Kuna vijana wengi tu ambao ni marafiki wakubwa hivi sasa wa kufa na kuzikana, lakini ukifuatilia historia za wazee wao, utakuta kuwa wazee hao walikuwa mahasimu wa kutukanana matusi ya nguoni. Bali kuna hata wale ambao mzee wa rafiki mmoja ndiye aliyemuua mzee wa rafiki mwengine, lakini leo hii watoto hawana khabari na hilo. Watu hawa, leo hii ukiwauliza wanataka nini, watakujibu Uzanzibari. Hiyo ndiyo Zanzibar ya sasa.
DHAMIRA ya makala hii ni kuchangia makala iliyoandikwa katika gazeti la RAI iliyopewa jina Kura za maruhani: Mzimu wa vyama vya kale. Yumkini, ingelikuwa bora zaidi ikiwa ningeliiandika makala hii kwenye gazeti hilo hilo, kwa kuwa mwiba uchomeako, ndiko utokeako, lakini kwa kuwa jambo lenyewe linaihusu Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari na kwa kuwa Dira ndilo jukwaa la Wazanzibari, basi nimeonelea bora kuutumia ukumbi wetu wenyewe kulizungumzia hili.

Ninalazimika kufanya marejeo ya moja kwa moja kwa makala yenyewe pamoja na vyanzo vyengine ili kukipa maana kile nikizungumziacho. Kwa hilo, naomba tokea mwanzo kabisa, mnisamehe na mnistahmilie ikiwa litaonesha kuwachosha haraka au kuonesha kuwa sehemu kubwa ya makala hii ni maneno ya watu wengine!
Hoja ya msingi katika makala ile inaelezewa katika maneno haya: “….tangu kale hadi leo, Zanzibar imegawika nusu kwa nusu kwa misingi ya vyama viwili dume…. (bila ya shaka vyama hivi kwanza vilikuwa ASP na ZNP na baadaye CCM na CUF)…. ambapo mzimu wake unaihangaisha Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi leo. Ni mzimu wa siasa za chuki na kulipiza kisasi (RAI, Nam. 505, Juni 12-18, uk. 8, kwenye mabano ni maneno yangu).
Kwa ufupi maelezo haya yanakusudia kuwa Wazanzibari wanahangaishwa na Dhambi ya Asili inayotokana na chuki na uhasama irithishwayo kutoka kizazi kimoja hadi chengine kupitia vyama vya kisiasa. Dhambi hii ya asili ndio huo uitwao Ugozi na Uhizbu.
Kuthibitisha kuwepo kwake, mwandishi wa makala hiyo anasema hivi: “Ukitazama matokeo ya uchaguzi wa 1995 nchini Zanzibar, mauaji ya waandamanaji wa CUF miaka mitatu iliyopita na matokeo ya uchaguzi wa Pemba mwaka huu, utaona kuwa nguvu za kisiasa Zanzibar za enzi za harakati za kupigania uhuru miaka ya 1950, na zilizopelekea mapinduzi ya 1964, hazijabadilika…. Siasa za chuki ni zile zile: ubaguzi kwa misingi ya koo na nasabu ni ule ule na udini halikadhalika ni ule ule.” (Chanzo ni hicho hicho)
Pia, ushahidi zaidi ni kuwa: “…ni nadra kuona wanachama wa CUF wakihamia CCM au wanachama wa CCM kuhamia CUF…. Majina kama vile HIZBU wanayoendelea kuitwa wafuasi wa CUF na GOZI wanaloitwa wafuasi wa CCM… yanaonyesha kwamba uhasama wa kisiasa wa zamani, bado unaendelea visiwani humo.” (RAI Nam. 506, uk. 16, Juni 19-25, 2003).
Kile kinachobainishwa hapa ni kuwa hata baada ya kupita miaka hamsini tokea siasa hizi za Uhizbu na Ugozi zibuniwe na kushamiri, Wazanzibari tumeshindwa kujinasuwa kutoka makuchani mwake na badala yake tumekuwa wahanga kwazo. Sasa nini kifanyike? Mwandishi anashauri kwamba: “Kwa mzani wa siasa ulivyo, ufumbuzi wa migogoro huko Zanzibar ni kukubali kuundwa kwa serikali ya mseto. Iwekwe wazi katika Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kwamba chama kitakachopata ushindi kwa kura chini ya asilimia 60, kilazimike kuunda serikali ya mseto.” Hili ni pendekezo zuri, au sio?
