UCHAMBUZI

Zanzibar ina wenyewe

TAARIFA iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Uchunguzi ya Kituo cha Katiba cha Afrika ya Mashariki inasema kuwa “Wazanzibari wana uzalendo wa hali ya juu na wanajivunia sana Uzanzibari wao… mila na utamaduni wao, bila ya kujali tafauti zao za kisiasa…. wanaamini kwamba Zanzibar ni dola na Muungano ni makubaliano kati ya dola mbili huru na ni muhimu hilo lieleweke hivyo”.

Taarifa hii ni matokeo ya uchunguzi uliofanywa baina ya Machi na Mei, 2003 katika maeneo ya Pemba, Unguja na Dar es Salaam. Tume ilifanya mazungumzo na Wazanzibari wa aina mbali mbali kutoka fani, vyama, umri na nafasi tafauti. Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa ugunduzi wake si wa kubuni, isipokuwa umechotwa kutoka vichwa vya Wazanzibari wenyewe.

"Zanzibar ina wenyewe, musijitie kiwewe"
“Zanzibar ina wenyewe, musijitie kiwewe”

Huenda ikawa ugunduzi wa tume hii si mpya kwa Wazanzibari wenyewe, maana unaeleza mambo yanayojulikana kwao tangu zamani. Lakini unaweza ukawa ni ugunduzi mpya kwa wenzetu wa Mrima, na hasa hasa As-haabul-Chimwaga, ambao inaonekana mchago wa kulala kwao na kistaftahi cha kuamka kwao ni mikakati ya kuimaliza Zanzibar na kuufuta kabisa Uzanzibari!

Taarifa hii ni suto kwao, kwamba mikakati hiyo imeshindwa na kamwe haiwezi kufanikiwa. Inawasuta kwa kuwaeleza wazi kwamba Uzanzibari ungalipo, licha ya miaka 40 ya kuubebenya. Kwamba bado umo katika hisia za watu ukirindima vifuani mwao kwa mrindimo ule ule wa siku za kabla ya Uhuru na Mapinduzi. Kwamba bado Zanzibar ina wenyewe!

Hadi leo Wazanzibari wangali wakiendelea kujinasibu, kujilabu na kujilindia Uzanzibari wao. Hii ikimaanisha kwamba kitu pekee ambacho Muungano huu umefanikiwa kukifanya kwao ni kuwavika tu guo la Utanzania kwa kutumia nguvu za katiba na sheria, na wala sio nguvu za imani na fikra.

Kamwe Muungano huu haujawahi kuwafanya Wazanzibari wauamini au wauhisi Utanzania waliovishwa. Kwa maneno mengine, hakuna Mzanzibari anayestaaladhi kwa kuwa kwake Mtanzania, ingawa kimsingi anatakiwa afanye hivyo kwa kuwa hivyo ndivyo ambavyo katiba na sheria za nchi zinamuelekeza.

Kwa hivyo, unapomsoma Mzanzibari kikatiba na kisheria, utamkuta kuwa ni Mtanzania, kwa kuwa ‘analazimishwa’ kuwa hivyo. Kwa mfano, anapaswa kuwa na pasi ya kusafiria ya Tanzania, kwa kuwa kikatiba uraia ni jambo la Muungano.

Lakini ukimsoma kiimani na kifikra, utamkuta kuwa ni Mzanzibari kindakindaki, anayejifakharishia na kujinasibishia Uzanzibari wake. Hata akiwa ugenini akaulizwa yeye ni nani, hujibu kwamba ni Mzanzibari na akibanwa sana ndio atasema kwamba ni Mtanzania kutoka Zanzibar.

Basi kwa Mzanzibari, Utanzania ni kitu kilichopo kikatiba tu, si kiimani. Ukimfunua huko ndani ya chembe cha moyo wake, utakuta kuna Uzanzibari. Na huo ndio anaouhisi na kuuamini. Ukimtukana kama Mtanzania, hashughuliki sana. Hudhani kwamba kuna wengine wa kuutetea Utanzania.

