UCHAMBUZI

Mufungao mwaionaje ladha ya dongo?

KUFUNGA na kushinda na njaa ni vitu viwili vyenye mfanano lakini pia vyenye mpishano. Kwa upande mmoja, kila afungaye hushinda na njaa lakini, kwa upande mwengine, si kila ashindaye na njaa kuwa amefunga. Maana yake ni kwamba, kufunga kunajumuisha, pamoja na mengine, kujizuwia na kula na kunywa, na hivyo kushinda na njaa. Katika funga, muumini huistahmilia njaa ili kutimiza ibada yake. Ustahmilivu huu ndio unaompa malipo kutoka kwa Mola wake.

Hapa, sio tu kwamba mtu huacha vyakula na vinywaji vyake vizuri akapambana na hasira za machango yake yanayosokotana tumboni, lakini pia hujizuwia hata kuvitamani vitu hivyo. Ndio maana kuna mapokezi (ambayo sina uhakika wa usahihi wake) yanayosema kuwa mtu aliyefunga, hatakiwi hata kusema kuwa ana njaa au kiu. Akisema hivyo, huambiwa funga yake imetenguka. Huo ni upande mmoja, wa mfungaji.

Upande wa pili, ni wa mtu anayeshinda na njaa akiwa hana nia ya kufunga wala ya kufanya dawa. Huyu ni yule anayefanya hivyo kwa, ama, kushindwa kukipata cha kukila au, kama amekipata, hakitoshi kuishibisha njaa yake. Hukaa na njaa yake kwa kuwa hana jengine la kufanya lisilokuwa hilo!

Ramadhani ya mara hii imekuja na kutukuta Wazanzibari katika yote mawili. Kama waumini, tunafunga hasa kwa maana ya kustahmilia njaa na kiu ili tupate ujira wa Mola wetu. Lakini pia, kama watu maskini tusio kitu, tunashinda na njaa. Tunashinda na njaa kwa kuwa hata unapofika huo wakati wa kufuturu, huwa tumekikosa cha kukila, katika baadhi ya kesi au, kama ilivyo katika kesi nyingi, tulichokipata ni haba sana kuyatosheleza matumbo yetu.

Inasikitisha sana, kusikia baadhi ya wahishimiwa wanatughadhibikia sisi raia tunaposema kuwa tuna hali ngumu za maisha. Wanafika hadi ya kututaka tuihame nchi. Yumkini ni kwa kuwa kwao vinapikwa vikipakuliwa, ndiyo maana inawawia vigumu kuamini kuwa maelfu yetu hatudiriki hata kuutimiza mlo wa mara moja kwa ukamilifu wake. Yumkini ghadhabu na ghamidha zao ni kuwa tunaposema hivyo, huwa ni kuwaambia kuwa wameshindwa kuongoza nchi vipasavyo kiasi ya kwamba watu wanakosa hata yale mahitaji ya lazima kwa maisha. Lakini, vyovyote viwavyo, huo si ndio ukweli wenyewe?

Ndio ukweli kwamba kwa wengi wetu huu ndio wakati wa ‘kula dongo’, alioutuahidi Marehemu Dk. Omari Ali Juma katika mizaha yake ya kisiasa. Si bado tunamkumbuka alipokuwa akiwakebehi wapinzani wake kwa kuwaambia kuwa watu wako tayari kula dongo, lakini sio kuwaweka wao (wapinzani) madarakani? Basi shere ile ndiyo hii sasa, ingawa mwenyewe hakubakia hai kuja kuyashuhudia maskhara yake yakiwa kweli. Kweli ya kula dongo!

Dongo lile aliloliahidi Dk. Omar halikuwa dongo hili la kujengea. Lilikuwa dongo kitaaswira, kwa maana ya maisha ya tabu, dhiki na mashaka. Maisha ya kiu bila ya maji, njaa bila ya chakula na maradhi bila ya dawa. Na, kwa hakika, hayo ndiyo tuliyonayo sasa. Maisha ya kula dongo!

Msamiati huu wa kula dongo una maana kubwa kwetu sisi, raia wa kawaida. Sisi, tunaoishi chini ya mstari wa umaskini kwa kutokutimiza hata pato la dola moja (shilingi 1000) kwa siku, dongo ndilo futari na daku yetu. Kwa wenzetu walioko juu kimadaraka na kiuwezo, huenda ikawa msamiati huu hawaujui wala hauwapitikii na ndio maana hawajali!

Hebu fikiri: fungu la muhogo, majimbi, viazi vikuu au viazi vitamu, ambalo kwa ‘kugongeana mwiko’ litawatosha watu watatu, ni shilingi 500. Shilingi kama hizo zinahitajika kwa kununua chana la ndizi mbichi lisilowashibisha watu wawili. Kidole cha ndizi mbivu shilingi 350. Kilo ya harage shilingi 700, ya tambi shilingi 500, ya sukari ni shilingi 500. Nazi ziwezazo kupika nyungu moja kati ya hizo ni shilingi 300. Dagaa, tonge kwa tonge, la angalau kupata vumba, kiingilio cha mwanzo ni shilingi 200.

