UCHAMBUZI

Kweli SAFINA itatweka?

WAKATI Dira ilipoanza kuuzungumzia ujio wa SAFINA, kuna waliodhani kuwa huo ulikuwa uzushi. ‘Mafundi’ wenyewe wa SAFINA walipojitokeza kutangaza kuwa wamo kazini kuiunda, wakaonekana wanatania tu. Na sasa, ikiwa safari yake imeshaanza, swali linaloulizwa ni ikiwa je, kweli itafika salama Suuqul Mathaan!?

Suuqul-mathaan, Soko la Viwili Viwili, ndipo inapoaminika kushukia Mtume Nuh (A.S.) na kaumu yake baada ya kupanda Safina iliyowanusuru na gharika iliyoshushwa dhidi ya watu wake ambao walikataa kuuitikia mwito wa mabadiliko. Ndipo kizazi cha viumbe tuvionavyo leo kilipoanza tena kuujaza ulimwengu. Ndipo matumaini mapya ya maisha yalipoanza kujengwa na kupewa maana.
Kwa Wazanzibari, Suuqul Mathaan ni ishara ya mahala ambapo SAFINA ingelitarajiwa kuwafikisha. Pahala penye Zanzibar hasa kwa maana ya Zanzibar – nchi yenye uhuru wa kujiamulia, kujipangia na kujifanyia. Penye Tanzania hasa kwa maana ya Jamhuri ya Muungano halali na wa hiari wa nchi mbili zilizo huru. Penye haki ya kujiita huru, ambapo matumaini mapya ya maisha ya Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari yataanza kujengwa na kupewa maana. Hayo ndiyo matarajio.
Penye matarajio haya, ndipo linapokuja hilo swali ikiwa kweli SAFINA hii itawashusha abiria wake katika kituo ilichowaahidi. Na swali hilo linakuja sasa kwa kuwa pameshaanza kuonekana dalili za kuvunja moyo. Tayari Safina imeshaanza kupigwa na mawimbi makubwa makubwa hata safari haijafika robo. Tayari pameshaanza kuwa na migogoro baina ya viongozi wake huku wakizuiana kujiunga na chama au kutoana madarakani. Je, kwa mwenendo huu, si karibuni tu misumari itakuwa i mbali mbali na mbao?
Tukubaliane kuwa huu ni mwanzo mbaya kidogo, ingawa katika harakati za kuleta mabadiliko si kitu cha kushangaza sana. Inaweza kuchukuliwa kuwa ni sehemu ya ‘kuitoharisha’ harakati, maana harakati si jambo rahisi hata kidogo: ni jambo gumu la kiroho, ambalo lazima liwe na watu walio tohara, sio wachafu. Tuseme ndio hivyo wana-SAFINA wameanza kutoharishana!Hata kwa safari ya Mtume Nuh (AS) yalikuwa yayo. Mpaka kuweza kutweka katika Suuqul Mathaan, safari yake ilikabiliwa na mengi, likiwemo la kuzuiwa kumuingiza mwanawe mwenyewe katika chombo hiki kwa kuwa hakuwa na sifa za kuingia. Bila ya shaka, jambo hili ni gumu sana kulimeza kifuani mwa mzazi.
Lakini kwa kuwa mtoto huyu alikosa ‘tiketi’ ya kuingia kwenye Safina, yaani kuuamini na kuuitakidi mfumo mpya wa maisha uliokuwa ukitangazwa na baba yake, hakuwa na haki ya kuingia katika chombo. Matokeo yake akaangamia pamoja na walioangamia! Waliokubaliwa kuingia mule na kuokoka na gharika ile, ni wale tu walioipokea na kuikubali imani hiyo – walioyapokea mabadiliko kwa nafsi zao. Maana ni wasafiri wa kweli tu ndio wa kuipanda Safina!
Kwa kuwa SAFINA, kama SAFINA, ni mwendelezo wa harakati za kisiasa Visiwani ulioanzia tangu zamani, na kwa kuwa huu ni mchakato wa jitihada za Wazanzibari wenyewe kujitafutia uhuru zaidi wa nchi yao kwa ajili ya maisha yao na vizazi vyao, basi uwezekano wa kuyakata mawimbi upo, japo isiwe rahisi hivyo.
Kwamba si rahisi kuendesha na kufanikisha harakati. Na harakati za SAFINA si za leo wala jana. Ni za kitambo mno, tokea Wazanzibari wajijuwe kuwa hawako huru na wathamini hali ya kuwa huru katika nchi yao. Hilo lina mizizi yake mbali sana kwenye historia ya harakati za ukombozi wa Visiwa hivi na kila mara huenda na kujirudia, kwa kuwa uhuru ni milki ya mwanaadamu asiyohimili kupokonywa.
