UCHAMBUZI

Masta Saimoni kasema mufe njaa!

NAKUMBUKA tulipokuwa wadogo, chini ya mwangaza wa mbaamwezi, tulikuwa tukicheza mchezo huu Masta Saimoni Kasema. Nitaelezea kidogo jinsi mchezo huu unavyochezwa. Huwa ni kundi la watoto linalopokea amri kutoka kwa kiongozi wao. Ukiona namna kiongozi huyu anavyojitia kuamuru kwa makeke na kamandi, unaweza kudhani kuwa ni afande wa jeshi; na vile kundi la watoto linavyoitikia amri kwa utiifu wa hali ya juu, bila ya kuhoji wala kujadili, unaweza kudhani kuwa ni makruti kambini.

Vijana wakiburuta mikokoteni karibu na bandari ya Malindi, Unguja.
Vijana wakiburuta mikokoteni karibu na bandari ya Malindi, Unguja.

Amri ya ‘afande’ huyu hutolewa mara moja tu, hairejewi. ‘Makruti’ hutakiwa waitekeleze kwa ghafla hiyo moja, bila ya kuongeza wala kupunguza chochote. Hakuna sekunde ya kufikiri wala kuzubaa. Amri gani ataitowa ‘afande’, inatokana na huyo Masta Saimoni anavyomtuma kichwani mwake. Kwa mfano, ‘afande’ wetu angelituamuru kwa sauti kali: “Masta Saimoni kasema mvutane masikio!” Hapo hapo, sote kwa mpigo, kama askari wa gwaride, tungeligeukiana na kuanza kuvutana masikio. Ole wako upate mtoto mtundu kuwa mwenzako katika kuvutana huku, na ‘afande’ kichaa, ambaye ataawachia katika hali hiyo kwa dakika nzima, utasikia moto ukikuwakia mawambani!

Mara nyengine, ‘afande’ angeliweza kutuamuru tufanye jambo la kipumbavu sana. “Masta Saimoni kasema mchekane!” Hapo, akina miye, tungelianza kunyoosheana vidole na kuchekana, hadi tunaanguka chini huku tumejishikilia mbavu. Bado tunachekana tu. Lakini mara ‘afande’ angeliweza kugeuza kibao: “Masta Saimoni kasema mlie!” Ni ngumu kwa mtu mzima na akili zake kubadilisha kicheko kuwa kilio kwa sekunde moja, lakini kwa mtoto anapokuwa mchezoni ni kupwesa na kupwesua tu.

Kwetu, kuendelea kubakia mule mchezoni ndio kitu cha thamani kubwa. Basi, haidhuru tungeligharamika kiasi gani, sisi tungelipigania tu mpaka dakika ya mwisho. Nakumbuka kuwa wakati mwengine afande wetu akituamuru tulie kama ng’ombe, turukeruke kama ndama, tukasirike kama baba, tusinzie kama pono, nasi tuliyafanya yote. Kwetu ni usugu tu, hakuna lisilowezekana mpaka tushinde. Hata hivyo, kwa kuwa lazima wengine waondoshwe duarani, basi kosa dogo tu lingelitosha kumfanya ‘afande’ amuambie mmoja wetu: “Nje!” Mwisho wa mchezo, au saa zinapokuwa nyingi na mama zetu kutuita ‘tushii tukalale’, wachache ndio ambao wangelibakia kuwa ‘makruti’ watiifu kwa ‘afande’ wa Masta Saimoni.

Hizo ni kumbukizi za utotoni. Lakini kumbe maisha yana tabia ya kwenda na kujirudia. Yale uliyokutana nayo utotoni huweza kukutana nayo tena katika mduara wa maisha yako ya utu-uzimani. Tafauti ni kwamba katika maisha haya sasa, hayo yanakuwa sio tena mchezo, bali ndio uhalisia wa mambo. Wewe, ukiwa kama raia wa kawaida, unajikuta kuwa u kruti tu wa afande wa Masta Saimoni (serikali yako); na kila unapozunguka, unamuona afande wako amekusimamia akikuamuru, japo si lazima kwa maneno. Na sasa, wewe na yeye, tafauti na kule utotoni, hamuigizi tena. Munafanya kweli kweli. Huyu ana uwezo wa kukuamuru: “Masta Saimoni kasema ubebe madumu ya maji!” Nawe ukayabeba kikwelikweli, maana kama hukuyabeba, unywe nini. Upikie nini? Unawie uso nini?

