UCHAMBUZI

Kwa mtaji huu, Zanzibar yetu itamezuka?

MSHAIRI mmoja aliwahi kuandika ushairi alilouita “Haifanyiki”, ambao naomba niunukuu hapa:

Ilivyovunjika, haikandiki
Ilipokatika, hapaungiki
Ishanjagika, haiundiki!

Ilipopelekwa, haivutiki
Ilikochomekwa, haichomoki
Ishapofundikwa, haifunduki!

Ishatuponyoka, haipatiki
‘Livyotatizika, haitatuki
Ishahusudika, haiongoki!

mohammedSiwezi kujuwa ni kipi hasa hicho anachokiona mshairi huyu kuwa kimeshaharibika mno kiasi hicho ambacho hakiwezi tena kutengenezeka. Kinaweza kuwa chochote. Yumkini ni yeye mwenyewe tu ndiye anayekijuwa kilichomchoma hata akaamua kutoa dukuduku lake kupitia ushairi huu.

Lakini, kwa haraka haraka tu, ninachoweza kukisoma baina ya mistari ya ushairi huu ni taswira ya kuvunjika moyo. Mshairi analia kilio cha kukata tamaa. Anaonekana kuwa hana hamu tena ya chochote wala lolote, maana hata akajitahidi vipi, ndiyo Haifanyiki! Haoni kuwa kuna mbinu yoyote inayoweza kufaa kuitengeneza hiyo iliyokwishaharibika. Hakuna tena linaloweza kuwa!
Nimesema siijuwi ni ipi hiyo isiyoweza kufanyika, lakini nimeamua kuutumia ushairi huu kuitafsiri nchi yetu. Kwa muktadha wa makala hii, hiyo iliyokwishafika pahala hapa Waingereza wapaitapo a point of no return, ni Zanzibar yetu.
Ingawa mimi bado sijavunjika moyo moja kwa moja kama alivyovunjika msahiri wetu, na bado naamini nasru minallahi fat-hun qariib, lakini, kama Mzanzibari, niseme kuwa sipendezewi hata kidogo na ushiriki huu mbovu wa wanasiasa wetu panapohusika nafasi ya Zanzibar katika Muungano wa Tanzania.
Sipendezewi, kwa kuwa naona badala ya kufanya jitihada za kuimezua Zanzibar, wao wanazidi kuikokomeza. Labda wanataka imezwe zaidi na zaidi hata ile ncha isionekane!
Wanazidi kuishindilia kwa mikono na miguu kusudi ijae tele, na ishindwe kabisa kutoka. Nakhofu kwamba kwa mtaji huu tusafiriao sasa, basi punde tu itakapotajwa Zanzibar, itafuatiwa na innalillahi wainna ilaihi raaji’uun!
Ninakhofu kwamba miaka ishirini tu ijayo, ikiwa kasi itakuwa ni hii hii, basi zitabakia khadithi tu kwamba Zanzibar iliwahi kuwa nchi yenye mamlaka yake, yenye utawala wake, iliyokuwa na hivi na vile. Waarabu husema kuntu fi’lu maadhi; ‘ilikuwa’ ni kitendo cha wakati uliopita. Sio sasa tena.
Hizo za ‘ilikuwa’ ndizo khadithi tusimuliwazo leo na wazee wetu. Wanatwambia eti Zanzibar ‘ilianzia’ Mogadishu ya Somalia na kuishia Pemba ya Msumbiji. Eti Zanzibar ‘ilikuwa’ ni dola, ni nchi na taifa huru.
Tukiwauliza ilikuwaje wakaacha ikamegwa hadi ikabakia hivi vijisiwa viwili vitatu tu, wanatwambia: “A Mwingereza, e Mjarumani, i Mwarabu, o Mapinduzi, u Muungano”. Sina hakika ikiwa historia inawahukumu vyema kwa majibu kama haya.
Na sisi, ikiwa tutaendelea na mtindo huu huu tulionao sasa wa kujikubalisha kuiwacha nchi yetu itokomee kwa maslahi ya kibinafsi na, au, ya kichama, basi tujitayarishe na kuja kusutwa na kizazi chetu.
Hapo tutakapokuja kuketi vibarazani tukawa tunawakhadithia wenetu Zanzibar Tuijuwayo (ikiwa watakuja kuwa na hamu ya kutusikiliza), basi nasi tutakuja wapa majibu hayo hayo ya ‘kelije na kelije’.
Maana baada ya kuwakhadithia Zanzibar tuijuwayo, watoto watasema kuwa hiyo ndiyo hasa Zanzibar waitakayo (na ndiyo wastahiliyo kuwa nayo). Sasa sisi wazee wao tuliipeleka wapi? Kutoka Zenj empire hadi Zenj region, tuje tuwaambie nini wenetu?
Hikima ya Kiswahili inasema: “Hekaya ya ukongweni, huandikwa ujanani”. Je, katika huu ujana wetu tunaiandika vipi hekaya yetu ya kuja kusomewa huko ukongweni kwetu?
Ikiwa tunaandika usaliti kwa nchi, bila ya shaka tutakuja kuitwa wasaliti hapo tutakapokuwa tunatembelea mikongojo. Hatutoitwa mashujaa, hatutonasibishwa na uzalendo. Na hata kama hatukufikia umri huo wa mikongojo, bado Siku ya Hisabu ipo. Huko tutalipwa kwa matendo yetu, yakiwamo haya ya kuinakamiza nchi.
