UCHAMBUZI

Kuwaambia wakubwa ‘Hapana’ kuna gharama zake

SIKUSUDII hata kidogo kuifanya makala hii kuwa hati ya kihistoria kwa kuchelea kuwachosha wasomaji wangu. Lakini nina lengo la kukizungumzia kisibu kinachoelekea kumsibu Sheikh Ali Nabwa, kwa upande mmoja, na Dira, kwa upande mwengine, katika muktadha wa yale yawapatayo wanaharakati walio na fikra tafauti na watawala wao. Kwa ajili hiyo, sitakuwa na budi illa kudokowa hapa na pale katika matukio yaliyopita huko nyuma ili kufikia lengo.

Kwamba ulimwenguni kote, na katika zama zote, jamii inapokuwa chini ya utawala ulioziba masikio, na macho na nyoyo, watawala hupenda waachiwe tu wafanye watakavyo. Huwa wamejirithisha wenyewe nchi na raia wake. Na kwa hili hawataki muhali, masahihisho, wala mabadiliko.

Anapotokea mtu kuwasahihisha, wao humchukulia kuwa ni adui wao nambari moja, na hivyo hujihalalishia kumuadhibu kwa namna yoyote waionayo inafaa. Yamkumbayo sasa Nabwa, na kwa ujumla Dira, ni miongoni mwa mambo yawezayo kuzungumzwa katika muktadha huu.
Kwangu mimi, ukosoaji nauona kuwa ni aina fulani ya harakati za kuleta mabadiliko na maendeleo, na hivyo naihisabu Dira na Nabwa katika kundi la wanaharakati na wanamaendeleo hao. Si jibu la haki, ingawa ndiyo kawaida ya watawala, kuwageuza wanaharakati hawa kuwa wahanga wa utamaduni huo mviya wa kutokutaka mawazo tafauti.

Ilikuwa stahili ya watawala hawa kubadilika kwa mujibu wa matakwa ya umma. Hapa matakwa ya umma yamewasilishwa na wanaharakati hawa. Wanamabadiliko si maadui kwa utawala ukubalio kunyumbuka kwa mujibu wa mahitaji ya wakati. Badala yake, wao ndio muhimili mkuu wa usaidizi.

Dhambi moja kubwa ya watawala wetu ni kuamini kuwa siku zote msaidizi wao ni yule tu anayewaitikia Ndiyo Mzee, na kwamba kila anayewaambia Hapana ni adui wao. Dhambi hii ni kubwa na gharama zake ni ghali mno kulipika. Ni dhambi itokanayo na kutawala kwa mkono wa chuma!

Kuwatawala watu kwa mkono wa chuma kuna matokeo mabaya, lakini hakuvizi khulka ya wanaadamu kupinga walionalo silo. Na ndio maana, kote ulimwenguni ambako tawala za aina hii zimepata kuweko, upinzani dhidi yake huzidi kukuwa na kukuwa kila kukicha, hata kama kila mbinu ya kuudidimiza hutumika kila saa na kila dakika.

Wakosoaji wa watawala wakizuiliwa njia hii ya kuwakosowa, huzumbuwa njia nyengine. Alimradi kila watawala wakaapo, hawawezi kustaaladhi nafsi zao, maana macho yote ya umma huwakodolea wao na vinywa vyao huhanikiza sauti: “Hivi sivyo, hilo silo!”

Mwangwi wa sauti hizi ni vitu vinavyoudhi sana mbele ya hadhara ya mtawala, lakini si vitu vinavyoweza kuepukika ikiwa mtawala huyo hakubali mwito wa mabadiliko. Kila mtawala akizidi kuwa muimla, ndipo anapozidi kuzalisha sauti zinazomsuta na macho yanayomkodolea. Hizi ni sauti na macho ya watu waliojitolea kumuambia mtawala wao makosefu yake na kumuonesha njia.

Lakini, utawala wa mkono wa chuma huambatana na ujigambi na majivuno. Mtawala hupandwa na kichaa anapoambiwa kuwa ana makosefu fulani na fulani. Maana, kwa kila hali, huwa kilevi cha madaraka kishamlevya na zile andasa zake humdanganya kwamba yeye yu Mr. Perfect – hawezi kuwa na mapungufu yoyote yale.

