MOJA ya njia zetu za kufundishiana, sisi Waswahili, ni kutumia visasili. Visasili ni matukio ya kibunifu na ya kizamani yanayooanishwa na sababu au asili ya jambo, kitu au hali Fulani. Tuna, kwa mfano, visasili vinavyozungumzia kwa nini ikawa vinyama kama paka na panya au tumbili na mbwa havipatani, au kwa nini kuna vinyama vyenye maumbile haya au khulka zile, kama vile sungura kuwa na masikio marefu, ndovu kuwa mpole, na au mbuzi kuwa na papara.
Kitu cha kukifahamu ni kuwa visasili si mikasa inayosimuliwa kwa kufurahisha barza tu, bali kusudio lake hasa ni kupeleka ujumbe au kutowa funzo fulani kwa mlengwa. Kwamba hao akina mbwa na tumbili, paka na panya, au sungura na fisi watajwao humu, huwa hawakusudiwi wao hasa, bali ni wanaadamu wenye sifa kama zao (hao wanyama). Maana kwenye maisha halisi wako wanaadamu wenye papara kama za mbuzi, uroho kama wa fisi au mahasimu kama mbwa na tumbili!
Makala hii inatumia kisasili cha nzi, kwa mintarafu ya kwamba ndicho kilichotumiwa na Wapemba mara hii kukipa funzo Chama cha Mapinduzi (CCM) na akina James Mbatia katika uchaguzi mdogo uliofanyika Pemba hivi karibuni.
Hebu mchunguwe nzi pale akituwa. Utamuona amesimamia miguu minne badala ya ile sita aliyonayo. Halafu hapo hapo utamuona anaichezesha kwa haraka haraka ile miguu yake miwili ya mbele kana kwamba anaipeleka mbele akiirudisha nyuma kwa kasi ya ajabu. Halafu tena husimamia ile miguu minne ya mbele na kuichezesha miguu yake miwili ya nyuma kwa namna ile ile ya mwanzo. Wazee wakatwambia kuwa, vile nzi akiichezesha miguu yake ya mbele, huwa anasema: “Ukiujuwa huu…” na vile akiichezesha ile ya nyuma, huwa anamalizia: “…huu huwiji!” Hiyo ndiyo asili ya Waswahili kuwa na msemo ukiujuwa huu, huu huwiji.
Hivyo ndivyo Wapemba walivyoiambia CCM na akina James Mbatia wao, kwamba wakiujuwa wa kuweka pingamizi kisheria, hawaujuwi wa kuziondoa pingamizi hizo kidemokrasia. Hawajuwi kuwa hapa petu pana mpishano mkubwa baina ya matakwa ya kisheria na matakwa ya kidemokrasia. Ndio maana, akina Mbatia walipofanikiwa kuitumia mahakama kuwazuia wagombea wa Chama cha Wananchi (CUF) wasigombee nafasi zao za uwakilishi kwa kudhani kuwa nafasi hizo watazichukuwa wao kirahisi, Wapemba wakatumia demokrasia kuonesha kwamba hao waliong’olewa, bado wanabakia kuwa chaguo lao.
Matokeo yake ni kuwa, baada ya yote, washindi wa kisiasa na kidemokrasia wamekuwa ni wale wale ambao tokea alfajiri umma wa Pemba ulishataka wawe, yaani CUF, na kwa akina Mbatia kukabakia aibu na tahayuri tu. Baada ya gharama zote walizotumia, wakati wote walioutupa na jitihada yote waliyoipitisha, wamerudi nyuso chini, huku kila mmoja akiwa amepoteza kwa kiasi chake.
CCM walikwenda Pemba mikono mitupu lakini wakiwa na matumaini tele. Watunga mikakati wao walikuwa wamewadanganya kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata majimbo kwa kuwa kunaonekana hali ya watu wa huko kuichoka CUF. Kisiasa matumaini yao hayakutimia, ingawa kisheria wamerudi na viti sita vya uwakilishi. (Nimeiandika hii kisheria kwa italiki, kwa kuwa haijulikani hadi sasa ikiwa kweli ilikuwa ni kisheria hasa au ni kimagube. Tusubiri tuone, suala hili liko mahakamani!)
