UCHAMBUZI

SMZ funga mlango mmoja, utaikuta kumi i wazi!

BAINA ya Athens ya zama za Socrates na Zanzibar ya zama za Dira hapana tafauti kubwa sana. Ukitowa tafauti za kijiografia na kiwakati, kwamba Athens iko Ulaya na ni ya miaka 400 K.K. na Zanzibar iko Afrika, miaka 2003 B.K, mengine mengi yanafanana. Kama ilivyokuwa kwa Athens, Zanzibar nayo inatawaliwa na tabaka la watu wasiotaka kuhojiwa wala wasiostahmilia mawazo tafauti na yao. Hatua ile ile waliyoichukua watawala wa Athens katika kuzima moyo wa kuhoji uliokwishaanza kujengeka katika jamii kwa kumnyonga Socrates ndiyo inayochukuliwa na watawala wetu. Hivi sasa, SMZ inataka kulinyonga Dira!

Waziri anayehusika na habari Zanzibar, Salim Juma Othman.
Waziri anayehusika na habari Zanzibar, Salim Juma Othman.

Lakini kama walivyoshindwa watawala wa Athens kuua u-Socrates, yaani utaratibu wa kudadisi na vuguvugu la ujenzi wa jamii mpya, ndivyo SMZ isivyoweza kuua u-Dira, kwa maana hiyo hiyo. Ndivyo isivyoweza kuikandamiza sauti ya kuhoji kutoka katika jamii ya Wazanzibari. Ndivyo inavyozitayarishia mazingira sauti nyingi zaidi kupaa na kusema kile kile isichotaka kisikikane.

Hiyo ndiyo kanuni ya kilimwengu, na SMZ haina ubavu wa kuiepuka. Kwamba kote ulimwenguni, hakuna serikali iliyofanikiwa kuishinda nguvu ya umma hata kama itakuwa na nyenzo na dhamira ya kiasi gani kufanya hivyo. Kote ulimwenguni, nguvu zinapotumika kuufunga mlango mmoja, ndipo zinapotowa fursa kwa mingine kumi kuwa wazi. Kama watu walipita kwa taklifa kwa mlango huo mmoja, ndipo sasa watakapopita kwa ‘kujinafasi’ kwa milango hiyo mingi!
Katika Athens hiyo ya Socrates, tabaka la watawala liliamini sana juu ya uadhamu wake (absolutism). Kiilivyo ni kwamba hawakuwa na uadhamu huo, na wenyewe walilijuwa hilo. Lakini, kwa makusudi kabisa, waliijenga jamii ya Waathens iamini kwamba wao (watawala) ni viumbe bora, waadilifu, wenye nia nzuri, wachapa kazi na wenye haki zaidi ya kutiiwa na kunyenyekewa kuliko kiumbe chochote chengine.
Walitaka iaminike, na kwa kweli walifanikiwa kuwafanya watu waamini, kuwa serikali inayoongozwa na wao kilikuwa ni chombo cha juu kabisa cha utawala kilichotukuka na kutakasika na kila ovu na kilicho na haki ya kuwa juu ya kila kitu.
Hivi ndivyo pia walivyo watawala wetu. Ingawa wanajuwa kuwa wana mapungufu chemvu kizima, wanataka tuamini kwamba wao ni absolute, wakamilifu. Hata kama wanajuwa kwamba serikali wanayoiongoza imetoka mikononi mwetu wananchi, wanataka ichukulike kuwa iko juu yetu na kwamba imetakasika. Haigusiki kwa lolote, kwa chochote na kwa hivyo isihojiwe wala isidadisiwe!
Kwa kuwa uongo wa aina hii ulidumu sana katika dola ya Athens, ulifika pahala pa kuzoeleka, na hivyo ukaonekana ndio ukweli wenyewe. Watawaliwa waliozibwa macho na kasumba ya absolutism ya watawala, hawakuwa na uthubutu wa kuuona upande wa pili wa shakhsia za watawala wao. Hata alipotokea mtu kuyaeleza mambo tafauti na uelewa wao, walikuwa wakimkana na kumtenga.