Ikiwa wewe ni mfanyakazi wa serikali, afande wako atakuamuru: “Masta Saimoni kasema fanya kazi siku thalathini, kula siku kumi!” Na wewe huna budi illa kutii kwa unyenyekevu na taadhima. Kumbe ufanye kipi chengine, ikiwa huyo Masta Saimoni ndiye mwenye kila kitu? Yeye ndiye mwenye mshahara na ndiye mwenye nguvu. Anakulipa siku atakayo (siku hizi tumeanza kurudia yale yale ya mshahara wa tarehe arubaini). Anakulipa kima akitakacho (kile kile kikia cha mbuzi cha maisha ya kijungu mwiko). Na, zaidi, anakupa kwa staili aitakayo (anakukata mafuta ya mwenge, mifuko ya maendeleo, maafa na mingineyo kibao). Unajikuta kuwa kumbe hata huu mshahara wako si wako, ni wake yeye afande.

Lakini, kwani una uchaguzi mwengine zaidi ya huo wa kuupokea na kuula kwa siku hizo kumi mshahara ulioufanyia kazi kwa mwezi mzima? Huna, na kama unao ufanye tukuone! Ni kuacha kazi, ukafa kwa njaa na watoto. Ni kukataa mshahara, ukazidi kudhulumika. Au ni kuendelea kufanya kazi, ukamalizika. Huu ndio mduara wako wa maisha. Kwamba wewe ni kruti wa Masta Saimoni tu. Na, hata baada ya yote hayo, ukijilegeza (ikiwa huku kweli ndiko kujikaza), utatolewa mchezoni. “Nje!” afande atasema. Na kesho yake, hata kama utatoka katika duara lile la ajira yake, bado unakokwenda kokote afande wa Masta Saimoni yuko. Nenda kajiajiri mwenyewe, uone atakavyoziziba tundu zako za riziki. Mfano ni huu wa serikali kuwafukuza makuli bandarini kwa kisingizio cha kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo. Hii ni sawa na kuwaambia: “Masta Saimoni kasema muzurure!”

Nao sasa wataanza kuzurura kama inavyoonekana kwa makuli hawa. Kumbe wafanye nini zaidi ya kutii kwa utiifu na taadhima – ishara ya uduni na udhalilifu wao mbele ya dola waliyoiweka madarakani wenyewe. Na kwa kuwa ile ndio kazi pekee waliyoitegemea kuendeshea maisha yao na ahli zao, kuwaondosha hapa ni sawa na kuwataka wafe kwa njaa.

Nakusudia kusema kuwa amri ya kuwafukuza makuli bandarini Zanzibar imetoka kipamba-mbavu na haina chembe ya busara. Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Zubeir Ali Maulid, anasema kwamba yeye haoni kuwa bandarini ni pahala pa kutafutia ajira, isipokuwa lile kundi la watu wanaojazana pale ni la vibaka na wahuni tu. Na, hivyo, kwa kuwa suala linalozingatiwa hapa ni usalama katika eneo la bandari, amri ya kuwafukuza haijadiliki! (Dira, Na. 41, Septemba 12-18, 2003)

Amri haijadiliki. Ndiyo kawaida ya amri za Masta Saimoni kutokujadiliwa – kama tulivyokuwa tukicheza utotoni. Ukishindwa kutekeleza haraka amri ya afande aliyetumwa na Masta Saimoni, ndiyo ujuwe kuwa umeshindwa, na adhabu yake ni kutoka mchezoni. Hakuna kufikiri wala kujadili!

