UCHAMBUZI

Msomi wetu hukoseshwa bega kwao, akalilia ugenini

ALIPOKUWA akiichora taswira ya msomi wa Kinigeria baada ya uhuru katika A Man Of the People, inawezekana kuwa Chinua Achebe hakujuwa kuwa alikuwa akiisemea pia hali ya msomi wa petu, Zanzibar. Ya mule hayamtokezei Odili wa Nigeria tu, bali pia Machano wa hapa. Chief Nanga, mwanasiasa asiye na uelewa mkubwa wa mambo lakini aliyefanikiwa kuzikwea ngazi za kisiasa kiujanjaujanja tu, aliwahi kumuambia Odili, kijana na msomi aliyekuwa ndio kwanza ametoka chuo kikuu: It doesn’t matter what you know, but whom you know! Kwamba si kitu ukijuwacho, bali maneno ni yule umjuwaye.

Naam, ni hivyo ndivyo nasi tumpokeavyo msomi wetu, mwenetu wenyewe kutoka matumboni mwetu. Baada ya kuwa tumeshatumia muda wetu mwingi kumsomesha, naye kutupa nishati yake nyingi kujituma katika masomo, msomi wetu hurudi katika mikono yetu kuja kukumbana na udunifu na udhalilifu uliopindukia mipaka.
Chote kile alichokisoma huko chuoni – chote alichokifumbata katika ubongo wake – anaambiwa si mali kitu. Kwamba hawezi kuishi maisha ya kitabuni (book life) katika uhalisia. Yaliyomo vitabuni ni nadharia tu, ambazo kamwe haziwezi kutekelezeka katika maisha halisi waishiyo watu.
Wa vitabuni ni ulimwengu wa kidhahnia umilikiwao na wanafalsafa na dhana zao juu ya vipi maisha yanatakiwa yawe, lakini haya yaliyomo katika uhalisia ni maisha ya kweli, ambayo mmiliki na muendeshaji wake ni mwanasiasa, si mwanafalsafa. Huku yeye, msomi, na mwenzake asiye msomi, wote, ni watenzwa wanaotenzeka na system.
Huu ni ukweli ambao humtesa msomi huyu si kiuchumi tu, bali pia kijamii na kisaikolojia. Hujikuta mgeni kwenye jamii yake mwenyewe aliyozaliwa, kukulia na kujiapia kuwa angekufia. Leo kuambiwa kuwa madhali amesharudi kwenye jamii, baada ya miaka yote ya kuinamia kitabu, anapaswa kufuata ipigwavyo, msomi wetu hujikuta katika kitahinani kikubwa.
Kama mwanaadamu, basi angelitamani kuishi kama waishivyo watu, angalau kwa kupata yale mahitaji yake muhimu ya kimaisha tu. Kama mwanajamii, basi naye angelihitaji awe mshiriki katika shughuli za kijamii, angalau kwa kuwasaidia watu wake, nao waone kuwa wamezaa; hawakupunguza machango tu. Na kama msomi, angelihitaji kupata utambulisho wake kutoka jamii hiyo kwa stahiki yake. Angelitaka aheshimiwe, angalau kwa maana nyepesi tu.
Lakini kwa mshangao wake ni kuwa anarudi na kujikuta hana fursa yoyote ya kuutumia usomi wake kuyapata hayo, maana hapa sio nini anakijuwa. Hapa ni nani ahli yake katika system, ndiye atakayeweza kumsaidia angalau apate kijisehemu cha kutarazaki, mkono uende kinywani!
Anatakiwa asahau kabisa mchango wake kwa watu wake, asifikirie kabisa heshima yake, ati kwa tu ana elimu aliyonayo. Tusi gani kwa msomi wetu. Ni tusi hili ndilo kiini na chimbuko la wasomi wetu wingi wa Kizanzibari kuselemea na kuselelea katika mataifa mengine, ambako huko huyapata haya wayakosayo hapa, na ziada yake.