Basi hapo hucharukwa na kuanza kumuadhibu kila amuhojiye, haidhuru hoja hiyo iwe makini kiasi gani. Na kila anavyoadhibu, huona bado – na huwa bado kweli! Huadhibu kwa ulimi wake, kwa mikono yake, kwa virungu, kwa jela, hata kwa risasi na kitanzi. Kwa kwa kila kitu.
Na bado wanaharakati huendelea tu. Angalia msuguano baina ya Bi Kirembwe na Mtolewa katika tamthilia ya Kivuli Kinaishi iliyoandikwa na Dk. Said Ahmed Mohammed uone anguko la kishindo la utawala ulioziba milango yake yote ya fahamu.

Dunia imejaa mifano ya visa na mikasa kama hii. Ni juu yetu kufundishika, ikiwa kweli tu watu wa kuzingatia kutokana na maandiko. Twapaswa kufundishika, maana vyenginevyo tutakuwa miongoni mwa wale waliotajwa kuwa na macho lakini wakawa hawaoni, masikio lakini hawasikii na nyoyo lakini hawafahamu. Ubaya ulioje kuwa miongoni mwao!

Mfano mmoja maarufu ulimwenguni ni ule wa Socrates, mmoja kati ya wanaharakati wa kale. Yaliyompata, yana tafauti ndogo sana na haya yaikumbayo Dira na Nabwa hivi sasa. Pengine tafauti ni kuwa Socrates alimaliziwa uhai wake kwa kunyweshwa kinywaji cha sumu kwa amri ya mahkama, Nabwa na Dira watamaliziwa uhai wao kwa staili nyengine.

Vyenginevyo, kilichomchongea Socrates ni uthubutu wake wa kuwapa changamoto watukufu na watendaji wa serikali ya Athens juu ya uadilifu na ilimu yao. Dira na Nabwa wanachongewa ni hicho hicho.

Tunasoma katika vitabu kwamba Socrates aliwaandama watawala wa Athens kwa kutumia mbinu ya udadisi na uchambuzi wa mambo yaliyoonekana ya kawaida tu, lakini muhimu sana kwa maisha ya watu. Hayo ni kama vile imani juu ya Mungu, uzuri wa matendo, uadilifu, ilimu, maumbile na kadhalika. Mbinu hii iliuvuta umma wa watu, wengi wao wakiwa vijana, ambao walimchukulia kuwa kigezo chao.

Hapa petu hivi sasa, Dira imekuwa ikiwavutia wengi kwa mbinu hiyo hiyo ya kudadisi na kuchambua masuala kama haya ya kawaida lakini muhimu. Hayo ni kama vile muungano, bandari, mafuta na haki za binaadamu. Kupitia uchambuzi na udadisi huu, huwa inatowa changamoto kwa watawala na kuuhoji udhaifu wao. Hilo hawalipendi hata kidogo.

Katika Phaedo, kitabu kilichoandikwa na Plato, aliyekuwa mwanafunzi wa Socrates, tunamsikia mwenyewe akijitetea mahkamani: “Wao (watawala) hukereka mno na hili, na si kuwa wanakerwa na udhaifu wao walionao, bali kwa kuwa udhaifu wao umedhihirishwa na kubainika, na basi huishia kunilaumu na kunichukia mimi.”

Khatima ya kukereka huku kwa wakubwa ikawa ni kumtoa muhanga Socrates, ambaye tunaweza kumuita kuwa ni aalimu mkubwa wa wakati wake na mwanaharakati jasiri. Alishitakiwa kwa makosa mawili. Kwanza ni kusambaza mafundisho ya kumkana Mungu. La pili ni kuwachochea vijana kuipinga serikali yao. Makosa haya mawili yalimuhalalishia adhabu ya kifo.

