UCHAMBUZI

Serikali, dini na maslahi ya kisiasa

NAMNA akili zetu zilivyolemazwa kwa siku nyingi, tumefikishwa pahala ambapo tunaogopa hata kuizungumzia nafasi ya dini katika maisha yetu wenyewe. Wenye khatamu za ulimwengu na za nchi wametufanya tuone, na tuamini, kuwa kuihusisha dini na maisha ya kila siku ni ugaidi, au kasoro yake huita siasa kali.

Misamiati hii ya ugaidi na siasa kali katika dini si yetu. Ni fupa tulilotupiwa na mabwana wa Magharibi wanaotaka kutimiza muradi wao. Nasi kwa bahati mbaya na kwa upumbavu wetu, tumo twaligwegwenya.
Na wanaotufanya hasa tuligwegwenye fupa hili ni hawa wakubwa wetu, kwa kuwa linaakisi matakwa yao. Wao hata hawajali linakotokea wala athari yake kwa mjengeko wa kijamii na kitamaduni wa taifa hili.
Haiwaumizi pahala kusikia dini yao ikinasibishwa na misamiati hiyo, maana katika mnasaba huo ndimo yalimo maslahi yao. Ndio maana ukasikia vyombo vyao vya khabari haviigeuzi, illa kuishadidia misamiati hiyo.
Ni ajabu na aibu kumsikia mtangazaji au mwandishi Muislam akiwataja Waislam wenzake kuwa ‘wa siasa kali’ au ‘magaidi’, huku akijuwa fika kuwa hizo ni lebo tu walizobandikwa ndugu zake na maadui wao.
Lakini kwa kufanya hivyo, huwa ameakisi matakwa ya mhariri wake; naye ya mkurugenzi wake; naye ya Waziri wake; naye ya Rais wake; naye ya Bwana wake wa Kimagharibi. Kila mmoja katika mnyororo huo, ana maslahi yake kutoka kwa mwenzake. Na hilo la kutafuta na kulinda maslahi ndilo linalowawezesha wao kutunga sharia za kuifungia dini katika majumba ya ibada tu.
Humo huitawisha na kuinyima nafasi katika mwenendo wa siasa za nchi na hivyo ikakosa nguvu katika ufikiaji wa maamuzi yanayouongoza mustakbali wa taifa. Hata inapotoka humo, dini huja nje mara moja tu kwa kuyatumikia maslahi ya watawala hawa. Huja kuwatilia Fat-ha au kuhudhuria Maulid ya Mfunguo Sita. Kisha, kidogo kidogo, ikarudi ilikotoka. Hivyo ndivyo watawala wanavyocheza karata yao ya kidini!
Kwa hivyo, ukweli ni kwamba watawala hawana ugomvi na dini, ingawa uswahiba baina yao ni wa kimaslahi tu. Kwamba katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu, illa kuna maslahi ya kudumu. Dini ni rafiki mkubwa wa watawala pale inapoyatumikia maslahi yao na adui nambari moja pale inapoyakhatarisha. Na lazima tuseme kuwa watawala wanayapenda mno madaraka yao kiasi ya kwamba yakikhatarishwa, hawachelei lolote. Hata kumkosa Mungu wao!
Hapa ndipo unapoona nusu ukweli katika ile kauli ya Karl Marx kwamba kama zilivyo taasisi nyingine za kidola, kama mahkama na polisi, basi pia dini nayo hutumika kama chombo cha kimabavu kukidhi matakwa ya wakubwa. Kama vile dola inavyotumia polisi na mahkama zake kuwakandamiza raia kwa jina la sharia, ndivyo pia inavyoitumia dini kwa kutanguliza jina la Mungu.
Ndiyo ile picha tunayoipata katika God’s Bits of Wood, ambapo Sembene Ousmane anatuchorea shakhsia ya Alhadji Mabigue, kiongozi wa kidini anayetumia ilimu yake ya kidini kuwasaidia wakoloni wa Kifaransa kuendeleza ukandamizaji na dhulma zao kwa Wasenegali wenzake. Wa Sembene ni mmoja, lakini akina Alhadji Mabigue wako wengi kila mahala. Hata hapa petu wapo.
Bila ya wao, serikali kandamizi haziwezi kudumu na kumudu kuendeleza ukandamizaji wake!