Nilibahatika kutembelea mji wa Hamburg, Ujarumani, mwishoni mwa mwaka uliopita. Huko miongoni mwa mambo niliyokutana nayo, ni hili la wasomi wa Kizanzibari ambao sasa wako katika nchi za Ulaya kwa miaka zaidi ya ishirini. Niliwakuta wengine wakihadhiri katika vyuo, wengine wakiwa katika mikutano na semina wakiwasilisha kile wakiitacho Paper. Na wote hawa niliwakuta wakipewa heshima ya hali ya juu na watu wa huko. Nilijuwa kuwa heshima na hadhi ile waliyonayo kule ugenini, hawakuipata kwa rangi zao, dini yao wala majina yao, lakini kwa ilimu zao.
Binafsi, kabla ya kukutana na watu hawa huku na, kwa hakika, hadi hivi karibuni tu, nilikuwa nimefungika na mawazo kuwa msomi anayeihama nchi yake na kwenda kufanya kazi katika nchi nyengine huwa ni mpungufu wa uzalendo katika nafsi yake. Nilijuwa kuwa wengi wao walikuwa wakitoa kisingizio cha hali ngumu ya maisha hapa pao ili kuhalalisha uovu wa kupakimbia. Nilikuwa ni mpinzani mkubwa wa wazo hili, maana nililiona lilikuwa njia ya kulikimbia tatizo, na ambayo haisaidii utatuzi wa tatizo lenyewe, isipokuwa hulifanya kuwa tata zaidi. Kwamba, kama ilikuwa ni shida tulizonazo petu, hapa ndipo pao, kwa hivyo kwa nini wasingelikaa tukashirikiana pamoja kupambana nazo?
Kwa nini wasikae kusaidia kuleta mabadiliko? Kwa nini wajikubalishe kuwa fimbo ya mbali? Hesabu yangu ilikuwa ni kiwango gani cha faida wanachokizalishia nchi ambazo wanazifanyia kazi. Ingelikuwa wapi nchi yao leo hii, ikiwa faida hiyo ingelikuwa wanaizalishia hapa? Kwa mfano, vijana wangapi wa Kizungu kwa mwaka humaliza digrii zao kwa kusomeshwa na wasomi wetu? Au miradi mingapi huiandika kwa mwezi na kuzalisha mamilioni ya dollar na euro katika kutekelezwa kwake?
Ni hivi majuzi tu, ndipo nilipong’amuwa kuwa kumbe nilikuwa ninakosea kuwahukumu hivyo. Hii ilikuwa ni baada ya kuzungumza na baadhi yao ambao walikuja hapa Zanzibar kikazi, na kuwatupia suali ikiwa wana dhamira yoyote ile ya kurudi kwao, kwa maana ya kuja kuishi na kufanya kazi na watu wao, kwa maendeleo ya nchi yao. Mmoja wao alinijibu kwa kuniondosha njiani tu, Inshallah nitarudi. Moyoni mwangu nilijuwa kabisa kuwa huyu, kama walivyo wengine, hana tena khabari na kwao, hana tena khabari na uzalendo wake. Tayari alilishasahau titi la mama – ardhi iliyozikiwa kitovu chake mwenyewe.
Lakini mwengine hakuniwachia hivi hivi, kama yule wa mwanzo. Ungeliniuliza kwa nini nikaondoka kwetu na sio kwa nini sirudi kwetu, labda lingelikuwa suali muwafaka zaidi. Aliniambia hivyo akiwa hana furaha, maana alikuwa ameshaliona lile jicho langu la kuwaona watu wa aina yake kuwa ni wakosefu wa uzalendo, wasio na chembe ya mapenzi na kwao. Nilikuwa nikimtaka ajuwe kuwa kurudi kwao na kuja kufanya kazi na watu wake halikuwa jambo la Sunna tu kwake, bali la Faradhil-ain. Kwamba ikiwa atakufa bila ya kulitekeleza, basi atakuwa mas-uul mbele ya Mungu.
Ndipo hapo akanitanabahisha kwa nini yeye na hao wenzake wanaondoka makwao na kwenda kuishi katika nchi za watu. Kwamba hawaondoki kwao kuzikimbia shida zilizopo, maana ni shida hizo ndizo zilizowalea na kuwasomeha hadi wakafikia walipofikia. Na pia ni shida hizo walizoapa kupambana nazo katika maisha yao yote ya masomo ili kuipa maana elimu yao katika maisha ya watu wao. Lakini linalowakimbiza pao ni kuwa hawatakiwi. Wanakanwa na nchi zao wenyewe, nchi za uzao wao. Na katika wakati huu ambao sisi ndugu zao tunawakana, kuna wenzetu wanawatafuta kwa udi na uvumba.