Naye, licha ya kupewa fursa ya kujitetea ili aisalimishe roho yake na mauti, kwa kuahidi kuwa angeliiwacha kabisa kazi hii, mwanaharakati huyu alikataa kwa kusema: “Waheshimiwa waungwana, licha ya kuwa mimi ni mtumishi niliyejitolea kwenu, lakini nina jukumu la kuonesha utiifu wangu wa kiwango cha juu zaidi kwa Mungu wangu na sio kwenu nyinyi; na madhali ninaendelea kuvuta upumzi huu na kuendelea kubarikiwa vipawa hivi nilivyonavyo, basi kamwe sitaacha kuifanya kazi hii ya kuufunua ukweli kwa kila mtu nimkutaye…. Na sitaliacha hili, hata kama itabidi nife mara mia moja!”

Maskini, Socrates akafa akiamini kuwa ni bora kuishi siku moja kama mwanaadamu, kuliko kuishi miaka alfu kama dude, maana ‘the unexamined life is not worth living’ maisha yasiyotathminiwa, hayana thamani kuyaishi. Maisha yake yalizimwa pale, lakini ukweli ni kuwa ameendelea kutukuzwa hadi leo hii ulimwenguni.

Hiyo ndiyo gharama ya kuwa mwanaharakati, na ndilo lipo la kuwaambia ‘hapana’ watawala wasiopenda kubadilika. Ndio maana nikasema kuwa ya Nabwa hayashangazi sana, hayo ni madogo tu. Salama kwamba roho yake ingalimo na kwamba mpaka leo bado yuko nje ya makuta manene, maana wanaharakati wengine wa aina yake huwakuta makubwa kushinda hayo. Na panapohusika Dira, wengi wetu husema: “Nabwa tayari, afuatiaye ni nani?”

Wala watawala wa aina hii hawahitaji sababu kubwa ili wapate kumvamia raia wake wanayemuhisi kuwa ni hatari kwao. Vile kuwa tafauti na wao tu, ni sababu inayotosha kabisa kukupambanisha na ghadhabu ya dola. Kwamba kama unahitaji kuishi salama usalimini chini ya tawala kama hizi, basi ni kukubali kuwa kama vile wakutakavyo wao uwe.

Wanakutaka uitikie wimbo wauimbao, na ucheze ngoma waipigayo. Na katika kufanya hivyo, usioneshe tafauti yoyote ile – hata ile ya kuuimba wimbo huo huo kwa ghuna nzuri zaidi au kunengua kwa minenguo mororo zaidi kuliko wao. Kwao, hilo litahesabika kuwa ni tendo la kiadui.

Yaliwahi kutokezea kule Somalia, wakati wa utawala wa Siad Barre, kama inavyosimuliwa na mmoja wa wahanga wa utawala ule, Dk. Adan Yussuf Abokor. Hayo yamo katika insha yake Why We Were Arrested iliyochapishwa katika kitabu kiitwacho The Cost of the Dictatorship, (Lilian Barber Press, Inc., 1995) cha Jama Mohammed Ghalib.

Dk. Abokor anasema kuwa kosa kubwa lililosababisha yeye na wenzake wakamatwe na kufungwa jela zaidi ya miaka sita, wakipewa mateso makali ya kimwili na kiakili, lilikuwa ni kujaribu kuleta maendeleo katika mji wa kwao wa Hargeisa. Mji huu ulikuwa umetupwa miaka nenda-rudi na utawala wa kidikteta wa Barre.

Yeye binafsi, akiwa kama daktari kwa taaluma na fani, alichangia sana kuifufua hospitali kuu ya Hargeisa. Hii, licha ya kuwa kwake hospitali kuu na iliyotegemewa na watu wa eneo hilo, serikali ilikuwa imeikana na kuinyima khidma yoyote ile.

Alipopelekwa kuwa mkurugenzi wa hospitali hiyo katika mwaka 1980, alikuta kila kitu kikiwa kimeshasambaratika, ama kwa kufa au kuharibika. Maabara ilikuwa inafanya kazi kwa tabu sana kutokana na ukosefu wa vifaa na kemikali. Benki ya damu, idara za wagonjwa wa dharura na wagonjwa wa nje zilikuwa zimefungwa. Mashine ya X-ray ilikuwa haifanyi kazi kwa miaka miwili sasa kutokana na ukosefu wa filamu na pia uchakavu wa baadhi ya vifaa vyake. Makaro yalikuwa yameziba kabisa kabisa kiasi ya kwamba wagonjwa walilazimika kuvizia usiku uingie wakamalize haja zao nje.