Na hata hapa Zanzibar hali ilikuwa vivyo kwa siku kadhaa huko nyuma. Ama kutokana na woga wao au ujinga wao, watu wengi walikuwa wanashindwa kumgeuza mtawala na kumuangalia kule mgongoni kwake. Walikuwa wanaamini tu yale waambiwayo majukwaani: “Huyu ni mwenzetu, hana doa, ni mpenda maendeleo, si mbinafsi!” Hata alipotokezea mtu kuwabainishia utoadilifu, uzembe, ubadhirifu na ufisadi wa mtawala wao, hawakuwa wakimuelewa.
Katika mkasa maarufu wa Allegory of the Cave, Plato anasimulia juu ya wafungwa waliofungwa mahala fulani katika pango na kuelekezwa nyuso zao ukutani. Nyuma yao, sehemu ya juu, kuna moto na mbele ya moto pamewekwa vitu. Kutokana na muangaza wa moto huu, vitu hivi hufanya vivuli vyake pale ukutani. Wafungwa hawa hawajapata kuviona vitu hivi katika uhalisia, na hivyo kwao wao vile vivuli ndivyo vitu vyenyewe!
Siku moja, mmoja wao anafunguliwa minyororo na kuja nje. Huku anaviona vitu halisi sio vivuli vyake – ukweli sio uzushi. Anang’amua kwamba ule aliokuwa akidhani mwanzo kuwa ni mti, kumbe haukuwa mti hasa, bali kivuli chake tu. Mti kweli una majani ya rangi kijani, una matunda rangi ya manjano, una kigogo rangi nyeusi na sifa nyenginezo.
Kwa hamu ya kupata uelewa huu mpya, anarudi kwa wenzake pangoni kuwapasha yaliyopo. Lakini wenzake wanakataa kwamba kile walichoamini siku zote kuwa ni ukweli, kumbe ulikuwa ni uzushi mtupu. Kwa kuwa ukweli huu unawaeleza kwamba siku zote hizo walikuwa ni wajinga, wanalichukulia kuwa ni tusi. Matokeo yake wanamuua mwenzao na hivyo wanaendelea kubakia katika ujinga wao!
Waathens walibakia na ujinga wao hadi alipotokea Socrates. Huyu alikuwa ni raia wa kawaida tu, mzee na mnyonge, lakini mwenye kipaji kikubwa cha kuvunja na kujenga hoja na kuuhakiki upya uadhamu huu wa watawala. Kuanzia hapo, taswira hii iliyojengwa na watawala juu ya shakhsia yao ikaanza kuchujuka. Na hilo likawashtua sana, wakijuwa kuwa punde kile kilicho nyuma ya pazia kingelidhihirishwa ukumbini!
Ingawa, kwa Zanzibar, watu walianza ‘kukarambuka’ na mapema, lakini ujio wa Dira hauna tafauti sana na ule wa Socrates kwa Athens. Dira imesaidia sana kujenga uelewa wao juu ya nchi yao na khatma yake, na kwa hivyo nafasi, dhima na shakhsia halisi ya watawala panapohusika staili yao ya kuitawala Zanzibar. Kwa kuiona khatari ya kuwekwa uchi na kujuilikana undani wao, wakubwa wameshtuka na sasa wanaisakama Dira.
Inachokifanya na inachofanyiwa Dira sasa si kipya, ni kile kile cha Socrates. Socrates alikuwa na mawazo tafauti juu ya msingi wa uadhamu uliojijengea tabaka la watawala. Alihoji uadilifu wao, ilimu zao, mipaka ya nguvu zao, ucha Mungu wao na, hivyo, hata uhalali wao wa kuwapo madarakani. Alidadisi maana ya uongozi, akitaka kujuwa tafsiri halisi ya uongozi ubora na mengineyo.
Staili yake ya kuhoji haya ilikuwa ni kuidadisi misimamo na imani za msingi walizonazo watu kuhusu mambo hayo. Kwa mfano, angelimwendea jaji ambaye anajichukulia mwenyewe na anachukuliwa kuwa muadilifu na kumuuliza: “Ni nini uadilifu?” Jibu lolote ambalo angelilipata, lingelizaa maswali mengine, hadi mwisho ingelidhihirika kuwa kumbe jaji yule haujuwi uadilifu ni nini. Basi, kwa hivyo, ikiwa yeye jaji mwenyewe haujuwi uadilifu, hawezi kabisa kujiita muadilifu na wala hawezi kuhukumu kiadilifu!