Ukweli huo kwamba SAFINA ni vuguvugu la kisiasa (political movement) na sio chama cha kisiasa tu, ndio unaorudisha matumaini kwamba haitoweza kufa kirahisi kiasi hicho hata kama jitihada za makusudi zitaendelea kufanywa dhidi yake. Harakati ya kisiasa ni imani, ni kitu cha kiroho, ambacho hujua kuanza tu lakini hakijuwi kumalizika. Hiyo ndiyo sifa muhimu ya roho, yaani kuwa kwake na mwanzo lakini kukosa ukomo.
Harakati ya kisiasa huongozwa na itikadi ya ndani kabisa ambayo huhitaji kuhuishwa katika maisha ya kawaida. Mwenye itikadi hiyo, kila siku huishi akiamini kuwa itikadi yake ndiyo na hivyo anahakikisha kuwa inafanya kazi na kushinda mahala popote na wakati wowote. Kwa ufupi, harakati ni imani iliyojengewa mfumo wa utekelezaji. Mwenendo wa matukio hapa petu, unaonesha kuwa SAFINA ni harakati kwa maana hiyo.
SAFINA ni matokeo ya dharau ya CCM kwa uhuru wa Zanzibar. Ni pande lililomeguka kutoka CCM, likiwa limekerwa, pamoja na mambo mengine, na nafasi ‘iliyowekwa’ Zanzibar katika Muungano. Ni maoni ya walio wengi kwamba Muungano huu unatumiwa na Tanganyika kuikandamiza na kuitawala Zanzibar kwa mlango wa uwani.
Kama nchi huru iliyoungana na nchi nyengine huru ‘kuiumba’ Tanzania hii, Zanzibar imetengwa kando katika masuala na maamuzi yahusuyo khatima ya nchi hii, bali hata kwa yale yanayoihusu khatima ya Zanzibar pekee kama Zanzibar. Katika Muungano huu, sauti ya Wazanzibari haisikilizwi wala haijaliwi, isipokuwa tu kama itaakisika na matakwa ya Tanganyika, chini ya kivuli cha Muungano wa Tanzania.
Mfano mmoja unaotajwa ni huu wa uteuzi wa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama kinachoongoza dola, CCM. Inasemwa kuwa katika kuelekea uchaguzi wa 2000, Wazanzibari waliweka mgombea wao, lakini kwa kuwa wao si chochote si lolote, CCM Dodoma ikamuondoa na kumuweka imtakae. Hii ilikuwa ni dharau isiyostahmilika kwa kuwa iliugusa uhuru wa Wazanzibari. Na basi ni hapo, pa kuusaka uhuru hasa wa Zanzibar, ndipo SAFINA ilipochipukia na kuotea!
Ikiwa hili la kuutafuta uhuru wa Zanzibar ndilo lililo nyuma ya azma ya SAFINA – na naamini ndilo – basi hizo ni harakati kongwe za Wazanzibari zilizopo tangu na tangu. Pengine kutokana na mabadiliko ya kiwakati, kitawala na kimwamko, harakati hizi zimekuwa zikibadilika sura na kujivisha koti hili au lile kwa mujibu wa mahitaji, lakini bado zimeendelea kubakia kuwa ni harakati hai.
Tawala zote zilizowahi kuvitawala Visiwa hivi zilikumbana na harakati hizo na hazikuwachwa zipumue, hadi lengo lilipofikiwa. Na kama ilitokezea wakati watu wakapitikiwa kidogo, na kuja kushtukizia baadaye kuwa kumbe uhuru wao umo katika khatari ya kuporwa, harakati hizi zilifufuka upya kwa morali ile ile. Na ni hilo hilo ndilo lililoiibua SAFINA hivi sasa. Je, kuna wa kuliviza?
Hakuna! Hakuna kwa kuwa dhati ya maisha, katika kiwango chochote na nyanja yoyote ile, ni uhuru. Kuanzia kiwango cha mtu binafsi, familia, kijiji, mji, hadi nchi, na zaidi ya hapo; iwe katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni au nyenginezo, ni uhuru tu ndio unaoyapa maana maisha. Bila ya uhuru maisha huwa chapwa, yakawa hayana thamani kuyaishi. Ndio maana ikasemwa kuwa ni afadhali kuishi siku moja kama mtu huru kuliko kuishi miaka mia moja kama mtumwa.
Hapa tunazungumzia uhuru katika kiwango cha nchi, ambapo kwa sasa ni shida sana kuuthibitisha uhuru wa Zanzibar kuliko kuukanusha. Hapa ndipo SAFINA ilipokuja, kama desturi ya kawaida tu ya wakati. Kwamba wakati wowote watu wanapong’amua kuwa kumbe uhuru wao na utu wao umekuwa ukikhatarishwa, kitu cha mwanzo wanachokifikiria ni kuulinda kwa nguvu zao zote.