Lakini, kama ninavyosema mara nyingi, hizi ni zama mpya: zama za kila jambo kujadiliwa, hata aliseme nani. Zubeir Ali Maulid si Mtume wa Mungu, wala maamuzi ya Baraza la Mawaziri, ambalo yeye ni mjumbe, si maamuzi kutoka kwenye Arshir-Rahman. Kwa hivyo, tutayadili. Hakuna asiyekubaliana na umuhimu wa kuimarisha ulinzi na usalama katika nchi yetu. Sote tunahitaji sana kuwa katika usalama – wetu, wa watoto wetu, na wa mali zetu. Kwa hivyo, mjadala sio kwamba tuimarishe au tusiimarishe usalama katika maeneo ya nchi yetu, lakini ni namna ya kuuimarisha usalama huo.

Kinachoonekana hapa, kwa amri hii ya Masta Saimoni kuwafungia makuli nje ya gati na kisha kututajia ulinzi na usalama, ni kubeba bango tu. Kila mara, serikali inapoumba matatizo kama haya yanayoyagusa maisha ya watu moja kwa moja, hujidai kunyanyuwa bendera nyeupe ya amani na utulivu. Ikasema kuwa inafanya hivyo kulinda usalama wa watu. Ili iweje? Watu warudi nyuma. Wale watakaosonga mbele, wawachukuwe wakawasweke ndani. Kisa? Wamevuruga amani na utulivu!

Angalia hapa. Serikali inaumba tatizo kwa makusudi, halafu watu wanapojipapatuwa kutokana na tatizo hilo, inawaandama. Kwa kufanya hivyo, ndio inajiona kuwa inalitatuwa. Kama mchezo vile, inaumba yenyewe na inaumbua yenyewe. Ndiyo, ulinzi na usalama unatumika kama kisingizio tu. Watu wana usalama gani ikiwa matumbo yao ni matupu? Nani anamlinda nani na anakilinda nini ikiwa hajashiba? Msamiati huu wa ulinzi na usalama unamuhusuje mzee wangu wa miaka sitini, ambaye ameyaishi maisha yake yote akitegemea rikwama au mgongo wake kuchukuwa mizigo pale bandarini? Unamuambia afe njaa na watoto wake, na bado unataka aamini kuwa unamlindia usalama wake?

Au kijana mwenzangu ambaye jaala yake ya maisha imemsukuma pale bandarini. Hajapenda kuwapo hapa, lakini yupo kwa kuwa ndipo penye tundu lake la kukingia riziki na kwa kuwa serikali imeshindwa kumpa ajira nyengine. Yeye ni dei waka. Hivi sasa amri ya afande wa Masta Saimoni inamuamuru: “Ondoka hapa. Wewe kibaka, wewe muhuni. Hapa hapana ajira!” Huku ni nini kama si kutukana wakunga na hali uzazi ungalipo?

Hawa si wizi, si wahuni. Wizi na wahuni wala hawatajwi kabisa. Hawa ni watarazaki wanaojitutumua na magunia kulijaza tumbo lao, tumbo tu. Si zaidi ya hapo. Pengine wengi wetu hatuna nafasi ya kujisomea riwaya, lakini hebu tupate wasaa mdogo wa kupitia riwaya ya Kuli ya Shafi Adam Shafi. Humo tutaipata picha kamili ya kuli wa bandarini Zanzibar. Ni mtu dhalili, masikini, fukara. Rasilimali yake kubwa ni nguvu yake. Siku nguvu ikiisha, ndio khatma yake imewadia. Hana mbele, hana nyuma. Utawaitaje watu hawa kuwa ni wahuni, kuwa ni vibaka?

Kwani kuna mtu muaminifu kama kuli wa bandarini Zanzibar? Unampa mzigo wako kutoka melini ukiwa humjuwi hakujuwi. Wewe unakwenda kumsubiri kituo cha daladala Darajani. Baina ya Malindi bandarini hadi Darajani, pana masafa makubwa na shughuli nyingi, ikiwa mtu ataamua kukuingiza mjini. Lakini mzigo wako unafika salama, hukuti hata sindano iliyopunguwa!