Kwa staili hii hii, ndivyo ambavyo Socrates aliwaandama wakubwa wengine katika nyanja nyengine za utawala na maisha: ilimu, siasa, uongozi, sanaa na kadhalika. Matokeo yake ni kuwa watu wengi wakubwa wakajikuta hishima zao zinatiliwa mashaka na raia wa kawaida. Kwa kipindi kifupi sana, hili likampatia Socrates umaarufu mkubwa na marafiki wengi miongoni mwa raia walioona ‘mwangaza mpya’.
Ni kipindi kifupi pia tangu Dira ianzishwe, lakini umaarufu wake na hishima iliyojijengea ni mkubwa kuliko umri wake. Watu wengi sasa wanaichukulia Dira kuwa ni skuli yao ya kujifunza mambo mapya na kuongeza ufahamu wao kwa wale waliyokuwa wakiyajuwa tangu kabla.
Kwa staili hii hii ya Socratic method, Dira inahoji uadhamu wa watawala wetu, utendaji kazi wao na namna wanavyoyatumia madaraka waliyokabidhiwa na umma. Inadadisi matumizi ya fedha za umma, inajadili mfumo wa kisharia, inauchambua Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, inaulizia ulipo uadilifu wa watawala, na kadhalika na kadhalika. Kama lilivyokuwa lengo la Socrates, Dira nayo inatazamia ujenzi wa jamii mpya. Si zaidi wala si pungufu ya hilo.
Lakini kufanya kazi kama hiyo katika mazingira ya utawala wa mkono wa chuma kama haya kunahitaji moyo mkubwa sana. Kwamba kadiri Dira, kama Socrates, inavyojiundia marafiki wengi kutoka tabaka la watawaliwa, ambao hawana silaha yoyote zaidi ya dhamira na kiu yao ya kujuwa, ndivyo inavyojiundia maadui wengi kutoka tabaka tawala, ambao wana kila aina ya silaha, isipokuwa busara. Kwamba kadiri wadogo wanavyopendezewa nayo, ndivyo wakubwa wanavyochukizwa!
Inuko la Socrates kama msomi mkubwa na mdadisi asiyeshindika, liliwashtua sana wakubwa wa Athens. Ilifika mahala kila aendapo hufuatwa na kundi la vijana kusudi kufaidika na uwezo wake mkubwa wa kiakili aliokuwa nao. Kuna baadhi ya wakubwa walikataa kuhojiana naye kwa kuogopa kuangushwa kitakotako na hoja zao. Hilo likamfanya yeye kuwa shujaa na vijana wakamhusudu sana.
Unapomhusudu mtu, ni wazi kwamba unaathirika naye; na unapoathirika naye, huwa unataka uwe kama yeye. Kwa hivyo, kidogo kidogo vijana wa Athens wakaanza kuchota tabia ya Socrates. Tahamaki vijana wengi wakawa wanathubutu kuwahoji wakubwa wa Athens, miongoni mwao wakiwa wazazi wao wenyewe.
Inuko na umaarufu wa Dira sio tu kama chombo cha khabari, bali zaidi kama taasisi ya kitaaluma hauwezi kubishika kwa yeyote anayeijuwa hali halisi ya Zanzibar tangu kuanzishwa kwake hadi hivi sasa linapokamilisha mwaka mmoja.
Hivi sasa uwezo wa Wazanzibari kuhoji umepanda kwa asilimia kubwa. Imekuwa jambo la kawaida sasa, kukuta ndani ya hata maskani za CCM kuna mijadala ya wazi kuhusu khatma ya Zanzibar na nafasi yake katika Muungano. Watu wengi sasa wanadadisi uwezo wa serikali na wanataka kujuwa viongozi wao wanafanya nini kuitetea nchi yao.
