UCHAMBUZI

Ya Raza na ya Feruzi: Nusu uongo, nusu ukweli

MOHAMMED Raza amesema. Kitu alichokisema ni muhimu sana katika siasa za ukweli na uwazi, lakini hakikuwapendeza wakubwa wa chama chake, CCM.

Kubwa alilolisema ni kuwa CCM Zanzibar imekuwa dhaifu sana, inameguka. Sababu kubwa ya hali kuwa hivyo, alisema, ni kudharauliwa kwa aliyekuwa makamo mwenyekiti wa chama hiki kwa upande wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour. Na akatowa changamoto kwamba ikiwa uchaguzi utafanyika leo hii Zanzibar, basi CCM itabwagwa.

Kuambiwa kuwa CCM Zanzibar ipo katika hali mbaya sana kiasi ya kwamba kuna khatari hata ya kupoteza uwezo na nafasi ya kuitawala Zanzibar kwa kipindi kijacho cha uongozi, kumewakera sana wakubwa wa chama hiki. Na kama tulivyotarajia, na pia kama ilivyo kawaida wa vingozi wa CCM, kauli hii wanaikanusha. Kukanusha imekuwa ni sehemu ya utamaduni wao. Saleh Ramadhan Feruz, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar, akavoromboka kumjibu Raza.

Jibu la kwanza likawa ni kumkana Raza na, la pili, la kuikana kauli yake. Ninaposema amemkana Raza, sikusudii kwamba ameukana u-CCM wa Raza, bali ameukana uweledi wake wa mambo ya CCM na nchi kwa ujumla. Kwamba Raza hana lolote alijualo zaidi ya kuwa msaka umaarufu, mbumbumbu na mrapiaji mambo.

Kwa mujibu wa Feruz, haikuwa stahili ya Raza, kama mwana-CCM, kujikurupuwa na ‘kumwaga radhi’ hadharani kwa kitu ambacho kingelifaa kuzungumziwa faraghani, ndani ya vikao vya chama.

Binafsi, nalichukulia jambo hili la kumuita Raza mbumbumbu, msaka umaarufu na mrapiaji mambo, kuwa ni mashambulizi ya moja kwa moja, na yasiyo ya kistaarabu. Sina hakika, lakini nakhofu kuwa kama Raza angeliambiwa maneno kama hayo na mtu wa chama chengine au chombo cha khabari, basi tayari angelikwishafunguwa kesi ya madai mahkamani kwa kudhalilishwa. Lakini hayo ni mambo ya Ngoswe!

Na, pili, Feruz akaikanusha kauli ya Raza: kwamba haina uwiano wowote na ukweli. Si kweli kwamba CCM-Zanzibar inameguka. Si kweli kwamba Komando anadharauliwa, na, kwa hivyo, si kweli kuwa CCM imo khatarini kupoteza udhibiti wa kisiasa Zanzibar.

Sasa ni nani mkweli kati ya hawa wawili? Mwenyewe Raza alipokuwa akimjibu Feruz alisema kuwa ni Watanzania, na hasa Wazanzibari, ndio watakaoamua ni nani mkweli kati yao. Na huo ndio ukweli. Sisi ndio waamuzi.

Mawazo yangu mimi ni kwamba hakuna hata mmoja kati ya wawili hawa ambaye ameusema ukweli wote kama ulivyo, isipokuwa wote wameisema ile sehemu moja tu ya ukweli wanayotaka ifahamike, tena kwa staili yao.

Tuanze na hili la msingi, yaani udhaifu na kumeguka kwa CCM Zanzibar. Kama tutaiangalia CCM kama chama cha siasa, yaani mkusanyiko wa watu wenye azma moja katika uendeshaji wa nchi, basi ni rahisi zaidi kuuthibitisha udhaifu na mmeguko wake kuliko kuukanusha. Angalau kwa hili, kama si kwa mingine, Raza alikuwa sahihi zaidi kuliko Feruz.

Kwamba kama chama cha siasa ni mkusanyiko wa watu wenye dhamira moja ya kuchukuwa au kuendelea kuwa na madaraka ya nchi, basi waliomo katika CCM hivi sasa ni watu wenye tafauti kubwa sana juu ya uongozi wa nchi hii. Ni hilo, bila ya shaka, ndilo lililopelekea kuibuka kwa SAFINA na SOFT.

Pengine inaweza kuhojiwa kuwa hakuna vyama hivyo hivi sasa kwa kuwa havijasajiliwa rasmi na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa. Si kitu. Almuhimu ni kuwa kama harakati za kisiasa, basi vyama hivyo vipo na kuwepo kwake ndiyo hiyo kasoro ya CCM.

Hii ni dalili inayotosha kuelezea kuwa CCM Zanzibar haisimami tena kama jumuiya moja, bali kama mkusanyiko tu wa vijijumuiya vidogo vidogo, huku kila kijijumuiya kikijipa haki zaidi ya kuwa bora na kujiona kuwa ndicho chenye uzalendo na nia nzuri zaidi na nchi hii.