Lakini kwa akina Mbatia, mambo yamekuwa mabaya zaidi. Hawa walikwenda Pemba na mengi lakini wamerudi watupu wakiwa amepoteza kila kitu. Hapa tusizungumzie pesa na wakati kama vitu vilivyopotezwa, bali tuzungumzie heshima zao katika jukwaa la siasa za upinzani. Kati ya vyote walivyovipoteza, hili litawagharimu sana na watahitaji siku nyingi mno kuweza kulirudisha tena, ikiwa wataweza. Waliyoyafanya Pemba yamewafanya waonekane si mpinzani wa kweli bali ni vibaraka tu wa CCM. Hivi sasa ukiwatia katika mnada wa kisiasa, inaelekea thamani yao haitafika tena hata shilingi kumi ya Tanzania.
Kuongeza msumari mmoto juu ya donda bichi, mara hii Wapemba wakakoleza makarama yao ya dhihaka katika siasa kwa kuja na hicho kilichoitwa maruhani, ambacho kimegeuza mwelekeo mzima wa nadharia ya siasa za uchaguzi. Katika nadharia hizo, kilichokuwa maarufu katika hali kama hii ambapo mgombea anayependwa na watu amezuiwa kugombea kwa sababu yoyote ile, ni wafuasi wa mgombea huyo kutokujitokeza kabisa kupiga kura. Walichokifanya Wapemba, badala yake, ni kujitokeza kwa wingi zaidi kwenda kupiga kura za ‘kuharibu kura’. Wanasayansi wa siasa wa siku zijazo watalazimika kuliweka hili katika somo lao.
Huu ulikuwa ni kama mzaha, moja ya tabia isiyokufa Pemba. Wasiowajuwa Wapemba kwa tabia yao hii, kila siku wanawaelewa vibaya. Hivi sasa tayari waandishi na wanasiasa wa Bara wameshaanza kulijengea hoja hasi tukio hili. Wameifanya kuwa sababu ya kuwakosowa Wapemba kuwa wanatumia vitimbi vya kishirikina katika siasa na wanauuwa utamaduni wa siasa za kipinzani.
Binafsi napingana na maoni hayo. Badala yake, kwa hishima kabisa, nawachukulia Wapemba kuwa ndio wajenzi wa siasa za upinzani na hata siku moja hawajapata kuusaliti, sambe kuuwa, utamaduni wa siasa hizi. Kinachofanywa na wao, na ambacho kinawashinda hao wanaolalama hivi, ni kumudu kuioanisha siasa na maisha yao halisi.
Maisha mazima ya Wapemba yamekuwa ni mapambano ya ukombozi na hivyo ndivyo zilivyo siasa zao. Kwa Pemba, kamwe siasa haitengwi na maisha ya kawaida ya mtu. Wapemba hawafanyi siasa kuwa ni biashara kama wafanyavyo akina Mbatia. Kwao, siasa ni njia ya kujikombowa kutokana na idhilali ya karne na dahari.
Ndio maana anapotokea mtu kuingilia kati kuyachafuwa mapambano yao, wanamchukulia kuwa huyo ni mtu mbaya sana kwao kama alivyo jini wa Subiani. Subiani ni jini adui kwa mwanaadamu, jini mkorofi na mnyonya damu. Mtu akikumbwa na Subiani na asipowahiwa, haponi. Huadhibika kwa swenene za maradhi na hatimaye akafa huku akiwa hana tone la damu mwilini. Hiyo ndiyo kazi ya Subiani.
Lakini Subiani ana mdawa wake, anaitwa Ruhani. Huyu naye ni jini lakini yeye si mkorofi wala si hasidi kwa mwanaadamu, bali ni rafiki na msaidizi wake. Ruhani akigunduwa kuwa kuna mwanaadamu fulani kakumbwa na Subiani, hangojei kuitwa kwenda kutoa msaada. Mbio huenda na kumkabili Subiani yule, akampapatuwa hadi akapapatuka. Hii ndio sababu kila siku mwanaadamu hujikurubisha kwa Ruhani na humkimbia Subiani.
Hili ndilo lililofanyika mara hii Pemba. Mule Wapemba walimobaini kuwa tayari masubiani wanamutambalia, waliwaweka maruhani wao. Walikuwa wameshanusa, kwa uhakika kabisa, harufu ya kuwepo kichafuzi kilichokuja kuwachafulia mapambano yao ya ukombozi. Basi wakaamua kuwakilisha upinzani wao dhidi ya kichafuzi hicho kupitia mizaha, maana, kama nilivyotangulia kusema, inda na tashtiti ni sehemu ya utamaduni wao.
