UCHAMBUZI

Alichokikosea Mkapa kuhusu Muungano

VYENGINEVYO Rais Benjamin Mkapa aishereheshe upya hotuba yake ya Miaka 40 ya Muungano lakini, ikiwachwa kama ilivyo, itabakia kuwa mtiririko wa sentensi zilizokosa mantiki na hoja ya kushika. Hata iwe kweli ujumbe uliomo ndani yake umefika, imekuwa hivyo kwa sababu ya hamasa na jazba, na wala sio kwa mkufu wa mantiki ama umadhubuti wa hoja.

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Rais Mkapa alichukuwa fursa ile kututisha sisi twenye maoni tafauti juu ya muundo wa Muungano. Akatubatiza majina yasiyotustahikia: wanafiki, mahasidi, waroho, wabinafsi na hata kufikia umbali wa kutuona wajinga. Tuseme kuwa haya hayakuwa matusi, lakini tuuite upotoshaji wa makusudi wa hoja. Kati ya marais waliowahi kuitawala nchi hii, Mkapa ni bingwa wa kutumia staili hiyo ya upotoshaji hoja iitwayo Straw Man Fallacy.

Hata hivyo, hilo haliufifilishi mtazamo wetu kwamba muundo wa serikali mbili ni kizungumkuti cha uhusiano (undefined relationship), na kwamba haufai kabisa. Kusema kuwa huu ndio unaofaa ati kwa kuwa umeendelea kudumu kwa miaka hiyo 40, bila ya kuzingatia ni vipi umedumishwa, ni hoja butu – kama ninavyokusudia kuonesha katika makala hii.

Kuuona Muungano huu kizungumkuti kuliwahi kuthibitishwa na hata Rais Julius Nyerere katika hotuba yake Bungeni tarehe 6 Julai, 1970: “Bila ya shaka, jinsi muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ulivyo na namna unavyoendeshwa ni jambo moja kubwa lisiloeleweka katika maendeleo ya kisiasa…” Kauli hii ya Mwalimu ilikuwa kweli wakati huo ilipotolewa, ni kweli leo hii ninapoandika makala hii na itakuwa kweli hata milele, ikiwa muundo huu haukubadilishwa. Bado, hadi leo, Muungano huu umebakia kuwa kituko ambacho, kwa hakika, hakiwezi kusimulika kwa misamiati michache tu kama wanavyotaka akina Rais Mkapa iwe.

Sehemu kubwa ya hotuba hiyo ya Rais Mkapa ilitawaliwa na nukuu kutoka masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha (Ammi) ili kuhalalisha muundo huu wa Muungano. Bila ya kuzingatia shaka zinazojitokeza juu ya usahihi wa rekodi zilizomo katika simulizi hizi zilizoandikwa na mwanajeshi Hosana Mdundo, zikahaririwa na kada wa CCM, Paul Sozigwa, zikatiwa utangulizi na muasisi wa Muungano na CCM, Julius Nyerere, na kuchapwa na Wizara ya Elimu na Utamaduni ya serikali ya CCM, bado ukweli ni kwamba hakuna popote katika nukuu hiyo, ambapo Ammi Thabit anazungumzia muundo wa Muungano.

Badala yake, anachokitetea Ammi, na ambacho kinatetewa na kila mwenye akili zake, ni kuwepo kwa Muungano na umuhimu wake kwa watu wa Tanganyika na Zanzibar. Kama anavyosema: “…hakukuwa na swali kama tuungane au tusiungane. Hoja ilikuwa tu muungano wetu uwe na sura gani…”. Maana yake ni kwamba, hata kama hoja na haja ya kuungana ilishaonekana mwanzo, lakini hadi siku chache kabla ya Muungano wenyewe palikuwa hapajaamuliwa vipi paunganwe. Hiyo ndiyo sababu, suala la aina gani ya Muungano iwepo ‘liliripuliwa’ tu, kama linavyoripuliwa leo, na ndiyo maana ukawa ni kizungumkuti.

Kuna ushahidi mwingi unaodhihirisha kwamba hadi anatia saini Makubaliano ya Muungano huu, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, alikuwa akiamini anaingia katika uhusiano wa shirikisho. Pitia kitabu cha Amrit Wilson, US Foreign Policy: The Creation of Tanzania, kwa ufafanuzi zaidi. Bali pia pata masimulizi ya watu waliokuwa karibu na Marehemu Karume juu ya vile alivyokuwa akiuchukulia uhusiano wake na Mwalimu Nyerere panapohusika mamlaka na madaraka ya Zanzibar.