Maana nchi ni urithi ambao Mungu huwakabidhisha waja wake ili waulinde na waudumishe kwa ajili yao na vizazi vijavyo. Ikiwa vizazi vyetu vitakuja kufikia mahala pa kuitwa na kuonwa wageni katika ardhi ya mababu na mabibi zao, kutokana na uzembe wetu sisi watangulizi wao, hiyo itakuwa ni dhulma tuliyowafanyia viumbe vyake. Na katika yote, Mungu hasamehe dhulma kwa kiumbe chake. Hata Mwenyewe amejikharamishia kudhulumu, iweje sisi viumbe kwa viumbe?
Nukta iliyo katika mjadala hapa ni hii hatua ya karibuni ya Baraza letu la Wawakilishi kuupitisha Mswaada wa Kuridhia Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Kuanzisha Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora.
Huko kulimaanisha kuipa mamlaka tume hiyo kufanya kazi zake Zanzibar kwa jambo ambalo kimsingi halikuwahi kuwa la Muungano. Kwa maana nyengine, ni kuongeza idadi ya mambo katika orodha ya Muungano. Mimi nashindwa kugundua tafsiri yoyote ya kulipa tendo hilo zaidi ya kukuita kuwa ni kuzidi kuimezesha Zanzibar.
Kabla ya kuifafanua, hata hivyo, naomba ruhusa yenu niuweke wazi huu msamiati wangu wa ‘kuimezua Zanzibar. Nafanya hivyo kwa kusudi la kuondoa shaka katika kile nikikusudiacho. Maana, wakati nilipoutumia kwa mara ya mwanzo katika Dira Na. 31, nilipokea lawama kutoka kwa watu wanaojiona kuwa na uchungu zaidi na nchi hii.
Nililaumiwa kuwa wangu ulikuwa ni msamiati wa kichochezi na kwamba kile nilichokikusudia hasa kwawo ni kuwa Zanzibar ijitowe katika Muungano. Niliambiwa kuwa mimi ni miongoni mwa wale mahasidi wa Muungano wa Tanzania. Kwamba kama ningelipewa mamlaka ya kuamua lipi liwe na lipi lisiwe katika nchi hii, basi la kwanza ambalo ningeliamrisha liwe ni kuvunjwa kwa Muungano huu!
Nataka niseme, na nieleweke hivyo, kwamba sijapata kutamani hata siku moja kuona kuwa Muungano huu unavunjika. Ingawa mimi si katika wale wanaoamini kuwa Zanzibar haiwezi kuishi bila ya kuwemo katika Muungano na Tanganyika, lakini naijuwa thamani ya Muungano kwa nchi yangu, Zanzibar. Nautaka Muungano huu uwepo milele na milele na uwe na mafanikio hadi wenzetu wengine akina Kenya, Uganda, Kongo, Burundi na Rwanda waje wajiunge nasi.
Hata hivyo, pamoja na uumini wangu huo usiotikiska kwa Muungano, nataka niseme, na nieleweke hivyo, kuwa nina mahaba makubwa mno na nchi yangu ya Zanzibar. Kiasi chochote nitakachouthamini Muungano, kamwe sitajaribu kuudhalilisha Watani wangu. Kwangu, kama ilivyo kwa malaki na malukuki ya Wazanzibari wengine, Zanzibar inatambulika kuwa Mama yetu na kwamba ndio utukufu wetu.
Hishima na utu wetu, kama jamii ya kibinaadamu, itaendelea kuwapo tu, pale ambapo nchi yetu ya Zanzibar itabakia kuwa nchi yenye hishima na utukufu wake. Kinyume cha hapo, ni kuwa sisi tutakuwa si kitu. Tutakuwa hatu chochote, hatu lolote, hata kama tutakuwa tunatembezwa kwenye msafara wa magari ya kifakhari uongozwao kwa ving’ora na tukawa tunaishi katika makasri ya vioo vitupu.
Kwa hali hiyo, popote na wakati wowote, mimi nitaendelea kuzungumzia hishima na utukufu wa nchi yangu ya Zanzibar. Na naapa kwa Ismu ya Mungu, Muumba wangu na wenu, kwamba hata siku moja sitostahmilia kuiona nchi hii ikidhalilishwa mbele ya macho yangu. Kuidhalilisha Zanzibar ni kuudhalilisha utu, hishima na utukufu wangu binafsi.
Na kwa hilo, hakuna la kulichelea wala wa kumchelea. Ama iwe mwananchi wa kawaida, kiongozi, chama, jumuiya, taifa kubwa la nje, au hata Umoja wa Mataifa, hishima na utukufu wa Zanzibar ukikhatarishwa, nina wajibu wa kusimama kama Mzanzibari kuutetea.

