakubidi upembejee hadi umrambe mtu nyayo, usijihisabu kuwa umeendelea. Jijuwe kuwa uko katika madhila, udhalilifu na unyonge na, kwa hivyo, kitu pekee unachokihitaji kwa haraka ni ukombozi!

Mimi na wewe bado tunaishi katika mfumo huo. Bado tunaishi katika jamii ambayo watu waliokabidhiwa dhamana za kuutumikia umma wamejigeuza kuwa mabwana wa umma – wanataka wasihojiwe wala wasiulizwe. Bado ‘wahishimika’ hawafika mahala pa kuamini kuwa hizo ofisi walizopewa kuziongoza ni za kuwahudumia watu. Wangali wakidhani kuwa hivyo ni vyumba vyao vya kulala, ambavyo wana nguvu na uwezo wa kumkaribisha wamtakaye na kumfungia milango wasiyemtaka. Kwa hivyo, bado hatuko huru wala hatujaendelea.

Hadi sasa, raia anapopatwa na haja inayomlazimu kumuona ‘bwana mkubwa’ au ‘bibi mkubwa’ fulani katika ofisi ya umma, hupaswa kwanza ajitie udhu – ajitoharishe atoharike – kisha aswali rakaateni kumuomba Mungu aulainishe ulimi wa muhishimiwa huyo usije ukamtapikia mijineno yake inayokirihisha. Bado tatizo ambalo lingeweza kutatuliwa kwa robo saa, watendaji katika ofisi zetu za umma huwachukuwa miezi miwili na nusu kulitatua – kama hata hapo watalitatua!

Kwa ufupi, ni kuwa watendaji katika ofisi za umma wana kibri, jeuri na dharau huku, kwa makusudi kabisa, wakituonesha sisi raia kuwa ofisini si pahala petu. Hapatustahikii. Hutakiwa tujijuwe kuwa hatuna haki yoyote pale, na kama ikitokea kuhudumiwa, basi tufahamu kuwa huo ulikuwa ni msaada tu, sio utekelezwaji wa wajibu.

Kwa watukufu hawa, vile kuwapo katika ofisi ya umma ni ishara ya ubwana, utukufu na uungu-mtu, na wanachukulia kwenda kwetu katika ofisi hizo kutaka huduma ni ishara ya utwana, udhalilifu na makosefu. Huu ni mfumo mbovu. Ni mfumo uliooza. Na kattu, kwa hapa jua lishapofika, mfumo huu haustahamiliki kuwepotena!

Mahitaji ya wakati huu ni tafauti kabisa na uwepo wa ubwana wa mezani. Kwamba sasa tunaishi katika zama ambazo ufahamu wa watu kuhusu dhana hii ya utawala na utumishi wa umma ni mkubwa zaidi kuliko vile ilivyokuwa hapo nyuma. Sasa ni wakati ambao jambo lolote lifanyikalo au lililopo kwa jina la umma, huwa na nafasi kubwa ya kuathiri maslahi ya umma na hivyo kugharimu madaraka ya utawala.

Kinyume na hapo nyuma, hivi sasa ofisi inapoitwa ofisi ya umma hutarajiwa iwe kweli ofisi ya umma: kwamba itokane na umma na ifanye kazi kwa ajili ya umma. Yeyote anayechukuwa nafasi katika ofisi kama hiyo, hulazimika kwanza kuakisika na ukweli huo. Hulazimika kwanza kukubaliana na ukweli kwamba hiyo si nyumba yake, bali ni nyumba ya watu wote.

Kwamba humo si chumbani mwake, ambamo angeliweza kukaa akajifungia madirisha na milango na kujilia vyake atakavyo, apendavyo. Bali hicho ni ‘chumba cha wazi’, ambacho kila kitendekacho ndani yake kinapaswa kujuilikana na mamia kwa maelfu ya watu ambao ni washirika wa njia moja ama nyengine katika yale yanayoihusu ofisi hiyo. Ndio maana kwa wenzetu hivi sasa ofisi ya umma hujengwa kwa vioo kusudi kila mtu aone yatendekayo humo!