Lakini, hebu natujipumbaze kwa kusema kwamba ni kweli kuwa wote wawili, Masheikh Thabit na Karume, waliuhalalisha muundo huu wa serikali mbili. Bado suali litabakia pale pale: uwili wenyewe ni upi hasa? Huu wa sasa? Kwamba hadi wanakufa marehemu hao, Zanzibar ilikuwa ingali Zanzibar, angalau kwa maana nyepesi, lakini sio dhaifu, ya kuwa Zanzibar. Ammi Thabit, ambaye alikufa mwisho, alimwacha Rais wa Zanzibar ndiye Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Wakati huo bandari, uvuvi wa bahari kuu, uhusiano wa kimataifa na mafuta yalikuwa hayajakuwa mambo ya Muungano. Hapakuwa na kitu kinachojuilikana kama usawazishaji wa viwango vya kodi (harmonization of tariffs). Alituwacha wakati ambapo maamuzi kamili ya kuiongoza Zanzibar, kwa mfano kama nani awe Rais, yanafikiwa pale Kisiwandui.

Hivi sasa ni miaka 18 tokea Ammi afariki dunia, na yote hayo aliyoyaacha hayapo tena. Uwezekano ni kwamba kama angelikuwa hai leo hii, simulizi zake zingelikuwa nyengine na wala mwanajeshi Mdundo asingelikuwa na uthubutu wa kuziandika. Wala Mwalimu Nyerere asingelitamani kuziwekea utangulizi. Wala Paul Sozigwa asingeliweza kuzihariri. Wala Wizara ya Elimu na Utamaduni isingelizichapisha. Na, hivyo, wala Rais Mkapa asingelidiriki kuzifanyia marejeo!

Simulizi hizo, bila ya shaka yoyote, zingeliakisika na hali halisi ilivyo. Na hilo lingelikuwa ni kinyume na maslahi ya yeyote kati yao. Nakusudia kusema kuwa hakuna kati yao ambaye angelikuwa na hamu wala maslahi ya kumsikiliza Ammi akizungumzia kudhalilika kwa Zanzibar, kwa kuwa hao wote ni wa mrengo mmoja. Wala kwa kuzungumza hivyo Ammi asingelikuwa akitaka kuuvunja Muungano, bali kutaka haki ya Muungano huo ichungwe. Ndivyo hivyo pia inavyotaka baki yetu.

Lakini hoja hiyo, kwa makusudi kabisa, ‘inageuziwa kibao’ na akina Rais Mkapa kwa kusema kuwa ina dhamira ya kuudhoofisha na hatimaye kuuvunja Muungano. Katika kuonesha kuwa aliposimamia ndipo, Rais anapigia mfano wa umuhimu wa kuwa na Muungano, hasa kwa upande wa Zanzibar: “Na wapo (Wazanzibari) wengi ambao wanatumia fursa (za kuboresha maisha yao katika arhi ya Tanzania Bara)…. Fursa hizo za kujiendeleza zingelipatikanaje bila ya Muungano?”

Huu ni upotoshaji wa makusudi wa hoja. Ukiachia mbali ukweli kuwa suala la kupata fursa halina uwiano na kuwemo au kutokuwemo katika Muungano (vyenginevyo hao ‘wanaouziwa’ nchi wasingezipata fursa hizo kwa kuwa hatuna Muungano na nchi zao), lakini hakuna anayehoji umuhimu wa kuwa na Muungano. Rais anajuwa, kuliko mtu yeyote, kuwa Muungano huu haujatishiwa kudhoofishwa sambe kuvunjwa. Lakini anachokifanya hapa ni kile kijuilikanacho kama Red Herring fallacy, mbinu ya kukwepa hoja ya msingi (central argument) kwa kushadidia hoja za pembeni (peripheral arguments).

Ni mithali ya pale watu wanapohoji juu ya uhalali wa serikali kutumia mabilioni ya pesa kununua ndege ya Rais ilhali kuna watu wanakufa kwa njaa, lakini waziri anayehusika akajibu: “Lazima tutumie kila senti kuhakikisha kuwa Rais wetu anapanda ndege yake mwenyewe. Hivi nani asiyejuwa umuhimu wa Rais kufanya ziara za nje katika ulimwengu huu wa utandawazi. Nani asiyeuona ulazima wa yeye kuwa na usafiri salama katika dunia hii ya ugaidi!?”