 

Sitamcha mwananchi, na wala mtawalawe
Kama hawaichi nchi, hishimaye na ummawe
Naapa kiapo hichi, sitawacha wapotowe

Sivunji kiapo hichi, hadi dongo nifukiwe
Simchi msicha nchi, hatta ndugu yangu awe
Nimche naye hatuchi, nikimcha nini iwe?

Huo ndio uzalendo ninaoujuwa. Siujuwi uzalendo wa kuitikia ‘Ndio mzee’ tu hata kama utukufu na hishima ya nchi yangu inadidimizwa. Ni kweli, kama Mohammed Ghassani, sina nguvu yoyote ya kuirudisha Zanzibar hata nyanda moja mikononi mwetu kama imeshachukuliwa pima mia, lakini kukaa kitako na kuyasubiri majaliwa si kitu nilichofundiwa.

Kwa hivyo, kuzungumzia kwangu kuimezua Zanzibar ni katika hizo jitihada za kuitetea nchi yangu. Lengo ni kuirejeshea hishima na utukufu wake, ambao kila siku unayoyomeshwa.
Narudia kwamba ningelitamani sana Muungano huu udumu milele na milele, lakini kattu nisingelitamani kuiona nchi yangu inadhalilika na inafutika katika uso wa ulimwengu. Nisingelitamani hata siku moja nchi hii kutanganyikishwa (kufanywa kuwa sehemu tu ya Tanganyika au kutumikia maslahi ya Tanganyika). Na ikiwa hilo la kuitanganyikisha ndilo linalofanyika sasa, kwa nini tusizungumzie kuimezua, tukaizanzibarisha?
Ningelipenda kuona kuwa pamoja na kuwa kwake katika Muungano na dola nyenzake huru, nchi yangu ya Zanzibar inabaki na inaendelea kuwa Zanzibar. Nisingelipenda hata kidogo kuona wala kusikia kuwa gharama za kudumu kwa Muungano huu ni kuangamia kwa Zanzibar. kwa nini tuangamie? Kwa udogo wetu? Uchache wetu? Ujinga wetu? Au kwa unyonge wetu? Hapana thamma hapana!
Hapa ndipo panapozuka msamiati huu wa kuimezua Zanzibar. Wale ‘wazalendo sana’ waelewe vyema. Wasijitie pambani na kutufanya sisi tunaozungumzia mabadiliko katika muundo wa Muungano kuwa tu maadui wa Tanzania. Baina yetu na wao, sisi tu marafiki zaidi wa nchi hii, maana kama nilivyokwishasema katika Dira Na. 31, Muungano si ukoloni.
Na hilo sikuwa wa mwanzo kulisema. Lilianza kusemwa miaka 40 nyuma. Linasemwa sasa; na litasemwa baadaye, ikiwa maoni ya Wazanzibari hayatazingatiwa katika muundo wa Muungano huu. Huo ndio msimamo wangu.
Mnisamehe kwa kutoka nje ya mstari. Turudi kwenye kiini cha mada ya leo. Binafsi kama ilivyo kwa wenzangu wengine, tumeshanganzwa na kusikitishwa sana na uamuzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutumia uwezo wao wa kisheria kuzidi ‘kuimezesha’ nchi yao katika kitahinani cha Muungano.
Mimi si mwanasheria, kwa hivyo sitaki nichokonowe kwamba aidha Baraza lilikuwa na uwezo wa kisheria kuongeza jambo katika mambo ya Mungano au la, lakini kama raia wa kawaida nataka niiangalie khatima ya nchi yangu katika mchezo huu wa ushindani wa kivyama. Nauita ushindani wa kivyama, maana inaonekana kuwa hapa Wawakilishi wetu wa Zanzibar wamezingatia zaidi maslahi ya kichama katika kuupitisha mswaada huu kuliko kuzingatia maslahi ya kiuwananchi, ya Kizanzibari.