Lakini ukimtukana kama Mzanzibari, huja juu hapo hapo. Hujuwa kama si yeye, hakuna mwengine wa kuutetea Uzanzibari wake. Kama yale maneno ya wanafalsafa: “hapana sharia, pasipo imani” ni ya kweli, basi kwa Wazanzibari ukitiwa Utanzania na Uzanzibari katika mizani moja, upande wa Utanzania utapaishwa juu.

Huo ndio ukweli, na kwa maneno ya Waziri Kiongozi, Maalim Shamsi: “Ni bora mtu aseme ukweli, japo ni chungu na hata kama atakimbiwa na marafiki” (Dira, Na. 48, Oktoba 31- Novemba 06, 2003).

Hawapendi ndugu zetu wa Mrima, hasa waumini wa Chimwaga Supremacy, kusikia haya yakisemwa. Kwao wao ni dhambi isiyosameheka kuuzungumzia Uzanzibari nje ya muktadha wa Tanzania kwa lugha kama hiyo. Kama Mwalimu Julius Nyerere angelikuwa hai, angelisema hii ni dhambi ya ubaguzi, maana alitutaka sote tuamini kuwa hakuna Uzanzibari nje ya Muungano.

Kwa nadharia zake za ajabu ajabu ni kuwa Mzanzibari asingeliweza kujiita Mzanzibari kama usingelikuwepo Muungano huu. “Nje ya Muungano hakuna Uzanzibari…. kuna Uzanzibari na Uzanzibara… Upemba na Uunguja…!”. Maskini, Mwalimu Nyerere hakubakia hai hadi leo, akaja kuushuhudia uhalisia ukimsuta na kuiaibisha nadharia yake!!

Taarifa hii imetoka katika wakati muwafaka kwa kuwa imesindikizwa na mfano hai. Ni majuzi tu ambapo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi huko Pemba, bila ya kujali tafauti zao za kisiasa, walidhihirisha kwamba bado Zanzibar ina wenyewe. Kwa sauti moja, bila ya kugwegwesa, waliupinga ule ulioitwa Mswaada wa Usafiri Majini 2003 ambao ulitayarishwa na Serikali ya Muungano.

Mswaada huu ulikuwa umepelekwa kwao ili waeleweshwe umuhimu na faida zake na baadaye ilikuwa uje ufikishwe na upitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Kupitishwa kwa mswaada huo, pamoja na mengine, kungeliuhalalisha na kuupa baraka ukandamizaji wa Tanganyika kwa Zanzibar kwa kuwa kungeliyaongeza mambo ya biashara, bahari na bima katika jumla ya mambo ya Muungano.

Hilo lingelimaanisha kuiibia Zanzibar maliasili yake, maana hivi ni Visiwa ambavyo rasilimali yake kubwa ni mazao yanayotokana na bahari. Hapa ikumbukwe kuwa kuna mafuta yaliyokwishagundulika katika bahari ya Mashariki ya Zanzibar, na mantiki inatupa sababu ya kusema kwamba mswaada huu umekuja sasa ili kutuporea mafuta yetu.

Na, kwa kuwa mambo hayo yangeliongezwa katika orodha ya Muungano, huo ungelikuwa ni ukiukwaji mkubwa wa katiba zote mbili, ya Zanzibar na ya Muungano. Kwamba, kwanza, katiba hizo zinatambua kuwa Zanzibar ni pamoja na eneo la bahari iliyovizunguka Visiwa hivi, na pili; huu sio utaratibu wa kuongeza mambo ya Muungano.

Huko pia kungelimaanisha kutoa idhini ya kutawaliwa Zanzibar kiuchumi, maana biashara na bahari ndio njia kuu za uchumi za Visiwa hivi. Kuzitawala njia hizo, ndiko kuwatawala Wazanzibari na nchi yao.

