UCHAMBUZI

Kwa nini Maridhiano na Umoja wa Kitaifa Zanzibar?

Hapa panaonekana pana undumilakuwili kutoka kwa wahafidhina wa Zanzibar wanaopinga maridhiano na umoja wa kitaifa visiwani mwetu. Kwa upande mmoja, hudai kwamba wao ndio wadumishaji wa umoja wa Wazanzibari, lakini kwa upande mwengine wao ndio wapinzani wake wakubwa. Labda tunatafautiana katika tafsiri ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, lakini hilo halihalalishi hata kidogo kuyaangalia mambo kwa makengeza.

Turudi nyuma kidogo, mwaka 2003, lilipofungiwa gazeti la Dira Zanzibar kwa madai kwamba lilikuwa likikiuka maadili ya uandishi wa habari kwa kuandika kwake habari na makala zilizozungumzia mambo yaliyokwishapita katika historia ya Zanzibar.

Kutokana na kauli za Mkurugenzi wa Habari wa SMZ wa wakati huo, Enzi Talib Aboud, Waziri aliyekuwa akishughulika na habari katika afisi ya Waziri Kiongozi, Salim Juma Othman, na hata ile ya Rais Amani Karume, katika Baraza la Idi la mwaka huo, ilionekana kwamba SMZ ina msimamo wa kusahau yaliyopita. Jambo zuri sana lau kama hivyo lisomekavyo ndivyo hasa lilivyo!

Kwa hatua ya kulifungia Dira kwa sababu hiyo, SZM ilitutaka tuamini kuwa kukumbushia yaliyopita ni hatari kubwa kwa usalama wa nchi na, hivyo, hatupaswi kabisa kuzigeuza shingo zetu na kuangalia kule nyuma tunakotoka. Lakini, ikiwa huu ndio msimamo wa serikali yetu juu ya historia yetu hadi sasa, mbona hauendani na ukaidi wake juu hoja na haja ya Umoja wa Kitaifa?

Jibu ni kwamba, si kweli kuwa wahafidhina wa SMZ hawayakumbuki na kuyakumbushia yaliyopita. Si kweli kwamba wenyewe hawaishi katika kumbukumbu hizo na si kweli kwamba wanataka mambo hayo yasahauliwe. Badala yake, wanachofanya ni kujitia makengeza ya kutazama kule, kumbe wanaona huku; na huo ni umbumbumbu. Ni umbumbumbu kwa kuwa wanapofanya uchaguzi wake huu wa kujiwekea yale ya kuyakumbuka na yale ya kuyasahau, hawafanyi hivyo kwa kuzingatia vigezo vyovyote vya kimantiki.

Kwa mfano, kigezo kimoja cha kimantiki kingelikuwa wakati, yaani wangelikuwa wanayakumbushia yale ya karibuni sana tu na kuyasahaulisha yale ya zamani mno. Au wangeliweka kigezo cha maafa, yaani kulikumbushia tukio lililoleta maafa kwa watu wengi na kulisahaulisha lile lililokuwa na maafa kwa wachache ili iwe somo kwa wengine yasije kujirudia.

Lakini hawafanyi hivyo, badala yake wanatumia hoja ya kihistoria kuhalalisha ung’ang’anifu wao kwenye ukinzani wa hoja ya kuwa na Umoja wa Kitaifa, ati kwa kuwa pana tafauti ya kihistoria kwenye chimbuko la CCM na CUF. Kwamba CCM imetokana na wapinduzi (Afro-Shirazi Party- ASP) na CUF imetokana na wapinduliwa (Zanzibar Nationalist Party- ZNP na Zanzibar and Pemba People’s Party- ZPPP).

Pamoja na kwamba ukweli unawasuta katika hili, maana ndani ya CUF muna waasisi na wanachama wengi kutoka ASP kama ilivyo kwa waasisi na wanachama wa ZNP/ZPPP kwenye CCM, baya zaidi ni kuwa wahafidhina hawa wameamua kujichagulia seti yao ya historia, iwe ya kweli au ya kubuni, na kuyabandika lebo ya YA KUKUMBUKWA, na vivyo seti nyengine kuwa ya YA KUSAHAULIWA. Ya kusahaulwa ndiyo haya inayotulazimisha tusiyataje na kutaka yafutike kabisa katika historia yetu na ya kukumbukwa ndiyo hayo wanayotaka wao iwe hoja ya kukataa umoja wa Wazanzibari.