Bila ya shaka. Nani asiyekubaliana na wazo la kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa? Kushirikiana katika kuiendesha nchi, kwa maana hii ya kuwa na uongozi unaowashirikisha wananchi kutokea vyanzo tafauti, ni jambo muafaka kwa kuyatulizanisha madaraka ya kiutawala mikononi mwa viongozi na, hivyo, kwa maendeleo. Uongozi unapokosa jambo hili la ushirikishi wa wananchi kutoka matapo tafauti, madaraka yake ya kiutawala huwa yako hatarini.
Lakini hii, kwa maoni yangu, si haja ya Zanzibar tu, bali ni haja ya kila taifa ulimwenguni. Kwa mfano, upande wa pili wa muungano, yaani Tanganyika, ambako kuna hayo makabila hasa kwa maana ya makabila, kunaonekana kutekelezwa jambo hili siku nyingi sana. Serikali ya muungano, ambayo ndiyo hiyo hiyo ya Tanganyika, mara nyingi huundwa na watu kutoka makabila tafauti, hata kama hilo halitajwi wazi
Kwa maana, serikali ya umoja wa kitaifa inahitajika popote pale ambapo jamii imejikusanya pamoja na kujiundia uongozi wao. Kwamba serikali, kama chombo cha utawala, ni kitu kipya sana kulinganisha na uwepo wa jamii yenyewe. Jamii ilikuwepo kwanza na makundi yake yenye madaraka na nguvu tafauti, kisha ndiyo kikaja chombo hiki na kuyakusanya makundi haya na madaraka yao, na kuyaweka chini ya mwamvuli mmoja wa kiutawala. Chombo hiki kuwashirikisha wanajamii wenyewe kutoka katika makundi yao tafauti katika utawala, sio jambo la hiari, bali ni jambo la lazima. Na, kwa hivyo, hilo ni hitajio la kila taifa ulimwenguni kwa kuwa kila taifa halikosi kuwa na mjengeko huu wa kijamii!
Kwa hivyo, mpaka hapo, sina mashaka na suluhisho lililomo katika makala ile. Lakini nisichokubaliana nacho ni hii dhana kwamba uhalali wa serikali hiyo ya umoja wa kitaifa kwa Zanzibar ni dhambi ya asili ya uhasama na chuki za Uhizbu na Ugozi iliyoganda Wazanzibari. Ushahidi wa uwepo wa dhambi hiyo ni upi?
Mwandishi wa makala ile anaona kuwa ni haya matukio ya kisiasa Zanzibar, la karibuni kabisa, na ambalo lilizaa makala hiyo, ni hili la Kura za Maruhani za Pemba. Kwa kiasi gani kura za maruhani zinahusiana na Uhizbu na Ugozi, haikuoneshwa katika makala hiyo. Ukweli ni kuwa ikiwa tutakuwa wayakinifu hasa, basi tutaona kuwa hapana uhusiano kabisa baina ya matokeo yale ya uchaguzi na siasa hizo za kale. Sasa Zanzibar hapana tena Ugozi wala Uhizbu, bali kilichopo ni Uzanzibari
Kwanza hoja kuwa CCM imetokana na ASP au kuwa CUF imetokana na ZNP/ZPPP na hivyo kila aliye katika vyama hivyo ana asili navyo, ina mapungufu kibao, kiasi ya kwamba hata haiwezi kuitwa hoja. Hapa sitaki nizungumzie hilo kwa undani, lakini itoshe kukumbusha kuwa hapa Zanzibar, ndani ya CCM kuna watu kibao waliokuwa mwanzo, wao au wazazi wao, ni wafuasi wa ZNP/ZPPP na vivyo katika CUF muna wanachama kibao ambao aidha wao wenyewe au wazazi wao walikuwa ASP.
Lakini hebu tuchukulie kuwa ni kweli kwamba CCM inatokana na ASP na CUF inatokana na ZNP/ZPPP, kama inavyoelezewa katika makala hiyo. Basi bado matokeo haya ya Pemba yanaonesha kuwa jambo hilo limeshasahaulika kipindi kirefu sana. Sehemu kama za Mkanyageni, Chake Chake na Wingwi zilikuwa zikijuilikana kuwa na wafuasi wengi wa ASP, na ukweli ni kuwa kila mara chati ya kura za ASP ilikuwa ikipanda angalao kwa watu 50 hadi 100 huko Pemba kabla ya Mapinduzi.