Twende kwenye historia kidogo. Tunaona kuwa takriban harakati zote za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni katika ukanda huu wa pwani ya Afrika ya Mashariki, zilianzia katika jumuiya za kidini. Humo ndimo walimochipukia wapiganaji kwa jina la Mungu. Haikuwa kosa kuwa mtu wa dini na kuwa mtu wa siasa kwa wakati mmoja. Kwamba katika maana zao halisi, dini na siasa hufanya kazi moja – hupinga uovu, husimamisha ustawi mwema wa kijamii na hutayarisha warithi wema wa nchi!
Wakati huo, alipokuwa akiambiwa mkoloni aondoke, lilikuwa ni neno la Mungu linalotumika. Katika kila mkutano wa kisiasa, kwanza palisomwa maneno kutoka vitabu vitukufu, pakateremshwa dua za nguvu. Siku za uchaguzi, palifanywa ibada maalum za kuomba ushindi. Waroma walikwenda Roma na wa Makka wakenda Hijja kutafuta msaada wa ukombozi kwa jina la dini zao na kwa jina la Mungu wao!
Ilipobidi, hata kama kiongozi alikuwa na dini tafauti, aliiingia katika nyumba za ibada za dini nyengine kufuata muradi wake. Kuna kiongozi mmoja wa Mrima aliyekuwa Mkatoliki, lakini akakesha wiki nzima katika makaburi ya Masharifu huko Bagamoyo.
Huko masheikh walimsomea visomo vyote kabla ya kupanda ndege kuelekea Umoja wa Mataifa ambako alitoa hotuba iliyokuja kumpa sifa kubwa baadaye. Tunasikia kuwa siku hiyo Wazungu walimpigia makofi mpaka viganja vikawauma. Matokeo yake ikawa ni kusainiwa kwa uhuru wa mezani wa Tanganyika na pia kumjenga yeye kimataifa.
Kwa hivyo, dini haikupata kukanwa na wanasiasa huko nyuma na, kwa kweli, haijapata kukanwa hadi leo, almuradi tu inayakidhi matashi yao. Dini ilianza kuonekana mbaya baada ya wanasiasa wetu kupata madaraka, yakawalevya na wakafeli. Na kwa kuwa dini, kama ilivyo siasa, ipo kusimamia ustawi mwema wa watu, kupambana na uovu na kuiondosha dhuluma, na kwa kuwa wao waligeuka kuwa hao waovu, mafisadi na madhalimu, basi sasa ikaanza kuwa adui wao nambari moja.
Tukaanza kuharibikiwa na mapema. Wakubwa wakakumbatia mifumo ya siasa za kilimwengu – za Mashariki na Magharibi – ambayo haikuwa na nafasi katika maisha ya watu wa nchi hii walioahidi kuwatumikia. Tamaa ya madaraka, vyeo na mali ikawajenga kiburi na ikawafelisha. Wakakosa kujiamini. Na kwa kudhani kuwa mwisho wao huenda ukawa karibu, wakajaribu kubuni njia za kukandamiza upinzani dhidi yao.
Bila ya shaka, kutokana na historia yake katika pande za kwetu, dini ingelizusha upinzani mkubwa zaidi kuliko taasisi nyingine yoyote ile ya kijamii. Si ndiyo hiyo hiyo iliyowaweka wao madarakani, sasa ingelishindwaje kuwaondoa kama ingelitumika? Kwa hivyo, ikawa wana uchaguzi mmoja tu kati ya mawili haya: aidha ‘waiteke nyara’ dini, waitumilie kwa maslahi yao au waikandamize. Yaani ama iwepo kwa ajili yao, au isiwepo kabisa, lakini wasiiruhusu kuwa ni silaha dhidi yao.
Mwanzo ilikuwa ni vigumu kuifanya dini kuwatumikia wao, kwa kuwa ilikuwa na waumini walio imara. Kwa hivyo wakapambana nayo kwa kusaidiwa na fikra za kimapinduzi za Karl Marx na Vladimir Lenin. Hicho ni kipindi ambacho siasa za nchi hii zilikuwa na masimbisimbi ya Usoshalisti.
Nasema ‘masimbisimbi’ tu, kwa kuwa haukuwa Usoshalisti hasa. Miongoni mwa wale waliochukuwa madaraka baada ya uhuru wa 1963 na Mapinduzi ya 1964 walikuwa wamelishwa masimbisimbi hayo kutoka Cuba, Urusi, Uchina, Ujerumani Mashariki na kwengineko katika kambi ya Warsaw. Walikuwa ni watu walioathiriwa na siasa za Kimashariki ambazo msingi wake ni kukana kuwepo kwa Mungu na dini ili kumkomboa mwanaadamu kifikra.