Vipi msomi wetu anakanwa katika nchi ya uzao wake? Kwa kuwa hapewi kazi ya mamilioni ya shilingi? Kwa kuwa hapewi gari la kifakhari, wala nyumba nzuri kama wapewavyo wanasiasa?
Hapana, hayo kwa msomi wetu si makubwa kiasi ya kwamba akiyakosa anahiyari kupasamehe pao, lakini kubwa na muhimu zaidi kwake ni kupewa utambulisho wake na kutambuliwa kama msomi.
Kuna mifano ya wasomi waliojikusuru kurudi kwao, baada ya masomo yao, ili waje wafanye kazi kwa ajili ya taifa lao, lakini walipofika hapa wakakumbana na kejeli za wanasiasa visirani, ambao kwao wao msomi ndiye adui nambari moja. Huku kwetu ugomvi baina ya wanasiasa na wasomi hawishi, maana wawili hawa kila siku huyaona mambo kutokea vipembe tafauti. Wakati mmoja huyaona kutokea kipembe cha kisiasa na kutaka kila kitu kifanywe kwa kufuata muono huo, mwengine huyaona kutokea kipembe ya kitaaluma, na haja yake ni kuyafanya mambo kupitia muono huo.
Wakati mwanasiasa anazinga mtu amuendeshe, msomi anagoma kuendesheka na hivyo kutangaza hatari kwa nguvu za mwanasiasa. Siku zote watu hawa ni Lila na Fila. Mara moja Henry Peter, aliwahi kusema: Education makes people easy to lead, but difficult to drive; easy to govern, but difficult to enslave. Kwamba elimu huwafanya watu wawe rahisi kuongozeka, lakini wagumu kuendesheka; rahisi kutawalika, lakini wagumu kuwatia utumwani!
Ubaya wa mambo kwa msomi, ni kuwa yeye huwa hana nguvu za kufanya maamuzi ambayo yatafuatwa hapo hapo. Mwanasiasa anazo nguvu hizo. Akisema mashine ya maji ifunguliwe Lumumba ikafungwe Bwejuu ili Mhishimiwa Sana akapate kufunguwa mradi wa maendeleo huko, jambo hilo litafanyika siku hiyo hiyo hata kama ni kinyume na ushauri na matakwa ya kitaalamu.
Msomi akiinuka kulisemea hilo, huyo anaanza kuwa mpinga maendeleo, mwanapinduzi, mchochezi na majina mengine msongo kwa msongo. Na usidhani kuwa hayo yataishia hapo. Huenda siku kumi zijazo akakuta kibarua kimeshaota majani. Kisa? Kukidhi mahitaji ya kitaaluma, badala ya mahitaji ya kisiasa!
Akiepukana na hilo, msomi wetu anakumbana na jengine kutoka kwa system. Kwa mfano, mtu anarudi nyumbani baada ya kumaliza kuchukuwa mafunzo ya Uhandisi huko atokeako, lakini akifika anakabidhiwa chaki akasomeshe Kiingereza kwa wanafumzi wa Darasa la Saba. Mwengine aliyesomea masuala ya kilimo wanasiasa humpangia akawe fundi wa vinu vya maji. Wapi na wapi?
Lakini kwa kuwa wanasiasa wetu wana ugomvi wa kudumu na wasomi hawa, basi si ajabu kuwa wanawafanyia haya kusudi washindwe na wapate la kuwadharaulia. Wawaite maofesa uhwara, mdaktari fki na majina mengine kama hayo ya inda na shitihizai. Hiyo ndiyo mbeleko tumbebeayo msomi wetu, atadumuje mgongoni petu?