Alimradi hali ilikuwa mbaya sana kiasi ya kwamba ili wagonjwa wapatiwe kitanda, walilazimika kuja na magodoro yao wenyewe, mashuka ya vitandani, mito na foronya zake. Mtu alipaswa kununuwa dawa zake na hata chakula chake mwenyewe. Huduma pekee, ambayo hospitali hiyo iliitowa, ilikuwa ni wale madaktari mafidhuli wasio hisia hata chembe kwa kuchanganyikiwa na maisha.

Dokta Abokor, akiwa na mawazo ya kimaendeleo na kimabadiliko, akaamua kushirikiana na wenzake kuleta matumaini mapya katika Hargeisa. Yeye na wenzake wakaamuwa kuanzisha kampeni ya makusudi ya kuwasaidia watu wa eneo hili. Na kwa kuwa tokea hapo watu hawakuwa wavivu, walishirikiana vizuri kujenga ustawi wa Hargeisa mpya.

Wakaamuwa kuwashajiisha wasomi wazawa, ambao walikuwa sehemu mbali mbali za ulimwengu, kurudi kwao kuja kuwasaidia watu wao. Mwito huu ukaitikiwa kwa kishindo. Ndani ya mwaka huu mmoja tu, wasomi wa Kisomali wa kila fani wakawa wameshamiminika Hargeisa. Miongoni mwao walikuwa walimu, madaktari, wahandisi, wachumi, wafanyabiashara na wengi wengineo. Kila mmoja akajitolea kuisaidia Hargeisa kwa uwanja wake.

Alimradi ndani ya kipindi kile kifupi, Hargeisa ikaanza kunawiri na kupendeza. Wahisani nao, kwa kuona kuwa watu wa hapa walikuwa na moyo wa kujisaidia wenyewe, wakaamuwa kuwaletea misaada yao moja kwa moja. Kundi la madaktari wa Kijerumani likaleta vitanda vipya, mashuka, vyandarua, gari la wagonjwa, madawa na vifaa vyengine vya hospitali.

Hata zile dawa, ambazo zilikuwa hazipatikani kwa raia wa Somalia ila kwa wale waliokuwa na jamaa zao katika nchi za Kiarabu, sasa zikawa zinapatikana hapa hapa. Wagonjwa wakawa wanatoka miji ya jirani kufuatia huduma za matibabu hapa. Kuna kujitolea na kuwa mzalendo kama huku?

Kumbe jambo hili lilikuwa linawakera sana wakubwa wa Mogadishu. Waliliona kuwa linahatarisha utukufu na ulwa wao. Waliona kuwa linawadhalilisha kwa kuonekana kuwa wao hawafai kitu. Kwamba jambo lililowashinda watawala kwa miaka 34, sasa lilikuwa limefanywa na raia kwa mwaka mmoja tu.

Kwao, hilo lilikuwa tusi. Noemba 2, 1981 mtu wa kwanza miongoni mwa wale wasomi waliojitolea, akaanza kukamatwa. Novemba 19, ikawa ni zamu ya Dokta Abokor mwenyewe kuwekwa kizuizini. Tena mkufu wa mahabusu ukaendelea hadi wakafikia 29. Wote watu muhimu katika jamii. Wote wanaharakati waliojaribu kuleta mabadiliko kwao.

Mashitaka waliyoshitakiwa ni kuunda kundi la kuipinga serikali na kupanga njama za kumpindua Siad Barre. Miongoni mwao wakahukumiwa vifungo vya maisha, kama Ahmed Mohammed Yussuf, aliyekuwa mwalimu bingwa wa Fizikia na Mohammed Barood Ali, aliyekuwa mkemia wa viwanda. Wengine 22 wakapewa kifungo cha miaka 30 kulla mmoja. Na adhabu nyengine za vifungo tafauti kwa watu kadhaa wa kadhaa.