Hilo lilikuwa ni kosa la mwanzo kwa nafasi ya dini katika dasturi za watawala wetu. Wakafanya timbwa za kukirihisha, kwa mfano, kwa kuichoma moto misahafu na kila maandishi ya Kiarabu, kuwadhalilisha masheikh wakubwa wakubwa na hata kumtukana Mungu hadharani. Mmoja wao aliwahi kusimama na kujigamba kuwa: “Hakuna Mungu na kama yupo, mimi naunyoosha mkono huu, yeye aukunje!”
Lakini kwa kuwa dini hugusa sana hisia za watu, na hivyo siasa za ndani, kuisakama dini kila siku huwagharimu watawala. Watu hawaachi dini zao na kufuata makaripio ya watawala wao, bali huwawacha watawala wao na kufuata dini zao. Kila watawala wanavyokaza kamba dhidi ya dini, ndivyo watu wanavyozidi kuwachukia na kuwapinga.
Sasa ndipo ikatumika hii njia ya pili ya kuiteka nyara dini na kuifanya iyatumikie maslahi ya watawala. Ndipo akina Alhadji Mabigue wanapopata nafasi. Kile kile alichokikataa Karl Marx, ndicho kinachofanyika sasa. Bali zaidi ni kuwa kile kile walichokikataa wao watawala, kwamba dini isichanganywe na siasa, ndicho wanachokifanya. Ni uchezaji wa karata, ambao haujali karata ipi unaicheza, lakini vipi na wapi unaitupa. Huenda garasa likawa na maana na ree likawa si kitu kutokana na namna na pahala ulipolitupa mchezoni!
Kwa hivyo, kimsingi watawala hawapingi dini kuchanganywa na siasa, bali wanachopinga ni dini kuchanganywa na ‘siasa za kuwapinga’ wao. Hawataki kusikia kwamba siasa, kwa maana ya madaraka na utawala, inazungumzwa na ‘watu wa dini’ wasiokubaliana na uendeshaji wa watawala waliopo madarakani.
Wanapinga jina la Mungu lisitumiwe dhidi yao hata kama wanatumia vibaya madaraka yao. Wanaogopa kusikia wanapewa changamoto kutoka kwa umma kwa kauli za Qaalallahu taala au Qaala swallallahu alayhi wasallam.
Hivi sasa, kwao ni vibaya kusema hivyo, ingawa huko nyuma walikuwa ni wao, au baba zao, ndio waliopanda kwenye viriri wakinadi kuwa: “Mungu yu pamoja nasi na kwa nguvu zake tutamshinda dhaalim huyu (mkoloni), maana walaa yazidi lidhaalimiyna illaa khasara!”
Ndio maana, kwa mfano, unakuta wanawakataza watu wasitumie mimbari za misikiti wala madhabahu ya makanisa kuzungumza siasa za kuwapinga wao, lakini hapo hapo wanawataka wawaombee dua na wawapigie kampeni za kuendelea kuwapo madarakani. Sasa kama wasitumie dini, watumie nini kuomba dua au kupiga kampeni hiyo ya kisiasa?
Kwao sheikh au padri akizungumza dhidi ya vyama vya upinzani hawamuoni kuwa anakhatarisha amani ya nchi kwa kuchanganya kwake dini na siasa, lakini akizungumzia dhidi ya chama tawala na serikali zake, siku ya pili atajikuta yuko Kiinua Miguu. Hawataki dini itumike dhidi ya maslahi yao. Ndio vile vile kwamba ama itumike kwa ajili yao, au isitumike kabisa, lakini sio iwe silaha dhidi yao!
Karibuni tulikuwa na mdahalo wa kitaifa ulioandaliwa na TVZ kuadhimisha mwaka mmoja wa Muwafaka wa Kisiasa baina ya CUF na CCM. Bila ya shaka, mdahalo huu ulikuwa wa kisiasa na ulitayarishwa na serikali, lakini pia walialikwa, na kuombwa wazungumze, viongozi wa kidini. Hii inaonesha kuwa dini haikataliwi na watawala. Wanaijuwa nafasi yake, na wanaitumilia.