Nakumbuka kuwa yalipoanza kuibuliwa masuala ya kero za Muungano katika Baraza, wakati wa kuchangia hotuba ya Waziri Kiongozi, nilisema kuwa haikuhitaji kuwa mpinzani wa CCM kuipinga sera ya serikali ya CCM. Nilisema kuwa kile kinachohitajika ni kuwa mzalendo tu kwa nchi yako.
Nilisema hivyo kwa kuwa nilikuwa nimeuona ule mshikamano wa Kizanzibari ndani ya Baraza la Wawakilishi wa watu wa Zanzibar, kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar. Wakati ule, Wawakilishi wote, bila ya kujali vyama vyao, walinyanyuka na kusema kuwa Zanzibar yao inaburuzwa na Tanganyika kwa jina la Muungano. Kwamba hilo si jambo linaloweza kustahamilika. Niliwasifu kwa kuwa nilidhani kuwa wanasifika!
Leo hapa nataka nikiri kwamba nilifanya haraka kutoa hukumu hiyo, na hivyo nilikosea. Kumbe inakuhitaji kwanza kuwa mpinzani wa CCM kama umeamua kupinga wazo la serikali inayoongozwa na CCM. Huwezi kuwa CCM, halafu ukajifanya kuwa na msimamo tafauti na serikali yako.
Lazima usahau kila kitu na ukumbuke u-CCM wako tu, kama kweli wewe ndiye. Sahau nchi, sahau uzalendo, sahau hukumu ya kihistoria, sahau mustakabali wa watoto wako mwenyewe miaka hamsini ijayo na kumbuka moja tu. Kumbuka kwamba wewe ni mwakilishi uliyepata kura kwa tiketi ya CCM na kwamba wajibu wako wa mwanzo ni kwa chama chako na sio kwa Uzanzibari wako.
Hiyo ndiyo ambayo ingelikuwa hukumu sahihi, maana ndiyo tuliyoishuhudia. Watu ambao wiki mbili nyuma tu waliichangia hotuba ya Waziri Kiongozi kwa nguvu zao zote kupinga suala la mafuta kuwa la Muungano. Watu ambao walipinga kuburuzwa kwa nchi yao. Na, zaidi, watu ambao hata muswaada huu walisema kuwa si wa haki kwa Zanzibar siku mbili tu kabla ya kuwasilishwa Barazani na wakaapa kuuzuia usipite kwa nguvu zao zote.
Watu hawa, Wawakilishi wa Wazanzibari, sasa wamenyanyuka wakaupinga kwa nusu saa, wakaufafanua kwa robo saa na kuukubali kwa dakika moja tu. Aaah! Mengine enhe na mengine kinenhe. Hili ni kinenhe!
Kama mtindo ni huu wa watu wetu wenyewe kuweka maslahi ya vyama vyao mbele na kusahau kabisa maslahi ya nchi, basi ni wazi kuwa jitihada za kuimezua Zanzibar hazitafinikiwa milele.
Kuna hadithi moja ya shoka na mti. Inasemekana wakati mwanaadamu alipogundua shoka kwa ajili ya kumsaidia shughuli zake za kukatia miti, miti iliambiana kuwa mwanaadamu angelishindwa tu. Kwa nini? Kwa kuwa shoka lake halikuwa na mpini.
Mwanaadamu aliposikia, akalitia mpini wa jiwe. Miti ikasema tena kuwa angelishindwa. Aliposikia, sasa akalitia mpini wa mti. Kuona hivyo, miti ikaambiana kuwa “sasa tumekwisha!”. Kwa nini? “Kwa kuwa sasa ndugu yetu (mti), ndiye anayeshirikiana na mwanaadamu kutuangamiza. Hatuponi!”