Kijuujuu maneno hayo yanashawishi, lakini ukweli ni kuwa yamekwepa hoja ya msingi ambayo ni uhalali wa kutumia mabilioni ya pesa, wakati wa njaa, kununulia ndege. Badala yake yanasokomeza matarajio ya utandawazi na khofu za ugaidi vichwani mwetu. Ndicho pia anachokifanya Rais Mkapa kwa kutujaza khofu za kuvunjika kwa Muungano, ilhali kinachohojiwa ni muundo tu wa Muungano na sio umuhimu wake.

Haistahiki hata kidogo kusema kuwa Rais hauelewi ukweli wa mambo kama vile isivyostahiki kutuita sisi majina maovu. Sisi ni raia wa nchi hii na kuwa kwetu na mawazo tafauti na watawala hakutufanyi kuwa waasi. Wala kuwa kwao watawala hakuwafanyi wawe wazalendo zaidi kuliko sisi, ingawa nasi hatu wazalendo zaidi yao. Wala mawazo yetu si mepesi, kama anavyotaka Rais ionekane, bali ni mazito zaidi.

Hicho ndicho hata kilichothibitika katika hotuba yake hii. Kwamba sisi tunazungumzia juu ya muundo mwengine wa uhusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Tunasema, kwa haki na kwa mantiki kabisa, kwamba muundo huo uwe ni wa serikali tatu. Naye kwenye hotuba hii, licha ya kuusemea sana muundo huu (wa CCM) wa serikali mbili, anagonganisha maneno panapohusika utambulisho wa Watanzania kama Watanzania, kwa upande mmoja, na Wazanzibari, kwa upande mwengine. Wakati mwanzo anasema kuwa watu hawaujuwi utambulisho mwengine isipokuwa Utanzania tu, mwisho anahitimisha kuwa serikali ya Muungano inatambua haja ya Wazanzibari kubakia na kuudumisha utambulisho wao.

Ukimuachilia Mtanzania wa Bara, hapa mgongano ni kwamba kwa Mzanzibari ana tambulisho mbili: mmoja Utanzania na mwengine Uzanzibari. Ukweli wa mambo ni kuwa Wazanzibari wengi hujinasibisha na huu wa mwisho kuliko wa mwanzo. Rejea ripoti ya Kituo cha Katiba cha Afrika ya Mashariki iliyotolewa 2003 na kuitwa Utafutwaji wa Mwelekeo Mpya kwa ufafanuzi zaidi. Kwa Mzanzibari kunakuwa na kile kiitwacho, katika Saikolojia, identity as confusion. Anachukua utambulisho wa Utanzania katika baadhi ya hali na wa Uzanzibari katika nyengine. Hiyo tafsiri yake, kisiasa, ni kwamba Mzanzibari ni mshirikisho kama vile alivyo raia kutoka jimbo la Dresden (tamka Dghesd’n) Ujarumani. Huyu ni Mdresdner kwa upande mmoja, lakini pia ni Mjarumani kwa upande mwengine. Hiyo ni kwa kuwa Ujarumani ni nchi ya shirikisho.

Na ikiwa hivyo ndivyo – na nina hakika ndivyo – basi Mkapa anakubali nini na anakataa nini? Maana anazungumzia kiwango kimoja cha utambulisho, anakitetea kwa hamasa na nukuu za watangulizi wetu, kisha mwisho anazungumzia kiwango chengine cha utambulisho, na anakipa haki yake. Kwa hivyo, aidha anarudi kule kule tuliko sisi, kwamba uhusiano huu ulikusudiwa, na unatakiwa hasa, uwe wa Shirikisho na, au, haamini kimoja kati ya hivyo anavyovisema. Yumkini, kuwa kwake CCM ndiko kunakomueka katika kizungumkuti cha kutokukisema akijuwacho au kutokukijuwa akisemacho katika kizungumkuti hiki. Nakusudia kuwa mgongano huu wa maneno hauwezi kuelekeza, kwa vyovyote vile, katika hitimisho la serikali mbili. Ni ama moja, bila ya Uzanzibari, au tatu, pakiwa na Uzanzibari!