Inaposoma barua na makala za wasomaji katika kurasa za Dira, Serikali ya Mapinduzi, kama ilivyokuwa ile ya Athens ilipowaangalia vijana wake, inaona kuna khatari mbele yake. Hii ni kwa kuwa mfumo wa kitawala una mapungufu mengi, na sio absolute kama inavyotaka ufahamike!
Kuwepo kwa mapungufu haya upande wa serikali ndiko kunakofanya iwe rahisi kwa watu kuielewa Dira haraka haraka. Kwamba inawaeleza kitu kilicho hai mbele ya macho yao, sio cha dhahnia. Na kwa kuwa ni rahisi kuielewa, ndiyo pia imekuwa ni rahisi kwao kuitumia staili hii ya Dira kujenga na kuvunja hoja.
Hivi sasa wakubwa wanapoingia vikaoni, wanashangaa kukumbana na hoja nzito nzito kutoka kwa wajumbe wa vikao vyao. Wanaona kuwa tabia hii ya kuhojihoji haikuwapo hadi hivi majuzi tu, sasa ghafla hii imetokea wapi? Wa Athens walivielekeza vidole vyao vyote kwa Socrates, wa SMZ wanavielekeza kwa Dira. Ni sawa. Watu wanaihusudu Dira, wameathirika nayo na sasa wanajigeza. Wanataka wawe kama iyo. Hilo linawauma mno wahishimiwa, watukufu wetu.
Na ni hapo tu, si penginepo, ndipo panapozuka ‘uhalali’ wa kuiandama Dira. Kwamba imezuka kama kizingiti kwa maslahi ya wakubwa. Inafundisha watu ‘vibaya’. Inafundisha kuhoji yasiyohojiwa, kuuliza yasiyoulizwa. Kwa tafsiri yao watawala, serikali ni chombo kilichotukuka, haipaswi kuulizwa wala kukosolewa. Na sasa hayo yanafanyika. Ni nini kama si kuichokoza serikali!
Wakati watawala wa Athens walipoona kuwa mafundisho ya Socrates yanahatarisha uadhamu wao, wakashindwa kuli-stomach hilo. Haraka haraka wakachukuwa hatua za kusitisha kile walichokiona kuwa ni ‘uasi’ dhidi yao. Wakamkamata na kumfungulia mashtaka ya uchochezi. Akaambiwa kuwa alikuwa anawaghilibu na kuwaharibu vijana wafanye maasi dhidi ya serikali yao.
Hapo ndipo kesi ya mwanzo ya uchochezi ilipofunguliwa katika historia ya ulimwengu. Kama ilivyokuja kuwa dasturi za baadaye za watawala wa mkono wa chuma, kama huu wetu, kesi hii ilifunguliwa na serikali dhidi ya raia wake yenyewe. Huyu alikuwa ni dhaifu, mzee na mnyonge. Hapa petu napo, kwa maneno ya Mkurugenzi wa Habari wa SMZ, nao sasa wameshashindwa ‘kuli-stomach Dira’ kwa kuwa ati linachochea watu waipinge serikali yao. Linajenga uasi.
Katika tawala za aina hii, hata kama raia hana kosa, si rahisi kwake kuibwaga serikali mahkamani. Sababu ni kuwa serikali na mahkama huwa ni Ambari na Zinduna. Hao hao wanaoshtaki, huwa ndio hao hao wanaohukumu. Kupigwa, hupigwa raia; kushtakiwa, akashtakiwa yeye; na mwisho wa khabari kufungwa, akafungwa yeye!
Kimsingi, Socrates hakuwa na makosa lakini alishindwa mahkamani. Inasemekana kwamba walichokuwa wakikitaka hasa wakubwa wa Athens katika kesi hii sio kuadhibiwa kwa Socrates. Walijuwa fika kwamba hakustahili adhabu kwa kuwa hakuwa na kosa.
Walichotaka ni kuwa aonywe na aache tabia yake ya udadisi na kisha mahkama imtake aombe radhi. Kwa kufanya hivyo kungeliwapelekea wale waumini wake waone kwamba kiongozi wao alikosea na hivyo, nao, wasingeliendeleza dasturi yake ya kuhoji. Walitaka hilo tu, basi!