Mwakilishi wa dini ya Kiislam pale aliyeletwa na serikali kutokea ‘tawi lake la kidini’, yaani Ofisi ya Mufti, akateta kuutetea mshahara wake kwa lugha ile ile ambayo watawala wangelipenda kuisikia: “Muwaffaqa ni jambo swahiih katika Uislam. Hata Mtume wetu swalawatullahi wasalaamuhu ‘alayhi aliwahi kuingia katika muwaffaqa ulioitwa Swulhu ya Hudaibiya. Lakini swulhu hii ilikuja kuvunjika baada ya vijineno vijineno kutoka kwa watu. Sasa na hapa petu kuna baa’dhwi ya wanasiasa, wameanza kutoa vijineno hivi, mara damu itamwagika, mara…”
Ndiyo. Namna hii ndivyo serikali inavyojua kuicheza karata yake katika dini. Hii typical ni kauli ya chama tawala iliyomezeshwa na kutapishwa katika mdomo wa sheikh huyu ili ipate ile tuni ya kidini – ya kiqafuqafu, kiswadiswadi na kighainighaini! Hao wanasiasa anaowakusudia sheikh huyu hapa ni wa CUF.
Chama hiki kimekuwa kikionya kuwa Muwafaka huu usipotekelezwa na hivyo kupelekea Uchaguzi ujao wa 2005 kutokuwa huru na wa haki, kama chaguzi zilizotangulia, basi nchi haitakuwa katika usalama. CCM, na kwa hivyo sheikh huyu aliyetumwa nayo, haitaki kulisikia onyo hilo, maana linawatia khofu kwamba kama wakiendelea na mchezo wao wa udanganyifu katika uchaguzi, watakuja kujikuta pabaya!
Ingelikuwa sheikh huyu kweli anaitumikia dini yake, na dini yake tu si chenginecho, basi cha kukifanya ilikuwa ni kuasa kuwa lazima uchaguzi uwe huru na wa haki ili nchi hii isije kuingia katika machafuko. Angelitumia aya na hadithi kuonesha namna gani ilivyo vibaya kwa wanaadamu kutayarisha mazingira ya uharibifu na ufisadi. Lakini huyu alikuwa anatumiliwa na serikali kufanya kazi ya siasa, na kamwe asingeliweza kumsema vibaya bosi wake.
Kama hayo yakajirudia tena katika semina ya siku moja ya Katiba na Muwafaka iliyofanyika Bwawani tarehe 25 Oktoba, 2003. Sheikh yule yule akasema kuwa nchi hii hapaswi kuachiwa mtu anayehubiri kuwa muwafaka ukivunjwa, nchi haitakalika. Aliowakusudia ni hao hao viongozi wa upinzani.
Serikali haijamuambia kuwa anaingia katika anga si zake, yeye mahala pake ni msikitini tu. Haijafanya hivyo kwa kuwa anachokifanya ndiyo dhima ya dini katika siasa, kwa tafsiri ya serikali. Serikali inamtaka sheikh akemee kauli hiyo inakhatarisha amani ya nchi na hivyo aipigie kampeni CCM iendelee kuwapo madarakani. Na hilo ni sadakta kwa watawala.
Lakini sheikh huyu hakumbuki, wala serikali haitaki hilo likumbushwe, kuwa kauli ya kuwadharau na kuwakebehi wananchi zinazotolewa na kiongozi mkubwa wa nchi, kwa mfano, kama kuwaita Wapemba wakosefu wa fadhila au kuwaambia watu wanaosema kuwa hali ya maisha ni ngumu wahame nchi, zinaweza kuchochea machafuko katika nchi. Sheikh hana aya wala hadithi ya kulikemea hilo.
Wala sheikh huyu hakumbuki kisa hata kimoja katika dini kinachowaonya wale watu wanaopa kuwa madhali nchi hii imepatikana kwa Mapinduzi ya kumwaga damu, haiwezi kutolewa kwa vikaratasi vya kura. Katika sira alizozisoma hakukumbana kabisa na hekaya inayowasimulia viongozi walioangamizwa kwa sababu ya kudhulumu haki za raia.
Kwa hivyo, haihitaji kuwa na akili nyingi sana kujuwa kuwa watawala wetu ni ndumilakuwili panapohusika nafasi ya dini katika siasa. Kwao wao, dini huwa imetumika vyema ikiwa inawasifu wao na kuwakashifu wapinzani wao wa kisiasa, na inakuwa imetumiwa vibaya kama itakuwa kinyume chake.
Dini, kwa hali hiyo, imekuwa ni chombo chao ambacho kinakuwa tayari kuwatumikia kadiri wapendavyo, na sio wao kukitumikia kama itakiwavyo. Unafiki ulioje!

Dira, Na. 48, Oktoba 31-Novemba 6, 2003

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.