Huko ni kujipumbaza, maana tafsiri hasa za utawala wa kikoloni na ukombozi zimeepukana kabisa na mipaka ya kiwakati, kijiografia au ya kirangi kwa mtawala na mtawaliwa. Ama iwe jamii inapambana kujipapatuwa kutoka mikononi mwa mtawala wa kigeni au mtawala mzawa, mweupe au mweusi, sasa au zamani, Afrika au Ulaya, kote huko ni kujikombowa na harakati hizo ni ukombozi. (Soma An Economic Strategy for the Second Liberation of Africa, Babu, A. M: 1994).

Wakati wowote jamii inapokuwa chini ya utawala wa kimazonge, na kujitambuwa hivyo, hunyanyuka na kutafuta ukombozi wake – iwe kisiasa, kiuchumi, kitamaduni au vyenginevyo. Harakati hizi zina nguvu na kasi kubwa ya kuzagaa na kusambaa mithili ya moto nyikani au maji kutoka mlimani. Mkururo wa matukio katika historia ni shahidi wa hayo. Mshairi mmoja, akifananisha nguvu ya harakati na ile ya maji, aliwahi kuandika:
Wayazuwiyaye mai, yasenende na ndiyaye.
Huoni hiyo si rai, kuyafanya yas’eneye?
Zuia uzuwiavyo, kila tobo yazibiye
Illa mai yashukavyo, i kubwa mno kasiye
Nawe sikiza yajavyo, isikize ngurumoye
(Angalia Malenga wa Uswahilini, uk. 18: Mdungi, A., 2001).
Ni kasi hii isiyozuilika ndiyo ambayo humuathiri kila mtu na kila kitu katika jamii iliyokumbwa na wimbi la harakati za mabadiliko. Huzifanya nyenzo na silaha za kufikia lengo kuwa nyingi. Ndio kama hivyo yalivyo maji yatiririkayo kwa kasi kutoka mlimani, yanazagaa mote na yanapenya kila mahali, na vitu vyote vilivopo juu ya mlima – magogo, majani, udongo, mawe – husombwasombwa na kuwa sehemu ya maporomoko.
Hapa petu, hivyo ndivyo ilivyokuwa wakati wa mapambano ya kudai uhuru kutoka kwa watawala wa kigeni, kuanzia mwishoni mwa miaka ya ‘40 hadi mwanzoni mwa miaka ya ’60. Wakati huo jamii ilitaka kujikomboa kutoka mikononi mwa watawala wa kigeni.
Watu walitaka wapate uhuru wa kujitawala na kujiamulia mambo yao wenyewe. Harakati za ukombozi zilijipenyeza kila mahali na zikaleta athari yake. Familia, miji, vijiji, viwanja vya michezo, elimu, sanaa, dini na, alimradi, kila mahali pakawa ni sehemu na ni taasisi ya ukombozi.
Ndiyo, kila taasisi ikafanya kazi yake vizuri katika mapambanao. Yalikuwa ni mapambano ambayo watawala wa kigeni walishindwa kuyahimili, ikawapasa kuondoka ilhali wakiwa na hamu ya kubakia. Walishindwa kubakia kwa kuwa kila mahali walipogeuka, palikuwa na mwito ule ule tu: “Ondokeni hatuwataki, tunataka kujitawala wenyewe!”
Kila mahali. Wakisoma magazeti, wanakuta hilo. Wakitembea njiani, wanasikia hilo. Wakipita mitaani, kuta za majumba zimechorwa hilo. Pakiitishwa mikutano ya hadhara, dharura au faragha, wanasikia hilo. Hata pakiimbwa nyimbo, wanasikia hilo hilo. Popote, momote na kokote, sauti ni moja tu: “Fungasheni na ondokeni, ondokeni!” Yakawashinda!
Hatimaye, matukio manne yaliyofuatana yakawa ndiyo athari iliyobakia kwa harakati zile za ukombozi kwa Watanganyika na Wazanzibari: Uhuru wa Tanganyika wa 1961, Uhuru wa Zanzibar wa 1963, Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa 1964.
Mambo haya manne, licha ya tafauti ya maoni iliyopo juu ushiriki au utoshiriki wa wananchi kwayo, hayawezi kuwachwa bila ya kuhusishwa na harakati za ukombozi zilizoendeshwa na raia.
Sasa ni miaka mingi tokea kizazi kilichopita kiendeshe harakati hizo na kufanikiwa kupata waliyoyapata, kubwa zaidi likiwa ni huko kujivua makuchani mwa mtawala wa kigeni. Hao walikuwa ni wazazi wetu. Nakumbuka nyimbo tuliyokuwa tukiimba skuli: ‘Sisi sote tumegomboka kwa ndugu zetu walopotea’. Ndiyo, wao ndio waliotukomboa!
Lakini kumbe kuondoshwa kwa mtawala mgeni haikuwa mwisho wa harakati za kujikomboa kisiasa na kiuchumi. Raia waliojikusuru huko nyuma kuikomboa nchi hii walisahauliwa siku moja tu baada ya ukombozi kupatikana. Wao na sisi vizazi vyao tumekuwa tukirithishana mashaka, tabu, idhilali na mateso. Na watawala wapya ambao – kinyume na wale wageni waliokuwapo wakati wa wazee wetu – ni wazawa, wanarithishana vyeo, uluwa, mali na israfu.