Hilo ndilo lililokuwa lipo la wanaharakati hawa, ambao hakuna msamiati wowote unaotosha kuzitaja sifa zao kwa ukamilifu. Watu hawa baadae waliachiwa, wakiwa wameshatumikia zaidi ya miaka sita jela. Na hata huko kuachiwa kwao hakukuwa bure. Ilikuwa ni baada ya shinikizo la vijana na wanafunzi, ambao walikuwa wakiandamana kila siku ya Februari 20 kuwakumbuka wanaharakati hawa na kupinga kukamatwa kwao. Maandamano haya yalimalizikia kwa zaidi ya wanafuzi hamsini kuuawa kwa kumiminiwa risasi na mgambo wa Siad Barre.

Nilitangulia tokea mwanzo kusema kuwa sina nia ya kuifaya makala hii kuwa kipande cha hati ya kihistoria. Lengo langu hasa katika kutumia mifano hii hai, iliyowahi kutokea katika sehemu mbali mbali ulimwenguni, ni kuonesha kwa kiasi gani ilivyo kazi ngumu kuwa mwanaharakati.

Mifano hii ni michache tu, panapohusika idadi ya mikasa na visa kama hivi. Ni mingi tu iliyokwishatokezea duniani. Hata hapa Zanzibar wanaharakati wamekumbwa na khabari nzito nzito, ambazo sikukusudia hasa kuzitaja leo hii. Sina pumzi za kuyazungumzia ya Kassim Hanga, Abdul Aziz Twala, Mdungi Ussi, Othman Sharif, Abdirahman Babu na makumi kwa mamia ya wengine.

Kuna waolipotea kiajabuajabu. Kuna waliopaswa kuihama nchi yao. Kuna waliodhalilishwa na kuteswa kwa mateso mabaya mabaya. Na wote hawa waliteseka kwa kusema kwao hivi sivyo, hili silo – kwa kuhojihoji kwao kusikokwisha. Lakini dunia shimo la sahau. Leo hii, wa wapi wateswa na watesaji? In’da Rabbihim yansiluun! Wameshawasili mbele ya Mola wao, naye ndiye Mbora wa walipaji na Mkali wa kuadhibu!

Basi yampatayo Nabwa na yaisibuyo Dira hii leo, ni katika kawaida za harakati. Na nadhani wengi wetu, katika sisi watawaliwa, tunalijuwa hilo. Sote tunajuwa kuwa kuwakosoa wakubwa kuna khatari zake nyingi sana. Tunajuwa kuwa watawala wana nguvu za kila aina na wanaweza kuzitumia nguvu hizo dhidi yetu, pindi wakitaka.

Tunajuwa kuwa wanaweza kutumia nguvu zao kutubambikia mashtaka ya uhalifu au hata uhaini. Wanaweza kuyafanya maisha yetu yawe kitendawili. Bali wanaweza hata kuwageuza wake zetu kuwa vizuka na wenetu kuwa mayatima. Wanaweza hawa, hakuna linalowashinda, pindi wakiamua.

Lakini kadiri tunavyoyajuwa hayo, ndivyo tunavyozidi kupata ujasiri wa kuzikosoa serikali kandamizi. Kwa maana nyengine ni kuwa kujuwa kwetu huko, hakupunguzi chochote katika dhamira yetu ya kurekebisha hali mbovu iliyopo.

Sisi raia tumeshajifunza na tumeshaielewa. Iliyokuwa haijajifunza wala kuelewa ni serikali yetu. Bado haijajifunza kuwa hakuna utawala wowote ulimwenguni uliodumu katika madaraka yake kwa kutumia mbinu hizi chafu.

Pengine inaiwia vigumu kuamini, lakini ni historia hii hii ndiyo inayotudihirishia kuwa kuinamako ndiko kuinukako, na kuinukako kukainama. Lini watawala wetu watakuwa tayari kukabiliana na ukweli huu?

Dira, Na. 18, Aprili 4-10, 2003

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.