Kwa Wapemba hii ni kanuni ya kawaida katika hisabati ya maisha: siasa, masikhara na ukweli. Tumia masikhara, ufanye siasa uibuwe ukweli. Kama huwajuwi, unaweza kushindwa kuwavumilia hata saa moja, lakini kama unawajuwa, utaweza kuishi nao milele hata kama munatafautiana kimtazamo.
Kwa hivyo, badala ya wanasiasa na waandishi wa Bara kukurupuka na kuwahukumu Wapemba kuwa ni watu hatari kwa Muungano, ni tishio kwa demokrasia au ni washirikina, ilikuwa kwanza waisome na kuijuwa hali ya Pemba, utamaduni na maisha ya Wapemba. Sio kubwabwaja tu kwa kutumia vigezo vyao vya Kidodoma au Kidarisalama.
Kwa Wapemba, utani na kejeli ni mambo ya kawaida katika maisha. Watu huko hutaniana wakati wa uzazi na harusi lakini pia hufanyiana hivyo wakati wa matanga. Ni jambo la kawaida sana kumuona mtu katika mkusanyiko wa matanga, wakati wengine wanalia, yeye amejivalisha kanzu na koti la marehemu anamuigiza mwendo wake au sauti yake. Si kwa kuwa haumizwi na msiba huo, lakini utani huu ni katika kuyapa maana maisha yao na kuzifunika huzuni zao.
Wapemba hutaniana popote wawapo na wakati wowote uwao. Wala si kwamba watu hawa hawako makini katika mambo yao, (kwa mfano, dhihaka ya maruhani haimaanishi kuwa hawakuumizwa na kupokwa viti vile sita na CCM kwa msaada wa Mbatia). Hapana. Lakini hawa ni watu wanaojuwa kuumia kwa staili yao.
Binafsi naamini kuwa jambo hili lina sababu zake kihistoria na kijamii. Na moja ya sababu hizo ni vile maisha ya huko kufanywa magumu kwa miaka nenda-rudi sasa, ambapo Wapemba wamekuwa wakisiginishwa katika ufukara uliokwishatitia. Wamekuwa wakijaribu kupambana na msigino huo, lakini mapambano haya hayakuwa rahisi kiasi hicho na yamechukuwa muda mrefu. Kuyahuisha mapambano haya, ndipo utani na maskhara yakaibuka kama pumbazo lao. Kwa hivyo, shida za maisha kule, ndizo zilizowajenga watu kuwa na kejeli zile na utani mwingi.
Pengine, katika hali ya kawaida, mtu aliyefunikwa na shida kama hizi na kwa miaka yote hii, hutandwa na hasira, chuki na kisasi: kila saa kavimba, kauchuna, hacheki, hakenui. Lakini hivyo sivyo walivyo Wapemba. Miaka mingi ya kuwa kwao katika shida, imewajusurisha kucheka hata pale wengine wanapolia, kutania hata pale wengine wanapomaka, na, zaidi ya hayo, imewapa uthubutu wa hata kujikebehi wenyewe, kitu ambacho wengine wengi hawakiwezi!
Na hapa nitowe mmoja kati ya mifano mingi niikumbukayo. Nakumbuka baada ya uchaguzi mkuu wa 1995, hali ya maisha kule Pemba iliongezeka ugumu. Kama ilivyokuwa mawazo ya waangalizi wengi, Wapemba pia waliamini kuwa Tume ya Uchaguzi ya wakati huo chini ya uenyekiti wa Zubeir Juma iliiba kura za mgombea urais wa CUF na kumpa wa CCM.
Kwa Wapemba, vile kuzidi hali kuwa ngumu wakati huo, kulikuwa kunahusiana moja kwa moja na dhulma waliyofanyiwa na Tume hii. Pamoja na hilo, kipindi hicho mvua zilikuwa zimekosekana kwa kipindi kirefu, jambo ambalo lilipelekea kupungua sana kwa mazao ya chakula kama vile muhogo, viazi na mashelisheli, ambayo ndiyo yanayowasitiri watu huko.