Yale yale aliyoyafanya mtawala mgeni, ndiyo ayafanyayo sasa mtawala mwenyeji. Al-watan kabisa! Ni kwa sababu hiyo, hivi sasa, karibuni nusu karne nzima tokea watawala wa kigeni kuondoka, harakati nyengine za kujikomboa zinazagaa kwa kasi ile ile ya mporomoko wa maji kutoka mlimani.
Vizazi vya wale raia waliowaondosha watawala wa kigeni vinajihisi kuwa thamani ya mapambano ya wazazi wao imepotoshwa na kudharauliwa. Wanaona kuwa damu ya wazazi wao imebezwa na kusalitiwa (Fungate ya Uhuru, uk. 5, Khatib, M. S, 1985).
Sasa nao wanataka mabadiliko. Na kama walivyofanya wazazi wao katika harakati za kujikomboa, nao wanazisambaza harakati hizi katika kila pembe na katika kila uwanja. Ni vile vile tu, hapana jipya.
Ukifungua gazeti, ukiangalia televisheni, ukisikiliza nyimbo, ukihudhuria mkutano, ukikaa kijiweni na wash’kaji au barazani na wazee, ukienda uwanjani kuangalia mechi, ama kwenye mhadhara wa kidini, mote humo kauli ni moja tu, ya mabadiliko.
Kasi ya harakati ina nguvu za ajabu, na kwa kweli haizuiliki. Ikifungiwa mlango huu, basi hujifungulia yenyewe milango mingine. Mtawala akiwazuia watu wasifanye mkutano kwa kuwa katika mkutano huo atapingwa, basi watampinga kwa kutumia chombo chengine – gazeti, televisheni au redio, na sasa kuna mitandao. Mtawala akikifunga chombo cha habari, atapingwa kupitia michezo. Na hata wakizuiliwa hapo, watatoboa kwengine tu.
Katika wakati kama huu, kila pahala na kila mtu, ama kama mmoja mmoja au katika ujumla wao, ni taasisi nzima na kamili ya harakati. Sijuwi watawala wetu watavifungia vingapi na watazuwia wangapi, ikiwa hata ndani ya tabaka la watawala wenyewe, munajengeka ghoba la harakati? (Fuatilia kuibuka kwa chama kipya cha SAFINA hapa Zanzibar).
Namna kasi na nguvu hii ya harakati za ukombozi ilivyozagaa na kuenea kila sehemu, ni sawa na vile nyumba inavyokuwa imekumbwa na hitilafu za umeme kutoka katika laini kubwa ya kusambazia umeme. Kila kitu na kila sehemu katika nyumba hiyo huwa yenyewe ni umeme. Ukigusa dirisha, shoti. Ukigusa mlango, shoti. Ukigusa kiambaza, shoti!
Wakati natayarisha makala hii, nilisikia nyimbo moja mpya ikiimbwa na mwimbaji maarufu wa muziki wa kizazi kipya Joseph Haule (Profesa J). Nyimbo hii inaitwa Siyo Mzee. Hapa sikusudii kufanya uhakiki wa kifasihi, lakini kutokana na maudhui yake, nimeonelea kuwa huu ni mfano halisi wa jinsi kasi ya harakati za ukombozi inavyosambaa kila mahali na kwa kila mtu. Hata katika kumbi za starehe, ambako huko nyuma usingelitarajia kukuta kitu zaidi ya ulimbwende na kulewa starehe za maisha, nako pia kuna shoti! Sijuwi vifungiwe vingapi?
Kwa wale wanaofuatilia muziki huu, ambao ni maarufu zaidi miongoni mwa vijana, wanajuwa kuwa huko nyuma mwimbaji huyu huyu aliwahi kuimba nyimbo aliyoiita Ndiyo Mzee. Ile ilikuwa ni kejeli kwa raia waliolevywa na kasumba za kitawala kiasi ya kwamba huamini kila wanaloambiwa kwa hishima na taadhima. Ilikuwa ni nyimbo iliyowataka wananchi wajihakiki na wajitathmini wenyewe na wakati huo huo kuwaambia watawala kuwa mbinu yao imeshajuilikana, nayo ni hii ya kuwafanya watu wawaitikie Ndiyo Mzee tu kila siku.
Lakini Siyo Mzee ni kinyume. Hili ni suto kwa watawala. Inawaonesha kuwa ile Arubaini yao ndiyo imewadia. Kwa kweli, hii ni nyimbo ya harakati za ukombozi. Inachora taswira ya unafiki wa wanasiasa walio katika tabaka la utawala. Hao ndio wale wanaopanda majukwaani kila baada ya miaka mitano kuwaomba kura wananchi na kuwaahidi mambo milioni, lakini wasitekeleze hata moja.