Hivi sasa, wakati wa CCM, chati hiyo imeshuka kwa asilimia za ajabu na hizo sehemu zilizokuwa zikisifiwa kwa kuwa na ASP wengi, hivi sasa zina CCM wa kuhesabiwa kwa vidole. Na hilo ndilo hasa lililodhihirishwa katika matokeo yale ya uchaguzi. Kwamba watu hawana tena cha Ugozi wala cha Uhizbu, sasa walichonacho ni cha Uzanzibari. watu walipiga kura kwa maslahi ya Zanzibar, na sio kwa maslahi ya makabila na nasaba.
Huo ndio ukweli. Zaidi ya asilimia 60 ya Wazanzibari hivi sasa, ni wale ambao aidha walizaliwa katika siku za Mapinduzi ya 1964 au baada ya hapo na hivyo hawana kumbukumbu zozote juu ya mambo yalivyokuwa hapo kabla. Mapinduzi, Ugozi, Uhizbu na mengineyo hayamaanishi chochote katika maisha yao, si kisaikolojia na kisoshiolojia.Wako wengi ambao hata hatuna khabari na huo Ugozi na Uhizbu ulikuwaje na ulitumikaje! Na hao ndio wapiga kura wa sasa.
Kuna vijana wengi tu ambao ni marafiki wakubwa hivi sasa wa kufa na kuzikana, lakini ukifuatilia historia za wazee wao, utakuta kuwa wazee hao walikuwa mahasimu wa kutukanana matusi ya nguoni. Bali kuna hata wale ambao mzee wa rafiki mmoja ndiye aliyemuua mzee wa rafiki mwengine, lakini leo hii watoto hawana khabari na hilo. Watu hawa, leo hii ukiwauliza wanataka nini, watakujibu Uzanzibari. Hiyo ndiyo Zanzibar ya sasa.
Kwetu sisi Wazanzibari, ambao tumo ndani ya Zanzibar hivi sasa, tunapatwa na wasi wasi sana juu ya dharau hii ya dhambi ya Ugozi na Uhizbu. Ndiyo, naiita hii kuwa ni dharau kwa kuwa inatudogosha na inatudhalilisha Wazanzibari. Inatuambia kuwa kila siku sisi tunaishi maisha ya miaka hamsini nyuma. Tunaishi kule kule kwenye Ugozi na Uhizbu. Huko nyuma, salama yetu ilikuwa ni kusaidiwa na wenzetu wa Tanganyika (pengine ndivyo tutakiwavyo tuamini hadi leo ni hivyo nivyo). Kwa hivyo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipofanya Muungano na Rais Abeid Amani Karume kuziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar na baadaye alipofanya makubaliano na Rais Aboud Jumbe Mwinyi kuviunganisha vyama vya TANU na ASP, ilikuwa ni katika kutusaidia sisi kupambana na dhambi hii ya asili!!!
Ni kwa kiasi gani Nyerere alikuwa na huruma hizo kwa Zanzibar na Wazanzibari, nalo pia ni suala linalohitaji mjadala mrefu. Lakini kwa maneno mafupi tu, kuna dalili chache sana zinazoonesha kuwa Mwalimu Nyerere kweli alisukumwa na huruma hizo katika kuleta vitu hivi viwili, yaani Tanzania na CCM. Dalili nyingi zaidi ni zile zinazoonesha kuwa aidha maslahi ya kibinafsi yalikuwa msukumo mkubwa nyuma ya azma ya Nyerere, Karume na Jumbe, au shinikizo kutoka mataifa makubwa liliwaelemea na wakashindwa kulihimili (Soma simulizi za Amrit Wilson katika US Foreign Policy: The Creation of Tanzania).