Mgawanyiko baina ya wa Kaskazini na wa Kusini, wa mjini na wa mashamba, baina ya wa maskani hii na wa maskani ile, ni wa ajabu sana ndani ya CCM hivi sasa, na hilo halina ubishi. Kwa hivyo, mpaka hapo credit ni ya Raza kwa kuuanika ukweli huo na ni makosefu kwa upande wa Feruz kwa kuukanusha.

Hata hivyo, hili nalo linazuwa swali linalomuoteza kidole Raza na wengine wa sampuli yake. Kwamba jee, udhaifu huu wa CCM umeanza na awamu hii ya utawala? Kwa namna gani tunaweza kuutenganisha udhaifu huu na udhaifu wa kisiasa wa utawala uliopita?

Ikumbukwe kwamba katika awamu iliyopita ya utawala, Raza alikuwa na jina na satuwa kubwa sana kiasi ya kuchukulika kama ‘mtoto wa Ikulu’. Kwa ukaribu wake na utawala wa wakati ule, ilikuwa ni sawa kumuita mmoja kati ya mawaziri au wasemaji wa serikali na chama kwa upande wa Zanzibar, hata kama cheo hicho hakikuainishwa wazi. Kwa hivyo, hatuwezi kumvua kando na mafanikio na, au, makosefu yoyote ya serikali na chama kwa wakati ule.

Sasa ni miaka mitatu tu tokea akina Raza watoke katika duara la siasa za wazi wazi hapa Zanzibar. (Nasema siasa za wazi wazi tu, maana si stahili hata kidogo kuamini kuwa wametoka moja kwa moja katika siasa zote). Lakini katika muda huu mchache, tayari CCM imekuwa haitamainiki.

Kwangu mimi, kama ilivyo kwa wengine pia, jambo hili linaonesha mambo mawili: moja ni namna gani viongozi waliopita walivyoshindwa kuijenga CCM kimfumo (systematic), na badala yake wakajijenga wao wenyewe tu katika ulwa. Walipobomoka wao, nayo imebomoka.

Kwamba hawakuwa wanasiasa wazuri, maana mwanasiasa mzuri hujenga mfumo wa kufuatwa. Kwamba hata akiondoka yeye, mfumo hubakia na kudumu. Mwanasiasa mbaya hujijenga yeye mwenyewe. Anapoondoka, kila kitu hupwaya na kudorora. Kuna uwezekano mkubwa kwamba benchi ya awamu iliyopita, ilijaa wanasiasa wa aina hiyo, na hiyo ndio sababu leo hii CCM Zanzibar imeshararuka raruraru.

Lakini jengine linaloonekana hapa ni ule uwezekano kwamba viongozi waliopita walimudu kuifanya CCM Zanzibar kuwa moja (kama kweli ilikuwa moja) kwa kutumia siasa chafu. Pengine uhuru wa kuwa na mawazo tafauti na kuyadhihirisha mawazo hayo, ulikuwa adimu sana ndani ya awamu iliyopita.

Yumkini kama ni enzi zao, basi SAFINA isingelifika kutweka, maana ingelibamizwa tangu ilipokuwa ikichongwa. Misumari na mbao zingelifichwa zisionekane hata zilipokwendea! Inawezekana hili ndilo lililoifanya picha nzima ya CCM Zanzibar wakati ule kuonekana imara kuliko ilivyo hivi sasa, lakini kwa ukweli hasa haikuwa madhubuti kisiasa, kwa maana ya umadhubuti wa kiushawishi.

Angalia kwamba hili haliukanushi udhaifu wa CCM Zanzibar kama ulivyobainishwa na Raza, lakini linaelezea kuwa udhaifu huo haukuanza leo. Kwamba kile alichokiona Raza kuwa CCM katika zama zao ilikuwa madhubuti na imara zaidi, kilikuwa ni magazigazi (mirrage) tu. Ukweli ulikuwa kando ya hapo.

Kwa sasa, nadhani Feruz anapoteza muda wake kujibizana na Raza kwa hili. Maana huko ni kupingana na hata ule ukweli anaouona kwa macho yake mwenyewe. Hata humo nafsini mwake mwenyewe haamini hicho anachokisema. Kwamba hata huko kujibizana na Raza tu, peke yake, ni ishara kubwa kuwa ndani ya CCM Zanzibar, mambo si shwari hata kidogo. Ambacho kingelimstahilikia hivi sasa Feruz, ni kuangalia nini chanzo cha udhaifu wa chama chake kisiasa, ili kama kuna makosa waliyoyarithi kutoka kwa watangulizi wao, wapambane nayo.

Nakumbuka katika hotuba yake ya kuwaaga wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM mwaka uliopita, alipokuwa akiacha nafasi ya umakamo mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Salmin Amour Juma alisema kuwa yeye anaondoka katika nafasi hiyo lakini anamuomba mtu atakayechukuwa nafasi yake aendeleze yale mema machache aliyoyatenda na yale maovu yote amuwachie mwenyewe.