Hao ndio wale wanaoponda maraha kwa mapesa ya walipa kodi wa nchi hii: wakulima na wafanyakazi, na kisha kuwatupa. Kwao wao watu hawa, thamani ya raia ipo katika kuwapigia wao kura tu. Wakati wote wa upigaji kura, wao na raia huwa dam’ dam’, lakini baada ya hapo, wanakuwa mbali mbali mfano wa mbingu na ardhi. Wasaliti wakubwa!
Kutoka Ndiyo Mzee hadi Siyo Mzee, Joseph Haule anaonesha kuwa jamii imebadilika sana na kwamba sasa ni saa ya ukombozi. Katika Ndiyo Mzee wananchi walikuwa mbumbumbu, lakini katika Siyo Mzee wananchi wameshakarambuka.
Pale mwanzo raia walikuwa wamezugwa na maneno ya kiongozi wao, tuseme walikuwa na nidhamu ya woga, lakini sasa raia hawa hawa wamekwishang’amua kuwa kiongozi wao anawadanganya. Sasa hawako tayari kumkubalia mbabaishaji huyu. Wanamwita katika kikao cha dharura na kumuuliza kuhusu zile ahadi alizowaahidi wakati wa kampeni.
Kwa mfano, katika Ndiyo Mzee, aliwaahidi wapiga kura wake kuwa angeliwapatia askari polisi vifaa vya kutosha, zikiwemo helikopta kila askari na yake, kusudi waweze kupambana na ujambazi ulioenea. Sasa anapoulizwa ziko wapi zile helikopta, kiongozi mbabaishaji anajibu:
Nafikiria kuanzisha kwanza chuo cha marubani
Vyenginevyo mutapata ajali nyingi hewani
Baskeli hamujuwi kuendesha, helikopta mutaendeshaje?
Kila mtu aendeshe yake, huko angani itakuwaje?
Anapoulizwa na wakulima ile ahadi yake ya kuwapatia matrekta imefikia wapi, kiongozi huyo muongo anajibu:
Wakulima mngeendelea kwa kutumia jembe la mkono
Serikali haina hela, bajeti imefika kikomo
Naona kilimo cha mkono kinaendelea vizuri
Jamani kazeni mikono, endeleeni kukaza msuli!
Katika jumla ya ahadi alizozitowa katika Ndiyo Mzee, ni kuwa angelisambaza mabomba yanayotowa maji na maziwa nchi nzima (wakati sasa hata hayo ya maji tu hakuna). Anapokumbushiwa hili, anakuwa mkali:
Jamani naomba muulize maswali ya kiutu uzima
Mabomba kutoa maji na maziwa haiwezekani
Mulininukuu vibaya, nasisitiza haiwezekani!
Lakini ahadi kubwa kuliko zote aliyowahi kuitoa katika Ndiyo Mzee ni kwamba ikiwa ingelitokezea hali ya maisha kuwa ngumu, basi yeye angelikuwa tayari kugawana na wananchi kile anachokipata. Hiki kilikuwa ni kijembe cha mwisho kiashiriacho namna watawala wetu walivyo wanafiki wa kupindukia. Naye anapouliziwa hilo, anang’aka kwa ukali:
Eeh! Kugawana vya kwangu hilo suala litakuwa gumu
Familia inanitazama, ebo! nina majukumu
Imeandikwa: kila mtu atabeba msalaba wake
Kila mbuzi ale kwenye urefu wa kamba yake
Kikao hiki cha dharura kinamalizikia kwa vurugu. Wanachi wenye hasira kwa kudanganywa na kufanywa watoto na mtu waliyemchaguwa kwa kura zao wenyewe, wanachachamaa. Sasa kila alisemalo mtawala huyu, wao haawakubalianai nalo:
Wananchi tuko pamoja? ‘Siyo mzee’
Watanzania tumeelewana kule? ‘Siyo mzee’
Washika dau na wapiga kura pale? ‘Siyo mzee’
Enh!? ‘Siyo mzee’
Eti!? ‘Siyo mzee’
Wakulima tuko pamoja pale? ‘Siyo mzee’
Wanafunzi tumeelewana kule? ‘Siyo mzee’
Mabaamedi na mapolisi pale? Siyo mzee
Enh!? ‘Siyo mze’e
Eti!? ‘Siyo mzee’.
Na kama ilivyo kawaida ya watawala wetu wanapoona kuwa hasira ya umma inawajia usoni pao, hutumia jeshi la polisi kuikandamiza. Mwisho wa nyimbo hii, kunachorwa picha hiyo hiyo. Mwenyekiti wa kikao cha dharura anawaomba maafande wawasaidie kuwanusuru na ghadhabu ya umma!
Nilipomaliza kuisikiliza nyimbo hii nilikumbuka yale maneno maarufu: Saa ya Ukombozi imewadia. Lakini kwa hapa petu sio tena suala la kuwadia, kwa kuwa hapo mwanzo saa hii hii pia iliwahi kufika, isipokuwa sasa ni kujirejea tu. Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa: Saa ya Ukombozi imerejea!
Makala hii ilichapishwa kwa mara ya mwanzo katika gazeti la Dira Zanzibar mwaka 2003