Hata hivyo, kukawa na neema kubwa ya maembe. Embe kikawa ndicho chakula kikuu, si kwa kupendwa lakini kwa kuwa ndicho kilichopatikana kwa urahisi na kwa wingi. Likawa linaliwa kwa kila staili, ama kwa kupikwa kitenei au kwa kuliwa bivu. Kawaida kitenei ni chakula kiliwacho kwa tunu tu, lakini kwa wakati huu hapakuwa na jinsi ila kukila kwa kujisitiri hasa, na sio tunu tena!
Basi, licha ya kuwa katika hali ngumu kama hiyo, huku wakiamini kuwa wamefikishwa hapo makusudi, bado Wapemba hawakuacha shtihizai zao. Unajuwa walizuka na misamiati gani? Embe lilikuwa linaitwa “Tume” wakimaanisha Tume ya Uchaguzi ambayo waliamini kuwa iliwapokonya ushindi wao na kuipa CCM. Njaa wakaiita “Komando” wakimaanisha Dokta Salmin ambaye waliamini kuwa ndiye sababu ya dhiki yote ile. Sembe waliliita Mkapa, pengine kwa kuwa ni chakula cha Bara, na dagaa likaitwa observers (wachunguzi wa uchaguzi).
Kipindi hicho pia ilikuwa ni wakati ambapo pigapiga ilitanda huko Pemba. Basi askari waliokuja usiku kuwapiga watu majumbani mwao wakaitwa “Melody” jina la mkato la kikundi cha Taarab cha East African Melody. Waliinasibisha pigapiga ile na kikundi hiki kwa sababu mbili: kwanza kwa kuwa upigaji wenyewe ulikuwa ukitokea usiku kama maonyesho ya kikundi hiki yanavyofanyika, lakini pili ni kuwa waliamini kikundi hiki kilichangia kuwachongea wao Wapemba kwa serikali kwa nyimbo zake kama ile Wasio haya wana mji wao.
Wakati huo, lilikuwa jambo la kawaida kumkuta mzee wa Kipemba ameingia dukani na kumuambia muuza duka: “Hebu yakhe mpa kilo moja ya Nkapa!” Wala si kwa kununa bali kwa tashtiti na inda. Au ungeliweza kumsikia mama akimuambia mwenzake: “Aa, n’kwambie mwenzangu, leo Komandoo kan’jaa nyumba tele!” Ukisikia hivyo, ndio watu wamelala na njaa hapo.
Labda unaweza kufikiria inakuwaje watu wako katika hali ngumu kama hiyo na bado wanadiriki kujenga kejeli na tashititi za namna hiyo. Ndiyo, kwamba hiyo ni sehemu ya maisha yao, ambayo yana ugumu usiomithilika. Utani ni kibwagizo cha ugumu wa maisha yao, ni bega la kubwagia zigo lao la matatizo ya maisha. Hutania na kukejeli ili kujirafariji na kujipumbaza na dhiki iwaandamayo kila uchao. Lakini pia hutania kuutapika ukweli mchungu unaowauma!
Hio ndio tafsiri ya Falsafa ya Uruhani iliyoibuliwa safari hii katika uchaguzi mdogo wa Pemba. Ilikuwa falsafa iliyoibuliwa baina ya kejeli na umaskini wa Wapemba kufikisha ujumbe wao. Si kwamba hawakuumizwa na kuyakosa majimbo yale. Mbatia hawezi kuwa kaumizwa zaidi kuliko walivyoumia Wapemba. Lakini Wapemba wanajuwa wenyewe namna ya kuyapa maana machungu yao na kusema na nyoyo zao!
Kwa uwezo wao huo, ndio maana wamemudu kuwafanya CCM walioyachukuwa majimbo yale wajione ovyo zaidi na wao waliowakabidhi maruhani kuibuka mashujaa zaidi. Wanamjuwa nani bora kwao kati ya Ruhani na Subiani.
Basi hao wanaojidai kutishwa na uchaguzi walioufanya Wapemba, ningeliwashauri kwanza nawende Pemba. Huko wakawasome Wapemba na waisome hali ya Pemba. Wayajuwe maisha yao, wazifahamu hisia zao na maana ya mapambano haya katika maisha yao. Halafu wakirudi, ruksa waandike na waseme walichokiona!
Kwa mara ya kwanza makala hii ilichapishwa katika gazeti la Dira Zanzibar, Na. 26, Mei 30-Juni 7, 2003