Ni kwa kiasi gani makamo mwenyekiti wa sasa ameyaacha yale mabaya ya Komando, na kwa kiasi gani ameyaendeleza yale mema yake? Hilo ndilo ambalo akina Feruz walitakiwa walichukulie kama changamoto kwao, na sio kukurupuka na kujibizana na Raza.

Chengine alichokisema Raza, ili kuhalalisha kauli yake ya udhaifu wa CCM Zanzibar, ni kwamba kama ukija uchaguzi leo, basi CCM itashindwa. Hapa alikuwa anatoa changamoto kwa kuilinganisha CCM ya jana na ya leo. Alikuwa anafanya comparative study.

Nadhani changamoto hili ndilo lililomkasirisha zaidi Feruz. Basi hata mwana-CCM mwenzake anathubutu kukaa mbele ya qadamnasi kukubali kuwa CCM itashindwa katika uchaguzi? Angalau neno hili si alikuwa aliseme mtu wa chama chengine, lakini mwana-CCM kindakindaki? Pengine ni upotofu wa kisiasa kwa Raza kutoa changamoto kama hili kwa chama chake mwenyewe, lakini pia ni upotofu mara mbili zaidi kwa Feruz kupambana naye jukwaani.

Ni kama ile hadithi ya mwendawazimu aliyekwenda kumkuta mtu mwenye akili zake timamu msalani anakoga. Yule mwendawazimu akazichukuwa nguo za yule mwenye akili na kukimbia nazo. Mwenye akili kuona nguo zake zinachukuliwa, akavoromboka mbio msalani, mtupu kama alivyozaliwa, kumfukuza yule mwendawazimu ili apate nguo zake. Sasa ni nani mwendawazimu zaidi kati yao?

Inawezekana changamoto la Raza likasadifu, lakini, je, ni kwa mlinganisho huo aliolinganisha? Maana kama kigezo ni mlinganisho huu, lazima niseme kuwa, hapa Raza hajausema ukweli wote. Kwani anakusudia uchaguzi upi hasa huo, ambao ukifanyika leo, CCM Zanzibar inaweza kubwagwa lakini ambao jana ingelishindikana? Uchaguzi huo ni huu wa kipetu wa kimagube, au ule uchaguzingwa, ulio huru, wa wazi na wa haki?

Ikiwa ni huu wa kipetu wa kimagube, basi ni wazi kuwa hata ukaja leo na kesho na keshokutwa, hakuna siku CCM itakayobwagwa na chama chochote kile, kama vile ambavyo haikubwagwa jana. Na hilo Feruz halina haja ya kumtia wasiwasi. Lakini kama ni ule ulio huru na wa haki, basi Raza hakuwa na haja ya ‘kujifyagilia’, maana hata hiyo jana, hapo Raza alipokuwa chibui wa Ikulu, kama ungelifanyika uchaguzi wa aina hiyo, basi CCM isingelishinda.

Kwa hivyo, hapo hapana la kujidaia wala la kulilinganisha. Si kweli kuwa katika zama zao walifanya kazi kubwa ya kuijenga CCM kiasi ya kuwa haikuweza kushindwa katika uchaguzi hata mmoja. Ushindi uliopatikana na CCM enzi za akina Raza haukuwa ukitokana na umahiri wa viongozi wake wala umakini wa wanachama wake katika kujenga siasa, bali ulitokana na magube yao. Na kama ni magube hayo, basi CCM hii ya leo haishindwi kuyafanya. Na kyei leo, wana uwezo wa kuyafanya kisayansi zaidi.

Mwisho nataka niseme, kwa kurudia tu, kuwa majibizano haya ya Raza na Feruz ni picha halisi ya hali ilivyo ndani ya chama hivi sasa. Tunaweza kusema kuwa Raza anawakilisha mawazo ya wanachama wa CCM wasiopendezewa na namna chama chao kinavyopelekwa; na Feruz anawakilisha viongozi wa CCM wasiokubali kuwa wanafanya makosa.

Kuna uwezekano kwamba akina Raza si mmoja na yeye katumwa tu na wenzake kulisemea hili, na ndio maana akachaguwa jukwaa la Bara, maana hapa hivi sasa hana mdomo wa kulisemea. STZ, TVZ na Zanzibar Leo visingeweza kumstahmilia kuyasema haya mbele ya nyuso zao.

Basi, kwa Feruz kukurupuka na kumuita Raza kuwa ni msaka umaarufu tu ndio maana akasema anayoyasema, ni kujipumbaza tu. Ukweli unabakia pale pale. Hata kama ni kweli kuwa Raza anaupenda umaarufu, basi yeye tayari ni maarufu zaidi kuliko Feruz. Cha kufanya sasa, kwa wote wawili na makundi yao kama wanayo, ni kujenga chama, kama kweli ni wajengaji,  maana chama ndio hivyo chabomoka


Dira, Na. 34, Julai 25-31, 2003

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.