Kwa nini wakafanya hivyo? Ni kwa kuwa kukumbukwa kwa mambo hayo kunaichora picha yao halisi. Kunayaanika yale maovu yao na ya watangulizi wao, ambao wote kwa hakika wana tabia ya kutawala kwa mkono wa chuma. Yanakumbusha ubadhirifu, idhilali na mateso yaliyoendeshwa na watawala wa serikali hii kwa kutumia jina la dola.

Ama ya kukumbukwa ndiyo haya tunayoyaona na kuyasikia kila siku yakiadhimishwa kwa ngoma na magwaride, kwa nyali na ng’ombe. Kwa kukumbukwa kwake mambo haya, kunawapa ‘ujiko’ wakubwa, kunawajengea hishima na kunawahakikisia kudumu kwa maslahi yao. Na hilo la kudumu kwa maslahi, ndilo pekee wanaloliabudia.

Mfano mmoja wa hili ni hayo Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Hadi leo hili ni tukio linaloadhimishwa kwa kila aina ya mbwembwe. Katika redio na televisheni za serikali, nyimbo zinazokumbusha yale yaliyotokea siku hiyo, huimbwa kila baada ya saa. Utasikia:

Mwenye panga, njooni
Mwenye shoka, njooni
Mwenye sime, njooni
Njooni, njooni, njooni!

Ikitoka hiyo, utasikia nyingine:

Chinja chinja, kata kata
Kanyanga kanyaga, ponda ponda!

Hakuna anayepingana, kimsingi, haja ya kuadhimishwa kwa siku hii kutokana na nafasi yake katika historia ya Zanzibar. Hata iweje, bado hili linabakia kuwa tukio lililoibadilisha kabisa historia ya Visiwa hivi, kwa ubaya au kwa wema. Baada ya Mapinduzi, Zanzibar haikuwa tena Zanzibar!

Lakini unaotilika mashaka hapa ni huu msimamo wa kusahau yaliyopita unaopigiwa parapanda na wahafidhina wa SMZ. Ikiwa kweli wanaamini kuwa kukumbushia yaliyopita kunahatarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwamba kunachokonowa hisia za visasi katika nyoyo za watenzwa, kwa nini wafanye kinyume chake?

Jamii ya Wazanzibari ni ya mchanganyiko, na wao wanalielewa hilo, maana ni sehemu ya mchanganyiko huo. Hadi leo ndugu na jamaa wa hao waliochinjwachinjwa, kupondwapondwa na kukatwakatwa kwa hayo mashoka na masime, sio tu kwamba wapo hai, bali pia wameshachanganyika na kizazi cha hao waliochinjachinja. Kizazi cha watenzwa na watenza ndicho hicho sasa kinachoiunda jamii ya Zanzibar tuliyonayo. Kwa mwenye akili, hii pekee ni sababu inayotosha kutetea Umoja wa Kitaifa.

Lakini wahafidhina wameligeuza hili kuwa kinyume mbele. Si kwamba hawajuwi kuwa kuendelea kuzungumzia machungu hayo kunautingisha umoja wa Wazanzibari, ambao mifano mingi imo ndani ya nyumba zao wenyewe, bali wanafanya kuwakebehi na kuwaudhi hata ndugu na watoto wao au wa kaka zao, na kisha kuchochea hisia mbaya za kisasi na machafuko.

Tatizo ni hawawachukulii ndugu zao hawa wanaoathirika na kumbukumbu hizi kuwa ni Wazanzibari kamili, au hata kama ni wanaadamu. Kama ilivyowahi kuimbwa huko nyuma “Mwana wa nyoka ni nyoka”, wahafidhina hawa wanawachukulia hawa kuwa ni hao wana wa nyoka, na leo hii wanapokataa kuingia nao katika mazungumzo na mashirikiano, ni kwa kuwa hivyo ndivyo wanavyowaangalia. Kimakosa, wahafidhina hawa wanataka iaminike kwamba CUF inaundwa na vizazi vya wale waliopinduliwa katika Mapinduzi ya 1964, hata kama kila ukweli unawasuta katika hilo.

Tukio hili la mapinduzi limetokea miaka 42 iliyopita, na bado linakumbushwa kwa mbwembwe na vimbwenga hivyo vinavyoibua hamasa na jazba miongoni mwa watu, wote Wazanzibari. Miaka 42 ni mingi sana kwa umri wa mwanaadamu. Ikiwa atachungwa vyema, ni muda unaotosha kumsahaulisha yale yaliyotokea.