Usizungumzie kula nyama, mboga au samaki, wala njugu mawe, mikate ya upawa, makombo-alawi, mikate ya mayai au chochote cha marango. Marango yana wenyewe wenye vyao, nawe hu katika hao! Zungumzia angalau kupata futari moja ya mataka na nyengine ya sukari kati ya hizo. Angalau kupata hilo fungu la dagaa na koroma la kupikia. Robo kilo ya unga wa uji kwa robo dumu ya maji. Zifikirie roho tano zilizomo katika familia yako, zilizostahmilia njaa tokea mawiyo hadi machweyo.

Wewe na wao mumeistahmilia njaa na kiu zaidi kwa kutaraji fadhila za Mungu wenu, lakini muadhini wa Magharibi akiadhini, lazima muyape kitu matumbo yenu. Gharama ya futari yenu, kwa makosefu, ni baina ya shilingi 1700 na 2000. Pato lako ni chini ya shilingi 1000 kwa siku. Je, bado tu hujakula dongo? Hapana shaka, harufu ya dongo unaisikia vyema puani mwako na unamkumbuka vyema Dk. Omar.

Hisabu hiyo haishirikishi daku, ambayo nyumba nyingi haipikwi tena siku hizi. Zile zama za kuamshana usiku wa manane kula daku hazipo tena, maana daku yenyewe haipo. Katika hizo sehemu chache ambazo vigoma vya daku vinaendelea kupita hadi leo, hufanya hivyo kwa ada tu.

Kwa nyumba nyingi, kuwaamsha watu wale daku ni kuwakebehi na kuwaudhi. Katika nyumba hizo, mlo wao wa mwanzo na wa mwisho wakati huu wa Ramadhani ni futari yao. Wala usidhani kuwa wanafanya hivyo kwa ucha Mungu kuwazidi, bali kwa kuwa hawana cha kukila.

Kwa hivyo, si kukithirisha maneno kusema kuwa Ramadhani inatuwia vigumu, ingawa tumo tunaifunga. Tusione watu wanafunga, tukadhani kwamba ndio wanacho cha kuwatosheleza kufuturu. Hapana. Ni hiyo ada ya kiibada tu.

Mtu huanza kuitafuta futari tokea kunapokucha, na Wallahi jua huchwa futari haijakamilika. Hata anapopinda goti kutia kikombe cha uji tumboni mwake, inayotangulia kuingia mdomoni huwa ni ladha ya dongo, sio ya uji huo. Hutangulia ladha ya tabu, dhiki na mateso aliyoyapata katika kuitafuta futari hiyo. Na sasa huwa angalau siku inapita, lakini kesho huwa inakuja. Anakunywa uji, akiyafikiri ya kesho. Hivyo ndivyo Mzanzibari anavyofunga na kufuturu – kwa kula dongo.

Na dongo atalila zaidi ikiwa katika wakati kama huu anaishi hapa Unguja Mjini na akawa na mgonjwa wake katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja. Sio tu kwamba atapaswa kuongeza hisabu ya kununua dawa katika bajeti ya futari, bali pia na madumu ya maji, maana hospitali kuu ya Zanzibar haina dawa wala maji. Ikiwa mtu ana uwezo wa kuyanunua hayo, ndiyo kheri, lakini kama hana, ndio mgonjwa wake adhalilike na ateseke kwa maradhi na uchafu. Hili ndilo dongo tunalolila.

Wakubwa wasitukasirikie tunapowaambia hili. Wasighadhibike tunaposimuliana ladha ya dongo wanalotulisha. Kwamba ni sisi ndio tunaolila, ni sisi ambao ‘tumelishiba’ na sasa ni sisi ndio tunaolipigia soga. Si ndiyo kawaida ya shibe! Sisi ndio tunaoijuwa ladha yake, si wao ambao hata vumbi lake haliwapati. Si stahiki yao kukasirika kwa hilo. Labda, labda la kuwakasirisha ni pale wanaposikia tunazungumzia majumba makubwa makubwa na magari ya kifakhari. Kwamba hayo ndiyo yao, na ndiyo yenye ladha zao. Tunapoyaota na kuyasimulia hayo, huenda ikawa tunawagusa katika nyoyo zao ambazo zinaonekana kughururika nayo.

Lakini ya nini kukasirikia hekaya zetu za dhiki ya fungu la muhogo sokoni, au tabu ya dumu la maji usiku wa manane, au woga wa kuandikiwa cheti bila ya dawa hospitalini? Ni sisi raia wa kawaida ndio tunayoijuwa ladha ya hayo, kwamba sisi ndio wala dongo!

Ingelikuwaje leo hii ikiwa Mhishimiwa Rais ndiye anayetangatanga na kapu lake kutarazaki futari ya siku moja? Ingelikuwaje ikiwa Mhishimiwa Waziri Kiongozi ndiye anayekesha kuvizia dumu la maji? Ingelikuwaje ikiwa watoto wao ndio wanaokosa matibabu hospitalini kwa kuwa hawana uwezo wa kununua dawa? Ingelikuwaje? Yumkini wangeliihisi ladha ya dongo hili tunalolila sisi. Lakini wapi! Nani kasema wakubwa wazima wale dongo? Wao ni wa kula mahanjumati, futari kwa maana ya futari na daku kwa maana ya daku!