Suala la Ugozi na Uhizbu linakereketa sana kulisikia linaoanishwa na matukio ya kisiasa yanayotokea sasa. Kwanza, linakereketa kwa hiyo maana yake inayohusihwa nalo, kwamba ni siasa za chuki na uhasama wa kulipizana kisasi baina ya Wazanzibari wenye asili tafauti za Afrika na Arabuni. Nasema maana inayohusihwa kwa kuwa si watu wote wanaokubali kuwa harakati za ukombozi Zanzibar zilichimbukia na kuongozwa na hamasa na chuki za ukabila. Unaweza kusoma insha ya B. D. Bowles iitwayo The Struggle for Independence katika Zanzibar Under Colonial Rule (Abdul Sheriff and Ad Ferguson: 1991) kupata mawazo tafauti kuhusiana na harakati za ukombozi za Zanzibar.
Lakini zaidi jambo hili linakereketa kwa kuwa linaonekana kana kwamba linadhamiriwa kuzitoa maana hizi harakati za sasa za Wazanzibari katika kupigania mabadiliko. Ni kana kwamba linatukalia mbele yetu na kutuambia kuwa: “Ah! Haya ni yale yale ya kubaguana na kudharauliana kwa makabila na nasaba!” Kwamba bado Wazanzibari tungali wahanga wa historia yetu – hatubadiliki, hatugeuki?
Nachelea kusema kuwa huu ni upotofu na upotoshaji (inawezekana wa makusudi au si wa makusudi) wa hali halisi ilivyo sasa Zanzibar kwa kisingizio cha kuitumia historia yetu. Kuwahukumu Wazanzibari wa sasa kwa kosa lililofanyika katika historia yao, sio tu kuwa ni koseo la kisiasa, lakini hata hiyo taaluma ya Soshiolojia (ambayo mwandishi anaonekana kuitumilia) inapingana na hilo. Kwani ni nchi gani isiyokuwa na historia yake? Ni nchi gani isiyopita katika giza kama hili, au hata zaidi ya hili, katika safari yake ya kujijenga?
Naomba nimalizie makala hii kwa kumnukuu Dk. Mohammed Ali Bakari katika mada yake: Tume ya Uchaguzi, Muafaka na Matarajio ya Wazanzibari aliyoitowa katika semina ya wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar huko Uwanja wa Gombani, Pemba, Machi 18-19, 2003:
“….kuna wanasiasa na wasomi wengi wa Tanzania Bara, na nje ya Tanzania, wanaoamini kuwa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar utachukua muda mrefu sana kuweza kupatiwa ufumbuzi kwa sababu mgogoro wenyewe ni matokeo ya miaka nenda miaka rudi ya mgawanyiko wa kijamii…..
“Bila ya shaka, historia ina sehemu yake ambayo haiwezi kupingika katika mwenendo wa kisiasa na kijamii, lakini itakuwa kosa kubwa sana la kuitusi historia kama mgogoro wa kisiasa Zanzibar hivi leo utahalalishwa kwa kisingizio cha historia. Mtazamo huu nautafsiri kwamba unatokana na kutokuielewa jamii na historia yenyewe ya Zanzibar au ni kejeli kwa Wazanzibari wa kizazi kilichopo kwamba hakina uwezo wa kufikiria nje ya misingi ya historia iliyowafanya wafarakane. Kwa tafsiri hiyo, chaguzi zinapovurugika kama vile ilivyokuwa 1995, 2000 (na hata pengine zitakazofuata), hiyo itatafsiriwa kwamba ni mwenendo na athari ya kitanzi cha historia ambacho kiko shingoni mwa Wazanzibari….
“Sina haja ya kuendeleza mjadala huu…. ila ninachotaka kusema ni kwamba Zanzibar ndiyo chimbuko la ustaarabu katika Afrika Mashariki, Wazanzibari walipata bahati ya kustaarabika mwanzo…Kusema kuwa Wazanzibari hawawezi kuendesha uchaguzi ulio huru na wa haki na ni vigumu kuelewana kwa sababu ya migawanyiko iliyopo kihistoria, lakini Wakenya wanaweza, hiyo ni kejeli na changamoto kwa Wazanzibari wote…watakapofanikiwa katika changamoto hiyo, yumkini watakuwa wamewatangulia sana wenzao wa Tanzania Bara ambao bado wanasuasua. Uwezekano huo wa mchakato wa kidemokrasia kuanzia Zanzibar ni mkubwa sana. na hiyo huenda ikawa cheche ya kuleta mabadiliko kwa upande wa Bara pia ” (Dira Nam. 22, uk. 3, Mei 2-8, 2003, msisitizo ni wangu).