Uhuru wa Wazanzibari, kama raia wa nchi huru, umekuwa ukichezewa sana. Nafasi ya nchi yao, kama nchi huru, imekuwa ikidunishwa mno. Hishima na utukufu wa Uzanzibari, kama utambulisho wa nchi, umekuwa ukidharauliwa kupita kiasi. Kufika hapo, hakuna lililobakia tena illa kurudi katika harakati za kukilinda kile ilichobakishiwa Zanzibar na kukirudisha kile ilichokwisha kupokonywa. Harakati kama hiyo haiwezi kuzimwa na yeyote.
Historia ya CCM inaonesha kuwa kila siku imekuwa ikiwakosea, na hivyo kuwakosa, Wazanzibari panapohusika suala la nchi yao kama nchi huru kwenye Muungano. Tunakumbuka ilipomlazimisha Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi kujiuzulu urais wa Zanzibar kwa kisingizio cha kuhatarisha Muungano. Tunakumbuka ilipowafukuza akina Maalim Seif Sharif Hamad kwa kupinga mwelekeo wa Muungano kwa Zanzibar. Hao wote walikuwa ni waendelezaji wa mchakato wa harakati hizi za kuutetea uhuru wa Zanzibar.
Kwa kuwafukuza katika chama, pengine CCM iliamini kuwa imefanikiwa kuziua harakati hizi. Lakini, kama inavyosemwa kwamba ukifunga mlango mmoja, mingine kumi iko wazi, ndivyo ilivyokuwa kwao pia. Harakati zikaendelea. Kwa hivyo, harakati hizi hazijapata kufa hata siku moja hata kama jitihada za makusudi hufanyika kuziua.
Kwa kuwa CCM haitaki kujihakiki upya – au tuseme haitaki kukubali tahkiki mpya – juu ya mtazamo wake mkongwe kwa nafasi ya Zanzibar katika Muungano, basi itarajie sana kuzidi kuwapoteza Wazanzibari wengine kadiri siku ziendavyo.
Ikiwa haitaki kukubali kuwa Zanzibar ni nchi huru, kwamba Wazanzibari ni watu huru, na kwamba waachiwe haki yao ya kujiamulia, kwa mfano nani awe rais wao, basi Safina zitaendelea kuundwa kila uchao kwa mbao za mti huu huu, Msisiemu.
Na si lazima kuwa zote ziitwe tena Safina. Sasa zinaweza kuitwa Manuwari au Nyambizi ili kuashiria nguvu, usasa na uwezo zaidi, lakini bado kilichopo nyuma yake kikawa ni kile kile: harakati za uhuru wa Zanzibar. Kuna mtu aliwahi kuuliza: “Je ingeliwezekana kuwepo kwa Marxism bila ya Karl Marx?” Akajibiwa: “Ndiyo, isipokuwa ungeliitwa kwa jina jengine tu!”
Na hapa, basi hata kama hapakuundwa SAFINA hii, bado harakati ndani ya CCM zingelikuwepo tu, kwa kuwa sababu za kuwepo kwake zipo. Na haiwezekani kuziua harakati hizi bila ya kuzizuia sababu zinazozifanya ziwepo. Haiwezekani hata kwa kufanya jitihada gani! Hivi sasa tunashuhudia SAFINA ikiandamwa, kama chama kipya cha kisiasa, ili isije juu. Ndiyo, kama chama cha kisiasa, SAFINA inaweza kufa kwa haraka sana kwa kuwa ni rahisi kukimaliza chama. Nunua viongozi wake. Funga jela wafuasi wake. Choma moto matawi yake. Chana bendera zake. Ua waandamanaji wake. Ama fanya chochote uwezacho, ikiwa kwako chama kinamaanisha haya unayoyaona kwa macho yako.
Lakini panapohusika harakati za umma kupigania uhuru na haki yao, hicho hakiwezekani asilan abadan. Harakati hazifi, na hudumu mfano wa chembe chembe za urathi katika kiwiliwili, genes, ambazo husafirishwa kizazi hadi kizazi. Harakati hazimalizwi kwa kununua watu, kuyachoma moto matawi yao, au hata kwa kuwaua. Bali humalizwa kwa kukidhiwa haja inayopiganiwa, yaani kuisimamisha imani inayoitakidiwa katika maisha ya watu.
Na hapa petu, ile imani kwamba Zanzibar ni nchi huru, kwamba Wazanzibari ni watu huru, na kwamba Uzanzibari ni uhuru, haijapata kusimamishwa. Ndio maana harakati za kuisimamisha haziwezi kufa mpaka hapo itakaposimama. Changamoto kwa wale maadui wa SAFINA ni kulijuwa hilo, kabla ya kuekeza mapesa, nguvu na wakati wao mwingi kukiua chama, kumbe harakati i pale pale!
_____________________________________________________
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Dira Zanzibar kabla ya kufungiwa gazeti hilo mwaka 2003.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.