Lakini bado wahafidhina hawa wanalikumbusha na kulishadidia kana kwamba jambo lenyewe limetokea jana asubuhi tu. Katika kampeni za uchaguzi uliopita Rais Amani Karume, wakati huo akiwa mgombea wa uraisi kupitia CCM, aliwahi kusema kwamba yale mapanga ya ’64 yangalipo na yangelitumika kama ingelibidi. Kiwango cha juu cha chuki na kutokuwajibika kwa kiongozi wa ngazi yake!

Turudi kwenye kadhia ya Dira Zanzibar ambayo ndiyo tulioanzia. Kama ni kukumbusha, Dira ilikuwa ikikumbusha yale yaliyotokea baada ya hapo, kiasi ya miaka 30 tu nyuma. Na nia ya Dira haikuwa chengine chochote zaidi ya kutafuta suluhu ya kudumu baina ya watendwa na watenda; na sio hii ya kufoji na ya kitambo iliyopo sasa.

Lakini kwa kuwa matukio hayo yalikuwa yakiichora picha halisi ya watawala wetu na ahli zao, basi SMZ ikalifungia gazeti hili. Kisingizio ni kwamba linachochea chuki na uhasama. Kama ni kweli kwamba kukumbusha yaliyopita kunachochea chuki na uhasama, hilo lilikuwa baya lilipofanywa na Dira tu?

Ni kipi kigezo cha ubaya na uzuri wa tendo hili? Kwa maneno mengine, kwa nini iwe wahafidhina wa SMZ wanapokumbushia ya nyuma ya miaka 42 iliyopita hawatafsiriwi kuwa inachochea chuki na uhasama, bali iwe hivyo, pale ilipofanya Dira kwa yale yaliyopita chini ya miaka 30 tu?

Huo sio unafiki tu wa wahafidhina, bali pia ni woga wao. Ni woga unaotokana na utoadilifu wao, maana kwa siku nyingi tabaka letu la watawala liliishi likijiaminisha kuwa liko juu ya sharia na mipaka yao ya haki haikuwa na ukomo. Waliichukulia nchi kuwa kama kikataa chao na sisi, raia, kama mifugo yao. Walijipa uwezo wa kufanya watakavyo bila kudadisiwa wala kuhojiwa.

Ndio maana, hapa Zanzibar, hadithi za mkubwa fulani kumpiga au kumuua mnyonge fulani, au za mtoto wa mkubwa huyo kumbaka mtoto wa fulani au kumpokonya mke mnyonge fulani, ni za kawaida. Hayo yalikuwa ni matokeo ya kundi la watu waliojichukulia madaraka ya nchi na kuifanya nchi kuwa milki yao na wana wao. Ni kama hayo na mengine mfano wake, ambayo yalifanyika Zanzibar kwa takriban miongo mitatu mizima, ndiyo yaliyokuwa yakipigiwa kelele na Dira, na ndiyo leo hii yaliyo nyuma ya hoja ya wahafidhina wa Zanzibar kukataa Umoja wa Kitaifa.

Kwa maneno machache, panapohusika historia ya Zanzibar, Dira ilikuwa inajaribu kuifanya nchi yetu isiwe milki ya Ibn Kinanata na Ibn Khuzaymata peke yao, bali iwe ya Wazanzibari wote. Dira ilikuwa ikililia haki ichukuwe nafasi yake, na kuilaani dhulma, iwe ya zamani au ya sasa, isiyatawale maisha ya watu.

Leo hii SMZ inapotutaka tuyasahau yaliyopita, lakini yenyewe ikawa inayakumbushia, sisi wengine tunashindwa kuielewa. Hatuielewi kwa kuwa tunaiona inadhihirisha unafiki. Haisemi hasa kile kilichomo katika nafsi za watawala, bali inafoji na hivyo haiwakilishi hata kidogo kile tunachokishudia jahara shahara.
Hakuna siku, tokea awamu yake ya mwanzo, ambapo SMZ imeyasahau yaliyopita au ikaacha kuyakumbusha. Isipokuwa, kama ilivyokwishaoneshwa, SMZ inajitahidi sana kujichagulia yapi ya kuyakumbushia na yapi ya kuyasahaulisha ili ichunge muradi wake. Na kwa hili, lazima SMZ iendelee kukosolewa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.