Na hapo ndipo tulipokwisha Wazanzibari. Wenzetu wa Tanganyika wanawatumia Wazanzibari wenzetu kufikia matashi yao ya kisiasa na kiuchumi kwa Zanzibar. Angalia hapa mkufu na mfungamano, kwa mfano, wa kupitishwa kwa mswaada huu. Mswaada wenyewe ulitayarishwa na serikali ya CCM. Kisha ukapitishwa na Bunge, ambalo linamilikwa na CCM.
Haihitaji kufanya utafiti sana kugundua kwamba CCM ina mashiko yake zaidi Bara kuliko Visiwani. Huko ndiko kwenye maamuzi yote kuhusu CCM na serikali zake. Kutokana na sababu, ambazo hapa nitaziita ‘za kiufundi’ (infrastructural), hata Baraza la Wawakilishi nalo limemilikiwa na CCM.
Kwa hivyo, uwezekano ni kwamba hakuna mswaada hata mmoja ambao utakuja hapa na utatokana na CCM, ukaacha kupitishwa. Hata kama mswaada huo utaliomba Baraza liidhinishe kuundwa kwa serikali moja, basi utapita tu, tena kwa kishindo. Wajumbe wa CCM watachukulia kwamba huko ni kukidhi matakwa ya chama chao, kwa upande mmoja, na kuwakomoa wajumbe wa CUF, kwa upande mwengine.
Kwa hali hiyo tutafika wapi? Zanzibar hii tutaifikisha mahala gani, ikiwa tunakubali kuburuzwa na tunaendekeza kukomoana kisiasa? Juu ya yote, ni nani mwengine azuke wa kuisemea na kuitetea Zanzibar ikiwa hao tuliowakabidhi madaraka ndio wa kwanza kuinakamiza?
Nataka nimalizie kwa kusema kwamba Zanzibar ni nchi yetu sote, sisi Wazanzibari. Tunachopaswa kuitendea nchi hii ni mema, na mema tu, si chenginecho. Ni hilo tu ndilo litakalokifanya kizazi kijacho kiikute nchi yao. Kwa hilo watatukumbuka na kututukuza kwa kuwarithisha urathi huu mtukufu.
Chama kilikuja na kitapotea, lakini Zanzibar itabakia. Hatuna uhakika ikiwa ni CCM tu ndiyo itakayoendelea kutawala daima Zanzibar na Tanzania. Kuna vyama vingi ulimwenguni ambavyo viliwahi kukaa madarakani miaka mingi zaidi ya hii 40 ya CCM na watangulizi wake. Lakini, mwito wa mabadiliko ulipodhihiri na kuitikwa, vyama hivyo viliondoka madarakani, iwe kwa hiari au vyenginevyo.
Waliopo leo madarakani lazima watanabahi kuwa madaraka yao yana mwisho na vyama vyao vitakwenda. Kuna siku watabakia peke yao, bila vyama vyao, lakini Zanzibar itakuwa ipo.
Wakati huo, watoto wao na wa wenzao watawauliza ni kipi walichoifanyia nchi yao. Hawatakuwa na jibu. Na ndipo hapo dharau, kejeli na suto zitakapofuatanishwa na mtajo wa majina yao. Mitaani watakejeliwa, majumbani mwao watadharauliwa na nyoyoni mwao watajisuta. Huo ni wakati wa kuwa chini kuliko walio chini. Nani yuko tayari kuukabili wakati huo!?
Dira, Na. 37, Agosti 15-21, 2003

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.