Alimradi katika kila msamiati tutakaoutumia hapa, tutakuta kuwa kupitishwa kwa mswaada huo kungelikuwa ni kuzidi ‘kuimezesha’ Zanzibar katika tumbo lisiloshiba la Muungano. Ungelikuwa udalali wa kuvichuuza Visiwa vyetu kwa bei chee, au chembilecho Mhe. Ali Juma Shamhuna, kungelikuwa: “ni kugongomelea msumari wa mwisho katika jeneza la Zanzibar.”

Na kwa hilo, angalau kwa hilo, la kuichuuza Zanzibar, hakuna Mzanzibari anayeweza kulistahmilia. Ndiyo maana Wawakilishi wa Wazanzibari wakalikataa. Kwamba, baada ya yote yaliyokwisha kutokezea, baada ya yote tuliyokwisha kupoteza kwa kuuengaenga Muungano huu, si stahili yetu tena kupoteza zaidi. Stahili yetu ni kuyalinda haya yaliyobakia na kuyarejesha walau baadhi ya yale yaliyokwisha kututoka, ikiwa si yote.

Hili linaweza kuchukuliwa na As-haabul Chimwaga kuwa ni kuukosea adabu Muungano na hivyo kuwaona waliohusika hawana manufaa kwao. Maana, kwao wao, kwa kiongozi wa Zanzibar kuwa na manufaa ni kukikubali kila wanachokitaka wao juu ya khatma ya Zanzibar. Akionesha kukikataa, huyo huwa si mwenzao, na kwa kuwa khatamu za nchi hii ziko kwao, basi si hasha kumbwaga chini. Hilo ndilo wanalopaswa kujitayarisha nalo wajumbe wa upande wa CCM ambao waliupinga mswaada ule.

Kwamba mang’weng’we wa Chimwaga hawajazowea kupingwa na Wazanzibari. Walichozowea ni kuleta kabrasha lao hapa, wakalifunguwa kwa mbwembwe na pozi, wahishimiwa wetu wakalipigia makofi na kisha wakalipitisha kwa asilimia zote. Chimwaga haijazowea kupokea changamoto kutoka Zanzibar, na hili la mara hii, lishakuwa tusi kwao.

Lakini, ikiwa watachukulia hivyo ni shauri yao. Huo ndio msimamo wa Wazanzibari na hiyo ndiyo kauli yao. Kwamba hawataki kuyasalimisha mamlaka ya nchi yao zaidi ya hapo walipokwisha kuyasalimisha. Kile wapaswacho kukielewa wenzetu hao ni kuwa Wawakilishi wetu waliposimama kuupinga mswaada ule, walifanya hivyo kwa niaba yetu Wazanzibari, tena sote.

Na kwa hakika, msimamo na mshikamano wa aina hii tuliutarajia zamani, lakini tukaukosa. Na, kwa bahati mbaya, kukosekana huko ndiko kulikowalemaza ndugu zetu wa Mrima hata wakafika pahala pa kuamini kuwa: “Haka kazanzibari ni kashamba ketu tu. Tunaweza kukiamulia tunavyotaka”. Hilo lilikuwa ni koseo.

Ni kosa kubwa kuichukulia Zanzibar, kutokana na udogo wake, kuwa ni shamba tu la Tanganyika ambalo lingeweza kupangiwa na kuamuliwa mambo yake yote kutoka Chimwaga. Haifai kuwachukulia Wazanzibari, kutokana na uchache wao, kuwa hawana ubavu wa kuyapinga maamuzi yafanywayo dhidi yao. Na haistahiki kabisa kuuchukulia Uzanzibari kuwa ni kansa, ambayo lazima ididimizwe na ikandamizwe kwa hali yoyote ile ili isije juu na kuwaambukiza wengine.