Sasa, mambo pekee niwaombayo walaji mahanjumati hawa ni mawili. La kwanza ndilo hilo, kwamba sisi wa kula dongo tunaposema kwamba ni kweli kuwa twalila, wasitukasirikie. Wasitutake tuihame nchi ya mababu na mabibi zetu ati kwa kuwa tunasema ukweli kuhusu hali halisi ilivyo. Twende wapi?

Kututaka tuhame nchi kwa kuwa tunasema ukweli ulivyo ni kutafuta viganja vya kufichia nyuso tu, bali bado tatizo linabakia pale pale. Tatizo ni kushindwa kwa sera zao kuyanyanyua maisha ya watu waliyoapa kuyatukuza. Tatizo ni ‘kutulisha dongo’. Ikiwa kuna lolote la kufanywa kwa sasa ni kupambana na sera hizo mbovu, ikiwa zimeonekana hazifai. Au ikiwa tatizo halimo katika sera hizo, isipokuwa ni watekelezaji waliopewa dhamana kwazo, basi suluhu ni kupambana nao na kuwashinda.

Sio kupambana na sisi tuliokwishaatilika na sera hizo. Sisi tayari tumeshakuwa wahanga wa mapambano, maana wao ndio waathirika wa kwanza na wa pekee. Hatuna tena tunalopoteza tukiendelea na mapambano. Wenyewe tu maiti kwenenda. Si hayati si mamati!

Ombi la pili niwaombalo wala mahanjumati wetu ni tafakuri yao tu. Kwamba asilimia yao kubwa ni Waislam. Msingi mmoja wa Uislam ni imani ya kuwepo kwa maisha baada ya haya, yaani tutafufuliwa tulipwe kwa matendo yetu na kisha tuishi milele na milele. Tusife tena. Basi, angalau kwa hilo tu, wanapaswa kuutumia mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kukaa na kutafakari dhamana walizojitwisha mabegani. Wanapaswa kuujuwa na kuukiri ukweli kwamba raia wanaowaongoza wana hali ngumu ya maisha na wao wakiwa kama watawala wana dhamana ya moja kwa moja kwa hali hii. Kwa kila raia anayelala na njaa, anayekosa matibabu, na anayekosa maji, hata pawe na sababu tisiini na tisa, basi ya mia moja ni maongozi yao mabaya ya nchi.

Kulijuwa hilo na kulifanyia kazi ndio stahili ya maisha yao ya kisiasa na ya kiroho. Kwamba baada ya yote wanawajibika moja kwa moja kwa umma na kwa Mungu kwa mabaya na mazuri yanayoambatana na maongozi yao. Kadiri wanavyojifanya wakaidi na kuepuka mzigo unaowastahikia, ndivyo wanavyojikaribisha karibu na ghadhabu na adhabu ya umma na ya Mungu. Na wajuwe kuwa kesho kuna hesabu.

Nimalizie makala hii kwa kumbukumbu ndogo. Katika gazeti la Majira la Aprili 5, 1999, Makamo Mwenyekiti wa CCM-Bara, John Samuel Malecela, alinukuliwa akisema kwamba ikiwa Marais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Daniel Arap Moi wa Kenya, Desire Kabila wa Kongo Kinshasa, Pierre Buyoya wa Burundi na Benjamin Mkapa wa Tanzania wangelikufa na kuhukumiwa kwa matendo yao, basi ni Rais Mkapa peke yake ambaye angelikwenda peponi. Wengine wote wangelitupwa motoni kwa kuwa katika nchi wanazoziongoza kuna maelfu ya watu wanaouliwa katika kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Maneno hayo yana maana kubwa sana, sio kwa kumtabiria kwake pepo Rais wetu, bali kwa kuwa yanawasilisha ujumbe na dharau ndani yake. Ujumbe wake ni kwamba kila kiongozi wa nchi ni dhamana kwa yale yanayotokezea katika nchi yake, ama ikiwa anashiriki moja kwa moja au ikiwa ni vyenginevyo. Hapa Malecela hakukusudia kuwa marais hawa wanashiriki katika vita hivyo na kutoa amri za watu wao kuuwana wao kwa wao, lakini alikusudia kuwa wao ndio wenye dhamana ya maisha na roho za watu hao. Kuendelea kuuana na wao (marais hawa) wako madarakani, ni kushindwa kwao kuyasimamisha mauaji hayo, na, kwa hilo, Mungu hatawasamehe.

Dharau yake ni kwamba Malecela aliyaona yaendelayo katika nchi za wenzake ni makubwa sana kuliko yale yanayoendelea katika nchi yake mwenyewe, hata akafika pahala pa kumtabiria pepo Mkapa. Ndani ya nchi yake, kuna watu wanaokosa maji, chakula na hata matibabu, na hivyo wanaokula dongo na kufa njaa. Hawa je, nao!?

Dira, Na. 49, Novemba 12-20, 2003

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.