Ni lazima liwe moja kati ya hayo, kwa kuwa hata ule ukweli kwamba zaidi ya 80% ya Watanzania wa leo wamezaliwa baada ya mwaka 1964 na, kwa hivyo, hawaujuwi utambulisho mwengine usiokuwa Utanzania, hauiungi mkono hoja ya serikali mbili. Kwa nini? Kwanza ni huko kupatikana kwa data ya asilimia hiyo. Ikiwa ni asilimia ya Watanzania wote kwa pamoja, ambapo Bara ina zaidi ya milioni 30 na Zanzibar milioni moja tu, basi asilimia hiyo inapatikana bila ya kujumuisha Wazanzibari. Kwamba Wazanzibari hawafiki hata asilimia kumi ya Watanzania wote. Na hiyo si haki kwa dola mbili huru zilizoungana. Ikiwa ni 80% ya Watanzania Bara na 80% ya Wazanzibari, itakuwa ni kinyume na tafiti zote zilizowahi kufanywa hapa na, kwa hivyo, si kweli. Ukiachilia mbali wafuasi wa vyama vya upinzani Zanzibar, hata ndani ya CCM yenyewe muna idadi isiyo ndogo ya watu wanaojinasibisha na wanaouhisi Uzanzibari wao. Kuibuka kwa chama kilichofutwa baadaye cha SAFINA ni dalili tosha.

Pili, vyovyote itakavyopatikana, data hiyo haiwezi kujengewa hoja kuwa watu hawaukumbuki utambulisho usiokuwa huu wa Utanzania. Historia na matukio ya kilimwengu yanapingana na hilo. Tuchukulie Falastina, kwa mfano, iliyochukuliwa na Waisraili tangu mwaka 1948. Sasa ni mwaka wa 56, ambapo pia zaidi ya 80% ya Wapalestina ni wale ambao wamezaliwa ndani ya miaka hiyo 50. Lakini hivi sasa, achilia mbali wale wenye umri wa kuanzia miaka 40, bali hata watoto wa skuli wanavipiga mawe vifaru vya Israel kwamba viondoke katika ardhi yao. Kwa nini, na hali wao walipozaliwa hata hiyo Falastina haipo tena? Si ilikuwa wasiikumbuke kabisa?

Pengine jibu ni kuwa wa Falastina ulikuwa ni uvamizi uliofanywa dhidi yake na Israel wakati wa Tanzania ni muungano wa hiari wa mataifa mawili huru. Jibu hilo linamaanisha, hata hivyo, kuwa sisi tulioungana kwa hiari na uhuru, tunastahiki zaidi kuwa na hiari na uhuru wa kujadili kuungana kwetu. Kama tutakuwa hatuwezi kujadili kwa kuwa tu tumefungwa minyororo ya maoni ya watangulizi wetu, basi wetu utakuwa mbaya zaidi kuliko huo uvamizi!

Ninachosema ni kuwa itaendelea kuwa ni hoja butu, isiyo mashiko, kusema kuwa muundo wa muungano tulionao ni halali hivi sasa, ati kwa kuwa tu tuliambiwa hivyo na waasisi wake. Kwamba sisi, watu tunaoishi miaka 40 baadaye, bado mipaka yetu ya kufikiri imefungwa na wale waliouasisi na kuishi miaka 40 mingine nyuma yetu? Sisi tuliozaliwa ndani ya kipindi hiki tumetafautina kwa kila hali na wao. Hawakuwa na haki ya kutuamulia musatqbali wetu hata kama walikuwa viongozi wetu, kama vile sisi tusivyokuwa na haki ya kuwaamulia wajao miaka 40 mbele. Upeo wetu wa kuona, kama ulivyokuwa wa watangulizi wetu, una mipaka ya kijiografia, kimazingira na kiwakati.

Na mfano wa hilo uko hai. Mwalimu Nyerere alianzisha mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea na kulitangaza Azimio la Arusha kama dira ya mfumo huo. Lakini baada ya kuonekana hauwezi kufanya kazi, mfumo na azimio lake vikaondoshwa. Kwa nini hatukukaa tukavienzi na kuvidumisha? Kwani Mwalimu wa Muungano na wa Azimio si huyu huyu mmoja? Sasa, kama alikosea kwenye Azimio, kipi kinachomfanya asiweze kukosea katika Muungano? Mwalimu hakuenziwa katika Azimio, badala yake viongozi waliomfuatia wameukumbatia na kuuabudu utandawazi ulio kinyume chake. Wala hakuenziwa katika Ujamaa, badala yake CCM inajenga jamii ya kibepari iliyo kinyume chake. Lakini ajabu ni kuwa inang’ang’ania kumuenzi katika muundo wa Muungano tu. Hivi huku kwenye Muungano kuna nini hasa?

Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Rai, toleo Na. 552 la Mei 6-12, 2004

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.