Jitihada za aina hiyo zimeshafanyika sana huko nyuma na kwa bahati mbaya zikapata mafanikio. Ndio sababu Zanzibar ikafikishwa hapa ilipofika sasa. Sababu kubwa ya kufanikiwa huko ni uzembe na ulafi wa baadhi ya Wazanzibari wenzetu waliokuwa na madaraka. Pupa yao ya vyeo vigaiwavyo Chimwaga ilitugharamu hadhi na nafasi ya nchi yetu katika Muungano.

Ni uzembe na ulafi huo ndio ulioiruhusu kasumba ya ubaguzi kupenya haraka katika vichwa vyetu hata tukashindwa kusimama kama watu wamoja. Kwa sababu tu ya cheo na madaraka, sisi ndugu wa baba na mama mmoja tukakubali tuitwe na tuitane kama Waafrika na Waarabu, Wapemba na Waunguja, na sasa kama Wakaskazini na Wakusini. Kwa nini tusiitwe na kuitana Wazanzibari? Huu ulikuwa, na unaendelea kuwa, upuuzi mtupu.

Usingelikuwa upuuzi huu, hivi sasa khadithi ya nafasi ya Zanzibar katika Muungano ingelikuwa ikisimuliwa vyengine. Aidha pasingelikuwa na malalamiko ya kudhalilishwa na kudunishwa au, kama yangelikuwepo, yangelitokea upande wa pili wa Muungano, na sio huu wetu.

Sasa, tuseme yashayopita si ndwele, tugange yajayo. Binafsi, kama Mzanzibari, nimefurahishwa hadi na msimamo na mshikamano uliooneshwa na wawakilishi wetu mara hii. Naogopa kutumai sana kwa kukhofia kutamauka, lakini lazima niseme kwamba inatia moyo kidogo kuona kuwa wawakilishi wa Wazanzibari wanasimama na kushikamana kama Wazanzibari kuitetea Zanzibar yao. Fakhari ilioje katika siasa za petu!

Ni fakhari kubwa kuwaona viongozi wako wanaitetea nchi yako na sio matumbo na vyeo vyao. Huu ni mwamko mpya ambao lazima upongezwe na uendelezwe. Inshallah, siku za kuyapigia makofi na kuyapitisha kila yashushwayo kutoka Chimwaga ziwe zimeshapita na upepo. Sasa ziwe ni siku za kuyajadili na kuyatolea maamuzi kwa mujibu wa maslahi ya Zanzibar, Uzanzibari na Wazanzibari. Kwamba hiyo ndiyo maana ya kuwa kiongozi bora kwa Zanzibar. Kuna haja gani ya kujiita kiongozi wa Zanzibar ilhali unashindwa kuitetea nchi yako?

Umoja wa wawakilishi wetu dhidi ya mswaada huu ndio picha halisi ya uongozi wa Zanzibar tuutakao. Unaweza kuwa uongozi ulioundwa na wanachama wa vyama tafauti, kutoka Visiwa na koo tafauti, lakini wote ni wana halisi wa Mama Zanzibar. Panapohusika Zanzibar, husimama kama viongozi wa Zanzibar wakausemea na kuutukuza watani wao. Hapo, chama chao, kisiwa chao na ukoo wao, unakuwa ni Uzanzibari tu!

Matumaini ya Wazanzibari sasa ni kuona kuwa umoja huu unaimarika na unaleta matunda mema kwa nchi yao. Kwa hakika Wazanzibari hawafurahishwi kuona kuwa wawakilishi wao wanaingia vikaoni na U-CUF au U- CCM wao mikobani na kuuwacha Uzanzibari wao majimboni. Ni mgawanyiko huu ndio uliotumiliwa na wasioitakia mema nchi hii kuimeza na kuinakamiza. Ya kuwagawa uwatawale, yanapaswa kufika khatima!

 

Dira, Na. 49, Novemba 7-13, 2003

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.