Lakini Socrates alikuwa mtu aliyeamini kile alichokifanya na badala ya kuomba msamaha, hata baada ya kutishiwa kunyongwa, alichokisema ni kwamba: “madhali bado naendelea kuvuta pumzi na bado nina kipawa cha kufikiri, sitaacha kamwe kuitumia na kuieneza falsafa kwa kuwahoji nyinyi na kuutafuta ukweli kwa yeyote yule nimuonaye. Sitaacha tabia yangu hii ya kuhoji hata kama itanibidi kufa mara mia moja”
Kwa watawala, hiki kilikuwa ni kibri na jeuri isiyopimika. Basi wakakasirika ukomo wa hasira zao na hukumu ikatolewa kwa Socrates kunyweshwa kinywaji chenye sumu hadi afe. Socrates akanyongwa na uhai wake ukamalizwa hapo.
Lakini, kama alivyotabiri mwenyewe kabla ya kifo chake, kumuua yeye halikuwa suluhisho. Kwamba yeye hakuwa tatizo lililoikabili jamii ya Waathens ya wakati ule. Tatizo la Waathens lilikuwa ni mfumo mbaya wa kiutawala uliowatukuza wachache na kuwadhalilisha wengi.
Na kama hivyo ndivyo, basi tayari palishakuwa na Socrates wengi tu katika jamii yao, kiasi ya kwamba hata wangeliwaua mia moja wa aina yake, wengine wangeliendelea na kile kile wasichokitaka watawala – kupinga uovu na kuhmiza mema. Kwamba tatizo lilikuwa mfumo na sio uwepo wa watu wanaoupinga mfumo huo.
Sasa SMZ imeshadhamiria, na kwa kweli inaweza kabisa, kuifungia Dira. Wanaifungia kwa kuwa ni kero kwao. Wanaichukulia kuwa inayashambulia maslahi yao na inahatarisha madaraka yao. Lakini Dira sio tatizo la Zanzibar hivi sasa. Tatizo ni mfumo waliojiundia watawala hawa, wa kujitukuza na kujikweza. Kama kuna kitu pekee cha kubadilika na kuondoshwa, basi ni mfumo huo na wala sio Dira.
Kabla ya kushusha ghadhabu na adhabu zake hizo juu ya Dira, SMZ imeitaka ijitetee. Na kujitetea kwenyewe inakokutaka, ni kuifanya Dira iitikie ‘Hewallah Bwana’ – iwe His Master’s Voice, kama zilivyo Sauti ya Tanzania Zanzibar, Zanzibar Leo na Television Zanzibar. Lakini, kama ilivyokuwa kwa Socrates, Dira nayo inajuwa na inakiamini inachokifanya. Kattu haiwezi kuutia ulimi wake puani hata kama ikibidi kufungiwa na kufungwa kabisa kabisa.
Hakuna hata mmoja kati ya wana-Dira aliye tayari kuacha kuidadisi serikali na kuikosoa pale inapostahiki. Ama Dira, kama gazeti, iwepo au isiwepo, Dira, kama muelekeo, tayari umeshapatikana na huo utadumu na kudumu. Itakuwa ni rahisi kwa SMZ kuifungia Dira makaratasi, lakini haiwezi na haithubutu kabisa kuufungia Udira, kama mfumo wa udadisi na ujenzi wa jamii mpya.
U-Socrates umeendelea kudumu kwa karne nyingi hata baada ya watawala wa Athens kumnyonga Socrates mwenyewe. Leo hii, vyuo vyote ulimwenguni vinaisoma na kuitukuza falsafa yake, na hata ameipelekea nchi yake ya Ugiriki kutambuliwa kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kuanzisha mfumo wa kidemokrasia.
Nao Udira utaendelea kuwapo hata baada ya watawala wa SMZ kuinyonga Dira yenyewe. Historia ya nchi hii italikumbuka na kulitukuza gazeti hili kwa siku kadhaa zijazo na ule ujumbe uliokuwa umebebwa nalo, kuna siku utatimia tu. Ni rahisi mno kuliua gazeti, lakini haiwezekani kuikandamiza mission yake!

Chanzo: Gazeti la Dira, Toleo Na. 52, Novemba 21-27, 2003

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.