Kuna watu hapa wanaokabidhiwa ofisi za umma wakiwa wanakaa kwenye nyumba za kupanga na wanachomiliki ni mkweche wa baiskeli tu. Miaka miwili baadaye, wana maghorofa na mabenzi manne. Ukiangalia mishahara yao, utakuta kuwa wasingeliweza kujenga hata nyumba moja kati ya hizo ikiwa walikuwa waadilifu. Nani kibaka hapo?

Zaidi ya hayo, huwezi kumuondosha kuli bandarini kwa kumuambia kuwa hapa si pahala pa ajira. Kwa anayeijuwa historia ya kiuchumi na kijamii (socio-economic history) ya Visiwa hivi, hawezi kabisa kupaita bandarini si pahala pa ajira. Kwa Zanzibar, bandari ndio kila kitu. Sio tu kwamba ndipo penye ajira, bali ndipo penye maisha yote ya Zanzibar.

Mzunguko mzima wa maisha ya Zanzibar, huanza na kumalizikia pale. Thamani na nafasi ya bandari kwa Zanzibar ni ile ambayo Waingereza wangeliiita sufficient and necessary condition. Bila ya bandari, hakuna Zanzibar, na hicho ndicho kinachodhihirika sasa. Na hilo sitaki nilirudie tena, limeshazungumzwa zaidi ya mara alfu kumi.

Kwa ufupi ni kuwa ajira zipo bandarini. Pana ajira za kuwaajiri vijana wetu wote na zitakazobakia tukawatafutia watu kutoka nje kuzifanya. Tatizo ni kuwa tumekosa dira ya kuifanya bandari kuwa mahala pa ajira. Hatuna watawala ambao wana uwezo na nia ya kisiasa kuifanya bandari ya Zanzibar kuwa kweli bandari yenye kuleta maslahi kwa watu wake.

Tuna watawala wanaodhani kuwa kila jambo huwa tu, bila ya kulipangia na kulifanya liwe. Ndio maana raia wenyewe, kwa kujuwa kuwa hapa bandarini ndipo yalipo maisha yao, ndipo zilipo roho zao, wanapachangamkia. Hawa si wizi wala si wahuni. Si watunga sera wala si wapitishaji maamuzi vikaoni. Hawa ni waganga njaa. Watarazaki tu!

Hili ni kundi la raia masikini, mafukara, dhalili. Na kuwepo kwake ni dalili za kushindwa kwa hao wanaovaa suti wakatimua vumbi na mabenzi makubwa makubwa kuelekea vikaoni kutunga sera. Uwepo wao ni ushahidi wa kushindwa kwa mfumo wa kiuchumi tunaokwenda nao. Hivi sasa ukipita pale bandarini utakuta mapote kwa mapote ya watu waliovalia mararu yao wakicheza bao au keramu. Maskini, wote wahanga wa Masta Saimoni Kasema.

Ziangalie zile nyuso zao. Ione ile sura ya umaskini walioufumbata, ule nyonge walionao na kukata kwao tamaa. Mlango wa bandari uko mbele yao. Lakini getini pana afande ambaye hamruhusu yeyote kuingia illa watu maalum. Kwa kuwa huko nyumbani hawana jengine la kufanya, mazoea huwasukuma hapa kila siku. Asaayakunkher, anaweza kutokea mtu akawaita wambembee mzigo angalao kutoka pale nje ya geti hadi Darajani.

Lakini wembe mkali. Huenda siku nzima ikapita wakilikodolea macho tu lile lango. Na mwisho huondoka, hawana walichoambulia. Wamekuja na njaa, wanarudi na njaa. Wametokea kubaya, wanapita pabaya na wanakwenda kubaya.

Huyu ndiye kuli wa bandarini Zanzibar, ambaye umasikini na unyonge wake unamfanya aonekane si mtu wa salama, si mtu wa hishima. Amezuiwa kuingia bandarini, kwa kuwa humo munalindwa usalama. Tabaan, na haya “yana mwisho” kama alivyosema Rashid wa Shafi Adam Shafi kwenye Kuli!

Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Dira, mwaka 2003, lakini mwandishi hakumbuki nambari ya toleo wala tarehe iliyotoka.