Hiyo ndio sababu ya ofisi kuitwa ya umma. Mtendaji asiyekubaliana na ukweli huo hulazimika kukabiliana na matokeo machungu ya ukaidi wake. Na hiyo ndiyo picha iliyojionesha hivi karibuni. Waliokabidhiwa dhamana kubwa kuiendesha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii walikifanya kile kitarajiwacho kufanywa na watu wa aina yao, lakini kisichopendeza hata kidogo.

Umma ulitaka kuujuwa msimamo wa serikali yao juu ya maradhi mabaya ya kupooza yaliyowakumba watu wa kisiwa cha Pemba kwa muda mrefu sasa. Walitaka kujuwa serikali yao imefanya nini na imefikia wapi kupambana na mashaka hayo.

Wizara ya Afya ni chombo cha umma na kwa hivyo watendaji wake ni watumishi wa umma, na uliotaka kujuwa khabari hizi ni umma. Hakukuwa na haja wala sababu yoyote kwa Katibu Mkuu, Dk. Omar Makame Shauri, kupandisha hasira kwa jambo hili, maana yeye yupo pale kuiwakilisha serikali yake katika utumishi wake kwa umma huo. Vile kuhamaki kwake, kumtolea maneno mabaya mwandishi aliyekwenda kuyaulizia hayo – na zaidi kumfukuza – kunajenga picha mbaya sana kwa utawala unaojilabu kuwajali watu wake.

Tendo hili la Dk. Shauri linatupa tafsiri nyingi chafu dhidi yake na dhidi ya serikali anayoiwakilisha katika utumishi huu aliokabidhiwa. Mosi, kama mwakilishi wa serikali, huenda alikuwa hajakuwa na taarifa yoyote ya kumpa mwandishi huyu, licha ya kwamba ugonjwa huu umezuka zamani kidogo. Ikiwa ilikuwa hivyo, basi huko kulikuwa ni kutokujali kwake, na hivyo kwa serikali, kuhusu afya za raia. Kama inajali, ni kwa nini hadi hapo haikuwa imekusanya taarifa za kutosha wakati ilishapita miezi tangu ugonjwa huu ubainike na kuripotiwa?

Pili, yayumkini Dk. Shauri alikuwa anajuwa lakini alikuwa anatumia madaraka yake vibaya kwa kuonesha nguvu aliyonayo ya kuamua ‘kuwa-isiwe’ katika eneo lake. Kwamba yeye ndiye boss kubwa pale, na sote wengine ni mburumatari tu tusio na uthubutu wa kumtaka afanye au asifanye jambo.

Mwenyewe akitaka anatowa habari, hataki hatowi. Yeye ndiye the master of his own fate, a captain of his own ship! Ikiwa ni hilo, basi nalo linaonesha ni namna gani mtumishi wa umma asivyo kweli mtumishi wa umma. Maana miongoni mwa sifa za utumishi wa umma ni kuwa muwazi kwa umma wenyewe.

Tatu, jambo hili linadhihirisha ukweli mwengine mchungu kwa serikali nzima kwa ujumla. Kwamba huyu ndiye mtendaji mkuu wa serikali katika wizara nyeti kama hii inayoshughulikia afya na ustawi wa raia wa nchi hii. Ndiye mwakilishi wa serikali hapa – daraja baina ya serikali na raia inaowatawala. Utendaji kazi wake unaakisi utendaji kazi wa serikali anayoiwakilisha. Basi ikiwa kibri na jeuri hii ndiyo itolewayo na mwakilishi wa serikali, hiyo ndiyo staili ya ufanyaji kazi wa serikali hii iliyokaa madarakani kwa kishindo!

Na kama hivyo sivyo, ni kwa nini Dk. Shauri akaendelea kubakia katika nafasi yake, hata baada ya jeuri na kibri chote hichi? Kwa nini asiwajibishwe kwa utovu wake dhidi ya umma ambao serikali iliyopo madarakani iliapa kuusitiri na sio kuuadhiri? Suala la afya za watu wa nchi hii ni muhimu sana kuliko kibri na jeuri hizi. Umma uko tayari kuzikosa jeuri hizo, lakini sio afya zao.

Dira, Na. 41, Septemba 02-18, 2003

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.