Hayo ya msomi kupangiwa kazi kinyume kabisa na taaluma yake, huenda yakawa madogo, lakini hebu fikiria mwenyewe mtu ambaye amepoteza miaka yake kumi kuchukuwa fani ya udaktari huko nje, anakuja hapa na kuamriwa kupiga deki hospitali, eti ni kumkomoa na usomi wake! Lipi tumfikirie atalifanya msomi huyu?
Lakini adui wa msomi wetu si mwanasiasa tu, hata jamii yenyewe anayokuja kuifayia kazi na kuishi nayo. Wengi wetu huwa tunadhani kuwako kwao nje kimasomo, huwa kumewapa fursa nzuri ya kuyatengeneza maisha na hivyo kuwapa wajibu wa kutusaidia kwa hali na mali. Kwetu, kwenda nje kunamaanisha kwenda kukunja mapesa na kuja nayo nyumbani. Anaporudi mikono mitupu, msomi huyu huonekana kayasaliti matarajio ya watu wake. Na akitaka ayatimize mahitaji hayo, basi lazima afanye kazi ya kuwatimizia haja zao. Na kazi ipi atakayoifanya hapa petu kuyakidhi mahitaji ya familia zetu kubwa?
Basi ni mchanganyiko wa mambo kama hayo, ambao humtia msomi wetu katika mtihani mkubwa maishani mwake – mkubwa na mgumu sana kuliko hata ile aliyoifanya kuchukulia Diploma na Digrii zake. Kwa hali hiyo, msomi wetu huwa amesukumwa ukutani, ambapo hana jinsi ya kung’amuka illa ajitolee muhanga kwa kufanya moja kati ya matatu haya: ama akae kupambana na mfumo kwa kucha na meno, au abadilike kwa mujibu wa mahitaji ya mfumo wenyewe au aikimbie nchi yake ya uzawa.
Kila moja kati ya matatu haya yana gharama kubwa sana, na lolote atakalolifanya, hujikuta anajilaumu kwa kutolifanya jengine. Kwa mfano, kuamua kubakia na kuukabili mfumo uliopo ni kujikubalisha kukosa na kupoteza kila kitu. Ni kukubali kujiundia maadui wengi na wenye nguvu kuliko yeye kutoka tabaka la watawala. Anaweza kukosa hata mlo wa siku moja yeye na familia yake na mwisho wa hadithi akafa dhalil-u-madhulum. Mifano ya wasomi wa aina hiyo ipo mingi sana.
Chaguo la kujibadilisha na kwenda sambamba na mahitaji ya mfumo uliopo ndilo linalofuatwa na baadhi ya wasomi ambao wameamua kurudi pao. Lakini chaguo hili huwa linamsuta msomi anayeheshimu maadili ya taaluma yake. Kuwa fisadi ni kitu alichojifunza na kuamini kuwa ni kiovu, sasa kuishi kwa mujibu wa matakwa ya mfumo ni kukubali kuwa fisadi.
Tunao hapa wasomi na digrii zao, lakini ndio hao wala rushwa wakubwa na ambao huhongwa kuitikia Ndio Mzee ili waidhinishe mambo maovu kufanyiwa watu wao kwa jina la taaluma zao.
Hawa si wasafi na wala hawawezi kusafika madhali wamesimama na wanaishi na wachafu. Hawa ni wasaliti wa taaluma zao, wasaliti wa uelewa wao wenyewe. Wanaweza wasife madhulumu, lakini hawawezi kuepuka kufa madhalimu.
Na, mwisho, yule asiyeweza kuyastahamilia hayo, basi hulazimika kupahama pao na kwenda ugenini. Huko ataweza kufanya kazi na kupata visenti vya kuwasaidia watu wake. Huko ataweza kuilinda na kuidumisha heshima yake kitaaluma. Huko kutamuepusha kufa dhalili au kufa dhalimu.
Lakini huko kutamnyima kwao, kutakidamirisha kizazi chake kisiyajuwe ya kwao. Atazaa watoto wasio utambulisho – Wazanzibari sio wala wazungu sio. Waislam sio, wala wakristo sio. Na hilo ni poteo kubwa kwa msomi wa kipetu, ambaye kujitowa kwake muhanga kwa staili hii kunamkosesha, yeye na wanawe, titi la mama.

Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Dira Toleo Na. 14 la  Machi 7-13, 2003

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.